Kuutazama Ulimwengu
“Wachina Wanaozeeka”
“Wachina wanaozeeka wanaongezeka kwa utaratibu,” laripoti gazeti China Today. “Kufikia mwisho wa 1994 China ilikuwa na wazee-wazee milioni 116.97 wenye umri unaozidi miaka 60, hilo ni ongezeko la asilimia 14.16 kupita 1990.” Watu wenye umri wa miaka zaidi ya 60 sasa ni karibu asilimia 10 ya watu wote katika nchi hiyo, na hao wazee-wazee wamekuwa wakiongezeka kwa karibu mara tatu kuliko watu wote. Wanatunzwaje? Ingawa mapato ya kazi, malipo ya uzeeni, bima ya kijamii, na msaada hutunza mahitaji ya wengi, zaidi ya asilimia 57 ya wazee-wazee wa China wanategemezwa na watoto wao au na watu wengine wa ukoo. “Kwa kuwa mahusiano ya familia katika China ni thabiti kwa kulinganisha, na China ina desturi nzuri ya kustahi na kutunza wazee-wazee, wazee-wazee wengi huishi pamoja na jamaa zao, nao hutunzwa vyema nao,” lasema China Today. “Ni asilimia 7 tu ya wazee-wazee wa China wanaoishi peke yao.”
Kufanyisha Watoto Kazi—Tatizo Linaloongezeka
Kulingana na ripoti moja ya majuzi ya Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi, asilimia 13 ya watoto wa ulimwengu wenye umri kati ya miaka 10 na 14—watoto wapatao milioni 73—hulazimishwa kufanya kazi. Ripoti hiyo iliongezea kwamba kama takwimu za watoto walio na umri wa chini ya miaka kumi na za wasichana wanaofanya kazi za nyumbani muda wote zingepatikana, idadi ya watoto wanaofanya kazi yaelekea ingekuwa mamia ya mamilioni. Ingawa shirika hilo lenye makao makuu huko Geneva limekuwa likijaribu kwa miaka 80 kukabili hali ya kufanyisha watoto kazi, hilo tatizo limeendelea kuongezeka na kupanuka, hasa katika Afrika na Amerika ya Latini. Ingawa kazi ngumu na hatari za kazi zao ndizo hali za mamilioni ya watoto hao, ukahaba ulitajwa kuwa tatizo kubwa hasa. Katika nchi fulani “watu wazima huona kutumia watoto kwa makusudi ya kingono kuwa njia bora zaidi ya kuepuka ambukizo la [HIV],” yasema ripoti hiyo. Gazeti International Herald Tribune la Paris lilisema kwamba shirika hilo “lililaumu maofisa wa serikali ambao . . . wamepuuza tatizo hilo.”
Kutimiza Mahitaji ya Watoto
Ripoti ya UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa), The State of the World’s Children 1995, yasema inashangaza kufikiria kwamba ulimwengu hauwezi kutimiza mahitaji ya msingi ya watoto wao. Ili kutoa kielezi cha jambo linalomaanishwa, UNICEF latoa tarakimu zifuatazo: Gharama ya ziada inayokadiriwa kuwa inahitajika ili kuandaa lishe ifaayo na utunzi wa msingi wa afya ulimwenguni pote ni dola bilioni 13 kwa mwaka mmoja; kwa elimu ya msingi, dola bilioni 6; kwa maji safi na usafi wa kutunza afya, dola bilioni 9; kwa mpango wa uzazi, dola bilioni 6—hiyo ni jumla ya dola bilioni 34 kwa mwaka mmoja. Wao wasema kwamba linganisha hiyo na kadirio la fedha ambazo tayari zinatumiwa kila mwaka kwa vitu vifuatavyo: gofu, dola bilioni 40; bia na divai, dola bilioni 245; sigareti, dola bilioni 400; jeshi, dola bilioni 800. Wao wasema kwamba kwa hakika watoto wa ulimwengu wanaweza kutunzwa ifaavyo ikiwa mambo yafaayo yanatangulizwa.
