Hula—Ile Dansi ya Hawaii
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HAWAII
TAJA Hawaii, na mara nyingi hula huja akilini. Ingawa hula huhusianishwa kipekee na Hawaii, vyanzo vyayo viko katika Pasifiki ya Kusini.
Katika nyakati za kale Wahawaii hawakuwa na lugha iliyoandikwa, kwa hiyo nyimbo zilitumiwa kusimulia historia na desturi zao. Hula, ikiwa na misogeo ya nyonga, mikono na miguu, pamoja na ishara za uso, ziliambatana na nyimbo hizi.
Hakuna njia yoyote ya kuweka katika maandishi chochote kinachohusishwa na hula kabla ya 1778, wakati ambapo Nahodha Cook na watu wake walifika. Kinachojulikana leo kinategemea kwa sehemu kubwa mazoea na nyimbo.
Hula za kwanza huenda ikawa zilikuwa desturi takatifu. Hata hivyo, haifikiriwi kwamba hula zote zilikuwa vitendo vya ibada au sehemu ya utendaji wa kidini.
Uvutano wa Wamishonari
Hula ilikuwa ikichezewa wavumbuzi na mabaharia waliokuwa katika meli zilizozuru katika karne za 18 na 19. Inawezekana kwamba wateja hawa waliokuwa wakilipa pesa walitaka hula ziwe wazi kingono.
Wamishonari walipofika katika 1820, walikuwa na sababu yenye nguvu ya kushutumu hula. Baada ya kupata kibali cha machifu, wamishonari hao walishambulia hula kuwa ya kikafiri, na kazi ya Ibilisi. Hata kabla ya hili, katika 1819, mabadiliko katika mazoea ya kale ya kidini yaliletwa na Malkia Mtawala Kaahumanu, mjane wa Mfalme Kamehameha 1. Hili lilitia ndani kuvunja-vunja sanamu na kuondoa desturi za kifumbo. Dansi na nyimbo zisizohesabika zilipotea milele pia.
Kaahumanu alikubaliwa kuwa mshiriki wa kanisa katika 1825. Katika 1830 alitoa amri ya kukataza maonyesho ya hadharani ya hula. Baada ya kifo chake katika 1832, machifu fulani walipuuza amri hiyo. Kwa miaka kadhaa, wakati ambapo vizuizi vya kiadili vilidhihakiwa na Mfalme mchanga Kamehameha 3 na waandamani wake, hula kwa muda mfupi ikapendwa na wengi tena. Lakini katika 1835 huyo mfalme alikubali kwamba njia zake hazikufaa, na ufalme huo ukarudi chini ya mamlaka ya Wakalvini.
Kuhuishwa kwa Hula
Wakati wa utawala wa Mfalme Kalakaua (1874-1891), uhuisho ulitokea kukiwa na kukubaliwa kamili kwa hula kwenye maonyesho ya hadharani. Kwa ajili ya kuvishwa kwake taji katika 1883, miezi mingi ya mazoezi na msisimko ilifikia upeo katika maonyesho ya hadharani ya nyimbo na hula nyingi, baadhi yazo zikiwa zimeandikwa hasa kwa ajili ya pindi hiyo. Kufikia kifo chake katika 1891, hula ilikuwa imepitia mabadiliko mengi katika miendo ya dansi na misogeo ya mwili, na mfuatano wa ala za muziki kama vile ukulele, gita, na zeze ulikuwa umeingizwa.
Baada ya mwisho wa utawala wa kifalme katika 1893, hula ilipunguka tena. Hata hivyo, kufikia katikati mwa karne ya 20 ilikuwa ikisitawi. Ili ivutie watazamaji wengi mno, mageuzo mengi yalifanywa. Kwa kuwa wengi hawangeweza kufahamu lugha ya Hawaii, maneno ya Kiingereza yalitumiwa. Hula ya kisasa hukazia zaidi dansi yenyewe—misogeo ya mikono na miguu, kusukasuka nyonga, na wonyesho wa uso.
Kadiri idadi ya wageni waliokwenda visiwani ilivyoongezeka, hula ikawa yenye kupendwa sana. Wasafiri kutoka bara walirudi kwao na dansi walizojifunza na kuanza kuzionyesha katika sinema za Hollywood pasipo wacheza-dansi wa Hawaii. Katika 1935 hata katuni Minnie Mouse alimchezea hula Mickey, ambaye alikuwa akicheza gita yake ya chuma.
Hula Leo
Kwa yale “Mabadiliko ya Kihawaii” katika miaka ya 1970, ujuzi wa waimbaji, wacheza-dansi, na walimu mahiri ukawa msingi wa kuhuisha namna za kale za hula. Leo kuna mahiri wa hula wanaotokeza upya dansi za kale na wale wanaobuni mpya. Katika visa vyote viwili, majaribio yao yametokeza maonyesho ya kupita kiasi na yenye kutazamisha.
Uhusiano wao wa kiroho pamoja na miungu mingi ya Wahawaii umeendelea kwa kiasi fulani hadi siku za kisasa. Kila mwaka kabla ya kuanza kwa Merrie Monarch Festival inayofanywa katika Hilo, Hawaii, shule za hula huzuru kwa madhumuni ya ibada shimo la moto la Pele au maeneo yaliyomwagika mawe ya volkeno yaliyoyeyuka hivi majuzi. Wao huimba, kucheza dansi, na kutoa matoleo ya maua, beri, na kileo aina ya gin, wakiomba baraka zake kwa jitihada zao katika mashindano. Vikundi kutoka ulimwenguni pote hushindana kwa siku tatu za mashindano yanayoonwa kuwa Olimpiki ya hula.
Hula imekuja kuwa sehemu kubwa ya kurudi tena kwa utamaduni katika Hawaii. Hutia ndani dansi zenye huzuni zikiambatana na nyimbo zenye kicho kwa miungu na miungu ya kike na vilevile maonyesho sahili ya maisha ya kila siku katika visiwa hivyo ambayo hayana umaana wowote wa kidini.
Wakristo wanapaswa kuwa wateuzi sana katika kucheza au kutazama hula za aina fulani. Wanapaswa kuhakikisha kwamba hawatoi heshima bila kujua kwa mungu fulani au mungu fulani wa kike. Uangalifu unapaswa kutolewa pia wakati wa kusikiliza au kuimba nyimbo. Nyingi za hizi huwa na maneno yenye maana iliyofichika au maana mbili. Hili likiwekwa akilini, mtazamaji au mshiriki anaweza kufurahia hula ikiwa aina ifaayo ya kitumbuizo.