Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 10/22 kur. 26-27
  • Kanisa Katoliki na Yale Maangamizi Makubwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kanisa Katoliki na Yale Maangamizi Makubwa
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupinga Wayahudi na Utamaduni Wao
  • Ukimya wa Pius 12
  • Kulaumu Wengine
  • Je! Ni Enzi Mpya kwa Wayahudi na Wakristo?
    Amkeni!—1992
  • Makanisa Yaungama
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Vatikani 2—Baraka au Laana?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 10/22 kur. 26-27

Kanisa Katoliki na Yale Maangamizi Makubwa

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Italia

TANGU mwaka wa 1987, kumekuwa na mazungumzo kuhusu mipango ya Kanisa Katoliki kutokeza hati inayoonyesha kwamba linakiri fungu lililochangia wakati wa yale Maangamizi Makubwa. Basi, kulikuwa na matazamio makubwa mnamo Machi 1998 wakati Tume ya Vatikani kwa Ajili ya Uhusiano wa Kidini pamoja na Wayahudi ilipotoa hati yenye kichwa We Remember: A Reflection on the Shoah.a

Ingawa wengine walithamini hati hiyo, wengi hawakuridhika na yaliyomo. Kwa nini? Hawakupenda nini katika hati hiyo?

Kupinga Wayahudi na Utamaduni Wao

Hati ya Vatikani inatofautisha kati ya kupinga utamaduni wa Kiyahudi, ambako kanisa linakiri kuwa na hatia, na kupinga Wayahudi, ambako kanisa linakataa kukiri hatia. Watu wengi hawaridhiki na tofauti hiyo na mkataa unaofikiwa. Rabi mmoja wa Ujerumani Ignatz Bubis alisema: “Kwangu hiyo ni kama Kanisa linasema si kosa letu; ni kosa la mtu mwingine.”

Ingawa mwanahistoria wa Katoliki aliye Mwitalia Giorgio Vecchio akubali kwamba kuna tofauti baina ya kupinga utamaduni wa Kiyahudi na kupinga Wayahudi, yeye asema kwamba “tatizo pia ni kuelewa jinsi ambavyo upinzani wa Katoliki dhidi ya utamaduni wa Kiyahudi huenda umechangia kuzuka kwa upinzani dhidi ya Wayahudi.” Ni jambo la kupendeza kwamba gazeti la Vatikani L’Osservatore Romano, la Novemba 22-23, 1895, lilichapisha barua iliyosema: “Mkatoliki yeyote mnyoofu, hasa ni mpinga-Wayahudi: na ndivyo ilivyo na ukasisi, kwa wajibu wa mafundisho na huduma.”

Hata hivyo, sehemu ya hati hiyo ya Vatikani ambayo ilichochea uchambuzi zaidi, ni kutetea matendo ya Pius wa 12, aliyewekwa rasmi kuwa papa kabla tu ya kufyatuka kwa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Pius wa 12 alikuwa ametumika akiwa mjumbe wa papa nchini Ujerumani kuanzia mwaka wa 1917 hadi 1929.

Ukimya wa Pius 12

Mwanasheria wa Italia Francesco Margiotta Broglio anaona kwamba hati hiyo “haina mambo mapya juu ya lile suala ambalo lilikuwa limejadiliwa sana liitwalo ‘ukimya’ wa Papa Pius wa 12, juu ya Wajerumani ambao alikuwa akiwapenda, na juu ya uhusiano wake wa kibalozi na utawala wa Nazi kabla ya yeye kuwa papa na wakati alipokuwa papa.”

Wachunguzi wengi wanakubaliana kwamba hata mtu aoneje umuhimu wa hati hiyo We Remember, swali la kwa nini viongozi wa Kanisa Katoliki walibaki kimya kuhusu mauaji ya kikatili katika kambi za mateso za Nazi “halijajibiwa.” Kulingana na mwanahistoria Mmarekani George Mosse, kwa kuamua kubaki kimya, Pius wa 12 “aliokoa kanisa lakini alidhabihu ujumbe wa maadili wa kanisa lake. Yeye alitenda kama kiongozi wa kisiasa, wala si kama papa.” Wachunguzi wenye kuarifiwa wa Vatikani waamini kwamba jambo lililokawiza kutolewa kwa hati hiyo lilikuwa ugumu wa kushughulikia fungu la Pius wa 12 katika yale Maangamizi Makubwa.