“Aina Mpya ya Vita ya Kasumba”
Hivyo ndivyo The Times of India lilivyofafanua jitihada kubwa za makampuni ya tumbaku ya Marekani za kujaribu kuuza bidhaa zao katika Asia. Ingawa katika India pekee angalau watu milioni moja hufa kila mwaka kwa sababu ya maradhi yanayohusika na tumbaku, serikali ya India haijatunga sheria dhidi ya tumbaku. Jambo hilo, kulingana na ripoti ya Times, limetokezwa na ushawishi mwingi wa makampuni ya tumbaku, ya kitaifa na ya kimataifa, na kutokezwa vilevile na “sheria za serikali ya Marekani ambazo hutisha kuwekea vikwazo vya kibiashara nchi ambazo zinakataa mauzo ya bidhaa za tumbaku za Marekani.” Imekadiriwa kwamba asilimia 99 ya watu wanaoishi katika sehemu za mashambani za India hawajui madhara yoyote yanayotokezwa na matumizi ya tumbaku. Matangazo ya vyombo vya habari mara nyingi huonyesha mvutaji akiwa mwenye uhakika, mwenye kuvutia, na mwenye usalama. Mashindano makubwa ya michezo ipendwayo, kama vile kriketi, hudhaminiwa na makampuni ya tumbaku. Pia, sigareti ni chanzo muhimu cha mapato kwa serikali, ambayo imeweka rasilimali katika makampuni manne ya tumbaku.
Itikadi ya Moto wa Helo Yakataliwa
Ripoti moja ya Kanisa la Uingereza imekataa yale maoni ya kidesturi kwamba helo ni mahali pa moto na mateso ya milele. Kulingana na ripoti ya Tume ya Fundisho ya kanisa, “Wakristo wamekubali mafundisho ya kidini yenye kushtua sana ambayo yanamfanya Mungu kuwa dubwana katili kabisa nayo yanaacha makovu ya kisaikolojia kwa watu wengi.” Ripoti hiyo iliongezea: “Kuna sababu nyingi za kufanya badiliko hili, lakini miongoni mwa sababu hizo ni mateto ya kiadili kutoka ndani na vilevile nje ya imani ya Kikristo dhidi ya dini ya hofu, na pia hisi inayoendelea kuongezeka ya wazo la kwamba Mungu ambaye amepeleka mamilioni kwa mateso ya milele hakuwa kabisa Mungu mwenye upendo aliyefunuliwa katika Kristo.” Hata hivyo, wao wasema kwamba kila mtu atakabili siku ya hukumu na kwamba wale ambao watashindwa na mtihani wataangamizwa, au hawatakuwapo. Gazeti Herald Tribune la New York lataja: “Ripoti hiyo ilielewesha wazi kwamba haiwezekani kwa watu wote wa dini zote kuokolewa tu.”
Nyani-Mtu Shujaa
Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka mitatu alianguka katika mahali ambapo nyani-watu (gorila) saba wa Afrika walikuwa wamewekwa kwa ajili ya maonyesho katika Hifadhi ya Wanyama ya Brookfield, kiungani mwa Chicago, naye aliokolewa na nyani-mtu wa kike. Mvulana huyo, ambaye alikuwa amemwacha mama yake, alipanda ukingo wa vyuma wenye kimo cha meta 1.2 na kuanguka karibu meta 6 chini kwenye sakafu ya simiti ya chumba hicho, na kujeruhi kichwa chake. Huyo nyani-mtu mwenye umri wa miaka minane aitwaye Binti Jua alimwendea polepole na kumbeba kwa uanana mtoto huyo aliyejeruhiwa. Huku mtoto wake mwenyewe akiwa angali anashikilia mgongoni mwake, Binti aliubeba polepole mwili wa mtoto huyo na kumpeleka hadi kwenye mlango wa utumishi, akimweka chini kwa uangalifu mahali ambapo watunzaji wa hifadhi hiyo ya wanyama waliweza kumfikia na kumwondoa. Binti, ambaye alikuwa ameachwa na mama yake, “alikuwa amefundishwa na watunzaji wake ustadi wa kulea watoto, hao walimpa wanasesere wa kibinadamu wa kutunza na kuangalia” kabla ya yeye kuzaa mtoto wake mwenyewe, laripoti Daily News la New York. Tangu wakati huo amevutia maelfu ya wageni naye amethawabishwa kwa kupewa matunda mengi. Mvulana yule aliyechubuka na kukwaruzwa, alipata nafuu.
