Miatuko ya Dunia Iliyofichika
KATIKA Agosti 18, 1994, angalau watu 171 walikufa Algeria kutokana na tetemeko la dunia lenye nguvu sana. Mamia walijeruhiwa, na maelfu wakaachwa bila makao. Majuma machache mapema zaidi Bolivia, Colombia, na Indonesia zilikumbwa pia na matetemeko makubwa ya dunia, yote pamoja yakisababisha kupotezwa kwa mamia kadhaa ya uhai wa wanadamu.
Je, ulijua kwamba misiba hii mikubwa ilikuwa imetukia? Huenda sivyo, isipokuwa ikiwa wewe binafsi uliathiriwa nayo au uliishi katika nchi jirani. Kwa upande mwingine, wakati matetemeko makubwa ya dunia yanapokumba eneo la California, Marekani, habari hizo huonekana kuenea upesi sana, na habari za kisayansi hutolewa karibu wakati huohuo.
Sababu ni kwamba hakuna eneo jingine ambalo limechunguzwa kwa bidii sana na wanasayansi kama kusini mwa California, ambapo vipima miendo ya ardhi zaidi ya 700 hurekodi matetemeko ya dunia yenye kiwango cha chini kama vile 1.5. Kuwepo kwa wataalamu wengi wa matetemeko ya dunia katika eneo hilo ndiyo sababu ya ule mmiminiko mkubwa wa habari za matetemeko ya dunia katika eneo hilo.
Ugunduzi wa Juzijuzi
Utafiti huu mwingi bila shaka umewasaidia wanasayansi katika nchi nyingi kuelewa matetemeko ya dunia na hata kujaribu kuyatabiri ili kuzuia misiba. Tekinolojia kama hiyo ni muhimu sana, kwa kuwa kila mwaka karibu matetemeko ya dunia 40 yenye ukubwa usioweza kupuuzwa hukumba sehemu mbalimbali za ulimwengu. Pia kuna matetemeko ya dunia yasiyo hatari lakini bado yaliyo makubwa vya kutosha kuhisiwa. Haya hutokea kati ya mara 40,000 na 50,000 kila mwaka!
Matetemeko mengi ya dunia yaonekana kuwa tokeo la kupasuka, kuvunjika na kubadilika kutokana na mkazo kwa yale mabamba makubwa ya miamba yaliyo chini ya ardhi. Kwa kawaida mipasuko hii hutokea kwenye nyufa katika uso wa dunia. Nyufa hizi huitwa miatuko.
Mara nyingi, wanasayansi wanaweza kujua sehemu miatuko hiyo iliko, hivyo waweza kuonyesha maeneo yawezayo kukumbwa na matetemeko ya dunia. Kwa nini twasema “mara nyingi”? Kwa kuwa hivi majuzi wanasayansi wametambua kwamba matabiri yao si sahihi sana kama walivyofikiri wakati mmoja. Kwa mfano, wanasayansi wanasumbuliwa na ufunuo wa karibuni wa kwamba mengi ya matetemeko ya dunia yawezayo kupimwa katika California hutokea kwenye miatuko iliyofichika—mara nyingi katika maeneo ambayo wanajiolojia mbeleni waliyaona kuwa hayana hatari ya matetemeko ya dunia.
Kulingana na wanasayansi wa dunia Ross Stein wa Uchunguzi wa Jiolojia wa Marekani na Robert Yeats wa Chuo Kikuu cha Serikali ya Oregon, “sehemu zenye vilima vinavyoinuka na kushuka kwa uanana au ya milima iliyojipinda haziogopeshi sana, nazo hustarehesha badala ya kuhatarisha.” Hata hivyo, uchunguzi wao ulionyesha kuwako kwa miatuko chini ya miamba iliyojipinda, nyingi kati yayo ikiwa imetolewa mafuta yaliyomo. Ni kwa nini miatuko hii ya chini ya ardhi imekosa kuonekana, nayo ni hatari kiasi gani?
Tisho Lisilopasa Kupuuzwa
Wanajiolojia wamegundua kwamba miamba yaweza kusongwa na kukunjwa kama kitambara kilichokunjwa-kunjwa. Lakini kwa ujumla hilo lilifikiriwa kuwa jambo linalochukua muda, na ambalo huendelea hatua kwa hatua. Hata hivyo, uchunguzi wa karibuni wa miamba iendeleayo kujipinda huonyesha kwamba hiyo hujipinda kuelekea juu kwa ghafula—hata kufikia meta 5 kwa muda wa sekunde chache tu! Mwendo huu wa kupinda husonga fungu la miamba lililo chini yao. Mkazo utokeao hupasua mwamba ulio chini ya mkunjo, na kipande kimoja cha mwamba huanza kusonga juu ya kile kingine. Mikunjo hii, inayoonekana kuwa isiyo hatari, pamoja na miatuko isababishayo mwamba kusonga juu ya mwingine huwa matetemeko ya dunia kabla ya wataalamu wa matetemeko ya dunia kuyagundua. Utendaji kama huo wa miatuko chini ya ardhi waweza kutokeza matetemeko ya dunia yenye nguvu kama tu vile itokezavyo miatuko ijulikanayo zaidi, ambayo yaonekana katika uso wa dunia.
Lile tetemeko la dunia la Januari 17, 1994, la Northridge katika eneo la Los Angeles ni kielelezo kimoja cha majuzi cha yale ambayo mwatuko uliofichika waweza kufanya. Hilo tetemeko la dunia lilisababishwa na utendaji wa mwatuko ulio chini sana ambao ulitokea kati ya kilometa 8 hadi 19 chini ya ardhi. Kabla ya hilo tetemeko la dunia, wanasayansi hawakujua kamwe kuwako kwa mwatuko huo. Mwatuko huo uliofichika ulisababisha uharibifu mkubwa wa mali, ukijeruhi watu zaidi ya 9,000, na kuua 61.
Wanasayansi hufikiri kwamba miatuko iliyofichika ndiyo kisababishi cha idadi fulani ya matetemeko ya dunia, si katika California pekee lakini pia katika Algeria, Argentina, Armenia, India, Iran, Japani, Kanada, New Zealand, na Pakistan. Kwa miongo michache iliyopita, maelfu ya watu yamekufa katika nchi hizi likiwa tokeo la matetemeko ya dunia ambayo huenda ilitokezwa na miatuko iliyofichika.
Wanasayansi sasa wanakabili ule mtihani wa kugundua mahali ambapo mikunjo hiyo itendayo hutokea na kutabiri hatari iwezayo kutokea kupitia tetemeko la dunia. Kwa wakati huu, wao hawapuuzi tena zile nguvu za kuharibu za mlima wenye kuinuka na kushuka unaoonekana kuwa usio hatari.
[Sanduku katika ukurasa wa22]
Je, Los Angeles Unapunguka?
Miatuko na mikunjo mingi sana inayopatikana chini ya Los Angeles, California, hufanya eneo hilo lisiwe thabiti hata kidogo. Bonde la Los Angeles huonekana kufyonza mwingi wa mkazo usababishwao na mkunjo ulio karibu katika San Andreas Fault. (Ona toleo la Amkeni! la Julai 22, 1994, kurasa 15-18.) Wanajiolojia wa huko wanakadiria kwamba kukunjika huko kusababishwako na mkazo huo huenda kwapunguza eneo la lile bonde la Los Angeles kwa robo ekari kila mwaka.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
Tufe: Mountain High Maps™ copyright © 1993 Digital Wisdom, Inc.