Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 4/15 kur. 177-182
  • Ulimwengu Mmoja, Serikali Moja, Chini ya Enzi Kuu ya Mungu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulimwengu Mmoja, Serikali Moja, Chini ya Enzi Kuu ya Mungu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • LINALOKOSEKANA JUU YA USHIRIKIANO WA MATAIFA YOTE
  • TUTAAMULIA ENZI KUU YA NANI?
  • Serikali Moja Ile ya Ulimwengu Mmoja Chini ya Enzi Kuu ya Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Wakati wa Kumchagua Mungu Awe Mwenye Enzi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Enzi Kuu
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Uzuri wa Enzi Kuu ya Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 4/15 kur. 177-182

Ulimwengu Mmoja, Serikali Moja, Chini ya Enzi Kuu ya Mungu

1. Enzi inafafanuliwa kuwa nini, nayo imekuwa na matokeo gani juu ya dunia yetu?

KWA KARNE nyingi imeonyeshwa kwamba enzi ya serikali inategemea hasa watu wanaotawaliwa.a Wataalamu wa siasa wanaisema enzi kuwa “uwezo mkuu zaidi katika Serikali ambao kupitia kwake serikali inasimamiwa.”b Katika nyakati za karibuni nchi zaidi na zaidi zimeshikilia maoni ya kwamba enzi inakaa na watu.c Walakini, katika nchi nyingine bado inatambuliwa kwamba uwezo ulio mkuu zaidi katika Serikali ni wa mwenye enzi, kama vile mfalme. Lo lote liwalo leo hakuna mwanadamu mmoja wala kikundi kimoja cha kitaifa kinachotumia enzi dunia yote. Bali, dunia yetu ina enzi nyingi. Hiyo ni sababu kubwa ya kuwako magomvi na mapigano. Dunia haina utulivu, haina amani ya ulimwengu wote.

2. Kwa sababu gani sote tunapatwa na matokeo ya enzi za kitaifa duniani pote, na wengine wanakuwa na maoni gani ya kizalendo juu ya serikali yao ya kitaifa?

2 Sote tunapatwa na matokeo ya enzi zinazotumiwa duniani pote. Ni wachache kati yetu tunaoweza kuitwa “mtu asiye na nchi.” Walio wengi kati yetu ni wana wa taifa fulani, raia za nchi fulani. Tukiwa hivyo, tunatazamiwa kuwa na kiburi cha kitaifa. Tunafanywa tufikirie sana taifa letu, hata tunaona uchungu na kukasirika wakati wo wote taifa tunalowakilisha linapoaibishwa. Katika majadiliano kati ya mataifa wafuasi wengi wa serikali ya kitaifa wanafuata maoni ya kizalendo yanayotajwa kwa maneno haya, “Iwe na haki au isiwe​—ni nchi yangu!”

3. Mataifa leo yanatumia enzi gani ya ndani na enzi gani ya nje?

3 Leo mataifa zaidi katika historia ya kibinadamu yanaamuru zaidi raia zao wawe waaminifu kwao kuliko wakati mwingine wo wote uliotangulia. Sasa kuna mataifa wanachama 138 ya siasa za namna mbalimbali katika baraza ya ulimwengu inayoitwa Umoja wa Mataifa. Yako mataifa mengine yaliyoko nje ya tengenezo la Umoja wa Mataifa. Kila moja la mataifa hayo lina wivu juu ya enzi yake ya ndani na enzi yake ya nje, liwe ndani au nje ya Umoja wa Mataifa. Kila taifa linadai na kulinda mamlaka hizo za kiserikali ambazo Serikali ya kisiasa inazo kwa ndani juu ya raia zake wenyewe na hata juu ya wageni wanaokaa ndani ya mipaka ya kitaifa na juu ya raia zake walio katika nchi za kigeni. Linapotumia enzi yake ya nje, kila taifa linasisitiza juu ya haki yake na kuitumia haki hiyo kuingia katika uhusiano na serikali yo yote ya kigeni ya kisiasa, kwa kufanya mkataba wa amani au kwa kutangaza vita. Kulingana na maoni ya kisasa ya kibinadamu, hayo yote yanaelekea kuwa ya haki na asili. Uzalendo huo!

