Je, Kitabu Hiki Chaafikiana Na Sayansi?
Dini haijaona sayansi kuwa rafiki yayo sikuzote. Katika karne zilizotangulia wanatheolojia fulani walikinza uvumbuzi mbalimbali wa kisayansi walipohisi kwamba huo ulihatarisha ufasiri wao wa Biblia. Lakini je, kwa kweli sayansi ni adui wa Biblia?
IKIWA waandikaji wa Biblia wangalikuwa wamekubali maoni yenye kuenea ya kisayansi ya siku yao, tokeo lingalikuwa kitabu chenye taarifa za kisayansi zisizo sahihi kabisa. Hata hivyo waandikaji hawakuendeleza maoni hayo yasiyokuwa ya kisayansi. Kinyume cha hilo, waliandika taarifa kadhaa zilizo thabiti kisayansi na pia zilizopinga moja kwa moja kauli zilizokubaliwa hiyo siku.
Dunia Ina Umbo Jipi?
Swali hilo limevutia wanadamu sana kwa maelfu ya miaka. Maoni ya kawaida katika nyakati za kale yalikuwa kwamba dunia ilikuwa tambarare. Kwa kielelezo, Wababiloni waliamini kwamba ulimwengu wote mzima ulikuwa sanduku au chumba ambacho dunia ilikuwa sakafu yacho. Makuhani wa Kivedi wa India waliwazia kwamba dunia ilikuwa tambarare na kwamba upande mmoja tu wayo ulikuwa umekaliwa na watu. Kabila la kikale katika Asia liliiona dunia kuwa sinia kubwa ya kubebea vikombe vya chai.
Mapema sana kuanzia karne ya sita K.W.K., mwanafalsafa Mgiriki Pythagoras alitoa nadharia kwamba kwa kuwa mwezi na jua ni tufe, lazima dunia pia iwe tufe. Aristotle (karne ya nne K.W.K.) aliafiki baadaye, akifafanua kwamba hali ya dunia kuwa tufe inathibitishwa na kupatwa mbalimbali kwa mwezi. Kivuli cha dunia kwenye mwezi ni mviringo.
Hata hivyo, dhana ya dunia tambarare (ikiwa imekaliwa na watu kwenye sehemu yayo ya juu tu) haikutoweka kabisa. Watu fulani hawakuweza kukubali lile dokezo la kupatana na akili la dunia iliyo duara—dhana ya antipodi.a Lactantius, mtetea-imani Mkristo wa karne ya nne W.K., alidhihaki hilo wazo lenyewe. Alisababu hivi: “Je, kuna mtu aliye mpumbavu sana aweze kuamini kwamba kuna watu ambao nyayo zao ziko juu kuliko vichwa vyao? . . . kwamba mimea na miti hukua kuelekea chini? kwamba mvua, na theluji, na mvua-barafu huanguka kuelekea juu?”2
Dhana ya antipodi ilitokeza hali ya kutatanisha kwa wanatheolojia wachache. Nadharia fulani zilishikilia kwamba ikiwa kulikuwa na watu wanaoishi katika upande ule mwingine wa dunia, wasingeweza kuwasiliana hata kidogo na wanadamu wajulikanao ama kwa sababu bahari ilikuwa pana mno isiweze kusafiriwa ama kwa sababu kanda yenye joto kali isiyoweza kupitika iliizunguka ikweta. Basi watu walioishi kwenye ule upande mwingine wa dunia wangeweza kuwa walitoka wapi? Kwa kutatanishwa, wanatheolojia fulani walipendelea kuamini kwamba kusingeweza kuwa na watu wanaoishi kwenye ule upande mwingine wa dunia, au hata, kama alivyojadili Lactantius, kwamba dunia hata isingeweza kuwa tufe!
