Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • sh sura 9 kur. 205-234
  • Dini ya Kiyahudi—Jitihada ya Kutafuta Mungu Kupitia Andiko na Pokeo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dini ya Kiyahudi—Jitihada ya Kutafuta Mungu Kupitia Andiko na Pokeo
  • Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sababu Tupendezwe na Dini ya Kiyahudi
  • Wayahudi Walitokeaje?
  • Musa, Torati, na Taifa
  • Taifa Lenye Makuhani, Manabii, na Wafalme
  • Dini ya Kiyahudi Yatokea Ikiwa na Vazi la Kigiriki
  • Dini ya Kiyahudi Chini ya Utawala wa Kiroma
  • Dini ya Kiyahudi Wakati wa Enzi za Kati
  • Kutoka “Mnurisho” Mpaka Siasa ya Wayahudi Kurudi Sayuni
  • Mungu Ni Mmoja
  • Kifo, Nafsi, na Ufufuo
  • Dini ya Kiyahudi na Jina la Mungu
  • Je! Wayahudi Wangali Wakimngojea Mesiya?
  • Kumjua Mungu wa Kweli—Kwamaanisha Nini?
    Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote?
  • Tafsiri ya Biblia Iliyoubadili Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Wayahudi, Wakristo, na Lile Tumaini la Kimesiya
    Amkeni!—1992
  • Je! Pengo Laweza Kuzibwa?
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
sh sura 9 kur. 205-234

Sura 9

Dini ya Kiyahudi—Jitihada ya Kutafuta Mungu Kupitia Andiko na Pokeo

1, 2. (a) Ni baadhi ya Wayahudi gani mashuhuri ambao wameathiri historia na utamaduni? (b) Ni swali gani ambalo huenda likatokezwa na watu fulani?

MUSA, Yesu, Mahler, Marx, Freud, na Einstein—wote hao walikuwa na jambo gani lililofanana? Wote walikuwa Wayahudi, na katika njia tofauti, wote wameathiri historia na utamaduni wa ainabinadamu. Kwa wazi sana Wayahudi wametokeza kwa maelfu ya miaka. Biblia yenyewe yashuhudia hilo.

2 Tofauti na dini na tamaduni nyingine za kale, mizizi ya Dini ya Kiyahudi ni katika historia, si katika ngano. Hata hivyo, huenda wengine wakauliza: Wayahudi ni wachache mno, karibu milioni 18 katika ulimwengu wa watu zaidi ya milioni elfu tano, kwa nini tupendezwe na Dini ya Kiyahudi yao?

Sababu Tupendezwe na Dini ya Kiyahudi

3, 4. (a) Ndani ya Maandiko ya Kiebrania mna nini? (b) Ni nini baadhi ya sababu kwa nini tumepaswa kufikiria Dini ya Kiyahudi na mizizi yayo?

3 Sababu moja ni kwamba mizizi ya Dini ya Kiyahudi yarudi nyuma miaka inayopata 4,000 katika historia na dini nyingine kubwa-kubwa zategemea kwa kadiri kubwa au ndogo Maandiko yayo. (Ona kisanduku, ukurasa 220.) Ukristo, ulioanzishwa na Yesu (Kiebrania, Ye·shuʹa‛), Myahudi wa karne ya kwanza, una mizizi yake katika Maandiko ya Kiebrania. Na kama ambavyo usomaji wowote wa Kurani unavyoonyesha, Uislamu pia wategemea sana maandiko hayo. (Kurani, sura 2:49-57; 32:23, 24) Kwa hiyo, tunapochunguza Dini ya Kiyahudi, pia tunachunguza mizizi ya mamia ya dini na mafarakano mengine.

4 Sababu ya pili na ya muhimu ni kwamba Dini ya Kiyahudi huweka kiunganishi cha lazima katika jitihada za ainabinadamu za kutafuta Mungu wa kweli. Kulingana na Maandiko ya Kiebrania, Abramu, babu ya Wayahudi, alikuwa tayari akimwabudu Mungu wa kweli karibu miaka 4,000 iliyopita.a Kwa kufaa, twauliza, Wayahudi na imani yao walisitawije?—Mwanzo 17:18.

Wayahudi Walitokeaje?

5, 6. Kwa ufupi, ni nini historia ya chanzo cha Wayahudi na jina lao?

5 Kusema kiujumla, Wayahudi ni wazao wa mlango wa kale wenye kusema Kiebrania wa mbari ya Shemu. (Mwanzo 10:1, 21-32; 1 Mambo ya Nyakati 1:17-28, 34; 2:1, 2) Karibu miaka 4,000 iliyopita, Abramu babu yao alihama kutoka mji wenye kusitawi wa Uru wa Wakaldayo katika Sumeri akaenda nchi ya Kanaani, ambayo juu yayo Mungu alikuwa ametoa taarifa hii: “Uzao wako nitawapa nchi hii.”b (Mwanzo 11:31–12:7) Anatajwa kuwa “Abramu Mwebrania” kwenye Mwanzo 14:13, ijapokuwa jina lake lilibadilishwa baadaye likawa Abrahamu. (Mwanzo 17:4-6) Kutoka kwake Wayahudi wanafuatisha nasaba inayoanza na mwanae Isaka na mjukuu wake Yakobo, ambaye jina lake lilibadilishwa kuwa Israeli. (Mwanzo 32:27-29) Israeli alikuwa na wana 12, ambao walikuja kuwa waanzilishi wa makabila 12. Mmoja wao alikuwa Yuda, ambaye kwake neno “Myahudi” lilitoka hatimaye.—2 Wafalme 16:6, JP.

6 Baada ya muda usemi “Myahudi” ulitumiwa kwa Waisraeli wote, si kwa mzao wa Yuda peke yake. (Esta 3:6; 9:20) Kwa sababu kumbukumbu za nasaba ya Kiyahudi ziliangamizwa katika 70 W.K. wakati Waroma walipoteketeza kabisa Yerusalemu, hakuna Myahudi yeyote leo anayeweza kuamua kwa usahihi yeye mwenyewe ni mzao wa kabila gani. Hata hivyo, katika maelfu mengi ya miaka iliyopita, Dini ya Kiyahudi ya kale imesitawi na kubadilika. Leo Dini ya Kiyahudi inazoewa na mamilioni ya Wayahudi katika Jamhuri ya Israel na Diaspora (mtawanyiko kuuzunguka ulimwengu). Msingi wa dini hiyo ni nini?

Musa, Torati, na Taifa

7. Mungu alitoa kiapo gani kwa Abrahamu, na kwa nini?

7 Katika 1943 K.W.K.,c Mungu alichagua Abramu awe mtumishi wake maalumu na baadaye akafanya kiapo kizito kwake kwa sababu ya uaminifu wake katika kuwa na nia ya kumtoa mwanae Isaka kuwa dhabihu, hata ingawa dhabihu yenyewe haikukamilishwa kamwe. (Mwanzo 12:1-3; 22:1-14) Katika kiapo hicho Mungu alisema: “Kwa Mimi mwenyewe naapa, BWANA [Kiebrania: יהוה, YHWH] najulisha rasmi hivi: Kwa sababu wewe umefanya hili na hukuzuia mwana wako, aliye mpendwa wako, nitatuza baraka Yangu juu yako na kufanya wazao wako kuwa tele kama nyota za mbingu . . . mataifa yote ya dunia yatajibarikia kwa wazao [“mbegu,” JP] wako, kwa sababu wewe umetii amri Yangu.” Kiapo hicho kilicholiwa kilirudiwa kwa mwana wa Abrahamu na kwa mjukuu wake, na kisha kikaendelea katika kabila la Yuda na mlango wa Daudi. Wazo hilo la Mungu mmoja tu mwenye utu anayeshughulika na binadamu moja kwa moja lilikuwa maalumu katika ulimwengu huo wa kale, na likaja kufanyiza msingi wa Dini ya Kiyahudi.—Mwanzo 22:15-18; 26:3-5; 28:13-15; Zaburi 89:4, 5, 29, 30, 36, 37 (Zaburi 89:3, 4, 28, 29, 35, 36, UV).

8. Musa alikuwa nani, naye alitimiza fungu gani katika Israeli?

8 Ili kutimiza ahadi zake kwa Abrahamu, Mungu aliweka msingi kwa ajili ya taifa kwa kusimamisha agano la pekee pamoja na wazao wa Abrahamu. Agano hilo lilianzishwa kupitia Musa, kiongozi mkuu Mwebrania na mpatanishi kati ya Mungu na Israeli. Musa alikuwa nani, na kwa nini yeye ni wa maana sana kwa Wayahudi? Simulizi la Biblia la Kutoka latuambia kwamba yeye alizaliwa katika Misri (1593 K.W.K.) na wazazi Waisraeli waliokuwa watumwa katika utekwa pamoja na Israeli wengine. Yeye ndiye “ambaye BWANA alimchagua” aongoze watu Wake kwenye uhuru katika Kanaani, Bara Lililoahidiwa. (Kumbukumbu la Torati 6:23; 34:10) Musa alitimiza wajibu wa muhimu wa kuwa mpatanishi wa agano la Torati lililotolewa na Mungu kwa Israeli, kuongezea kuwa nabii, hakimu, kiongozi, na mwanahistoria wao.—Kutoka 2:1–3:22.

9, 10. (a) Ni Torati gani iliyopitishwa kwa kutumia Musa? (b) Ni sehemu gani za maisha zilizotiwa ndani ya Amri Kumi? (c) Ni wajibu gani ambao agano la Torati liliweka juu ya Israeli?

9 Torati ambayo Israeli walikubali ilitia ndani Maneno au Amri Kumi, na sheria zaidi ya 600 zilizojumlika kuwa orodha ya mielekezo na miongozo kwa ajili ya mwenendo wa kila siku. (Ona kisanduku, ukurasa 211.) Ilitia ndani mambo ya kidunia na matakatifu—matakwa ya kimwili na ya kiadili na pia ibada ya Mungu.

10 Agano hilo la Torati, au katiba ya kidini, liilipa imani ya wazee hao wa kale muundo na maana. Kwa njia hiyo, wazao wa Abrahamu wakawa taifa lililowekwa wakfu kwa utumishi wa Mungu. Kwa hiyo Dini ya Kiyahudi ikaanza kupata muundo kamili, na Wayahudi wakawa taifa lililofanywa kitengenezo kwa ajili ya ibada na utumishi wa Mungu wao. Kwenye Kutoka 19:5, 6, Mungu aliwaahidi: “Ikiwa nyinyi mtatii Mimi kwa uaminifu na kushika agano Langu, . . . nyinyi mtakuwa Kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.” Kwa njia hiyo, Waisraeli wangekuwa ‘watu waliochaguliwa’ kutumikia makusudi ya Mungu. Hata hivyo, utimizo wa ahadi za agano hilo ulitegemea sharti la “Ikiwa nyinyi mtatii.” Taifa hilo lililowekwa wakfu sasa lilikuwa na daraka kwa Mungu walo. Kwa hiyo wakati wa tarehe ya baadaye (karne ya nane K.W.K.), Mungu angeweza kusema kwa Wayahudi: “Mashahidi Wangu ni nyinyi—ajulisha rasmi BWANA [Kiebrania: יהוה, YHWH]—Mtumishi Wangu, ambaye mimi nimechagua.”—Isaya 43:10, 12.

Taifa Lenye Makuhani, Manabii, na Wafalme

11. Ukuhani na ufalme ulisitawije?

11 Taifa la Israeli lilipokuwa lingali jangwani na likielekea kwenye Bara Lililoahidiwa, ukuhani ulianzishwa katika nasaba ya Haruni nduguye Musa. Hema kubwa, au tabenakulo, lenye kuchukulika, likawa kitovu cha ibada na dhabihu ya Kiisraeli. (Kutoka, sura 26-28) Mwishowe taifa la Israeli likawasili Kanaani, Bara Lililoahidiwa, na kulitiisha, sawa na ambavyo Mungu alikuwa ameamuru. (Yoshua 1:2-6) Hatimaye ufalme wa kidunia ulisimamishwa, na katika 1077 K.W.K., Daudi, kutoka kabila la Yuda, akawa mfalme. Katika utawala wake, ufalme na ukuhani, vyote viwili viliimarishwa kabisa katika kitovu kipya cha kitaifa, Yerusalemu.—1 Samweli 8:7.

12. Ni ahadi gani ambayo Mungu alikuwa ametoa kwa Daudi?

12 Baada ya kifo cha Daudi, mwanae Sulemani alijenga hekalu la kupendeza ajabu katika Yerusalemu, ambalo lilichukua mahali pa tabenakulo. Kwa sababu Mungu alikuwa amefanya agano pamoja na Daudi ili ufalme ubaki katika mlango wake milele, ilieleweka kwamba Mfalme mpakwa-mafuta, Mesiya, siku moja angetokea katika mlango wa Daudi. Unabii ulidokeza kwamba kupitia Mfalme huyo wa Kimesiya, au “mbegu,” Israeli na mataifa yote yangeonea shangwe utawala mkamilifu. (Mwanzo 22:18, JP) Tumaini hilo liliimarika, na asili ya Kimesiya ya Dini ya Kiyahudi ikawa wazi sana.—2 Samweli 7:8-16; Zaburi 72:1-20; Isaya 11:1-10; Zekaria 9:9, 10.

13. Mungu alitumia nani kusahihisha Israeli wenye kutenda maovu? Toa kielelezo.

13 Hata hivyo, Wayahudi walijiruhusu wavutwe na dini bandia ya Wakanaani na mataifa mengine yaliyowazunguka. Kama tokeo, walivunja uhusiano wao wa agano pamoja na Mungu. Ili awasahihishe na kuwaongoza warejee, Yehova aliwatuma manabii mfululizo ambao walipelekea watu ujumbe wake mbalimbali. Kwa njia hiyo, unabii ukawa sehemu nyingine maalumu ya Dini ya Wayahudi na hufanyiza sehemu kubwa ya Maandiko ya Kiebrania. Kwa kweli, vitabu 18 vya Maandiko ya Kiebrania vina majina ya manabii.—Isaya 1:4-17.

14. Matukio yalionyeshaje waliyosema manabii katika Israeli yalikuwa kweli?

14 Waliokuwa wenye kutokeza kati ya manabii hao ni Isaya, Yeremia, na Ezekieli, wote walionya juu ya adhabu ya Yehova iliyokuwa inakaribia juu ya taifa kwa ajili ya ibada yalo ya sanamu. Adhabu hiyo ikaja katika 607 K.W.K. wakati Yehova aliruhusu Babuloni, iliyokuwa mamlaka yenye kutawala ulimwengu wakati huo, ipindue Yerusalemu na hekalu lalo na kupeleka taifa hilo katika utumwa kwa sababu ya uasi-imani wa Israeli. Manabii walithibitishwa kuwa wa kweli katika yale waliyokuwa wametabiri, na uhamisho wa Israeli wa miaka 70 kwa sehemu kubwa ya karne ya sita K.W.K. ni jambo lililomo katika maandishi ya kihistoria.—2 Mambo ya Nyakati 36:20, 21; Yeremia 25:11, 12; Danieli 9:2.

15. (a) Namna mpya ya ibada ilitiaje mizizi miongoni mwa Wayahudi? (b) Masinagogi yaliathirije ibada kule Yerusalemu?

15 Katika 539 K.W.K., Koreshi Mwajemi alishinda Babuloni na akaruhusu Wayahudi wakaikae nchi yao na kujenga upya hekalu katika Yerusalemu. Ijapokuwa baki lilikubali, Wayahudi walio wengi walibaki chini ya uvutano wa jumuiya ya Kibabuloni. Baadaye Wayahudi waliathiriwa na utamaduni wa Kiajemi. Kama tokeo, makazi ya Kiyahudi yalitokea katika Mashariki ya Kati na kuzunguka Mediterrania. Katika kila jumuiya namna mpya ya ibada ikatokea iliyohusisha sinagogi, kitovu cha kutano la Wayahudi katika kila mji. Kama ilivyo, mpango huo ulipunguza mkazo juu ya hekalu lililojengwa upya katika Yerusalemu. Wayahudi waliokuwa mbali sasa walikuwa Diaspora kweli kweli.—Ezra 2:64, 65.

Dini ya Kiyahudi Yatokea Ikiwa na Vazi la Kigiriki

16, 17. (a) Ni uvutano gani mpya uliokuwa ukisambaa katika ulimwengu wa Mediterrania katika karne ya nne K.W.K.? (b) Ni nani waliotumika kuwa chombo cha kueneza utamaduni wa Kigiriki, na jinsi gani? (c) Basi ni jinsi gani Dini ya Kiyahudi ilivyotokea kwenye tamasha ya ulimwengu?

16 Kufikia karne ya nne K.W.K., jumuiya ya Kiyahudi ilikuwa katika hali ya kubadilika na kwa hiyo ikashambuliwa na mawimbi ya utamaduni usio wa Kiyahudi uliokuwa ukifunika ulimwengu wa Mediterrania na mbele zaidi. Dhoruba hizo zilitoka Ugiriki, na Dini ya Kiyahudi ikatoka kwazo ikiwa na vazi la Kiyunani.

17 Katika 332 K.W.K. jemadari Mgiriki Aleksanda Mkuu alishinda Mashariki ya Kati kwa kasi kama ya umeme naye alikaribishwa na Wayahudi alipofika Yerusalemu.d Waandamizi wa Aleksanda waliendeleza mpango wake wa kufanya mambo yote kuwa ya Kiyunani, sehemu zote za milki zikienezwa lugha, utamaduni, na falsafa ya Kigiriki. Kama tokeo, tamaduni za Kigiriki na za Kiyahudi zikachanganyikana, jambo ambalo likaja kuwa na matokeo ya kushangaza.

18. (a) Kwa nini tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint ya Maandiko ya Kiebrania ikawa ya lazima? (b) Ni sehemu gani ya utamaduni wa Kigiriki hasa iliyoathiri Wayahudi?

18 Wayahudi wa Diaspora walianza kuzungumza Kigiriki badala ya Kiebrania. Kwa hiyo kuelekea mwanzo wa karne ya tatu K.W.K., tafsiri ya kwanza ya Maandiko ya Kiebrania katika Kigiriki, iitwayo Septuagint, ilianzwa, na kupitia kwayo, wengi Wasio Wayahudi wakaja kuheshimu na kuizoelea Dini ya Kiyahudi, wengine hata wakawa waongofu.e Kwa upande mwingine, Wayahudi walikuwa wakizoelea sana wazo la Kigiriki na wengine hata wakawa wanafalsafa, jambo lililokuwa geni kabisa kwa Wayahudi. Kielelezo kimoja ni Filo wa Aleksandria wa karne ya kwanza W.K., aliyejitahidi kueleza Dini ya Kiyahudi kulingana na falsafa ya Kigiriki, kana kwamba zote mbili zilieleza kweli kamili zile zile.