Kutetewa kwa Papa Pius wa 12 kumeudhi wengi. “Ukimya juu ya ‘ukimya wa papa’ unafanya hati hii ivunje moyo,” aandika Arrigo Levi. Elie Wiesel, mshindi wa Tuzo la Amani la Nobeli la 1986, alisema: “Naona kudai kwamba sisi Wayahudi twapaswa kumshukuru Pius wa 12 ni uzushi, nikitaja tu kwa upole.”

Kulaumu Wengine

Hati hiyo inafuata tofauti ya kidesturi ambayo imefanywa na wanatheolojia Wakatoliki, nayo inadai kwamba katiba ya kanisa ni takatifu na imehifadhiwa na Mungu isiwe na kosa, huku washiriki wake, ambao ni watenda-dhambi, wana hatia ya maovu yoyote yanayofanywa. Tume ya Vatikani yaandika: “Ungetarajia kwamba kwa kufuatia maadili Wakristo wengine wangepinga mnyanyaso dhidi ya Wayahudi na kwamba [Wakristo] wangechukua hatua madhubuti ya kuwasaidia. . . . [Wakristo hao] hawakuwa na nguvu sana ya kuteta. . . . Tunaghairi sana kwa makosa na kasoro za hao wana na binti wa Kanisa.”

Lakini, kusema kwamba washiriki mmoja-mmoja wa kanisa ndio wenye hatia badala ya kukubali hatia kwa ujumla kulionekana kwa wengi kuwa kupiga hatua kubwa sana ya kurudi nyuma, kukilinganishwa na maombi ya wazi ya hivi majuzi ya kutaka msamaha. Kwa mfano, Kanisa Katoliki la Roma nchini Ufaransa lilitoa “Tangazo Rasmi la Toba,” likiomba Mungu na Wayahudi msamaha kwa ajili ya “kutojali” kwa Kanisa Katoliki wakati wa mnyanyaso wa Wayahudi chini ya serikali ya Ufaransa ya wakati wa vita. Katika taarifa iliyosomwa na Askofu-Mkuu Olivier de Berranger, kanisa lilikubali kwamba liliruhusu mapendezi yake yenyewe “yafunike amri ya Biblia ya kustahi kila mtu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu.”

Tangazo la Ufaransa lilisema hivi kwa sehemu: “Ni lazima kanisa litambue kwamba kuhusu mnyanyaso wa Wayahudi, na hasa kuhusu hatua nyingi zenye kupinga Wayahudi zilizotolewa na wenye mamlaka wa Ufaransa wa wakati wa vita, kutojali kulienea zaidi kuliko chukizo. Ukimya ukawa ndio kawaida, na maneno yenye kupendelea wahasiriwa yalikuwa machache sana. . . . Leo, twakiri kwamba ukimya huo ulikuwa kosa. Pia twatambua kwamba kanisa nchini Ufaransa lilishindwa katika jitihada zake za kufundisha dhamiri za watu.”

Zaidi ya miaka 50 baada ya msiba mbaya wa Shoah, au yale Maangamizi Makubwa, Kanisa Katoliki halijakubali ukweli wa historia yake yenyewe—historia ya utata na ukimya, tukisema tu kwa upole. Lakini kuna wengine ambao hawajapata kamwe kuwa katika hali kama hiyo. Mashahidi wa Yehova, kikundi kidogo cha kidini ambacho kilinyanyaswa na Wanazi, hawakunyamaza wala kuridhiana.

Kama ambavyo imekuwa wazi katika nyakati za karibuni, tofauti na washiriki wa kanisa, Mashahidi walishutumu ukatili wa Nazi. Na si mtu mmoja-mmoja tu aliyefanya hivyo. Wasemaji wao rasmi walifanya hivyo na vichapo vyao pia vilifanya hivyo. Mwanahistoria Christine King, ambaye ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Staffordshire nchini Uingereza, alieleza: “Mashahidi wa Yehova waliteta. Wao waliteta tangu mwanzoni. Wao walisema kwa umoja. Na walisema kwa ujasiri mkubwa kabisa, ambao una somo kwetu sisi sote.”

[Maelezo ya Chini]

a Shoah ni neno la Kiebrania kwa yale Maangamizi Makubwa, ambamo Wanazi waliwaua kwa wingi Wayahudi, Wajipsi, Wapoland, Waslavi, na wengine katika Vita ya Ulimwengu ya Pili.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Papa Pius wa 12 alinyamaza wakati wa Maangamizo Makubwa

[Hisani]

U.S. Army photo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki