UKIMWI Katika Afrika—Jumuiya ya Wakristo Ina Lawama Kadiri Gani?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Afrika
Kama litumiwavyo katika makala hii, neno “Jumuiya ya Wakristo” hurejezea dini zenye kudai kuwa za Kikristo, kwa kutofautisha na Ukristo wa Biblia.
Jumuiya ya Wakristo
“Sehemu za ulimwengu ambapo wakazi wazo hudai kuwa na imani ya Kikristo.”—Webster’s New World Dictionary.
UKIMWI
“Hali ya kuwa na ukosefu wa kinga mwilini inayoshirikishwa na kuambukizwa kwa chembe za mfumo wa ukingaji kupitia kirusi-retro.” —Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary.
UKIMWI umeenea kwenye tufe lote. Inakadiriwa kuwa watu milioni 17 tayari wameambukizwa HIV, kirusi kisababishacho UKIMWI. Nao waenea upesi sana.
Ingawa uangalifu mwingi umeelekezwa kwa masuala ya kitiba, kisiasa, na kihisia-moyo yahusianayo na mwenezo huu, machache yamesemwa juu ya masuala ya kidini yahusikayo. Wazo la dini kuhusishwa na mweneo wa UKIMWI laweza kuonekana kuwa lisilo halisi kwa wasomaji fulani. Lakini si la kipumbavu ufikiriapo hali ambayo imeendelea katika kontinenti ya Afrika.
UKIMWI hasa umepiga Afrika kwa nguvu.a Watu fulani husema kuwa hiyo kontinenti ina asilimia 67 ya visa vya UKIMWI ulimwenguni pote. Katika Chad idadi ya visa ambavyo vimeripotiwa katika miaka mitano iliyopita imeongezeka mara 100. Na bado yakadiriwa kuwa ni thuluthi tu ya visa vyote imeripotiwa. Kulingana na ripoti ya Benki ya Ulimwengu, UKIMWI umekuwa kisababishi kikuu cha kifo miongoni mwa watu wazima katika miji mingi ya Afrika.
Dini—Je, Ilikuwa na Fungu?
Bila shaka, Ukristo—dini iliyofundishwa na Yesu Kristo—hauwezi kulaumiwa kwa sababu ya msiba huu. Hata hivyo, kama ilivyoonyeshwa hapa chini, neno “Jumuiya ya Wakristo” hutia ndani zile nchi ambazo watu hudai kuwa Wakristo. Nayo Jumuiya ya Wakristo kwa wazi ina hatia. Si kwamba makanisa yalianzisha au kueneza kirusi cha UKIMWI kwa njia ya moja kwa moja. Lakini UKIMWI umeenea katika Afrika kwa sababu ya kufanya ngono ovyoovyo.b Hivyo, UKIMWI waweza kuitwa tatizo la kiadili na, hivyo hutokeza maswali ya kidini yenye kusumbua. Kwani, “Ukristo” wa Afrika ulitoka moja kwa moja katika nchi za Magharibi. Viongozi wa kidini walichukua daraka la kuwageuza Waafrika na kuwaingiza katika aina yao ya dini, wakidai kuwa ilitoa njia ya maisha ishindayo zile njia za kidesturi za Afrika. Je, kwa kweli uchochezi wa Jumuiya ya Wakristo uliboresha maadili ya waumini wao wapya? Lile tatizo la UKIMWI laonyesha wazi kwamba ni jambo lililo tofauti kabisa lililotendeka.
Kwa kielelezo, fikiria taifa la Chad. Kati ya miji minne yalo, mitatu ina idadi kubwa ya “Wakristo.” Sehemu kubwa ya ule mwingine ni Uislamu. Lakini, ni kwenye ile miji mitatu ya “Ukristo” ambapo kirusi hicho kwa sasa chaenea sana! Kigezo hicho hupatikana kote kwenye hiyo kontinenti. Afrika ya kati na ya kusini, ambazo kwa jina ni Wakristo, zina kiwango cha juu zaidi cha maambukizo kuliko Afrika Kaskazini, iliyo na Waislamu walio wengi.
Jinsi Afrika Ilivyopata Kuwa ya “Kikristo”
Ni kwa nini kirusi hicho kimeenea sana kati ya watu wadaio kuwa wafuasi wa Kristo? Kwa kweli, ingawa Waafrika wengi hujiita Wakristo, ni wachache kwa kulinganisha wadumishao viwango vya kiadili vya Ukristo, vilivyo katika Biblia. Hili huonekana kuwa tokeo la moja kwa moja la njia ambayo wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walitumia “kugeuza” Waafrika.
Katika karne za 18 na 19, itikadi za kidesturi za Jumuiya ya Wakristo zilishambuliwa. Uhakiki wa Biblia ulienea sana, ukiishusha Biblia machoni pa wengi kuwa fasihi ya zamani tu. Nadharia ya mageuzi pia ikaanza kukubaliwa, hata miongoni mwa makasisi. Mbegu za mashaka zilipandwa. Imani katika Maandiko Matakatifu ilitiliwa mashaka. Katika hali hizo haishangazi kuwa jitihada za Jumuiya ya Wakristo za “kugeuza” Waafrika zilikazia mambo ya kimwili. Wamishonari wa kanisa walihubiri gospeli ya kijamii, wakikazia zaidi kutimiza matendo ya kusaidia jamii badala ya kusaidia waliogeuzwa kuishi kulingana na kanuni za Biblia za maadili. Huenda kwa kutojua, wamishonari hasa walisaidia kupuuza mfumo wa maadili uliokuwapo.
Kwa kielezo, ndoa ya wake wengi ilikuwa zoea la muda mrefu katika jumuiya nyingi za Afrika. Hata hivyo, ngono za ovyoovyo zilikuwa chache sana, kwa kuwa makabila mengi yalikuwa na sheria kali kuhusu uzinzi. Joseph Darnas, mwalimu mstaafu, ajulikanaye sana katika Chad, aliliambia Amkeni! kuwa kabla ya kuja kwa wamishonari wa kanisa, “ilifikiriwa kuwa uzinzi ulileta bahati mbaya.” Likiwa tokeo, “wenye hatia waliadhibiwa vikali kwa kuhatarisha jamii—mara nyingi kwa kifo.” Ushirikina? Ndiyo, lakini itikadi kama hizo zilipunguza ngono za ovyoovyo.
Kisha wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo wakaja. Wakahubiri kwa kupinga ndoa ya wake wengi lakini walifanya machache sana kutilia nguvu kanuni za Biblia za adili. Ingawa Biblia husema kuwa waasherati na wazinzi wasiotubu wapaswa kufukuzwa kutoka katika kutaniko la Kikristo, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo huchukua mara chache sana hatua za kinidhamu kuwaelekea wakosaji. (1 Wakorintho 5:11-13) Kufikia wakati huu, wanasiasa wengi Waafrika wamezidi katika mwenendo wao usio wa adili, na bado hubaki wakiwa washiriki wa kanisa wenye msimamo mzuri. Uaminifu katika ndoa ni adimu sana kati ya Wakristo wa jina katika Afrika.
Kisha kuna kile kielelezo kiovu kiwekwacho na makasisi wenyewe. Katika utamaduni huu wa kifamilia, ni jambo la kawaida kuoa na kuwa na watoto wengi. Huenda hii ndiyo sababu inayofanya idadi yenye kushangaza ya makasisi wa Katoliki kuhisi wana haki ya kupuuza viapo vyao vya usafi wa kiadili na useja. Gazeti la The New York Times la Mei 3, 1980 liliripoti: “Katika sehemu nyingi huko mashambani, . . . makasisi na maaskofu huoa wake wengi.”
Kama ilivyo, ndoa kama hizo hazihalalishwi, nao “wake,” kihalisi ni masuria tu. Mwenendo mpotovu kama huo hauwezi kufutiliwa mbali kuwa si kitu. Kulingana na Times, “kasisi Mkatoliki ajulikanaye sana” akubali kwamba “kasisi wa Afrika ni ufananisho wa mamlaka, uwakilisho wa uweza badala ya mtumishi wa Yesu Kristo.” Ujumbe kutoka kwa huo “uwakilisho wa mamlaka” waonekana kuwa, “Fanya nisemavyo lakini si nitendavyo.”
Uvamizi wa Vitumbuizo vya Magharibi
Lisilopaswa kupuuzwa vilevile ni furiko la vitumbuizo visivyo vya adili kingono ambalo limeenea katika Afrika katika miaka ya majuzi. Katika Chad vyumba vya video vya umma visivyosimamiwa vizuri vitumbuizavyo vimetokea kotekote—kwenye nyumba za kibinafsi, kwenye magereji, na, mara nyingi zaidi, kwenye nyua baada ya giza kuingia. Maonyesho haya si ghali, yakigharimu fedha kidogo kama franka 25 (senti 5 za Kimarekani). Watoto wachanga huhudhuria. Vitumbuizo vyote hivyo hutoka wapi? Vingi vyavyo hutoka Marekani—nchi idaiyo kuwa ya Kikristo!
Lakini je, uvamizi huu wa utamaduni wa Magharibi umekuwa na matokeo yoyote halisi kwa watazamaji? Mishonari mmoja wa Mashahidi wa Yehova, mwenye uzoefu wa miaka 14 katika Afrika ya Kati, asema: “Watu wa huku mara nyingi hawana uhusiano sana na ulimwengu wa Magharibi ila tu kupitia waonayo kwenye kaseti za video. Wao hutaka kuwa kama watu wa Magharibi wawaonao kwenye sinema. Sijagundua bado uchunguzi wowote ulioripotiwa uthibitishao hilo, lakini yaonekana kuwa wazi kwa watu wengi hapa kwamba vitumbuizo kama hivyo huendeleza ukosefu wa adili katika ngono.”
Jinsi inavyoshangaza kwamba huku maofisa wa afya wakijaribu kwa bidii kuzuia kuendelea kwa ugonjwa huu wa kufisha upitishwao kingono, mataifa yaitwayo ya Wakristo hutokeza propaganda ziendelezazo tabia hatari sana isiyo ya adili! Ingawa makanisa yamefanya machache ili kupunguza wimbi hilo nyumbani au ugenini, serikali kadhaa za Afrika, kama vile Chad na Kamerun, zimejaribu kuzuia au angalau kuwekea mipaka kuingizwa kwa vitu vya kiponografia nchini. Lakini jitihada zazo mara kwa mara hazijafanikiwa.
Tokeo la haya yote limekuwa kudidimia kwa maadili kulikoenea miongoni mwa “Wakristo” wa Afrika. Hali mbaya za kiuchumi pia zimekuwa na matokeo ya kichinichini. Kwa kuwa kazi ni adimu, wanaume mara nyingi hulazimika kuziacha familia zao kwa miezi kadhaa mfululizo ili kupata kazi. Wanaume wa aina hiyo kwa wazi huwa lengo la makahaba wa huko. Ingawa hivyo, hao makahaba kwa kawaida huwa maskini. Kule kudai kwa wazazi mahari nyingi pia ni kisababishi. Wanaume wengi hawaoi kwa sababu hawawezi kupata fedha zihitajikazo ili kulipia mahari. Hivyo wengine huishi kwa kuwa na mahusiano mengi haramu ya muda tu. Katika hali hiyo ya kiadili na kiuchumi, UKIMWI umeenea upesi.
Suluhisho kwa Hilo Tatizo
Ni wazi kwamba Jumuiya ya Wakristo haibebi lawama zote kwa ajili ya UKIMWI katika Afrika. Lakini uhakika wa kwamba hiyo hubeba sehemu kubwa ya lawama hizo ni wazi na la kuhuzunisha. Hilo huwa na maana nzito kwa ajili ya watu ambao hutaka kuwa miongoni mwa wale ambao Yesu aliwaita “waabuduo halisi.”—Yohana 4:23.
Licha ya lawama hizo, ni nini kiwezacho kufanywa ili kuzuia kuenea kwa UKIMWI? Serikali za Afrika zimeanzisha kampeni za kuzuia UKIMWI, kwa kupendekeza utumiaji wa kondomu. Lakini Dakt. Samuel Brew-Graves, mwakilishi wa Nigeria wa Shirika la Afya Ulimwenguni, alikubali hivi kwa unyoofu: “Mtu binafsi apaswa kuwa na mtindo-maisha mzuri . . . , nayo familia yapaswa . . . kuepuka ngono za ovyoovyo.”
Muda mrefu kabla ya UKIMWI kujulikana, Biblia ilishutumu ngono za ovyoovyo na kupendekeza usafi wa kiadili, kujidhibiti, na uaminifu katika ndoa. (Mithali 5:18-20; 1 Wakorintho 6:18) Mamia ya maelfu ya Mashahidi wa Yehova katika Afrika waweza kutoa uthibitisho wa kwamba kufuata kanuni hizi huandaa ulinzi wa kadiri fulani kutokana na UKIMWI na magonjwa mengine yapitishwayo kingono. Kushikamana kwao sana na Biblia hutoa lawama kubwa kwa Jumuiya ya Wakristo. Wakristo hawa wa kweli huweka tumaini lao katika ulimwengu mpya ujao ambamo “haki yakaa ndani yake.” (2 Petro 3:13) Kwa watu wa imani, hilo ndilo suluhisho la pekee kwa lile tatizo la UKIMWI.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, ona ule mfululizo “UKIMWI Katika Afrika—Utaishaje?” katika toleo letu la Agosti 8, 1992, Kiingereza.
b Huo ugonjwa waweza pia kuenezwa kupitia utiaji-damu mishipani na kwa kutumia pamoja sindano zitumiwazo kutia dawa za kulevya mishipani. Baadhi ya Wakristo wasio na hatia wamepata huo ugonjwa kutoka kwa wenzi ambao wamekuwa na ukosefu wa adili katika ngono au waliotumia dawa za kulevya.
[Blabu katika ukurasa wa 20]
“Katika sehemu nyingi huko mashambani, . . . makasisi na maaskofu huoa wake wengi.”—The New York Times
[Picha katika ukurasa wa 20]
Kielelezo kiovu cha makasisi wa Jumuiya ya Wakristo kimeongezea ule mweneo wa ngono za ovyoovyo katika Afrika
[Picha katika ukurasa wa 21]
Vijana wamo hatarini itokezwayo na vitumbuizo visivyo vya kiadili vitokavyo kwenye mataifa ya “Kikristo”