4. Wakati wa karne hii, ni maelekeo gani ya kisiasa yameongezeka sana, na ni ulizo gani linalotokezwa juu ya undugu kati ya mataifa na watu mmoja mmoja?

4 Mambo ya hakika ya historia ya kisasa yaonyesha kwamba utukuzo wa taifa umekuwa maarufu katika karne hii ya 20, tangu vita ya kwanza iliyopiganwa katika dunia yote. Kulingana na upande wenye kushinda, ilifanywa ili kuusalimisha ulimwengu kwa demokrasi. Kushindania kwa watu kila mahali enzi za kitaifa kwa kufanyizwa kwa serikali mpya za kisiasa kulienea mahali pote. Utukuzo wa taifa ukawa pigo kwa wanadamu wote. Badala ya kutuliza hali za ulimwengu kwa kuridhisha watu wa mahali wanaotaka utaifa, uliongeza matatizo ya kitaifa na ya mataifa yote. Baada ya miaka kumi na tisa ya kutenda kwa Ushirika wa Mataifa ambao sasa hautendi, kisha miaka 30 ya kutenda kwa Umoja wa Mataifa, leo hakuna undugu wa mataifa, kama vile hakuna “undugu wa wanadamu.” Ingawaje, je! wanadamu wote si ndugu wa jamaa moja? Je! mataifa yote si ndugu, yenye raia ambao ni ndugu wa jamaa moja? Mbona, basi, kuna ukosefu huu ulimwenguni pote wa undugu unaopaswa ufanye wanadamu wote kila mahali watende kama ndugu wenye upendo wa jamaa kubwa moja ya kibinadamu?

5. Je! duniani tunao “ulimwengu mmoja” ukiwa chini ya “serikali moja,” nalo hilo lingekuwa jambo lenye kutamanika sana kwa nani?

5 Ni lazima tukubali kwamba wanadamu leo si “ulimwengu mmoja” na kwamba, ijapokuwa kuna Umoja wa Mataifa, hawako chini ya “serikali moja.” Je! tungependa wanadamu wote wanaoishi wawe “ulimwengu mmoja” wakiwa chini ya “serikali moja”? Kulingana na mambo ambayo yamewapata wanadamu kwa miaka elfu sita iliyopita, hilo lingekuwa jambo lenye kutamanika sana kwa wale wote kati yetu tunaotamani upatano, amani, haki usalama, undugu na furaha ya kuishi.

6, 7. (a) Kwa sababu gani hakuna wakati wo wote zamani ambapo watu wa dunia walikaribiana sana na kutegemeana kama sasa? (b) Ni wangapi wangepatwa na matokeo ya vita ya ulimwengu nyingine ikitokea, na kwa sababu gani?

6 Sisi sote, bila kujali mahali tunapoishi katika sayari hii, tu watu wa kuishi hapa duniani. Ni kweli kwamba miruko sita ya angani imewatusha wanadamu mwezini, lakini ili kuishi, imewapasa wanadamu hawa warudi kwenye dunia hii. Wamefurahia kurudi kwenye dunia hii. Hapa ndipo walipokusudiwa waishi, na ni hapa peke yake ndipo viumbe vya kibinadamu vyaweza kuishi milele kama wanadamu. Po pote wawezapo kuishi katika sayari hii, wanadamu ni jirani za mmoja na mwenzake, maana wote ni wakazi wa dunia moja. Wote wana haja zile zile za maisha. Na sasa njia za kuwasiliana upesi kwa njia ya simu ya mdomo, simu ya barua, redio na televisheni, na njia za namna nyingi za kusafiri katika nchi kavu, baharini na angani, zimewaleta watu wote karibu zaidi kuliko zamani. Hakuna wakati wo wote zamani ambapo watu wa dunia walitegemeana kama sasa.

7 Kama katika jamaa kubwa moja ya kibinadamu, kila sehemu nyingine ya jamii ya kibinadamu inapatwa na yanayotukia kwa sehemu moja ya jamaa ya kibinadamu. Usoni mwa maendeleo katika sayansi ya vita vya kisasa, vita nyingine ya ulimwengu, vita yenye kutumia silaha za atomiki zilizo na fataki ziwezazo kupigwa kutoka bara moja mpaka bara nyingine, ingeleta msiba juu ya viumbe vyote, wanadamu na wanyama, katika dunia yetu.

8, 9. (a) Ni hatari gani inayowapata wanadamu wote, na ni nini linalohitajiwa kwa upande wa mataifa ili kuzuia, mabaya zaidi? (b) Ni onyo gani la msiba mkuu lililotolewa Mashariki ya Mbali Januari uliopita, nalo lilihitaji nani washirikiane?

8 Hatari ya kufa inawapata sasa wanadamu wote. Sasa inakubaliwa kwamba kunahitajiwa wanadamu wote wajitahidi pamoja kuzuia msiba huo wa ulimwengu. Ili watu wapate faida kamili lazima jambo hilo lifanywe. Lakini kweli uhitaji mkubwa wa kushirikiana pamoja ili kuzuia msiba unaonekana na watu wenye kujipendeza leo? Mwito wa kufanya hivyo watoka Mashariki ya Mbali:

9 Chini ya vichwa “Miki: Bila Ushirikiano Wanadamu Watapata Msiba Mkuu,” gazeti Times la Singapore, Asia, la tarehe ya Januari 26, 1975, latoa taarifa hivi: “TOKYO, Jumamosi.​—Waziri mkuu Takei Miki alionya jana kwamba ikiwa faida moja moja za kitaifa zatimizwa ‘katika njia ya kutofikiria matokeo ya baadaye,’ ulimwengu utapata msiba mkuu. Bw. Miki akasema katika hotuba kuu iliyotolewa katika Diet (bunge): ‘Ulimwengu unaendelea kuwa mdogo zaidi na zaidi na wanadamu wote wanashiriki msiba ule ule katika hali moja.’ Alikazia uhitaji wa ushirikiano wa mataifa yote na utegemeano miongoni mwa mataifa. . . . ‘Walakini, linalotusikitisha ni kwamba ulimwengu haujafikia hatua ya kutimizwa kabisa kwa utegemeano huu. Ikiwa hali hii yaendelea, ni wazi kwamba tutapata msiba mkuu karibuni sana. Katika kizazi hiki, hakuna taifa moja au mtu mmoja anayeweza tena kuendelea kufaulu akiwa peke yake. Bila shaka, lengo peke yake la usuluhishi wa wa nchi yo yote ni kusalimisha faida zake za kitaifa. Walakini, usemi huu usifahamike kuwa unamaanisha kutofikiria matokeo ya baadaye.’”

LINALOKOSEKANA JUU YA USHIRIKIANO WA MATAIFA YOTE

10. Ni nini kingeharibu nguvu yenye kuunganisha ya ushirikiano wa mataifa yote uliopendekezwa?

10 Kweli hili lilikuwa onyo zito alilotoa waziri mkuu wa Japan. Anaendelea kusadiki kwa nguvu kwamba ni lazima sasa wanadamu wachague kati ya ushirikiano kamili wa mataifa yote na msiba mkuu! Walakini, katika maoni yake enzi ya kitaifa ya kila serikali ya kisiasa haipaswi iachwe, hata ingawa ushirikiano huu unafikiwa. Kwa hiyo, “lengo peke yake la usuluhishi” lapaswa liwe lile la kusalimisha faida za kitaifa za kila nchi. Katika njia hii kila mahali mataifa yangekuwa yakishikimana na enzi yao ya kitaifa. Hii ingeruhusu kidumu kiburi cha kitaifa pamoja na matokeo yake yote yenye kugawanya. Hivyo hii ingezuia umoja wa kweli wa ndani kati ya mataifa. Ungekuwa udhaifu unaoharibu nguvu ya ushirikiano wa mataifa yote. Matokeo hayangekuwa “serikali moja” kamwe! Wala hayangekuwa “taifa moja”!

