Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 6/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuhesabu Nyota
  • Wauaji Wanaoongoza Katika Marekani
  • Watoto na Vita
  • Iodini Katika Chumvi
  • Stediamu “Yabarikiwa Upya”
  • Matetemeko ya Dunia 80,000 Katika Miaka 40
  • Ule Ukuta Mkubwa wa Kijani-Kibichi
  • Uabudu Shetani Gerezani
  • Mikondo ya Chini Katika Bahari za Kusini
  • Uchunguzi wa Kiargentina Kuhusu Ulalwaji-Kinguvu
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
  • Jitihada za Kuwaokoa Watoto
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 6/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kuhesabu Nyota

Je, umepata kutazama juu kwenye anga la usiku lililojaa nyota na kujiuliza ni nyota ngapi ungeweza kuona? Gazeti Sky & Telescope hivi majuzi lilijibu swali hili la miaka mingi, na jibu si rahisi kupata kama mtu awezavyo kudhania. Hilo gazeti lilionelea kwamba kulingana na vitabu vya marejezo vya astronomia, mtazamaji wa kawaida aweza kuona nyota 2,862 katika anga kwenye kiunga kilicho na giza la kiasi katika latitudo za kimagharibi. Lakini si nyota hizi zote ziko juu ya upeo-macho wa mahali penyeji kwa wakati wowote ule; nyingi huzuka na kutua. Na zaidi, nyota nyingi ambazo huonekana kwa urahisi zinapokuwa juu moja kwa moja hazionekani zinapokuwa karibu zaidi na upeo-macho. Hiyo ni kwa sababu kwenye umbali-wima wa chini namna hiyo, nuru ya nyota lazima ipitie katikati ya sehemu kubwa ya angahewa la dunia ili ifike kwenye macho ya mtazamaji. Sky & Telescope humalizia kwamba kwa mtazamaji aliye kwenye latitudo ya digrii 40 kaskazini, yapata nyota 1,809 zingeonekana wakati wote mwakani.

Wauaji Wanaoongoza Katika Marekani

Ni visababishi gani vya kifo vinavyoongoza katika Marekani? Uchunguzi wa hivi majuzi uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association ulitafuta visababishi vikuu vya nje ya mwili, visivyoamuliwa na mfanyizo wa kijeni, visababishi ambavyo vilichangia vifo katika mwaka mmoja. Baada ya uchunguzi mwingi wa tarakimu, uchunguzi huo ulifikia mkataa kwamba kati ya vile vifo 2,148,000 katika Marekani katika mwaka wa 1990, 400,000 hivi vilisababishwa na tumbaku; 300,000 na mazoea ya ulaji na mazoezi ya mwili; 100,000 na alkoholi; 90,000 na vijiumbe maradhi; 60,000 na vitu vyenye sumu kama vile vichafuaji vya mazingira au vichafuaji katika chakula au maji; 35,000 na bunduki; 30,000 na tabia za kingono; 25,000 na magari; 20,000 na utumizi usio halali wa dawa za kulevya. Kwa yote hayo, uchunguzi huo ulipata kwamba visababishi vya nje ya mwili vilichangia nusu ya vifo vyote katika mwaka mmoja.

Watoto na Vita

Katika miaka kumi iliyopita, vita imethibitika kuwa hatari zaidi kwa raia—hasa watoto—kuliko kwa wanajeshi, kulingana na ripoti ya majuzi kutoka shirika la Uingereza la msaada Save the Children. Msemaji wa ng’ambo wa shirika hilo alinukuliwa katika ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press akisema hivi: “Tisa kati ya 10 ya wajeruhiwa wa vita ni raia. Watoto mara nyingi huwa wajeruhiwa wakubwa—na kwa kweli wao wana uelekeo mkubwa zaidi wa kuwa wajeruhiwa wa vita kuliko wanajeshi.” Ripoti hiyo ya kurasa 25 huorodhesha kiwango cha juu cha miaka kumi iliyopita kwa watoto wa ulimwengu, ikitoa tarakimu zifuatazo zenye kuhuzunisha. Zaidi ya watoto milioni 1.5 waliuawa katika vita ulimwenguni pote; zaidi ya milioni 4 walilemazwa, kupofushwa, kuharibiwa ubongo, au kulemazwa; zaidi ya 12 milioni walipoteza makao yao; milioni 10 wakawa wakimbizi; milioni 5 walilazimishwa kuishi katika kambi za wakimbizi, na milioni 1 walitenganishwa na familia zao. Mmoja kati ya watoto 200 ulimwenguni aliumizwa vibaya na vita katika miaka kumi iliyopita na alihitaji msaada ili kushinda msononeko wa kihisia moyo.