19. Mtungaji mmoja Myahudi aelezaje juu ya kipindi cha kuchanganyika kwa tamaduni za Kigiriki na za Kiyahudi?

19 Akijumlisha kipindi hiki cha nipe-nikupe kati ya tamaduni za Kigiriki na za Kiyahudi, mtungaji Myahudi Max Dimont asema: “Wakiwa wametajirishwa na mawazo ya Kiplato, kusababu kwa Kiaristotel, na sayansi ya Kiekulidi, wasomi Wayahudi waliiangalia Tora wakiwa na zana mpya. . . . Walichukua hatua ya kuongezea kusababu kwa Kigiriki kwenye ufunuo wa Kiyahudi.” Matukio ambayo yangekuja kutendeka chini ya utawala wa Roma, ambao ulifyonza Milki ya Kigiriki na halafu Yerusalemu katika mwaka 63 K.W.K., yangetazamiwa kufyeka njia ya mabadiliko makubwa hata zaidi.

Dini ya Kiyahudi Chini ya Utawala wa Kiroma

20. Hali ya kidini kati ya Wayahudi ilikuwa nini katika karne ya kwanza W.K.?

20 Dini ya Kiyahudi ya karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida ilikuwa katika hatua ya aina yake. Max Dimont atoa taarifa kwamba ilisitasita kati ya “akili ya Kigiriki na upanga wa Roma.” Matazamio ya Kiyahudi yalikuwa makubwa kwa sababu ya dhuluma ya kisiasa na kufasiri unabii mbalimbali wa Kimesiya, hasa ule wa Danieli. Wayahudi walikuwa wamegawanyika katika vikundi mbalimbali. Mafarisayo walikazia sheria ya mdomo (ona kisanduku, ukurasa 221) badala ya dhabihu ya hekalu. Masadukayo walikazia umaana wa hekalu na ukuhani. Halafu walikuwako Waesene, Wazeloti, na Waherode. Wote walikuwa wanapingana kidini na kifalsafa. Viongozi wa Kiyahudi waliitwa marabi (walimu, wafundishaji) ambao, kwa sababu ya maarifa yao ya Torati, walikuwa na cheo kikubwa na wakawa aina mpya ya kiongozi wa kiroho.

21. Ni matukio gani yaliyoathiri vibaya Wayahudi wa karne mbili za kwanza W.K.?

21 Hata hivyo, migawanyiko ya kindani na ki-nje iliendelea katika Dini ya Kiyahudi, hasa katika nchi ya Israeli. Mwishowe, uasi wa moja kwa moja ulitokea juu ya Roma, na katika 70 W.K., majeshi ya Kiroma yalizingira Yerusalemu, yakalifanya jiji hilo kuwa ukiwa, na kuteketeza hekalu lalo mpaka ardhi, na kuwatawanya wakaaji walo. Mwishowe, ikaamriwa Wayahudi hawaruhusiwi kamwe katika Yerusalemu. Bila ya hekalu, bila ya nchi, watu walo wakiwa wametawanywa kote-kote katika Milki ya Kiroma, Dini ya Kiyahudi ilihitaji jambo jipya la kidini ikiwa ingeendelea kuwapo.

22. (a) Dini ya Kiyahudi iliathiriwaje na hasara ya hekalu katika Yerusalemu? (b) Wayahudi huigawanyaje Biblia? (c) Talmud ni nini, nayo ilisitawije?

22 Hekalu lilipoharibiwa, Masadukayo walitokomea, na sheria ya mdomo ambayo Mafarisayo walikuwa wameitetea ikawa msingi wa Dini ya Kiyahudi mpya ya Kirabi. Badala ya dhabihu za hekalu na kuhiji, kukawa funzo la bidii zaidi, sala, na matendo ya utawa. Kwa njia hiyo, Dini ya Kiyahudi ikawa yaweza kuzoewa kila mahali, wakati wowote, katika mazingira yoyote ya kitamaduni. Zaidi ya kuitungia mafafanuzi, Marabi waliandika sheria hiyo ya mdomo, halafu mafafanuzi kuhusu mafafanuzi hayo, yote pamoja yakaja kujulikana kuwa Talmud.—Ona kisanduku, kurasa 220-1.

23. Ni badiliko gani la mkazo lililotukia chini ya uvutano wa kufikiri kwa Kigiriki?

23 Tokeo la uvutano huo mbalimbali likawa nini? Max Dimont asema katika kitabu chake Jews, God and History kwamba ingawa Mafarisayo walishikilia tochi ya mawazo na Dini ya Kiyahudi, “tochi yenyewe ilikuwa imewashwa na wanafalsafa Wagiriki.” Ingawa sehemu kubwa ya Talmud ilishikilia mno sheria, mifano na maelezo yayo yalionyesha uvutano ulio dhahiri wa falsafa ya Kigiriki. Kwa kielelezo, mawazo ya kidini ya Kigiriki, kama vile kutoweza kufa kwa nafsi, yalielezwa kwa njia ya Kiyahudi. Kweli kweli, katika muhula huo mpya wa Kirabi, kuheshimu mno Talmud—wakati huo ikiwa mchanganyiko wa sheria na falsafa za Kigikiri—kuliongezeka kati ya Wayahudi mpaka, kufikia Enzi za Kati, Talmud ikaja kuheshimiwa sana na Wayahudi zaidi ya Biblia yenyewe.

Dini ya Kiyahudi Wakati wa Enzi za Kati

24. (a) Ni jumuiya gani mbili kubwa zilizotokea kati ya Wayahudi wakati wa Enzi za Kati? (b) Zilikuwa na uvutano gani kwa Dini ya Kiyahudi?

24 Wakati wa Enzi za Kati (kuanzia 500 hadi 1500 W.K.), jumuiya mbili za Kiyahudi zilizo tofauti zilitokea—Wayahudi Wasefardi, ambao walisitawi chini ya utawala wa Kiislamu katika Hispania, na Wayahudi Waashikenazi katika Ulaya ya Kati na Mashariki. Jumuiya zote mbili zilitokeza wasomi wa Kirabi ambao maandishi na mawazo yao hufanyiza msingi wa fasiri ya kidini ya Kiyahudi mpaka wa leo. Yafaa kuangaliwa kwamba desturi na mazoea mengi ya kidini yanayopatikana leo katika Dini ya Kiyahudi yalianza wakati wa Enzi za Kati.—Ona kisanduku, ukurasa 231.

25. Kanisa Katoliki hatimaye lilichukulia Wayahudi katika Ulaya hatua gani?

25 Katika karne ya 12, kulianza wimbi la kufukuza Wayahudi kutoka nchi mbalimbali. Kama anavyoeleza mtungaji Mwisraeli Abba Eban katika My People—The Story of the Jews: “Katika nchi yoyote . . . iliyokuja chini ya uvutano wa upande mmoja wa Kanisa Katoliki, hadithi ni ile ile: kuvunjiwa heshima kwa kusikitisha mno, mateso, machinjo, na kufukuzwa.” Hatimaye, katika 1492, Hispania, ambayo kwa mara nyingine ilikuwa imekuja chini ya utawala wa Katoliki, ikachukua hatua iyo hiyo na kuagiza Wayahudi wote wafukuzwe katika eneo layo. Hivyo kufikia mwisho wa karne ya 15, Wayahudi walikuwa wamefukuzwa kutoka karibu Ulaya ya Magharibi yote, wakakimbilia Ulaya ya Mashariki na nchi nyingine kuzunguka Meditterania.

26. (a) Ni nini kilichoongoza kwenye mzinduko kati ya Wayahudi? (b) Ni migawanyiko gani mikubwa iliyoanza kusitawi kati ya Wayahudi?

26 Wakati wa karne nyingi za dhuluma na mateso, Wamesiya wengi wa kujitangaza walitokea kati ya Wayahudi katika sehemu tofauti-tofauti za ulimwengu, wote wakikubaliwa kwa kadiri hii au hii, lakini mwisho ukiwa ni mzinduko. Kufikia karne ya 17, hatua mpya zilihitajiwa ili kutia nguvu mpya Wayahudi na kuwaondoa katika kipindi hiki cha giza. Katikati ya karne ya 18, Wayahudi waliokosa tumaini wakapata jibu. Lilikuwa ni Hasidim (ona kisanduku, ukurasa 226), mchanganyiko wa mafumbo na raha nyingi mno ya kidini ulioonyeshwa kwa ujitoaji na utendaji wa kila siku. Kinyume cha hilo, karibu wakati uo huo, mwanafalsafa Moses Mendelssohn, Myahudi Mjerumani, alitoa suluhisho jingine, njia ya Haskala, au mnurisho, ambayo ilikuja kuongoza kwenye ile inayoonwa kihistoria kuwa “Dini ya Kiyahudi ya Kisasa.”

Kutoka “Mnurisho” Mpaka Siasa ya Wayahudi Kurudi Sayuni

27. (a) Moses Mendelssohn alikuwa na uvutano gani juu ya mitazamo ya Kiyahudi? (b) Ni kwa nini Wayahudi wengi walikataa tumaini la Mesiya aliye mtu?