11. Ni jambo gani lililo bora sana ambalo lingekuwa limekosekana katika ushirikiano huo wa mataifa yote?

11 Hivyo, basi, je! linalohitajiwa ili kuuokoa ulimwengu wa wanadamu na msiba mkuu ni ushirikiano tu kati ya serikali zenye enzi ya kisiasa? Kwa wazi jambo fulani zaidi lahitajiwa, jambo ambalo ni bora sana. Ushirika wa Mataifa ambao sasa umekufa haukutoa uhitaji huo. Hata Umoja wa Mataifa unaotenda sasa hauutoi. Labda wataalamu wa siasa wa ulimwengu watauliza hivi, Ni jambo gani linalohitajiwa, linalokosekana kwa matengenezo hayo ya ushirikiano wa mataifa yote? Twajibu, Ni ushirikiano usio wa choyo pamoja na Yeye ambaye mataifa mengi hujidai kuabudu. Twaweza kumjua Huyo kutokana na wimbo uliokuwa ukitumiwa kama wimbo wa taifa katika nchi moja ya Amerika ya Kaskazini. Unaitwa “Nchi Yangu, Nchi Yako,” au, “Amerika.” Fungu la mwisho la wimbo huu, ambalo lilipokuwa linaimbwa watu walisimama husomwa hivi: (Likitafsiriwa kutoka Kiingereza)

“Mungu wa baba zetu,

Chanzo cha uhuru, twakuimbia Wewe.

Nchi yetu iangaze daima nuru takatifu ya uhuru.

Utulinde kwa uweza Wako,

Mungu Mkuu Mfalme wetu.”

12. (a) Ni kwa njia gani taifa fulani linadai kwamba Mungu ndiye Mwenye Enzi wao wa kimbinguni? (b) Taifa hilo lenye kuimba linahakikishaje kama Mungu ndiye au siye Mwenye Enzi wao?

12 Tena, wimbo huu wa taifa uliimbwa kwa sauti ya wimbo wa taifa wa Waingereza, unaoitwa “Mungu Mwokoe Mfalme (Malkia) Wetu Mtukufu” (“God Save Our Gracious King [Queen]”). Kupatana na fungu hilo la mwisho la wimbo wa “Amerika,” Mahakma Kuu ya taifa imeamua kwamba United States ni taifa la Kikristo. Pia, katika Uingereza kungali kuna mwungano wa Kanisa na Serikali, Kanisa la Uingereza likiwa Kanisa la Serikali lililokubaliwa. Mungu wa Biblia Takatifu ndiye mungu anayemaanishwa hapa. Mataifa yote ya Jumuiya ya Wakristo wanajidai kumwabudu Mungu huyu wa Maandiko Matakatifu. Kwa kumwimbia maneno haya “Mungu Mkuu Mfalme wetu,” Waamerika wanaoweza kushiriki wimbo huo wa kizalendo wanamkiri Mungu kwa umoja, “Mungu wa baba zetu,” kama mwenye enzi kuu, ambaye ni mkuu zaidi kuliko mtekelezaji mkuu wa United States ya Amerika. Lakini je! waimbaji wa wimbo wa taifa husema zaidi kuliko wanavyomaanisha? Je! kweli wanamwacha awe Mwenye Enzi Kuu wa taifa lao wenyewe na pia sehemu nyingine ya ulimwengu wote? Kwa kushirikiana naye kwa unyenyekevu au kushindwa kufanya hivyo, waimbaji wanaonyesha kama Yeye ndiye au siye Mwenye Enzi Kuu wao wa kweli.

13. (a) Biblia ya King James Authorized Version inamwonyesha nani kuwa ndiye Mwenzi Enzi kuu wa Ulimwengu Wote? (b) Kwa hiyo, ni kwa njia gani peke yake unavyoweza kutokea “ulimwengu mmoja” ukiwa chini ya “serikali moja”?

13 Tafsiri ya Biblia Takatifu katika Kiingereza iliyoruhusiwa na Mfalme James I wa Uingereza katika mwaka wa 1611 ipate kusomwa katika makanisa ya nchi hiyo inaelekeza kwenye enzi kuu ya Mungu huyu. Katika Zaburi 83:18 inasomwa hivi: “Wanadamu wapate kujua kwamba wewe, ambaye jina lako peke yako ni YEHOVA, ndiwe wa juu juu zaidi ya dunia yote.” Katika utimizo wa sala hiyo iliyo katika Zaburi, watu wote, wakaaji wote wa kibinadamu wa dunia, bado watajua kwamba Mungu ambaye jina lake ni Yehova ndiye Mwenye Enzi Kuu Zaidi kuliko wote na, hivyo, Mwenye Enzi Kuu juu ya dunia yetu pia. Leo idadi kubwa zaidi ya mataifa ya kisiasa hawamwabudu Yehova kama Mungu wao, kama mataifa ya Jumuiya ya Wakristo wanavyojidai kufanya. Lakini, ijapokuwa mataifa yaitwayo “ya Kikristo” hujidai kumwabudu Mungu ambaye jina lake Biblia husema ni Yehova, kwa kweli hawashirikiani na Yeye. Hivyo, kwa hakika, hakuna mojawapo la mataifa ambayo ni wanachama wa tengenezo la Umoja wa Mataifa linaloshirikiana na Mungu Yehova, Aliye Juu Zaidi. “Ulimwengu mmoja” chini ya “serikali moja” waweza kutokea wanadamu wote wanaoishi wakishirikiana kwa utii na Mwenye Enzi Kuu tu wa Ulimwengu Wote.

TUTAAMULIA ENZI KUU YA NANI?

14. Kwa sababu gani sasa ni lazima kila mmoja wetu ajifanyie uamuzi juu ya ulizo ambalo lazima liamuliwe kwa ajili ya dunia yote?

14 Je! hilo ndilo jambo tunalotaka kwa mioyo yetu yote? Kwa kuwa serikali za kisiasa hazitaki jambo hilo lifanywe kwa njia ya Mungu na kwa kuwa wanakataa kushirikiana na Yeye, basi ni juu ya kila mmoja wetu kujiamulia mwenyewe juu ya ulizo ambalo lazima karibuni lijibiwe kwa ajili ya dunia yote. Je! kila mmoja tutaiheshimu enzi kuu ya Yehova ya ulimwengu wote na kuishi kupatana nayo? Ni kwa kufanya hivyo tu tutakavyofurahia “ulimwengu mmoja, serikali moja, chini ya enzi kuu ya Mungu.”

15. Ni nini iliyo sababu ya kushindwa kwa mipango ya mataifa ujapokuwapo ushirikiano wa mataifa yote?

15 Sote tunaposhirikiana na kutenda kama jamii moja, kwa kawaida twaweza kutimiza mambo. Tunapofanya kazi pamoja na Bwana Mungu Yehova Mwenye Enzi Kuu, twaweza kuwa na hakika ya kufaulu. Uhakika huu watusaidia tufahamu kwa nini mataifa hawakufaulu katika mipango yao ya mataifa yote. Ni kweli kwamba katika hali mbaya yao leo, mataifa wanajaribu kuunganisha ulimwengu chini ya mpango mmoja wa ulimwengu. Kwani, hata wanasema juu ya kulikabidhi tengenezo la Umoja wa Mataifa enzi kuu ya ulimwengu. Walakini, je! “ulimwengu mmoja” wa wanadamu chini ya “serikali moja” ambao mataifa wangependa kutokeza kwa ajili ya amani na usalama wa ulimwengu ndio “ulimwengu mmoja” chini ya “serikali moja” ambao Bwana Mungu Mwenye Enzi Kuu anafikiria? Je! ndio Yeye ametabiri katika Neno lake lisilokosa, Biblia Takatifu?

16, 17. (a) Mataifa yalishirikianaje kwa njia mbaya karne kumi na tisa zilizopita katika Yerusalemu? (b) Waliosali na kuutaja ushirikiano huo mbaya walimwita Mungu nani, nao walimwomba afanye nini?

16 Twajua kwamba viumbe vya kibinadamu na mataifa vyaweza kushirikiana katika kazi mbaya na pia katika kazi njema. Punde kuliko miaka elfu mbili iliyopita mataifa yaliungana pamoja kufanya kazi mbaya. Walishirikiana pamoja, lakini si kwa kushirikiana na Mungu wa mbinguni Aliye Juu Zaidi. Jambo hili lilitukia kwa sherehe sana katika mji wa Yerusalemu, wakati wanaume wawili walipokuwa wamekwisha kukamatwa kwa sababu ya kuhubiri katika hekalu la mji, wakawa wamekwisha kuhukumiwa na Mahakma Kuu na kufunguliwa kwa vitisho. Kwa habari ya kupingana kwa enzi zilizohusika wakati huo, masimulizi ya kihistoria yatuambia hivi, katika maneno yafuatayo, kulingana na The New English Bible:

17 “Mara walipofunguliwa wakawarudia rafiki zao na kuwaambia kila jambo ambalo makuhani wakuu na wazee walikuwa wamesema. Waliposikia juu yake, wakainua sauti zao kama mtu mmoja wakamwomba Mungu: ‘Bwana Mwenye Enzi Kuu, mfanya mbingu na dunia na bahari na kila kitu ndani yavyo, wewe ambaye Kwa Roho Takatifu, kupitia kwa kinywa cha Daudi mtumishi wako, ulisema, “Kwa nini Mataifa walikasirika na watu wakatunga hila zao bure? Wafalme wa dunia walijipanga na watawala wakashauriana pamoja juu ya Bwana na juu ya Masihi wake.” Kweli walishauriana pamoja katika mji wenyewe huu juu ya mtumishi wako mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta kama Masihi. Herode na Pontio Pilato walifanya shauri baya pamoja na Mataifa na watu wa Israeli ili wafanye mambo yote yaliyotangulia kuagizwa kwa mkono wako na kwa amri yako. Na sasa, Ee Bwana, angalia vitisho vyao, uwezeshe watumishi wako kusema neno lako kwa ujasiri wote.’”​—Matendo 4:23-29; pia The New American Bible; Revised Standard Version; Moffatt; NW.

18. Wakristo hao wenye kusali walimwomba Mungu awasaidie kufanya nini, na matokeo ya kujibiwa sala yao yalikuwa nini?

18 Wanafunzi hao wa Yesu Masihi walijifanyia wenyewe maamuzi wakajipanga upande wa enzi kuu ya ulimwengu wote ya Muumba wa mbingu na dunia. Ndiyo sababu walisali Kwake awasaidie wasijali amri na vitisho vya Mahakma Kuu ya kitaifa na kuendelea tu na kazi iliyokatazwa ya kuhubiri ujumbe wa Mungu juu ya Mtumishi wake aliyetiwa mafuta, Yesu Masihi. Walifunua shauri baya la kisiasa la Mfalme Herode Antipa, aliyewakilisha taifa la Waidumia, na Gavana Pontio Pilato, aliyewakilisha Milki ya Kirumi na Tiberio Kaisari, na Wayahudi wasiofanywa kuwa Wakristo. Sala yao ilijibiwa, na kazi ya kuhubiriwa kwa habari njema na wategemezaji hawa wa enzi kuu ya Bwana Mungu Yehova ikaendelea, miongoni mwa Wayahudi na, baadaye, miongoni mwa Mataifa pia. Kwa sababu hiyo, maelfu ya wenye kuamini walijipanga upande wa Yehova Bwana Mwenzi Enzi Kuu, washirikiane naye katika kusudi lake la Kimasihi.

19. Tofauti na hali iliyokuwako karne kumi na tisa zilizopita, sisi leo tumefikia utimizo gani wa maneno ya Daudi yaliyomo katika Zaburi ya Pili, na kwa sababu gani imetupasa tuwe waangalifu juu ya uamuzi tutakaofanya?

19 Leo tumeufikia upeo katika mwendo huu wa matukio ulioongozwa na Mungu unaoelekeza kwenye “ulimwengu mmoja” chini ya “serikali moja” ambao Mungu ndiye Mwenzi Enzi Kuu wa Ulimwengu Wote juu yake. Maneno ya unabii ya Daudi yaliyotiwa katika sala iliyotolewa na wanafunzi wa Masihi karne kumi na tisa zilizopita katika Yerusalemu yalikuwa na utimizo wa kwanza au mdogo tu. Ilikuwa imemtia ndani Mfalme Herode na Gavana Pontio Pilato na Wayahudi na askari wa Kirumi ambao hawa walitumia kumpigilia misumari Yesu Masihi kwenye mti wa mateso. Katika karne yetu ya 20, matukio ya ulimwengu tangu kutokea Vita ya Ulimwengu ya Kwanza katika mwaka wa 1914 yanatoa uthibitisho wa kwamba tumeufikia utimizo wa mwisho na ulio mkubwa wa maneno hayo ya Daudi yanayopatikana katika zaburi ya pili. Sasa, kuliko wakati wo wote zamani, ulizo lile la enzi kuu ya kimungu li karibu kujibiwa. Uamuzi wetu kila mtu peke yake juu ya ulizo hilo utakuwa na matokeo mazito sana juu yake.

20, 21. (a) Ili tupate uongozi wa kufanya uamuzi unaofaa tunaweza kumwendea nani hata tufaulu? (b) Kulingana na Zaburi 73:24, 25, 28, mtunga zaburi alimgeukia nani apate mashauri?

20 Ili kutusaidia tufanye uamuzi utakaotufanya tufurahie “ulimwengu mmoja, serikali moja,” chini ya enzi kuu ya kimungu, twahitaji uongozi. Je! twaweza kuyaendea mataifa ya ulimwengu tupate uongozi katika hili? La, kwa maana wameduwaa, wanazidi kufadhaika kwa sababu hawajui njia ya kutokea katika matatizo yao yanayoongezeka. Hatuwezi kufaulu ikiwa tunaviendea vyama vya kidini vya mataifa, kwa maana shauri la kidini ambalo vyama hivi vimewapa watawala wa kisiasa limepoteza mataifa yote. Ili tupate shauri la kisasa, la kweli, lenye kufaa, linalohitajiwa na linalotuongoza katika njia ya kweli, lazima tuliendee Neno lililoandikwa ambalo tumepewa na Yule aliyetabiri zamani taabu hii ya ulimwengu. Huu ndio mwendo wenye hekima uliochukuliwa na mtunga Zaburi wa nyakati za kale. Akimwambia Mtungaji wa kimungu wa Neno hilo la unabii, mtunga zaburi alisema hivi:

21 “Utaniongoza kwa shauri lako, na baadaye hata unitukuze. Nina nani katika mbingu? Na zaidi yako sina furaha nyingine duniani. Lakini mimi, kumkaribia Mungu ni kuzuri kwangu. Katika Yehova Bwana Mwenye Enzi Kuu ndimo nimeweka kimbilio langu, nipate kuzitangaza kazi zako zote.”​—Zab. 73:24, 25, 28, NW.

22. Kwa hiyo, tunaweza kuwa na hakika juu ya nini, kulingana na maneno ya mtunga zaburi?

22 Kwa kumchagua sasa Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote awe kimbilio letu, sisi, pia, twaweza kuwa na hakika kwamba atatuongoza kwa shauri lake na baadaye kutuletea utukufu usiofifia.

[Maelezo ya Chini]

a Tangazo la Kiamerika la Uhuru, lililoazimiwa na Continental Congress katika Philadelphia, Pennsylvania, Julai 4, 1776, lilisema hivi katika fungu lake la pili: “ . . . Kwamba ili kujipatia haki hizi, serikali zinaanzishwa miongoni mwa watu, zikipata mamlaka zao za haki kwa kuruhusiwa na watawaliwa.”

b Tazama Encyclopedia Americana, Volume ya 25, ukurasa 317, chapa ya mwaka wa 1959.

c Tangu kumalizika kwa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza Novemba 11, 1918, jamhuri mpya na serikali za kidemokrasi zimeanzishwa, kufikia zaidi ya 60 wakati wa kuandikwa kwa gazeti hili.

[Blabu katika ukurasa wa 178]

‘Mbona kuna ukosefu ulimwenguni pote wa undugu unaopaswa kufanya wanadamu wote kila mahali watende kama ndugu wenye upendo wa jamaa moja kubwa ya kibinadamu?’

[Blabu katika ukurasa wa 179]

‘Linalokosekana ni ushirikiano usio wa kichoyo pamoja na Mungu wa Biblia Takatifu, Yehova, Mwenye Enzi Kuu wa Ulimwengu Wote.’

[Blabu katika ukurasa wa 181]

‘Sasa, kuliko wakati wo wote zamani, ulizo lile la enzi kuu ya kimungu li karibu kujibiwa. Lazima ujifanyie uamuzi wa kipekee juu ya ulizo hilo.’

[Picha katika ukurasa wa 177]

“Naye BWANA atakuwa Mfalme juu ya nchi yote.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki