Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w91 7/1 kur. 3-4
  • Kutoka Kuwa Mama Dunia Hadi Kuwa Miungu-Wake wa Uzazi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutoka Kuwa Mama Dunia Hadi Kuwa Miungu-Wake wa Uzazi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kiolezo cha Kibabuloni
  • Ibada ya Mama Mungu-Mke Yaenea
  • Je! Ibada ya Mama-Mungu-Mke I Hai Bado?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Nyuzi Zile Zile Katika Ngano
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Je, Maria Ni Mama ya Mungu?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Mambo Hakika ya Krismasi, Ista, na Halowini
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
w91 7/1 kur. 3-4

Kutoka Kuwa Mama Dunia Hadi Kuwa Miungu-Wake wa Uzazi

JE! UNATAMBUA mungu-mke aliye kwenye picha ya jalada la gazeti hili? Ni Isisi, mama-mungu-mke wa kale wa Misri. Ikiwa umezuru jumba la kuhifadhi au ukachungulia kitabu juu ya historia ya kale, labda umekwisha ona sanamu hiyo au moja kama hiyo. Hata hivyo fikiria hili: Je! ungeinamia na kuabudu mungu-mke Isisi?

Kama wewe ni mshiriki wa moja ya dini za Jumuiya ya Wakristo, hilo huenda likaonekana kuwa swali la kushangaza. Yaelekea utasisitiza kwamba wewe huwa unaabudu Muumba, Yule anayeelekezewa maneno, “Baba yetu uliye mbinguni.” (Mathayo 6:9) Wazo la kuinamia mama-mungu-mke huenda likaonekana kuwa la ajabu, hata lenye kuchukiza. Hata hivyo, ibada hiyo imeenea sana katika historia, na huenda ukagutuka kwa kujua ni nani hasa ambao huabudu mama-mungu-mke mkuu leo.

Hata hivyo, kabla ya kuzungumzia jambo hilo, acheni tupate habari ya mandhari-nyuma kwa kuchunguza kadiri ya mweneo wa ibada ya mama-mungu-mke katika nyakati za kale. Aina hiyo ya ibada yaonekana ilikuwa namna ya mapema sana ya dini bandia. Visanamu na mifano ya akina mama miungu-wake walio uchi vimefukuliwa na wanaakiolojia kwenye mahali mbalimbali pa kale kotekote Ulaya na kutoka mabara ya Mediterrania hadi India.

Mama Dunia alionwa kuwa chanzo cha daima cha aina zote za uhai, aliyetoa uhai na kisha kuuchuka tena kwake mwenyewe wakati wa kifo chazo. Kwa hiyo, aliabudiwa lakini pia kuhofiwa. Mwanzoni, iliaminiwa kwamba, nguvu zake za uzazi hazikuwa za kingono. Halafu, kulingana na hekaya, alizaa Baba Anga wa kiume na akawa mke wake. Wenzi hao walizaa miungu na miungu-wake wengine wasiohesabika.

Kiolezo cha Kibabuloni

Miongoni mwa miungu ya Kibabuloni inayotambuliwa kirasmi, Ishtari alikuwa ndiye mungu-mke mkuu, aliyekuwa sawa na Innanna mungu-mke wa uzazi wa Kisumeria. Jambo la kinyumenyume ni kwamba, alikuwa mungu-mke wa vita na mungu-mke wa upendo na wa ashiki pia. Katika kitabu chake Les Religions de Babylonie et d’Assyrie (Dini za Kibabuloni na za Kiashuri), mwanachuo Mfaransa Édouard Dhorme alisema hivi juu ya Ishtari: “Alikuwa mungu-mke, bibi, mama mwenye rehema asikiaye sala na kutetea mbele ya miungu wenye hasira na kuwatuliza. . . . Alitukuzwa juu ya wote, akawa mungu-mke wa miungu-wake, malkia wa miungu wote, mwenye enzi kuu wa miungu wa mbingu na dunia.”

Waabudu wa Ishtari walimwelekezea maneno “Bikira,” “Bikira Mtakatifu,” na “Mama Bikira.” “Sala ya Maombolezo kwa Ishtari” ya kale ya Kisumeria na Kiakkadia yataarifu hivi: “Nasali kwako, Eh Bibi wa mabibi, mungu-mke wa miungu-wake. Eh Ishtari, malkia wa jamii zote za watu. . . . Eh mwenye uwezo wote wa kimungu, anayevaa taji la utawala. . . . Vikanisa, mahali mahali patakatifu, mahali mahali pa ibada, na vihekalu hukutii wewe. . . . Ni wapi ambapo mapenzi yako hayatimizwi? . . . Nione mimi Eh Bibi yangu; kubali sala zangu.”a

Ibada ya Mama Mungu-Mke Yaenea

Mwenye elimu ya nchi za mashariki Édouard Dhorme asema juu ya “kuenea kwa ibada ya Ishtari.” Ilienea kotekote Mesopotamia, na ama Ishtari mwenyewe ama miungu-wake wenye majina tofauti-tofauti lakini wenye sifa zilizofanana na zake waliabudiwa katika Misri, Foinike, na Kanaani, na pia katika Anatolia (Esia Ndogo), Ugiriki, na Italia.

Mama-mungu-mke mkuu aliyeabudiwa katika Misri alikuwa Isisi. Mwanahistoria H. G. Wells aliandika hivi: “Isisi alivutia watawa wengi, walioweka nadhiri ya uhai wao kwake. Sanamu zake zilisimama katika hekalu, akiwa amevikwa taji kuwa Malkia wa Mbingu na akimbeba kitoto kichanga Horusi mikononi mwake. Mishumaa iliwaka na kuchururika mbele yake, na matoleo ya nta ya wakfu yaliangikwa juu ya madhabahu.” (The Outline of History) Ibada ya Isisi ilipendwa sana katika Misri. Ilienea pia kotekote katika eneo la Mediterrania, hasa katika Ugiriki na Roma, hata kufikia Ulaya ya magharibi na kaskazini.

Katika Foinike na Kanaani, ibada ya mama-mungu-mke ilikazia juu ya Ashtorethi, au Astarte, aliyesemekana kuwa mke wa Baali. Kama kifani chake cha Kibabuloni, Ishtari, alikuwa mungu-mke wa uzazi na wa vita pia. Katika Misri miandiko ya kale imepatikana ambayo katika hiyo Astarte anaitwa bibi wa mbingu na malkia wa mbinguni. Waisraeli walipaswa washindane daima dhidi ya uvutano wenye kushusha wa ibada ya mungu-mke wa uzazi huyo.

Kuelekea kaskazini-magharibi katika Anatolia, aliyelingana na Ishtari alikuwa Cybele, aliyejulikana kuwa Mama Mkuu wa miungu. Aliitwa pia Mwenye Kuzaa Wote, Mwenye Kuwalisha Wote, Mama ya Wabarikiwa wote. Kutoka Anatolia mazoea ya Cybele yalienea kwanza katika Ugiriki halafu Roma, ambapo yalidumu hadi Wakati wa Kawaida. Ibada ya mungu-mke wa uzazi huyo ilitia ndani kucheza kwa wazimu, kujijeruhi kwa makuhani, kujihasi kwa waliotaka kuwa makuhani, na miandamano ambayo katika hiyo sanamu ya mungu-mke ilibebwa kwa fahari nyingi.b

Wagiriki wa zamani waliabudu Gaea, aliye mungu-mke Mama-Dunia. Lakini miungu-wake wa aina ya Ishtari wakaja kuingizwa miongoni mwa miungu yao waliofahamika kirasmi, kama vile Afrodito, mungu-mke wa uzazi na upendo; Athena, mungu-mke wa vita; na Demeteri, mungu-mke wa kilimo.

Katika Roma, Venus alikuwa mungu-mke wa upendo, na akiwa hivyo, alilingana na Afrodito wa Kigiriki na Ishtari wa Kibabuloni. Hata hivyo, Waroma waliabudu pia miungu-wake Isisi, Cybele, na Minerva (Athena wa Kigiriki), ambao wote walionyesha katika njia moja au nyingine ulinganifu na kielelezo cha kwanza Ishtari wa Kibabuloni.

Kwa wazi, kwa maelfu ya miaka, ibada ya mama-mungu-mke ilikuwa ushindani wenye nguvu wa ibada safi ya Muumba mkuu, Yehova. Je! ibada ya mama-mungu-mke mkuu ilififia? Au je, imedumu hadi siku ya leo? Tafadhali endelea kusoma.

[Maelezo ya Chini]

a Ancient Near Eastern Texts, iliyohaririwa na James B. Pritchard, Matbaa ya Chuo Kikuu cha Princeton, kurasa 383-4.

b Mungu-mke mwingine wa uzazi aliyeabudiwa katika Esia Ndogo alikuwa Artemisi wa Kiefeso, ambaye atazungumziwa katika makala ifuatayo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

ISHTARI wa Babuloni

Aliyepewa umbo la nyota

[Hisani]

Kwa hisani ya The British Museum

[Picha katika ukurasa wa 4]

ISISI wa Misri pamoja na kitoto kichanga aliye mungu Horusi

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki