Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuungua Nishati Asanteni kwa ule mfululizo “Je, Wewe Huungua Nishati?” (Januari 8, 1995) Ingawa natumika nikiwa painia, kwa miezi mingi nimehisi kunyong’onyea na kukosa hamasa. Hiyo makala ilinipa hoja ambazo nitazitumia kibinafsi, hasa lile dokezo la kuepuka kuchambua wengine.
M. S., Ujerumani
Hizi zilikuwa makala zisizo za kawaida kwangu kwa sababu hatimaye nilitambua tatizo langu. Mimi ni mke, mama wa watoto wanne, nami nina kazi nyingi mno ya kufanya nyumbani. Kwa kuhuzunisha, mimi hupata uthamini mchache sana kutoka kwa familia yangu. Nahisi vyema zaidi kujua kwamba hili ni tatizo la kawaida miongoni mwa watu wenye hisia nyepesi. Msiache kamwe kuchapisha makala kama hizi!
J. M., Italia
Nimekuwa nikipata uchovu, ukosefu wa idili, kutokuwa na uwezo, kutokuwa na tumaini, na kudhoofika. Baada ya kusoma hiyo makala, nafahamu mambo yaliyoongoza kwenye hisia hizi. Nataka mjue jinsi ilivyo vyema kueleweka na kujua kwamba Yehova na tengenezo lake hujali vya kutosha hata kuandika makala zenye kutia moyo.
Z. L., Marekani
Kuungua nishati kulichangia kuacha kwangu utumishi wa Betheli na baadaye kuacha kupainia. Nilikuwa ukingoni mwa kuacha kutumika nikiwa mzee! Sasa naweza kuona mahali ambapo nilishindwa kuwasilisha ifaavyo tatizo langu katika wakati uliopita. Nimejirekebisha katika sehemu hii, na mtazamo wangu wa akilini ni bora zaidi.
E. R., Marekani
Ilikuwa yenye kutia moyo kujua kwamba wahudumu wengine wa Kikristo wamevumilia tatizo hili na kwamba wamelishinda.
C. L., Uswisi
Akina Mama Wasioolewa Asanteni kwa ile makala “Vijana Huuliza . . . Akina Mama Wasioolewa Waweza Kushughulikiaje Hali Yao Vizuri Iwezekanavyo?” (Oktoba 8, 1994) Mnakubali kwamba huo ujauzito ulitukia kupitia utendaji-makosa. Lakini badala ya kudumu katika hili na kumfanya msichana ahisi vibaya hata zaidi, mnatoa miongozo yenye kutumika na yenye msaada.
J. D., Marekani
Nilikuwa mzazi asiye na mume miaka kumi iliyopita. Lakini kwa msaada wa Yehova na wazazi wangu Wakristo, nimefanya vyema. Baada ya kuhitimu kutoka shuleni, nilitumika nikiwa mhudumu wa wakati wote kwa miaka sita na kuolewa na mwanamume Mkristo ambaye sasa anatumika akiwa mzee. Nimenufaika sana kutokana na rehema na fadhili za Yehova na ninaweza kutumia ono langu kusaidia wengine.
A. M., Marekani
Singeweza kuzuia machozi nilipokuwa nikisoma hiyo makala. Nilipitia hali sawa kabisa na ile mliyofafanua. Kwa kuwa sasa mimi ni Mkristo, ninafurahi kuweza kulea binti yangu kwa ufahamu wenye kina.
C. R. S., Brazili
Kukoroma Ile makala “Wewe Hukoroma?” (Septemba 8, 1994) ilionya juu ya hatari za kukoroma ziwezazo kutokea. Lakini mlimaanisha kwamba ikiwa wewe ni mkoromaji wa kupindukia, una tatizo la pumzi kukatika-katika usingizini. Si lazima iwe hivyo. Ule mwelekeo wa kukoroma hutukia kadiri tunavyozeeka. Kwaweza pia kutukia kwa sababu ya mizio na matatizo ya sinusi. Lakini ikiwa kukoroma kwa kupindukia kunaambatana na vipindi vya kutopumua, vikifuatiwa na mitweto au miguno, na kuhisi usingizi au kutukia kwa uchovu wakati wa mchana, tatizo la usingizi la apnea yamkini ndilo lenye hatia. Tiba ya kawaida zaidi si upasuaji, bali ni vidude vinavyotumia hewa iliyoshindiliwa ili kuweka vipitio vya hewa vikiwa bila kuzuiwa wakati wa usingizi.
C. S., Marekani
Twathamini maelezo haya na twasikitika ikiwa habari yetu ilitokeza hali yoyote ya kuelewa kimakosa. Mamlaka za kitiba zakubali kwamba kukoroma kwa pindi kwa pindi si jambo lisilo la kawaida. Kuhusu matatizo yote ya kitiba, ukaguzi wa daktari ni wa maana kwa ajili ya tiba ifaayo.—Mhariri.