Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ucheshi Ningependa kuonyesha uthamini wangu kwa ile makala “Ingiza Ucheshi Katika Maisha Yako.” (Mei 22, 1994) Nimekuwa mwenye kujitenga nyakati zote, mara nyingi nikiwa mwenye hasira. Nilipojifunza kuweka ucheshi katika maisha yangu, mambo yalibadilika. Kicheko kwa kweli ndio “mwendo ulio mfupi zaidi kati ya watu wawili.”
A. Q. G., Brazili
Kansa Hivi karibuni nilimpa daktari wa mama yangu nakala ya toleo lenu la Aprili 8, 1994, juu ya “Kansa ya Matiti—Hofu ya Kila Mwanamke.” Kwenye ukurasa wa 10 mnaelezea sulfati-hidrazini kuwa “dawa isiyo na sumu.” Daktari huyo alituonyesha fasihi ya kitiba inayoorodhesha dawa hiyo kuwa yenye sumu sana.
D. M., Ufaransa
Kwa kuwa usumu wa kemikali hii kwa ushuhuda uliopo ni jambo linalobishaniwa, tulikosea kwa kuita dawa hiyo kuwa isiyo na sumu. Chunguo moja la utafiti wa Kirusi ulikiri kwamba dawa hiyo ilithibitika kuwa yenye sumu sana ilipopewa panya wa maabara kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, katika chunguo moja la kitiba juu ya kansa ya wagonjwa wa kibinadamu lililofanywa katika Kitovu cha Kitiba cha UCLA, usumu wa hidrazini uliripotiwa kuwa “usio mkali” asilimia 71 ya wagonjwa ikiripoti kutokuwa na athari zo zote za sumu. Hakuna shaka kwamba utafiti zaidi utahitajika kufanywa kabla hatari na manufaa yawezayo kupatikana ya dawa hii kuchanganuliwa kikamili.—Mhariri.
Opera Nyakati zote nimekuwa nikiona makala zenu kuwa nzuri sana, na nyakati zote nimekuwa na hisi ya kwamba ziliandikwa kwa ajili yangu hasa. Lakini sikufikiri kuwa mngeandika kuhusu kitu nikipendacho kikweli, opera. Singeweza kuacha kulia nilipoona ile makala “Usiku Mmoja Kwenye Opera.” (Julai 8, 1994) Asanteni sana.
S. S., Rumania
Hadithi ya Addie Ile makala “Addie Alipata Jibu Akiwa Amechelewa Lakini Si Kuchelewa Mno” (Julai 22, 1994) ilikuwa nzuri ajabu! Ilikuwa kama kusoma kitabu cha hadithi, isipokuwa ilikuwa hadithi ya kweli. Niliguswa hisia nilipongundua kuwa somo lenye kutumika la hadithi yake lilikuwa kwamba njia yenye matokeo zaidi ya kusaidia majirani wetu ni kwa kuhubiri!
D. L., Italia
Nimesoma tu masimulizi ya maisha ya Addie Clinton Few, na kwa mara ya kwanza katika miaka 19 ambayo nimekuwa nikisoma Amkeni!, ninaandika kusema asante! Mimi pia ni mweusi na nimeteseka kwa ukosefu wa haki wa kijamii kwa maisha yangu yote. Lakini nimejifunza kuwa Yehova kwa kweli hujali taabu za watu wasio weupe na ulimwengu mpya wake ulioahidiwa utasahihisha makosa yote.
L. N., Marekani
Makala hiyo ilionyesha akili yake na ucheshi uliochanganywa na unyenyekevu wake. Alikuwa msimulia-hadithi mkubwa! Niliona umalizio ukiwa wenye kugusa moyo sana. Mimi huyo katika basi dakika moja nikicheka na kulia dakika iliyofuata.
D. M., Marekani
Uzito Kupita Kiasi Nilipendezwa na makala “Vijana Huuliza. . . Mbona Mimi Ni Mnene Sana?” (Aprili 22, 1994) Nyakati zote nilikuwa nakasirishwa na uzito wangu, lakini makala hiyo ilisema kuwa Yehova haangalii jinsi unavyoonekana bali kilicho moyoni mwako. Asanteni.
N. C., Marekani
Ingawaje mimi si mnene kwa kweli, nyakati fulani natamani ningeonekana kama hao violezo. Nyakati fulani ninashuka moyo na kulia tu. Makala yenu ilinisaidia kuona kwamba si mimi pekee ninayehisi hivyo, na hilo lilikuwa lenye kufariji.
R. M., Marekani
Mimi si mnene kupita kiasi, lakini ni msichana aliyejenga na mwenye mabega mapana. Mimi hufanyiwa mzaha na binamu na ndugu zangu wakubwa. Nilithamini hoja yenu kwamba ingawa huenda nikawa mnene-mnene, hiyo haimaanishi napaswa kupunguza uzito.
M. T., Marekani