Iodini Katika Chumvi

Ukosefu wa iodini katika ulaji huathiri hali-njema ya angalau watu milioni 600, wakadiria Wakf wa Watoto wa Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa wanaoathiriwa, uhaba huo waaminika kusababisha watoto 100,000 hivi wazaliwe wakiwa kretini (waliovia akili na mwili kwa sababu ya uhaba mkubwa mno wa thiroidi) na kulemaza ukuzi wa kimwili na kiakili wa watoto wengine milioni 50. Ukosefu wa iodini pia husababisha rovu kuvimba kwa tezi thiroidi. Ni rahisi na si ghali kukinga uhaba wa iodini—kwa usahili tumia chumvi yenye iodini. Jitihada zinafanywa ili kutia iodini kwenye ugavi wa dunia wa chumvi katika mwaka 1995 na kuondoa matatizo ya uhaba wa iodini kufikia mwaka 2000.

Stediamu “Yabarikiwa Upya”

Timu ya kandanda katika Pescara, Italia, hivi majuzi ilitafuta msaada kutoka kwa askofu Mkatoliki ili kufukuza “bahati mbaya” iliyokuwa ikiwashambulia, laripoti gazeti La Repubblica. Wakiwa wamechoshwa na kipindi kirefu cha “bahati mbaya” inayohusianishwa kwa ukawaida na stediamu hiyo, msimamizi wa timu hiyo aliomba uingilio wenye nguvu na makasisi. Wakati fulani mbeleni, kasisi fulani alikuwa amebariki stediamu hiyo, na timu hiyo ikashinda mchezo wayo uliofuata. Wafanyakazi, mashabiki, na wachezaji waliohudhuria “kubarikiwa upya”—sherehe ya Misa iliyofanywa na askofu mwenyewe kwenye vibanda vya stediamu—wanatumaini kwamba wakati huu timu hiyo itafanya vyema hata zaidi. Wakati stediamu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza, ilibarikiwa pia, lakini “ni wazi kwamba kunyunyizwa kwa uvumba kwenye kuwekwa wakfu kumepoteza nguvu,” lasema La Repubblica.

Matetemeko ya Dunia 80,000 Katika Miaka 40

“Kituo cha matetemeko katika Bensberg karibu na Cologne [Ujerumani] kimeweka katika rekodi zaidi ya matetemeko ya dunia 80,000 katika sehemu zote za dunia,” laripoti Frankfurter Allgemeine Zeitung. Hilo lilitangazwa na Profesa Ludwig Ahorner, msimamizi wa kituo hicho, ambacho kimekuwa kikifuatilia matetemeko ya dunia na mitikisiko kwa miaka 40. Hicho kituo chawezaje kuweka katika rekodi matetemeko ya dunia yaliyotokea katika sehemu nyingine za ulimwengu? Kwa kutumia vifaa viwezavyo kuonyesha tofauti ndogo mno hivi kwamba huweza kutambua hata mitetemo hafifu mno katika dunia yasababishwayo na mawimbi ya dhoruba ya majira ya baridi yanayotwanga kwenye Pwani ya Bahari ya Kaskazini, yapata kilometa 200 kutoka hapo. Tetemeko la dunia lenye nguvu zaidi kupita yote katika Ujerumani yaliyopata kuwekwa rekodini na hicho kituo lilipiga Aprili 1992. Lilikuwa 5.9 kwenye kipimio cha Ritcher.

Ule Ukuta Mkubwa wa Kijani-Kibichi

Ule Ukuta Mkubwa wa China, ambao ulikuwa na mafanikio kwa sehemu tu katika kufukuza majeshi ya Mongol karne nyingi zilizopita, huenda ulikuja kupata utambuliwaji ulioustahili hatimaye. Kulingana na Science News, tangu miaka ya 1950, kanda kubwa za miti zimepandwa kando ya kijia cha ukuta huo. Ukuta huu Mkubwa wa Kijani-Kibichi, kama unavyoitwa, una yapata miti milioni 300. Kusudi layo: kuwa kizuizi kwa dharuba za vumbi zinazoingia China kutoka Jangwa la Gobi na maeneo mengine makame. Matokeo ni nini? Katika miaka ya 1950, jiji la Beijing lilipatwa na dharuba 10 hadi 20 kila wakati wa hari, ikipunguza uwezo wa kuona kwa zaidi ya kilometa moja kwa saa 30 hadi 90 kila mwezi. Lakini kufikia miaka ya 1970, idadi ya dharuba ilikuwa imepungua hadi chache kuliko tano kila vuli, ikisababisha mapunguo yaliyoshuka ya uwezo wa kuona kwa chini ya saa kumi kila mwezi. Science News lanukuu mwanakemia mmoja wa kianga-hewa akisema kwamba kanda hizi nyingi za miti “yaelekea ndiyo moja ya programu zenye nguvu zaidi ya zote za kurekebisha halihewa katika karne ya 20.”

Uabudu Shetani Gerezani

Maofisa wa gereza katika Colorado, Marekani, walikuwa wamemnyima mfungwa haki ya kufanya desturi za kidini za kishetani katika seli yake. Maagizo ya kiserikali ya gereza yalikataza ibada ya Ibilisi; na zaidi, hao maofisa walisababu kwamba baadhi ya vitu alivyoomba mfungwa kwa ajili ya ibada—kutia ndani fimbo fupi ya mbao, upatu, joho jeusi, mishumaa na vishikio vya mishumaa, kikombe cha ushirika mtakatifu na uvumba—vingeweza kutumiwa kama silaha. Hata hivyo, hakimu wa Serikali katika Denver majuzi aliondosha huo uamuzi, akiamua kwamba huyo mfungwa ana haki ya kikatiba ya kutekeleza dini yake akiwa gerezani. Hakimu huyo alifikia mkataa zaidi kwamba agizo dhidi ya ibada ya Ibilisi halikuwa la kikatiba. Kulingana na ripoti moja ya Shirika la Habari la Associated Press, hakimu huyo aliandika hivi katika uamuzi wake: “Twapaswa kumpa ibilisi anayostahili.” Mfungwa huyo anatumikia kifungo cha miaka kumi kwa sababu ya utoroshaji.

Mikondo ya Chini Katika Bahari za Kusini

Ripoti moja kwa Kongamano la Makanisa la Pasifiki lenye makao yalo makubwa katika Fiji hufunua kwamba mamlaka za makanisa makubwa zimetiwa hofu kwa ukuzi wa kile wanachoita NRGs (Vikundi Vipya vya Kidini) katika Pasifiki ya Kusini. Kwa msingi, NRGs vinavyozungumziwa ni Assemblies of God, Seventh-Day Adventists, Mormons, Mashahidi wa Yehova, na washiriki wa dini ya Baha’i. Tayari asilimia 20 hivi ya wanakisiwa wamejiunga na dini hizi, yasema ripoti iliyoandikwa na Manfred Ernst. Hayo makanisa yanalalamika kwamba NRGs huzuia mabadiliko ya kisiasa kwa sababu vingine kati yavyo havijiungi na vyama vya kisiasa au harakati za kupinga; vingine havijiungi na vyama vya wafanyakazi. “Kulingana na Ernst,” lasema Mainichi Daily News, “NRGs vyawa maarufu zaidi kwa sababu ya ukosefu wa uvutio wa dini kubwa za Kikristo za kimila.”

Uchunguzi wa Kiargentina Kuhusu Ulalwaji-Kinguvu

Kutoka Januari hadi Oktoba 1994, mkoa mmoja wa Kiargentina, Córdoba, uliripoti visa 254 vya ulalwaji-kinguvu. Gazeti la Buenos Aires Clarín lilionelea kwamba ripoti ya polisi kutoka Córdoba “iliachilia mbali ile ngano inayohusu jeuri ya kingono.” Walalaji-kinguvu sikuzote si wale walio wapotovu wa kingono ambao huvizia majeruhi wasiojulikana chini ya ufuniko wa giza; kulingana na ripoti hii, 4 kati ya watu 10 wanaolalwa kinguvu wanatendewa vibaya katika nyumba zao wenyewe na baba zao wenyewe, babakambo, au watu wengine wa ukoo. Tarakimu zingine katika ripoti ya polisi zaonyesha kwamba ‘kati ya visa 254 vilivyoripotiwa mwaka huu, asilimia 36 vilifanyika katika nyumba za majeruhi; asilimia 23 wakati wa kuondoka kwenye majumba ya dansi; asilimia 13 kwenye barabara za umma; asilimia 10 mashamba yasiyo na watu; asilimia 6 kwenye mahali pa ujenzi; na asilimia 3 kwenye viwanja vya mpira wa miguu, katika vyoo vya vituo vya basi, katika seli za gereza, na kwenye mabasi ya kuendea tafrija.’ Ripoti hiyo yamalizia kwa kutaja kwamba polisi wamesuluhisha asilimia 66.54 ya hivyo visa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki