Maisha na Huduma ya Yesu
Kufanya Kazi Njema Siku ya Sabato
NI MASIKA ya mwaka 31 W.K. Miezi michache imepita tangu Yesu aliposema na mwanamke kwenye kisima katika Samaria akiwa njiani kutoka Yudea kwenda Galilaya.
Sasa, baada ya kufundisha sana katika sehemu zote za Galilaya, Yesu anaondoka tena kuelekea Yudea, ambako anahubiri katika masinagogi. Kwa kulinganisha na vile watu walivyomsikiliza katika huduma yake Galilaya, Biblia haituambii mengi juu ya utendaji wa Yesu katika Yudea wakati wa ziara hii na wakati wa miezi aliyotumia hapa baada ya sikukuu ya Kupitwa iliyopita. Ni wazi kwamba huduma yake haikupokewa vizuri katika Yudea kama ilivyokuwa katika Galilaya.
Baada ya muda mfupi Yesu anaelekea kwenye mji mkuu wa Yudea, Yerusalemu, kwa ajili ya sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 31 W.K. Hapa, karibu na lango la kondoo la mji huu, ndipo kilipo kile kidimbwi kinachoitwa Bethzatha, ambapo wagonjwa wengi, vipofu, na viwete wanakuja. Wao wanaamini kwamba watu wanaweza kuponywa kwa kuingia ndani ya maji ya kidimbwi wakati yanapokorogwa.
Ni siku ya sabato, naye Yesu anaona mtu mmoja kwenye kidimbwi ambaye amekuwa mgonjwa kwa miaka 38. Kwa kujua kwamba mtu huyo amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu, Yesu anauliza: “Wataka kuwa mzima?”
“Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa,” anajibu, “ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.”
Yesu anamwambia: “Simama, jitwike godoro lako uende.” Hapo mtu yule anakuwa na afya nzuri mara hiyo, anachukua godoro lake, na kuanza kutembea!
Lakini Wayahudi wanapomwona mtu yule, wanasema: “Leo ni sabato, wala si halali kwa kujitwika godoro.”
Mtu yule anajibu: “Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende.”
“Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani?” wanauliza. Yesu alikuwa amegeukia kando kwa sababu ya makutano ya watu, na kwa hiyo mwenye kuponya hakujua jina la Yesu. Lakini, baadaye Yesu na mtu yule wanakutana hekaluni, naye mtu yule anamjua yeye aliyemponya.
Kwa hiyo mtu huyo aliyeponywa anawatafuta Wayahudi kuwaambia kwamba Yesu ndiye amemfanya awe na afya nzuri. Wanapojua hivyo, Wayahudi wanamwendea Yesu. Kwa sababu gani? Je! ni kujifunza njia anayotumia kufanya ajabu hizo? Hapana. Bali ni kumtafuta makosa kwa sababu yeye anafanya mema siku ya sabato. Na hata wanaanza kumtesa! Luka 4:44; Yohana 5:1-16.
◆ Ni karibu muda gani umepita tangu Yesu alipozuru Yudea mara ya mwisho?
◆ Kwa sababu gani kidimbwi cha Bethzatha kilikuwa kikiendewa na watu wengi?
◆ Ni muujiza gani ambao Yesu alifanya kwenye kidimbwi hicho, na Wayahudi wakawa na maoni gani?