Sababu Ya Wao Kutumia Visalio Vya Waonwao Kuwa Watakatifu Katika Ibada
NAPLES, katika Italia. Wazia kwamba uko huko katika miaka ya mapema ya karne ya 18 ya Wakati wa Kawaida wetu. Katika kathedro yayo, George Berkeley, mwanafalsafa Mwailandi asimama mbele ya kisalio maarufu cha kidini. Atazama akitilia shaka ule uonekanao kuwa myeyuko wa damu ya “San Gennaro,” Januarius “mtakatifu” Mkatoliki.
Naples haijabadilika sana kwa habari hiyo. Kwa mfano, ingawa kulikuwako hali mbaya ya anga pindi moja katika miaka ya hivi karibuni, kanisa hilo lilikuwa limejaa watu tena, na muujiza ulionekana kwamba ulikuwa umetukia. Kisalio hicho na mwandamano ulioongozwa na kardinali Askofu Mkuu walisalimiwa kwa makofi yenye uchangamfu. Naam, hiyo ilikuwa mara nyingine kati ya nyingi ambayo damu ya “San Gennaro” ilionekana kana kwamba inayeyuka. Inaripotiwa kwamba miujiza inayohusika na kisalio hicho cha kidini imekuwa ikitukia tangu karne ya 14.
Kulingana na mapokeo ya Kikatoliki, kisalio (ambacho kwa Kiingereza ni relic kutokana na neno la Kilatini relinquere, linalomaanisha “kuacha nyuma”) ni kitu kilichoachwa na mtu aonwaye kuwa mtakatifu. Kama Dizionario Ecclesiastico ionyeshavyo, visalio hivyo “vinafafanuliwa kwa maana hususa [kuwa] mwili au sehemu ya mwili na majivu ya Mtakatifu, na vinafafanuliwa kwa maana pana zaidi kuwa kitu kilichogusa mwili wa mtakatifu na kwa hiyo kinastahili uchaji.”
Kibali cha Kipapa
Yaelekea, wengi hutoa kicho chenye staha kwa visalio vya kidini kwa sababu ya miujiza inayoonekana kutukia ambayo hushirikishwa navyo. Kibali cha kipapa chaonekana kuwa jambo jingine linalosababisha visalio vipate umaarufu mwingi.
Angalau mapapa wanne katika miaka 70 iliyopita wametoa uangalifu wa kipekee kwa visalio hivyo. Gazeti la Kikatoliki linafunua kwamba Papa Pius wa 12, kama mtangulizi wake Papa Pius wa 11, “alivaa mwilini mwake visalio vya mwanamke mtakatifu wa Lisieux.” Paul wa 6 “aliweka kidole cha mtume [Tomaso] juu ya dawati lililokuwa katika chumba chake cha kusomea,” na John Paul wa 2 “huweka, katika nyumba yake mwenyewe, vijipande vya . . . mabaki ya miili” ya “Mtakatifu Benedict” na ya “Mtakatifu Andrew.”—30 giorni, Machi 1990, ukurasa 50.
Kwa sababu ya kibali cha kipapa cha jinsi hiyo, haishangazi kwamba uhitaji wa visalio hivyo kwa ajili ya uchaji wa faraghani na wa peupe pia unaongezeka. Lakini je! uchaji wa visalio vya waonwao kuwa watakatifu humpendeza Mungu?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Chombo cha kuhifadhia visalio vya kidini
[Hisani]
Kwa hisani ya The British Museum