Bado, dhana ya kwamba dunia ni tufe ilienea, na hatimaye ilikubaliwa na watu wengi sana. Hata hivyo, ni baada tu ya enzi ya anga kuanza katika karne ya 20, ndipo imewezekana kwa wanadamu kusafiri mbali angani vya kutosha kuthibitisha kwa kujionea moja kwa moja kwamba dunia ni tufe.b
Na msimamo wa Biblia ulikuwa nini katika suala hili? Katika karne ya nane K.W.K., wakati maoni yaliyoenea yalipokuwa kwamba dunia ilikuwa tambarare, karne kadhaa kabla ya wanafalsafa wa Kigiriki kutoa nadharia kwamba dunia yamkini ilikuwa tufe, na maelfu ya miaka kabla ya wanadamu kuiona dunia ikiwa tufe kutoka angani, nabii Mwebrania Isaya alitaarifu hivi kwa usahili wa ajabu: “Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia.” (Isaya 40:22, italiki ni zetu.) Neno la Kiebrania chugh, linalotafsiriwa hapa “duara,” laweza pia kufasiriwa kuwa “tufe.”3 Tafsiri nyingine za Biblia husema, “tufe la dunia” (Douay Version) na “dunia mviringo.”—Moffatt.c
Mwandikaji wa Biblia Isaya aliepuka ngano za kawaida juu ya dunia. Badala ya hivyo, aliandika taarifa ambayo haikutishwa na maendeleo ya uvumbuzi wa kisayansi.
Ni Nini Kinachoitegemeza Dunia?
Katika nyakati za kale, wanadamu walitatanishwa na maswali mengine juu ya ulimwengu: Dunia inakalia nini? Jua, mwezi, na nyota hutegemezwa na nini? Hawakuwa na ujuzi wowote juu ya sheria ya nguvu za uvutano za ulimwengu wote mzima, zilizofanyizwa na Isaac Newton na kuchapishwa mwaka wa 1687. Wazo la kwamba kwa kweli, magimba ya kimbingu huning’inia katika anga tupu pasipo kitu halikujulikana kwao. Hivyo, mafafanuzi yao mara nyingi yalidokeza kwamba vitu au dutu zenye kugusika ziliitegemeza dunia na magimba mengine ya kimbingu huko juu.
Kwa kielelezo, nadharia moja ya kale, labda yenye kuanzishwa na watu walioishi kwenye kisiwa fulani, ilikuwa kwamba dunia ilizungukwa na maji na kwamba ilielea katika maji hayo. Wahindu waliwazia kwamba dunia ilikuwa na misingi kadhaa, mmoja juu ya mwingine. Ilikalia ndovu wanne, hao ndovu walisimama juu ya kobe mkubwa mno, huyo kobe alisimama juu ya nyoka mkubwa sana, na nyoka huyo aliyejikunja alielea juu ya maji ya ulimwengu wote mzima. Empedocles, mwanafalsafa Mgiriki wa karne ya tano K.W.K., aliamini kwamba dunia ilikalia kisulisuli na kwamba kisulisuli hicho kilikuwa ndicho kisababishi cha mwendo wa magimba ya kimbingu.
Miongoni mwa maoni yenye uvutano zaidi yalikuwa yale ya Aristotle. Ingawa alitoa nadharia kwamba dunia ni tufe, alikana kwamba ingeweza kwa vyovyote kuning’inia katika anga tupu. Katika maandishi yake On the Heavens, alipokuwa akikanusha dhana ya kwamba dunia hukalia maji, alisema hivi: “Si asili ya maji, sawa na vile si asili ya dunia, kuning’inia hewani: lazima yakalie kitu.”4 Kwa hiyo, dunia ‘hukalia kitu gani’? Aristotle alifundisha kwamba jua, mwezi, na nyota zilikuwa zimeshikamana na sehemu ya juu ya tufe zito, jangavu. Tufe moja lilikuwa ndani ya jingine, dunia ikiwa—bila kujongea —katikati. Matufe hayo yalipozunguka moja likiwa ndani ya jingine, vitu vilivyokuwa juu yayo—jua, mwezi, na sayari —vilijongea kuivuka anga.
Ufafanuzi wa Aristotle ulionekana kuwa wenye kupatana na akili. Ikiwa magimba ya kimbingu hayakuwa yameshikamana imara na kitu fulani, yangeweza kukaa juu kwa njia gani nyingine? Maoni ya Aristotle aliyestahiwa yalikubaliwa kuwa jambo la hakika kwa miaka ipatayo 2,000. Kulingana na The New Encyclopædia Britannica, katika karne ya 16 na ya 17 mafundisho yake “yalifikia kiwango cha kuwa fundisho la kidini” machoni pa kanisa.5
Darubini-upeo ilipobuniwa, waastronomia walianza kutilia shaka nadharia ya Aristotle. Bado, jibu liliwaepuka mpaka Sir Isaac Newton alipofafanua kwamba sayari zinaning’inia katika anga tupu, zikiwa zimeshikiliwa katika mizingo yao na kani isiyoonekana—nguvu za uvutano. Ilionekana kutosadikika, na baadhi ya wafanyakazi wa Newton waliona ni vigumu kuamini kwamba anga lingeweza kuwa tupu, bila dutu yoyote kwa ujumla.d6
Biblia ina mambo gani ya kusema juu ya swali hilo? Miaka karibu 3,500 iliyopita, Biblia ilitaarifu kwa uwazi usio wa kawaida kwamba dunia inaning’inia “pasipo na kitu.” (Ayubu 26:7, BHN) Katika Kiebrania cha awali, neno litumiwalo hapa kwa “pasipo na kitu” (beli-mahʹ) humaanisha kihalisi “bila kitu.”7 Union Version ya Kiswahili hutumia maneno, “nafasi isiyo na kitu.”
Watu walio wengi katika siku hizo hawakuifikiria hata kidogo dunia kuwa sayari inayoning’inia katika “nafasi isiyo na kitu.” Hata hivyo, kimbele sana kuliko wakati wake, mwandikaji wa Biblia alirekodi taarifa iliyo thabiti kisayansi.
Biblia na Sayansi ya Kitiba—Je, Zaafikiana?
Sayansi ya kitiba ya kisasa imetufunza mengi juu ya kuenea na kuzuia kwa maradhi. Maendeleo ya kitiba katika karne ya 19 yaliongoza kwenye kuingizwa katika zoea la kitiba uzuiaji wa ukuzi au ongezeko la viini—usafi ili kupunguza maambukizo. Tokeo lilikuwa la kutazamisha. Kulikuwa na upunguo mkubwa katika maambukizo na vifo vya kabla ya wakati wavyo.
Hata hivyo, matabibu wa kale hawakuelewa kikamili jinsi maradhi huenea, wala hawakung’amua umaana wa usafi wa kutunza afya katika kuzuia magonjwa. Si ajabu sana kwamba mazoea yao mengi ya kitiba yangeonekana kuwa ya kikatili kulingana na viwango vya kisasa.
Mojawapo ya maandishi ya zamani zaidi ya kitiba yapatikanayo ni Mafunjo ya Ebers, mkusanyiko wa ujuzi wa kitiba wa Kimisri, wenye tarehe inayorudi nyuma kuanzia karibu mwaka wa 1550 K.W.K. Hatikunjo hiyo ina tiba 700 kwa maradhi mbalimbali “kuanzia umo la mamba hadi maumivu ya ukucha wa kidole cha mguu.”8 Kichapo The International Standard Bible Encyclopaedia chataarifu hivi: “Ujuzi wa kitiba wa matabibu hao ulikuwa wa kimajaribio tu, wa kimizungu sanasana na usio wa kisayansi hata kidogo.”9 Tiba zilizo nyingi zilikuwa hazina matokeo kabisa, lakini baadhi yazo zilikuwa za hatari sana. Ili kutibu jeraha, agizo moja la daktari lilidokeza kupaka mchanganyiko uliofanyizwa kwa kinyesi cha kibinadamu pamoja na dutu nyinginezo.10
Maandishi hayo ya matibabu ya Kimisri yaliandikwa karibu wakati uleule ambapo vitabu vya kwanza vya Biblia viliandikwa, vilivyotia ndani Sheria ya Kimusa. Musa, aliyezaliwa mwaka wa 1593 K.W.K., alikulia Misri. (Kutoka 2:1-10) Akiwa mshiriki wa nyumba ya Farao, “[ali]funzwa katika hekima yote ya Wamisri.” (Matendo 7:22) Aliwafahamu “waganga” wa Misri. (Mwanzo 50:1-3) Je, mazoea yao ya kitiba yasiyokuwa na matokeo au yaliyokuwa hatari yaliathiri maandishi yake?
La. Kinyume cha hilo, Sheria ya Kimusa ilitia ndani kanuni za usafi wa kutunza afya zilizokuwa za kimbele sana kuliko wakati wazo. Kwa kielelezo, sheria kuhusu kambi za kijeshi ilitaka kuzikwa kwa kinyesi mbali na kambi. (Kumbukumbu la Torati 23:13) Hilo lilikuwa hatua ya kimaendeleo sana ya kuzuia maradhi. Ilisaidia kuzuia maji yasichafuliwe na iliandaa kinga dhidi ya ugonjwa uitwao shigellosis uenezwao na mainzi na magonjwa mengine ya kuhara ambayo bado huua mamilioni ya watu kila mwaka katika nchi zilizo na hali mbaya zenye uchafu na takataka.
Sheria ya Kimusa ilikuwa na kanuni nyingine za usafi wa kutunza afya zilizokinga Israeli dhidi ya mweneo wa maradhi ya kuambukiza. Mtu aliyekuwa na maradhi ya kuambukiza au aliyeshukiwa kuwa nayo aliwekwa karantini. (Mambo ya Walawi 13:1-5) Mavazi au vyombo vilivyogusa mnyama aliyekuwa amekufa mwenyewe (labda kutokana na maradhi fulani) vilipasa ama kuoshwa kabla ya kutumiwa tena ama kuharibiwa. (Mambo ya Walawi 11:27, 28, 32, 33) Mtu yeyote aliyegusa maiti alionwa kuwa asiye safi na alihitaji kufuata utaratibu wa kusafishwa uliotia ndani kuosha mavazi yake na kuoga. Katika kile kipindi cha siku saba cha kutokuwa safi, alipaswa aepuke uhusiano wa kimwili na wengine.—Hesabu 19:1-13.
Sheria hiyo ya usafi wa kutunza afya inafunua hekima isiyokuwa ya matabibu wa mataifa ya jirani wakati huo. Maelfu ya miaka kabla ya sayansi ya kitiba kupata kujua juu ya njia ambazo maradhi huenea, Biblia iliagiza hatua zifaazo za kuzuia zikiwa kinga dhidi ya maradhi. Si ajabu kwamba, Musa aliweza kusema juu ya Waisraeli kwa ujumla katika siku yake kuwa wakiishi hadi umri wa miaka 70 au 80.e—Zaburi 90:10.
Huenda ukakiri kwamba taarifa za Kibiblia zilizotangulia ni sahihi kisayansi. Lakini kuna taarifa nyingine katika Biblia zisizoweza kuthibitishwa kisayansi. Je, hilo lamaanisha kwamba ni lazima iwe kwamba Biblia hupingana na sayansi?
Kukubali Yasiyothibitika
Taarifa isiyothibitika si lazima iwe isiyo ya kweli. Ithibati ya kisayansi inawekewa mipaka na uwezo wa binadamu wa kuvumbua uthibitisho wa kutosha na wa kufasiri habari kwa usahihi. Lakini kweli fulani hazithibitiki kwa sababu hakuna uthibitisho ambao umehifadhiwa, uthibitisho si dhahiri au haujavumbuliwa, au uwezo na ustadi wa kisayansi hautoshi ili kufikia mkataa usiokanushika. Je, huenda hali ikawa hivyo kwa habari ya taarifa fulani za Kibiblia ambazo hazina uthibitisho wa kiasili wenye kujitegemea?
Kwa kielelezo, marejezeo ya Biblia kwenye makao yasiyoonekana yanayokaliwa na watu wa roho hayawezi kuthibitishwa—au kukanushwa—kisayansi. Hilohilo laweza kusemwa juu ya matukio ya kimuujiza yanayotajwa katika Biblia. Hakuna uthibitisho dhahiri wa kijiolojia wa kutosha unaopatikana kuridhisha watu fulani juu ya Furiko la tufeni pote la siku ya Noa. (Mwanzo, sura ya 7) Je, lazima tufikie mkataa wa kwamba hilo halikutukia? Matukio ya kihistoria yaweza kufanywa yasiwe dhahiri kwa sababu ya kupita kwa wakati na kubadilika kwa mambo. Kwa hiyo, je, haiwezekani kwamba maelfu ya miaka ya utendaji wa kijiolojia imefuta uthibitisho mwingi wa kuwako kwa Furiko?
Kweli, Biblia ina taarifa zisizoweza kuthibitishwa au kukanushwa na uthibitisho wa kiasili unaopatikana. Lakini je, hilo litushangaze? Biblia si kitabu cha mafundisho ya sayansi. Hata hivyo, hiyo ni kitabu chenye kweli. Tayari tumechunguza uthibitisho wenye nguvu wa kwamba waandikaji wayo walikuwa wanaume wenye uaminifu-maadili na wenye kufuatia haki. Na wanapotaja mambo kuhusiana na sayansi, maneno yao ni sahihi na hayatii ndani kabisa “nadharia” za kale za kisayansi ambazo baadaye zilithibitika kuwa ngano tu. Hivyo sayansi si adui wa Biblia. Kuna sababu za kutosha za kupima yale ambayo Biblia husema ukiwa tayari kupokea mawazo mapya.
[Maelezo ya Chini]
a “Antipodi . . . ni mahali pawili panapokabiliana barabara tufeni. Mstari wenye kunyooka kati ya mahali hapo pawili hupitia katikati ya dunia. Neno la Kiingereza antipodes lamaanisha wayo kwa wayo katika Kigiriki. Watu wawili wanaosimama kwenye antipodi wangekuwa karibu zaidi kwenye nyayo za miguu yao.”1—The World Book Encyclopedia.
b Kulingana na maana hususa, dunia ni tufe lililo na sehemu tambarare kidogo kwenye ncha zalo.
c Kwa kuongezea, ni kitu kilicho tufe tu ndicho kionekanacho kuwa duara kutoka kila upande kinakoonwa. Diski bapa ingeonekana mara nyingi zaidi ikiwa umbo yai, si duara.
d Maoni ya watu wengi katika siku ya Newton yalikuwa kwamba ulimwengu wote mzima ulikuwa umejaa kiowevu—“mchuzi” wa kilimwengu —na kwamba mizunguko ya maji katika kiowevu hicho ilifanya sayari zizunguke.
e Mwaka wa 1900, urefu wa uhai katika nchi nyingi za Ulaya na katika Marekani ulitarajiwa kuwa usiozidi miaka 50. Tangu wakati huo, urefu huo umeongezeka kwa njia ya kutazamisha si kwa sababu tu ya maendeleo ya kitiba katika kudhibiti maradhi bali pia kwa sababu ya usafi wa kutunza afya na hali nzuri zaidi za maisha.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Taarifa isiyothibitika si lazima iwe isiyo ya kweli
[Picha katika ukurasa wa 18]
Maelfu ya miaka kabla ya wanadamu kuiona dunia ikiwa tufe kutoka angani, Biblia ilirejezea “duara ya dunia”
[Picha katika ukurasa wa 20]
Sir Isaac Newton alifafanua kwamba sayari zinashikiliwa katika mizingo yazo na nguvu za uvutano