Fanya Uchaguzi
“Je, mwaka wako umeanza vibaya?” ikauliza makala moja katika gazeti New Scientist. “Usiwe na wasiwasi, kuna angalau miaka mipya 14 ulimwenguni pote ambayo bado unaweza kuchagua mmoja kati yayo.” Kwa kweli ni nchi zinazotumia kalenda ya Gregory pekee ndizo huona Januari 1 kuwa siku ya kwanza ya mwaka. Ni Juliasi Kaisari ambaye, katika 46 K.W.K., aliamua kwamba mwaka wa kalenda uanze na Januari 1, na mfumo huo ulidumishwa na Papa Gregory alipofanya mabadiliko katika kalenda katika 1582. Tamaduni mbalimbali zilipositawisha mifumo yazo zenyewe ya kalenda, angalau Siku za Mwaka Mpya 26 zilijitokeza. Kati ya zile ambazo ziko leo, kalenda ya Kichina ndiyo ya kale zaidi. Kwao Mwaka Mpya unaanza mwaka huu katika Februari 7. Mwaka Mpya wa Kiyahudi utaanza Oktoba 2. Kalenda ya Kiislamu, ambao hutegemea kabisa mwezi wa angani, pia ina Mwaka Mpya wayo yenyewe—Mei 8.
Kuvuta Sigareti Kwahusianishwa na Vifo vya Vitoto
Watoto wachanga na wanawake waja-wazito hawapasi kuwekwa mahali penye moshi wa sigareti, wasema watafiti wa Uingereza. Uchunguzi wa miaka miwili uliofanywa na Hospitali ya Watoto Wagonjwa ya Royal, katika Bristol, ulichunguza kila kisa cha ugonjwa wa kifo cha ghafula cha vitoto (SIDS), ambacho pia huitwa vifo vya vitoto, katika maeneo matatu ya Uingereza. Wakiwahoji wazazi wa watoto wachanga 195 ambao walikuwa wamekufa na wale wazazi wa watoto wachanga 780 ambao walikuwa wameishi, walipata kwamba kati ya akina mama ambao watoto wao wachanga walikufa, asilimia 62 walikuwa wavutaji, kwa kulinganisha na asilimia 25 ya akina mama wenye kuvuta ambao watoto wao wachanga hawakufa. “Utafiti huo wa majuzi waonyesha wazi kwamba akina baba wanaovuta sigareti pia ni tatizo,” asema Joyce Epstein, wa Wakfu wa Uchunguzi wa Vifo vya Vitoto. “Tukiweza kuondoa uvutaji wote karibu na mazingira ya mtoto mchanga, twakadiria kwamba vifo [visa vya SIDS] vitapunguka kwa asilimia 61.”
Damu Yafunua Siri
Hemoglobini imechunguzwa kwa uangalifu sana kwa zaidi ya miaka 60 na inasemwa kwamba labda hiyo ndiyo protini ambayo imechunguzwa zaidi katika biolojia. Imejulikana kwa muda mrefu kwamba hiyo hubeba oksijeni kutoka kwa mapafu hadi kwenye tishu na kurudisha kaboni dioksidi na oksidi nitriki. Lakini, matabibu na wanasayansi walishangaa kwa ugunduzi wa majuzi ambao ulionyesha fungu la ziada la hemoglobini—fungu la kupeleka aina nyingine ya oksidi nitriki, ambayo huitwa oksidi-nitriki kuu, kwa sehemu zote za mwili. Oksidi-nitriki kuu hasa inatimiza fungu muhimu katika afya na katika kudumisha uhai wa chembe na tishu, kutia ndani kudumisha kumbukumbu la kujifunza, kuchochewa kingono, na msongo wa damu. Hemoglobini, kwa kudhibiti kiasi cha oksidi nitriki ambazo zaweza kupatikana katika mishipa ya damu, yaweza kufanya mishipa ya damu ipanuke au kufinyaa. “Ugunduzi huo waelekea utachangia sana tiba ya msongo wa damu na kutengenezwa kwa damu-sanisia,” laripoti The New York Times. Kwa wakati huu, vibadala vingi vya damu vina mwelekeo wa kupandisha msongo wa damu. Hiyo huenda ikawa hivyo kwa sababu ya ukosefu wa oksidi-nitriki kuu, watafiti hao wasema.