27 Kulingana na Moses Mendelssohn (1729-86), Wayahudi wangekubaliwa kama wangetoka kwenye vizuizi vya Talmud na kujipatanisha na utamaduni wa Magharibi. Katika siku yake, yeye alikuja kuwa mmoja wa Wayahudi walioheshimiwa zaidi na ulimwengu wa Wasio Wayahudi. Hata hivyo, mashambulizi mengine ya jeuri ya kupinga wazao wa Shemu katika karne ya 19, hasa katika Urusi ya “Kikristo,” yalizindua wafuasi wa chama hicho. Walikataa wazo la Mesiya mtu ambaye angeongoza Waisraeli warudi Israeli na wakaanza kufanya kazi kusimamisha Serikali ya Kiyahudi kwa njia nyingine. Basi hili likawa wazo la siasa ya Wayahudi kurudi Sayuni: ‘kufanya umesiya wa Kiyahudi uwe wa kilimwengu,’ kama mwenye mamlaka mmoja anavyosema.

28. Ni matukio gani katika karne ya 20 ambayo yameathiri mitazamo ya Kiyahudi?

28 Mauaji ya Wayahudi wa Ulaya wapatao milioni sita katika Machinjo Makubwa yaliyochochewa na Wanazi (1935-45) yaliipa nguvu ya upeo siasa ya Wayahudi kurudi Sayuni nayo ikaungwa mkono sana ulimwenguni pote. Ndoto ya siasa ya kurudi Sayuni ilitimia katika 1948 kwa kusimamishwa kwa Serikali ya Israel, jambo ambalo latuleta kwenye Dini ya Kiyahudi katika siku yetu na kwenye swali, Wayahudi wa kisasa huamini nini?

Mungu Ni Mmoja

29. (a) Kifupi, Dini ya Kiyahudi ya kisasa ni nini? (b) Utambulisho wa Kiyahudi waonyeshwaje? (c) Ni nini baadhi ya misherehekeo na desturi za Kiyahudi?

29 Kifupi, Dini ya Kiyahudi ni dini ya jamii fulani ya watu. Kwa hiyo, mwongofu huwa sehemu ya watu wa Kiyahudi na pia Dini ya Kiyahudi. Ni dini inayoamini mungu mmoja kabisa na hushikilia kwamba Mungu hujiingiza katika historia ya kibinadamu, hasa kuhusiana na Wayahudi. Ibada ya Kiyahudi yahusisha misherehekeo kadhaa ya kila mwaka na desturi mbalimbali. (Ona kisanduku, kurasa 230-1.) Ingawa hakuna itikadi zinazokubaliwa na Wayahudi wote, kukiri Mungu kuwa mmoja kama inavyosemwa katika Shema, sala moja inayotegemea Kumbukumbu la Torati 6:4 (JP), ni sehemu ya msingi ya ibada ya sinagogi: “SIKILIZA, E ISRAELI: BWANA MUNGU WETU, BWANA NI MMOJA.”

30. (a) Wayahudi wamwelewaje Mungu? (b) Maoni ya Kiyahudi juu ya Mungu yapinganaje na yale ya Jumuiya ya Wakristo?

30 Itikadi hii ya Mungu mmoja ilipitishwa kwa Ukristo na kwa Uislamu. Kulingana na Dakt. J. H. Hertz, ambaye ni rabi: “Tamko hilo kamili la kuamini kuwapo kwa Mungu mmoja tu lilikuwa ni tangazo la vita juu ya itikadi katika miungu mingi . . . Katika njia iyo hiyo, Shema haitii ndani utatu wa itikadi ya Kikristo kwa kuwa huhalifu Umoja wa Mungu.”f Lakini sasa acheni tugeukie imani ya Kiyahudi juu ya habari ya maisha ya baada ya kifo.

Kifo, Nafsi, na Ufufuo

31. (a) Fundisho la nafsi isiyoweza kufa liliingiaje katika mafundisho ya Kiyahudi? (b) Fundisho la kutoweza kufa kwa nafsi lilisababisha tatizo gani?

31 Mojawapo imani za msingi za Dini ya Kiyahudi ya kisasa ni kwamba binadamu ana nafsi isiyoweza kufa ambayo huendelea kuishi baada ya kifo cha mwili wake. Lakini je! hilo latokana na Biblia? Encyclopaedia Judaica hukubali hivi waziwazi: “Yaelekea ilikuwa chini ya uvutano wa Kigiriki kwamba fundisho la kutoweza kufa kwa nafsi likaingia katika Dini ya Kiyahudi.” Hata hivyo, jambo hilo lilitokeza tatizo la kimafundisho, kama ambavyo chanzo icho hicho kinavyotoa taarifa hii: “Kwa msingi imani hizo mbili za ufufuo na kutoweza kufa kwa nafsi zinapingana. Moja yarejezea ufufuo wa ujumla kwenye mwisho wa zile siku, yaani, kwamba wafu waliolala katika ardhi watainuka kutoka kaburini, na ile nyingine yarejezea hali ya nafsi baada ya kifo cha mwili.” Tatizo hilo lilisuluhishwaje katika theolojia ya Kiyahudi? “Ilishikiliwa kwamba wakati mtu alipokufa bado nafsi yake iliendelea kuishi katika makao mengine (hilo lilitokeza imani zote zinazohusiana na mbingu na mahali pa moto wa mateso) nao mwili wake ukalala katika kaburi ukingojea ufufuo wa kimwili wa wafu wote hapa duniani.”

32. Biblia husema nini juu ya wafu?

32 Mhadhiri wa chuo kikuu Arthur Hertzberg aandika hivi: “Katika Biblia [ya Kiebrania] yenyewe uwanja wa maisha ya binadamu ni ulimwengu huu. Hakuna fundisho la mbingu na mahali pa moto wa mateso, ila tu wazo lenye kukua la ufufuo wa upeo wa wafu kwenye mwisho wa siku.” Hayo ni maelezo ya kifupi na yaliyo sahihi ya wazo la Kibiblia, yaani, kwamba “wafu hawajui lolote . . . kwa maana hakuna tendo, wala kuwaza, wala kujifunza, wala hekima katika Sheoli [kaburi la ujumla la ainabinadamu], ambako wewe unaenda.”—Mhubiri 9:5, 10; Danieli 12:1, 2; Isaya 26:19.

33. Fundisho la ufufuo wa wafu hapo awali lilionwaje na Wayahudi?

33 Kulingana na Encyclopaedia Judaica, “Katika kipindi cha kirabi fundisho la ufufuo wa wafu huonwa kuwa mojawapo mafundisho makuu ya Dini ya Kiyahudi” na “lapasa kutofautishwa na imani katika . . . kutoweza kufa kwa nafsi.”g Hata hivyo, leo ingawa kutoweza kufa kwa nafsi hukubaliwa na vikundi vyote vya Dini ya Kiyahudi, sivyo ilivyo kwa ufufuo wa wafu.

34. Kinyume cha maoni ya Biblia, Talmud yaelezaje juu ya nafsi? Waandikaji wa baadaye hutoa maelezo gani?

34 Tofauti na Biblia, Talmud, ambayo iliathiriwa na Uyunani, imejaa maelezo na hadithi na hata masimulizi ya nafsi isiyoweza kufa. Baadaye fasihi ya kifumbo ya Kiyahudi, Kabbala, yasonga hatua moja mbele kufundisha maisha katika umbo jingine (kuhama kwa nafsi kuingia katika umbo jingine), ambalo kwa msingi ni fundisho la Uhindu wa kale. (Ona Sura 5.) Katika Israel leo, hilo hukubaliwa na wengi kuwa fundisho la Kiyahudi, na pia hutimiza fungu la maana katika imani na fasihi za Hasidim. Kwa kielelezo, Martin Buber atia ndani katika kitabu chake Tales of the Hasidim—The Later Masters hadithi juu ya nafsi kutoka kwa kikundi chenye mawazo tofauti cha Elimelekh, rabi mmoja wa Lizhensk: “Katika Siku ya Upatanisho, wakati Rabi Abrahamu Yehoshua angekariri Avodah, sala inayorudia ibada ya kuhani mkuu katika Hekalu la Yerusalemu, na kufikia kifungu hiki: ‘Naye akasema hivyo,’ yeye hakusema maneno hayo kamwe, bali angesema: ‘Nami nikasema hivyo.’ Kwa maana yeye hakuwa amesahau wakati ambao nafsi yake ilikuwa katika mwili wa kuhani mkuu wa Yerusalemu.”

35. (a) Dini ya Kiyahudi ya Reform yachukua msimamo gani juu ya fundisho la nafsi isiyoweza kufa? (b) Fundisho la Biblia lililo wazi juu ya nafsi ni nini?

35 Dini ya Kiyahudi ya Reform imefikia hatua ya kukataa imani katika ufufuo. Ikiwa imekwisha kuondoa neno hilo katika vitabu vya sala vya Reform, hiyo hutambua tu imani katika nafsi isiyoweza kufa. Jinsi wazo la Kibiblia linaloelezwa katika Mwanzo 2:7 lilivyo wazi zaidi: “BWANA Mungu akamfanya mtu kutoka kwa mavumbi ya ardhi, na kupuliza katika mianzi ya pua yake pumzi ya uhai; na mtu akawa nafsi inayoishi.” (JP) Muunganisho wa mwili na roho, au kani ya uhai, ndio hufanyiza “nafsi inayoishi.”h (Mwanzo 2:7; 7:22; Zaburi 146:4) Basi, inakuwa mtenda dhambi wa kibinadamu anapokufa, nayo nafsi hufa. (Ezekieli 18:4, 20) Kwa njia hiyo, wakati wa kifo binadamu huacha kuwa na fahamu zozote. Kani ya uhai wake humrudia Mungu aliyeitoa. (Mhubiri 3:19; 9:5, 10; 12:7) Tumaini la kweli la Kibiblia kwa ajili ya wafu ni ufufuo.—Kiebrania: techi·yathʹ ham·me·thimʹ, au “kuhuishwa kwa mfu.”

36, 37. Waebrania waaminifu wa nyakati za Biblia waliamini nini juu ya maisha ya wakati ujao?

36 Ingawa kukata maneno hivyo huenda kukashangaza hata Wayahudi wengi, ufufuo umekuwa ndio tumaini halisi la waabudu wa Mungu wa kweli kwa maelfu ya miaka. Yapata miaka 3,500 iliyopita, Ayubu mwaminifu mwenye kuteseka alisema juu ya wakati ujao ambapo Mungu angemwinua kutoka Sheoli, au kaburi. (Ayubu 14:14, 15) Nabii Danieli pia alihakikisha kwamba angeinuliwa “mwisho wa siku hizo.”—Danieli 12:2, 12 (13, JP; UV).

37 Hakuna msingi katika Maandiko wa kusema Waebrania hao waaminifu waliamini walikuwa na nafsi isiyoweza kufa ambayo ingeendelea kuishi katika ulimwengu wa baadaye. Kwa wazi wao walikuwa na sababu ya kutosha ya kuamini kwamba Bwana Mwenye Enzi Kuu, ambaye huhesabu na kuongoza nyota za ulimwengu wote mzima, angewakumbuka pia kwenye wakati wa ufufuo. Wao walikuwa wamekuwa waaminifu kwake na kwa jina lake. Yeye angekuwa mwaminifu kwao.—Zaburi 18:26 (25, UV); 147:4; Isaya 25:7, 8; 40:25, 26.

Dini ya Kiyahudi na Jina la Mungu

38. (a) Ni jambo gani limetukia kwa karne nyingi kuhusiana na matumizi ya jina la Mungu? (b) Ni nini msingi wa jina la Mungu?

38 Dini ya Kiyahudi hufundisha kwamba ingawa jina la Mungu limo katika mwandiko, ni takatifu mno kutamkwa.i Matokeo yamekuwa kwamba, kwa miaka zaidi ya 2,000 iliyopita, matamshi sahihi yamepotea. Hata hivyo, huo haukuwa msimamo wa Kiyahudi sikuzote. Karibu miaka 3,500 iliyopita, Mungu alinena na Musa, akisema: “Hivi ndivyo utasema na Waisraeli: BWANA [Kiebrania: יהוה, YHWH], Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu nyinyi: Hili litakuwa jina Langu milele, huu mtajo Wangu kwa umilele wote.” (Kutoka 3:15; Zaburi 135:13) Jina na mtajo huo lilikuwa nini? Kielezi-chini cha Tanakh hutoa taarifa hii: “Jina YHWH (kimapokeo lilisomwa Adonai “BWANA”) hapa lashirikishwa na chanzo hayah ‘kuwa.’” Kwa hiyo, hapa tuna jina takatifu la Mungu, Tetragrammatoni, zile konsonanti nne za Kiebrania YHWH (Yahweh) ambazo katika namna yazo ya Kilatini zimekuja kujulikana katika karne zote kuwa YEHOVA katika Kiswahili.

39. (a) Ni kwa nini jina la kimungu ni la maana? (b) Ni kwa sababu gani Wayahudi waliacha kutamka jina hilo la kimungu?

39 Katika historia yote, Wayahudi sikuzote wametilia mkazo mkubwa juu ya jina la kibinafsi la Mungu, ingawa mkazo juu ya kulitumia umebadilika sana tangu nyakati za kale. Kama ambavyo Dakt. A. Cohen anavyotoa taarifa katika Everyman’s Talmud: “Heshima ya pekee iliambatanishwa na ‘Jina lenye kutokeza sana’ (Shem Hamephorash) la Mwabudiwa ambalo Yeye alikuwa amelifunua kwa watu wa Israeli, yaani, tetragrammatoni, JHVH.” Jina hilo la kimungu liliheshimiwa sana kwa sababu liliwakilisha na kuonyesha utu wenyewe wa Mungu. Ingawaje, Mungu mwenyewe ndiye aliyelitangaza jina lake na kuwaambia waabudu wake walitumie. Hilo lakaziwa na kuonekana kwa jina hilo katika Biblia ya Kiebrania mara 6,828. Hata hivyo, Wayahudi wa kidini, huhisi si staha kutamka jina la kibinafsi la Mungu.j

40. Mamlaka fulani za Kiyahudi zimeeleza nini kuhusu matumizi ya jina hilo la kimungu?

40 Kuhusu katazo la kale la kirabi (si la Kibiblia) la kutotamka jina hilo, A. Marmorstein, rabi mmoja, aliandika katika kitabu chake The Old Rabbinic Doctrine of God: “Kulikuwako wakati ambapo katazo hilo [la kutumia jina la kimungu] halikujulikana hata kidogo kati ya Wayahudi . . . Wala katika Misri, wala katika Ubabuloni, Wayahudi hawakujua au kushika sheria ya kukataza kutumia jina la Mungu, Tetragrammatoni, katika maongezi ya kawaida au salamu. Hata hivyo, kuanzia karne ya tatu K.W.K. mpaka karne ya tatu B.W.K. katazo hilo lilikuwapo nalo lilifuatwa kidogo.” Si kwamba tu matumizi ya jina hilo yaliruhusiwa katika nyakati za mapema bali, kama anavyosema Dakt. Cohen: “Kulikuwako wakati ambapo matumizi ya uhuru na ya wazi ya Jina hilo hata na watu wa kawaida yalihimizwa . . . Imedokezwa kwamba pendekezo hilo lilitegemezwa juu ya tamaa ya kutofautisha Mwisraeli na [asiye Myahudi].”

41. Kulingana na rabi mmoja, ni mavutano gani yaliyotokeza katazo la kutumia jina la Mungu?

41 Basi, ni nini kilichotokeza katazo la kutumia jina la kimungu? Dakt. Marmorstein ajibu hivi: “Upinzani wa Kiyunani [wenye kuvutwa na Ugiriki] juu ya dini ya Wayahudi, uasi-imani wa makuhani na wakuu, ulianzisha na kuimarisha amri ya kutotamka Tetragrammatoni katika Patakatifu [hekalu katika Yerusalemu].” Katika bidii yao ya kupita kiasi ya kuepuka kulichukua jina hilo la kimungu bure, walikomesha kabisa matumizi yalo katika usemi na wakapindua na kutohoa utambulisho huo wa Mungu wa kweli. Chini ya mkazo ulioungana wa upinzani wa kidini na uasi-imani, jina la kimungu liliacha kutumiwa miongoni mwa Wayahudi.

42. Maandishi ya Biblia yaonyesha nini juu ya matumizi ya jina la kimungu?

42 Hata hivyo, kama Dakt. Cohen anavyotoa taarifa hii: “Katika kipindi cha Kibiblia haielekei kulikuwako kizuizi chochote cha kutumia [jina la kimungu] katika uneni wa kila siku.” Mzee wa kale Abrahamu “aliomba dua kwa BWANA kwa kutumia jina.” (Mwanzo 12:8) Waandikaji walio wengi wa Biblia ya Kiebrania walitumia jina hilo kwa uhuru lakini wakiwa na staha mpaka wakati wa kuandikwa kwa Malaki katika karne ya tano K.W.K.—Ruthu 1:8, 9, 17.

43. (a) Ni jambo gani lililo wazi zaidi kuhusu matumizi ya Kiyahudi ya jina hilo la kimungu? (b) Ni nini lililokuwa tokeo moja lisilo la moja kwa moja la Wayahudi kuacha kutumia jina hilo la kimungu?

43 Ni wazi kabisa kwamba Waebrania wa kale walitumia na kulitamka jina la kimungu. Marmorstein akubali hivi kuhusu badiliko lililokuja baadaye: “Kwa maana katika wakati huu, katika nusu ya kwanza ya karne ya tatu [K.W.K.], badiliko kubwa katika matumizi ya jina la Mungu laonekana, ambalo lilitokeza mabadiliko mengi katika elimu ya Kiyahudi ya kitheolojia na kifalsafa, mavutano ya hayo yakiwa yanahisiwa mpaka leo hii.” Moja la matokeo ya kupotea kwa jina hilo ni kwamba wazo la Mungu asiyejulikana lilisaidia kutokeza uwazi wa kitheolojia ambao katika huo fundisho la Utatu la Jumuiya ya Wakristo lilisitawishwa kwa urahisi.k—Kutoka 15:1-3.

44. Ni matokeo gani mengine yaliyosababishwa na kuzuiwa kwa jina hilo la kimungu?

44 Kukataa kutumia jina la kimungu kwapunguza ibada ya Mungu wa kweli. Kama ambavyo mfafanuaji mmoja alivyosema: “Kwa kusikitisha, Mungu anapotajwa kuwa ‘Bwana,‘ usemi huo, ingawa ni sahihi, hauna shauku wala upendezi . . . mtu ahitaji kukumbuka kwamba kwa kutafsiri YHWH au Adonay kuwa ‘Bwana’ mtu huingiza katika vifungu vingi vya Agano la Kale mtajo usio wa wazi, urasmi na umbali ambao ni wa kigeni kabisa kwa maandishi ya awali.” (The Knowldege of God in Ancient Israel) Jinsi inavyosikitisha kuona adhama na jina kuu la Yahweh, au Yehova, likikosekana katika tafsiri nyingi za Biblia na hali laonekana mara maelfu katika maandishi ya awali ya Kiebrania!—Isaya 43:10-12.

Je! Wayahudi Wangali Wakimngojea Mesiya?

45. Kuna msingi gani wa Kibiblia wa kuamini Mesiya?

45 Kuna unabii mwingi katika Maandiko ya Kiebrania ambao kutoka huo Wayahudi miaka zaidi ya 2,000 iliyopita walipata tumaini lao la Kimesiya. Samweli wa Pili 7:11-16 kilionyesha kwamba Mesiya angekuwa wa mlango wa Daudi. Isaya 11:1-10 kilitabiri kwamba angeleta uadilifu na amani kwa ainabinadamu yote. Danieli 9:24-27 kilitoa tarehe za kutokea kwa Mesiya na kukatiliwa mbali kwake katika kifo.

46, 47. (a) Wayahudi walioishi chini ya utawala wa Kiroma walitazamia Mesiya wa aina gani? (b) Ni badiliko gani ambalo limetokea katika matazamio ya Kiyahudi kuhusiana na Mesiya?

46 Kama ambavyo Encyclopaedia Judaica kinavyoeleza, kufikia karne ya kwanza, matazamio ya Kimesiya yalikuwa makubwa. Mesiya alitazamiwa kuwa “mzao wa Daudi mwenye uvutio mkubwa ambaye Wayahudi wa kipindi cha Kiroma waliamini angeinuliwa na Mungu kuvunja kongwa la washenzi na atawale juu ya ufalme uliorudishwa wa Israeli.” Hata hivyo, Mesiya wa kivita ambaye Wayahudi walikuwa wanatazamia hakuonekana.

47 Hata hivyo, kama The New Encyclopædia Britannica kinavyosema, tumaini la Kimesiya lilikuwa la muhimu katika kuunganisha watu wa Kiyahudi pamoja wakati wa taabu zao nyingi: “Bila shaka kwa kadiri kubwa, kuwapo kwa Dini ya Kiyahudi ni kwa sababu ya imani yayo imara katika ahadi ya kimesiya na wakati ujao.” Lakini Dini ya Kiyahudi ya kisasa ilipotokea kati ya karne ya 18 na 19, Wayahudi wengi waliacha kungojea Mesiya kwa kujikalia kitako. Hatimaye, baada ya Machinjo Makubwa yaliyochochewa na Wanazi, wengi walipoteza subira na tumaini lao. Wakaanza kuona ujumbe wa Kimesiya kuwa mzigo na kwa hiyo wakaufasiri upya kuwa enzi mpya ya fanaka na amani. Tangu wakati huo, ingawa kuna wachache walio tofauti, haiwezi kusemwa hata kidogo kwamba Wayahudi kwa ujumla wanangojea mtu aliye Mesiya.

48. Ni maswali gani yanayoweza kutokezwa kwa kufaa juu ya Dini ya Kiyahudi?

48 Badiliko hilo la kuwa dini isiyo ya Kimesiya latokeza maswali mazito. Je! Dini ya Kiyahudi ilikuwa yenye kosa kwa maelfu ya miaka katika kuamini kwamba Mesiya alitazamiwa kuwa mtu fulani? Ni Dini ya Kiyahudi gani itasaidia mtu katika jitihada ya kutafuta Mungu? Je! ni Dini ya Kiyahudi ya kale pamoja na madoido yayo ya falsafa ya Kigiriki? Au je! ni mojawapo ya namna zisizo za Kimesiya za Dini ya Kiyahudi iliyogeuka-geuka wakati wa miaka 200 iliyopita? Au je! kungali kuna njia nyingine ambayo kwa uaminifu na kwa usahihi yahifadhi tumaini la Kimesiya?

49. Ni mwaliko gani unaotolewa kwa Wayahudi wenye mioyo myeupe?

49 Maswali hayo yakiwa akilini, twadokeza kwamba Wayahudi wenye moyo mweupe wachunguze tena habari inayohusu Mesiya kwa kupeleleza madai yanayohusu Yesu wa Nazareti, si kama ambavyo Jumuiya ya Wakristo imemwakilisha, bali kama ambavyo waandikaji Wayahudi wa Maandiko ya Kigiriki wanavyomwakilisha. Kuna tofauti kubwa. Dini za Jumuiya ya Wakristo zimefanya Wayahudi kumkataa Yesu kwa fundisho lazo lisilo la Kibiblia la Utatu, ambalo kwa wazi halikubaliki kwa Myahudi yeyote anayependa fundisho halisi kwamba “BWANA MUNGU WETU, BWANA NI MMOJA” (Kumbukumbu la Torati 6:4, JP) Kwa hiyo, twakualika wewe usome sura inayofuata ukiwa na akili iliyofunguka ili upate kujua Yesu wa Maandiko ya Kigiriki.

[Maelezo ya Chini]

a Kulingana na Mwanzo 5:22-24, New World Translation of the Holy Scriptures—With References, kielezi-chini cha pili juu ya mstari 22.

b Mitajo yote katika sura hii, isipokuwa imetolewa taarifa vingine, ni kutoka Tanakh, A New Translation of the Holy Scriptures ya kisasa (1985), ya wasomi wa The Jewish Publication Society.

c Tarehe za matukio zilizotolewa hapa zategemea maandishi ya Biblia kuwa mamlaka. (Ona kitabu “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa,” kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of N.Y., Inc., Funzo 3, “Kupima Matukio Katika Mkondo wa Wakati.”

d Mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Yoseph ben Mattityahu (Flavio Yosefo) asimulia kwamba Aleksanda alipofika Yerusalemu, Wayahudi walimfungulia malango na kumwonyesha unabii kutoka kitabu cha Danieli ulioandikwa miaka zaidi ya 200 mapema ambao ulieleza waziwazi ushindi mbalimbali wa Aleksanda akiwa ‘Mfalme wa Ugiriki.’—Jewish Antiquities, Kitabu cha 11, Sura ya 8 aya ya 5; Danieli 8:5-8, 21.

e Wakati wa kipindi cha Wamakabayo (Wahasmona, kutoka 165 mpaka 63 K.W.K.), viongozi Wayahudi kama vile John Hirkano hata walilazimisha wongofu wa kadiri kubwa wa kukubali Dini ya Kiyahudi kwa kutumia vita ya kutiisha. Ni jambo la kupendeza kwamba mwanzoni mwa Wakati wa Kawaida, asilimia 10 ya ulimwengu wa Mediterrania ilikuwa ya Kiyahudi. Tarakimu hiyo yaonyesha wazi uvutano wa wongofu wa Kiyahudi.

f Kulingana na The New Encyclopædia Britannica: “Itikadi ya kidini ya utatu wa Kikristo . . . huutenganisha na zile dini mbili nyingine ambazo ni kielelezo cha dini zinazoamini Mungu mmoja [Dini ya Kiyahudi na Uislamu].” Utatu ulisitawishwa na kanisa hata ingawa “Biblia ya Wakristo haitii ndani masisitizo yoyote juu ya Mungu ambayo ni ya kiutatu hasa.”

g Kuongezea mamlaka ya Kibiblia, lilifundishwa kuwa itikadi katika Mishnah (Sanhedrin 10:1) na lilitiwa ndani kama ya mwisho ya kanuni 13 za imani ya Maimonides. Mpaka karne ya 20, kukana ufufuo kulionwa kuwa ni uzushi.

h “Biblia haisemi sisi tuna nafsi. ‘Nefesh’ ni mtu mwenyewe, uhitaji wake wa chakula, ile damu katika mishipa yake, kuwapo kwake.”—Dakt. H. M. Orlinsky wa Hebrew Union College.

i Ona Kutoka 6:3 ambapo katika chapa ya Tanakh ya Biblia Tetragrammatoni ya Kiebrania huonekana katika maandishi ya Kiingereza.

j Encyclopaedia Judaica inasema: “Kuepuka kutamka jina YHWH . . . husababishwa na kuielewa vibaya Amri ya Tatu (Kut. 20:7; Kum. 5:11) kuwa humaanisha ‘Wewe hutalichukua jina la YHWH Mungu wako bure,’ hali kwa halisi humaanisha ‘Wewe hutaapa kwa ubandia kwa jina la YHWH Mungu wako.’”

k George Howard, profesa-mshirika wa dini na Kiebrania kwenye Chuo Kikuu cha Georgia, atoa taarifa hii: “Kwa kadiri wakati ulivyopita, watu hao wawili [Mungu na Kristo] waliletwa kwenye umoja wa karibu hata zaidi hivi kwamba mara nyingi ikawa haiwezekani kutofautisha kati yao. Kwa hiyo yaweza kuwa kwamba kuondolewa kwa Tetragrammatoni kulichangia sehemu kubwa ya mabishano juu ya Kristo na Utatu yaliyotatiza kanisa la karne za mapema. Vyovyote iwavyo, kuondolewa kwa Tetragrammatoni yawezekana kulitokeza mazingira ya kitheolojia yaliyo tofauti na yale yaliyokuwapo wakati wa muhula wa Agano Jipya wa karne ya kwanza.”—Biblical Archaeology Review, Machi 1978.

[Blabu katika ukurasa wa 217]

Wayahudi Wasefardi na Waashikenazi walifanyiza jumuiya mbili

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 211]

Amri Kumi kwa Ajili ya Ibada na Mwenendo

Mamilioni ya watu wamekwisha kusikia juu ya zile Amri Kumi, lakini ni wachache ambao wamepata kuzisoma. Kwa hiyo, hapa twaandika tena sehemu kubwa ya maneno yazo.

◼ “Wewe hutakuwa na miungu mingine zaidi Yangu.

◼ “Wewe hutafanya kwa ajili yako mfano uliochongwa, au ufananisho wowote wa kilicho mbinguni juu, au duniani chini, au katika maji chini ya dunia. Wewe hutaviinamia wala kuvitumikia. . . [Kwenye tarehe hii ya mapema, 1513 K.W.K., amri hiyo ilikuwa maalumu katika kukataza ibada ya sanamu.]

◼ “Wewe hutaapa kibandia kwa jina la BWANA [Kiebrania: יהוה] Mungu wako . . .

◼ “Ikumbuke siku ya sabato na kuitunza takatifu. . . . BWANA alibariki siku ya sabato na kuitakasa.

◼ “Heshimu baba yako na mama yako . . .

◼ “Wewe hutaua kimakusudi.

◼ “Wewe hutafanya uzinzi.

◼ “Wewe hutaiba.

◼ “Wewe hutatolea jirani yako ushahidi wa bandia.

◼ “Wewe hutatamani nyumba ya jirani yako . . . mke . . . mtumwa wa kiume au kike . . . fahali au punda wake, au chochote ambacho ni cha jirani yako.”—Kutoka 20:3-14.

Ijapokuwa ni amri nne za kwanza tu zinazohusiana moja kwa moja na imani na ibada ya kidini, zile amri nyingine zilionyesha ukamatano kati ya mwenendo sahihi na uhusiano unaofaa pamoja na Muumba.

[Picha]

Ijapokuwa sheria hiyo maalumu kutoka kwa Mungu, Israeli waliiga ibada ya ndama ya majirani wao wapagani (Ndama wa dhahabu, Byblos)

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 220, 221]

Maandishi Matakatifu ya Waebrania

Maandishi matakatifu ya Kiebrania yalianza na “Tanakh.” Jina “Tanakh” hutokana na migawanyiko mitatu ya Biblia ya Kiyahudi katika Kiebrania: Torah (Sheria), Nevi’im (Manabii), na Kethuvim (Maandishi), kwa kutumia herufi ya kwanza ya kila kisehemu kufanyiza neno TaNaKh. Vitabu hivi viliandikwa katika Kiebrania na Kiaramu kuanzia karne ya 16 hadi karne ya 5 K.W.K.

Wayahudi huamini kwamba viliandikwa chini ya upulizio tofauti na wa kadiri zenye kupungua. Kwa hiyo, wao huvipanga katika umaana ufuatao:

Torah—vitabu vitano vya Musa, au Pentateuki (kutokana na neno la Kigiriki la “hati-kunjo tano”), Sheria, yenye kutia ndani Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu, na Kumbukumbu la Torati. Hata hivyo, usemi “Torah,” waweza pia kutumiwa kurejezea Biblia ya Kiyahudi yote na pia sheria ya mdomo na Talmud (ona ukurasa ufuatao).

Nevi’im—Manabii, kuanzia Yoshua mpaka manabii wa umaana mkubwa, Isaya, Yeremia, na Ezekieli, na halafu manabii “wa umaana mdogo” 12 kuanzia Hosea mpaka Malaki.

Kethuvim—Maandishi, yanayohusisha vitabu vya kishairi, Zaburi, Mithali, Ayubu, Wimbo Ulio Bora, na Maombolezo. Kuongezea Ruthu, Mhubiri, Esta, Danieli, Ezra, Nehemia, na Mambo ya Nyakati cha Kwanza na cha Pili.

Talmud

Kwa maoni ya Wasio Wayahudi, “Tanakh,” au Biblia ya Kiyahudi, ndiyo ya maana zaidi kati ya maandishi ya Kiyahudi. Hata hivyo, maoni ya Kiyahudi ni tofauti. Wayahudi wengi wangekubaliana na maelezo yaliyotolewa na Adin Steinsaltz, rabi fulani: “Ikiwa Biblia ndiyo jiwe la pembeni la Dini ya Kiyahudi, basi Talmud ndiyo nguzo ya katikati, yenye kuinuka juu ya misingi na kutegemeza jengo zima la kiroho na la kiakili . . . Hakuna maandishi mengine yoyote ambayo yamekuwa na uvutano unaolinganika juu ya maisha ya Kiyahudi ya kinadharia na kihalisi.” (The Essential Talmud) Basi, Talmud ni nini?

Wayahudi wa Orthodox hawaamini tu kwamba Mungu alimpa Musa sheria, au Torah, iliyoandikwa kwenye Mlima Sinai bali pia kwamba Mungu alimfunulia ufafanuzi fulani wa wazi juu ya jinsi ya kutekeleza Sheria hiyo, na kwamba ingepitishwa kwa maneno ya mdomo. Hiyo iliitwa sheria ya mdomo. Kwa hiyo, Talmud ni muhtasari ulioandikwa, ukiwa na maelezo na ufafanuzi wa baadaye, wa sheria hiyo ya mdomo, iliyotungwa na marabi kuanzia karne ya pili W.K. mpaka Enzi za Kati.

Kwa kawaida Talmud hugawanywa katika sehemu mbili kubwa:

Mishnah: Mkusanyo wa maelezo ya kuongezea Sheria ya Kimaandiko, kwa kutegemea ufafanuzi wa marabi wanaoitwa Tannaim (walimu). Iliandikwa katika mwisho-mwisho wa karne ya pili na mapema katika karne ya tatu W.K.

Gemara (awali iliitwa Talmud): Mkusanyo wa maelezo juu ya Mishnah ya marabi wa kipindi cha baadaye (karne za tatu mpaka sita W.K.).

Kuongezea migawanyo hiyo mikubwa miwili, Talmud pia huingiza ndani maelezo juu ya Gemara yaliyofanywa na marabi ndani ya Enzi za Kati. Maarufu kati yao walikuwa ni marabi Rashi (Solomon ben Isaac, 1040-1105), aliyefanya lugha ngumu ya Talmud ikawa yenye kueleweka zaidi, na Rambam (Moses ben Maimon, anayejulikana vizuri zaidi kama Maimonides, 1135-1204), ambaye alipanga upya Talmud kuwa mtungo mfupi (“Mishneh Torah”), kwa njia hiyo akaifanya ieleweke na Wayahudi wote.

[Picha]

Chini, Torah ya kale kutoka kwa linalojulikana kuwa Pango alimozikwa Esta, Iran; kulia, wimbo katika Kiebrania na Kiyidi wa kusifu Mungu wenye msingi wa mistari ya Kimaandiko

[Sanduku katika ukurasa wa 226, 227]

Dini ya Kiyahudi—Dini Yenye Sauti Nyingi

Kuna tofauti kubwa-kubwa kati ya vikundi mbalimbali vya Dini ya Kiyahudi. Kimapokeo, Dini ya Kiyahudi hukazia mazoea ya kidini. Mabishano juu ya mambo hayo, badala ya imani, yamesababisha mvutano mkubwa kati ya Wayahudi na kuongoza kwenye kuundwa kwa vikundi vitatu vikubwa katika Dini ya Kiyahudi.

DINI YA KIYAHUDI YA ORTHODOX—Tawi hili si kwamba tu linakubali kwamba “Tanakh” ya Kiebrania ni Maandiko yaliyopuliziwa bali pia huamini kwamba Musa alipokea sheria ya mdomo kutoka kwa Mungu kwenye Mlima Sinai wakati ule ule alipopokea Sheria iliyoandikwa. Wayahudi wa Orthodox hushikilia sana amri za sheria hizo mbili. Wao huamini kwamba Mesiya angali atatokea na kuingiza Israeli katika enzi bora. Kwa sababu ya tofauti za maoni ndani ya kikundi hicho cha Orthodox, vikundi mbalimbali vimetokea. Kielelezo kimoja ni Hasidim.

Hasidim (Chasidim, kumaanisha “wachaji”)—wao huonwa kuwa wa orthodox (kawaida) kabisa. Ilianzishwa na Israel ben Eliezer, ajulikanaye kuwa Ba‛al Shem Tov (“Bwana wa Jina Jema”), katika kipindi cha katikati ya karne ya 18 kule Ulaya ya Mashariki, wao hufuata fundisho linalokazia muziki na dansi, zinazosababisha shangwe ya kifumbo. Nyingi za imani zao, kutia ndani mtu kuishi katika umbo jingine, zategemea vitabu vya kifumbo vya Kiyahudi vinavyojulikana kuwa Kabbala (Cabala). Leo wanaongozwa na marebe (neno la Kiyidi la kumaanisha “marabi”), au zaddikim, ambao huonwa na wafuasi wao kuwa wanaume walio waadilifu kabisa kabisa au watakatifu.

Hasidim leo hupatikana hasa katika United States na katika Israel. Wao huvaa joho la mtindo wa kipekee wa Ulaya ya Mashariki ya karne ya 18 na 19, sana sana jeusi, ambalo huwafanya waonekane wazi sana hasa katika mazingira ya jiji la kisasa. Leo wamegawanyika katika mafarakano yanayofuata marebe tofauti walio mashuhuri. Kikundi kimoja chenye kutenda ni Walubavitcher, ambao hutafuta waongofu kwa bidii miongoni mwa Wayahudi. Vikundi fulani huamini kwamba ni Mesiya peke yake aliye na haki ya kurudisha Israeli kuwa taifa la Wayahudi na kwa hiyo wanapinga Serikali ya kibinadamu ya Israel.

DINI YA KIYAHUDI YA REFORM (pia huitwa “Ya Uhuru” na “Ya Maendeleo”)—Chama hicho kilianza katika Ulaya ya Magharibi kuelekea mwanzo wa karne ya 19. Chategemea mawazo ya Moses Mendelssohn, Myahudi mwenye akili wa karne ya 18 ambaye aliamini Wayahudi wanapaswa kutwaa utamaduni wa Magharibi badala ya kujitenga kutoka kwa Wasio Wayahudi. Wayahudi wa Reform (badiliko) hukanusha kwamba Torah ilikuwa ukweli uliofunuliwa kimungu. Wao huziona sheria za Kiyahudi juu ya chakula, utakato, na mavazi kuwa kuukuu. Wao huamini wanachoita “enzi ya Kimesiya ya udugu wa ulimwenguni Pote.” Katika miaka ya karibuni wamerudia Dini ya Kiyahudi ya kimapokeo.

DINI YA KIYAHUDI YA CONSERVATIVE—Ilianza katika Ujerumani katika 1845 ikiwa chipukizi la Dini ya Kiyahudi ya Reform, ambayo, ilihisiwa, ilikuwa imekataa mazoea mengi mno ya kimapokeo ya Kiyahudi. Dini ya Kiyahudi ya Conservative (isiyotaka mabadiliko) haikubali kwamba sheria ya mdomo ilipokewa na Musa kutoka kwa Mungu bali hushikilia kwamba marabi, waliotaka kupindua Dini ya Kiyahudi ifaane na enzi mpya, walibuni Torah ya mdomo. Wayahudi wa Conservative hufuata maagizo ya Kibiblia na sheria za Kirabi ikiwa “zinafaana na matakwa ya kisasa ya maisha ya Kiyahudi.” (The Book of Jewish Knowldege) Wao hutumia Kiebrania na Kiingereza katika sherehe zao za kidini na hushikilia kabisa sheria zinazohusu chakula (kashruth). Wanaume na wanawake huruhusiwa kuketi pamoja wakati wa ibada, jambo lisiloruhusiwa na Orthodox.

[Picha]

Kushoto, Wayahudi kwenye Ukuta wa Kilio katika Yerusalemu na, juu, Myahudi akisali, Yerusalemu likiwa upande wa nyuma

[Sanduku katika ukurasa wa 230, 231]

Baadhi ya Misherehekeo na Desturi za Maana

Msingi wa misherehekeo ya Kiyahudi ni Biblia na, kwa ujumla, ama ni misherehekeo ya majira kuhusiana na mavuno tofauti-tofauti au yahusiana na matukio ya kihistoria.

◼ Shabbat (Sabato)—Siku ya saba ya juma la Kiyahudi (kuanzia Ijumaa jua linapotua mpaka Jumamosi jua linapotua) huonwa kuwa ikitakasa juma hilo, na mwadhimisho wa pekee wa siku hiyo ni sehemu ya lazima ya ibada. Wayahudi huhudhuria sinagogi kwa ajili ya kusomwa kwa Torah na sala.—Kutoka 20:8-11.

◼ Yom Kippur—Siku ya Upatanisho, msherehekeo wa kuchukuliwa kwa uzito unaohusisha kufunga na kujichunguza binafsi. Upeo wao ni Siku Kumi za Toba zinazoanza na Rosh Hashanah, Mwaka Mpya wa Kiyahudi, unaoanza Septemba kulingana na kalenda ya maisha ya Kiyahudi.—Mambo ya Walawi 16:29-31; 23:26-32.

◼ Sukkot (juu, kulia)—Msherehekeo wa Vibanda, au Mahema, au Kukusanya. Huadhimisha mavuno na mwisho wa sehemu kubwa ya mwaka wa kilimo. Hufanywa katika Oktoba.—Mambo ya Walawi 23:34-43; Hesabu 29:12-38; Kumbukumbu la Torati 16:13-15.

◼ Hannukkah—Msherehekeo wa Wakfu. Msherehekeo maarufu unaofanywa katika Desemba unaokumbuka kurudisha kwa Wamakabayo uhuru wa Kiyahudi kutoka utawala wa Washami-Wagiriki na kuwekwa wakfu tena kwa hekalu Yerusalemu katika Desemba 165 K.W.K. Kwa kawaida hutofautishwa na kuwashwa kwa mishumaa siku nane.

◼ Purim—Msherehekeo wa Kura. Huadhimishwa mwisho-mwisho wa Februari au mapema Machi, kwa kuadhimisha kukombolewa kwa Wayahudi katika Uajemi wakati wa karne ya tano K.W.K. kutoka kwa Hamani na hila yake ya kuangamiza taifa zima.—Esta 9:20-28.

◼ Pesach—Msherehekeo wa Kupitwa. Ulianzishwa ili kuadhimisha kukombolewa kwa Israeli kutoka utumwa wa Misri (1513 K.W.K.). Ndio mkubwa zaidi na wa kale zaidi kati ya misherehekeo ya Kiyahudi. Hufanywa Nisani 14 (kalenda ya Kiyahudi), kwa kawaida huwa mwisho-mwisho wa Machi au mwanzo wa Aprili. Kila familia ya Kiyahudi hukusanyika ili kushiriki chakula cha Kupitwa, au Sederi. Wakati wa siku saba zinazofuata, hakuna chachu inayoruhusiwa kuliwa. Kipindi hicho huitwa Msherehekeo wa Mikate Isiyotiwa Chachu (Matzot).—Kutoka 12:14-20, 24-27.

Desturi Fulani za Kiyahudi

◼ Tohara—Kwa ajili ya wavulana Wayahudi, ni sherehe ya maana ambayo hufanywa wakati mtoto ana umri wa siku nane. Mara nyingi huitwa Agano la Abrahamu, kwa kuwa tohara ilikuwa ishara ya agano la Mungu pamoja naye. Watu wa kiume wanaoongoka kuwa wa Dini ya Kiyahudi lazima pia watahiriwe—Mwanzo 17:9-14.

◼ Bar Mitzavh (chini)—Sherehe nyingine ya Kiyahudi iliyo ya lazima, ambayo kwa halisi humaanisha “mwana wa amri,” “usemi unaoonyesha kufikia ukomavu wa kidini na wa kisheria na pia pindi ambayo hali hiyo hufikiwa kirasmi na wavulana wakati wa umri wa miaka 13 na siku moja.” Ilikuja kuwa desturi tu ya Kiyahudi katika karne ya 15 W.K.—Encyclopaedia Judaica.

◼ Mezuzah (juu)—Makao ya Kiyahudi kwa kawaida yanatofautika kirahisi kwa sababu ya mezuzah, au kikasha cha hati-kunjo, kwenye upande wa kulia wa mwimo wa mlango anapoingia mtu. Kwa halisi mezuzah ni kipande kidogo cha ngozi ambacho juu yacho yameandikwa maneno yaliyotajwa kutoka Kumbukumbu la Torati 6:4-9 na 11:13-21. Hicho hukunjwa ndani ya kikasha. Ndipo kikasha hicho huangikwa kwenye kila mlango wa kila chumba kinachotumiwa kwa makao.

◼ Yarmulke (kofia ya fuvu la kichwa kwa ajili ya watu wa kiume)—Kulingana na Encyclopaedia Judaica: “Uyahudi wa Orthodox . . . haukuona kufunikwa kichwa, nje na ndani ya sinagogi, kuwa ishara ya kutii pokeo la Kiyahudi.” Kufunikwa kichwa wakati wa ibada hakutajwi popote katika Tanakh, kwa hiyo Talmud hutaja hilo kuwa jambo la kidesturi ya kujichagulia. Wanawake wa Hasidim wa Kiyahudi ama huvaa kifunika-kichwa nyakati zote au hunyoa vichwa vyao na kuvaa nywele bandia.

[Picha katika ukurasa wa 206]

Abramu (Abrahamu), babu ya Wayahudi, alimwabudu Yehova Mungu miaka karibu 4,000 iliyopita

[Picha katika ukurasa wa 208]

Nyota ya Daudi—ishara isiyo ya kibiblia ya Israel na dini ya Kiyahudi

[Picha katika ukurasa wa 215]

Mwandishi Myahudi akinakili maandishi ya Kiebrania

[Picha katika ukurasa wa 222]

Familia ya Wayahudi wa Kihasidimu ikiadhimisha sabato

[Picha katika ukurasa wa 233]

Wayahudi wa kidini wamevaa filakteri, au vikasha vya hati-kunjo ya sala, kwenye mkono na kipaji cha uso

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki