Mathayo
11 Basi Yesu alipokuwa amemaliza kuwapa maagizo wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akafundishe na kuhubiri katika majiji yao.
2 Lakini Yohana, akiwa amekwisha kusikia katika jela juu ya kazi za Kristo, akatuma kupitia wanafunzi wake mwenyewe 3 na kumwambia: “Je, wewe ndiwe Yule Anayekuja, au je, twapaswa kutarajia aliye tofauti?” 4 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Shikeni njia yenu mwende na ripotini kwa Yohana yale mnayosikia na kuona: 5 Vipofu wanaona tena, na vilema wanatembea huku na huku, wenye ukoma wanasafishwa na viziwi wanasikia, na wafu wanafufuliwa, na maskini wanatangaziwa habari njema; 6 na mwenye furaha ni yeye asiyepata sababu ya kukwazika katika mimi.”
7 Hao walipokuwa wameshika njia yao kwenda, Yesu akaanza kuambia umati habari ya Yohana: “Mlitoka kwenda nyikani kuona nini? Tete likitikiswa na upepo? 8 Basi, ni nini mlitoka kwenda kuona? Mwanamume aliyevaa mavazi mororo? Naam, wale wanaovaa mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. 9 Basi, kwa kweli kwa nini mlitoka kwenda? Kuona nabii? Ndiyo, nawaambia nyinyi, na zaidi sana kuliko nabii. 10 Huyu ndiye ambaye kuhusu yeye imeandikwa, ‘Tazama! Mimi mwenyewe ninatuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, ambaye atatayarisha njia yako mbele yako!’ 11 Kwa kweli nawaambia nyinyi watu, Miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake hakujainuliwa mkubwa zaidi kuliko Yohana Mbatizaji; lakini mtu ambaye ni mdogo zaidi katika ufalme wa mbingu ni mkubwa zaidi kuliko yeye. 12 Lakini kutoka siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa ufalme wa mbingu ndio mradi ambao kuelekea huo watu hukaza mwendo, na wale wanaokaza mwendo mbele wanaukamata. 13 Kwa maana wote, Manabii na Sheria, walitoa unabii mpaka Yohana; 14 nanyi mkitaka kukubali hili, Yeye mwenyewe ndiye ‘Eliya ambaye akusudiwa kuja.’ 15 Acheni yeye aliye na masikio asikilize.
16 “Nitalinganisha kizazi hiki na nani? Ni kama watoto wachanga ambao wameketi katika mahali pa masoko ambao hupaaza kilio kwa wachezaji wenzao, 17 wakisema, ‘Tuliwapigia nyinyi filimbi, lakini hamkucheza dansi; tulitoa sauti za kuomboleza, lakini hamkujipiga wenyewe kwa kihoro.’ 18 Kwa kulingana na hilo, Yohana alikuja akiwa hali wala hanywi, na bado watu husema, ‘Ana roho mwovu’; 19 Mwana wa binadamu alikuja akiwa anakula na kunywa, na bado watu husema, ‘Tazama! Mtu aliye mlafi na mwenye tabia ya kunywa divai, rafiki ya wakusanya-kodi na watenda-dhambi.’ Hata hivyo, hekima huthibitishwa kuwa yenye uadilifu kwa kazi zayo.”
20 Ndipo akaanza kuyashutumu majiji ambayo katika hayo nyingi zaidi za kazi zake zenye nguvu zilikuwa zimetendeka, kwa sababu hayakutubu: 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! kwa sababu kama zile kazi zenye nguvu zingalifanyika katika Tiro na Sidoni ambazo zilifanyika katika nyinyi, wangalitubu zamani za kale katika nguo ya gunia na majivu. 22 Kwa sababu hiyo nawaambia nyinyi, Litakuwa jambo lenye kuvumilika zaidi kwa Tiro na Sidoni Siku ya Hukumu kuliko kwenu. 23 Na wewe, Kapernaumu, je, labda utakwezwa hadi mbinguni? Utateremka kuja chini hadi Hadesi; kwa sababu kama zile kazi zenye nguvu zilizofanyika katika wewe zingalifanyika Sodoma, lingalidumu hadi siku hiihii. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia nyinyi watu, Litakuwa jambo lenye kuvumilika zaidi kwa nchi ya Sodoma Siku ya Hukumu kuliko kwenu.”
25 Wakati huo Yesu kwa kujibu akasema: “Nakusifu wewe hadharani, Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa sababu umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye akili na umeyafunua kwa vitoto. 26 Ndiyo, Ee Baba, kwa sababu kufanya hivyo kulikuja kuwa ndiyo njia iliyokubaliwa nawe. 27 Vitu vyote vimekabidhiwa kwangu na Baba yangu, na hakuna yeyote amjuaye Mwana kabisa ila Baba, wala yeyote hamjui Baba kabisa ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia. 28 Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaomenyeka na kulemezwa mizigo, nami hakika nitawaburudisha nyinyi. 29 Chukueni nira yangu juu yenu na mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mwenye tabia-pole na wa hali ya chini moyoni, nanyi mtapata burudisho kwa ajili ya nafsi zenu. 30 Kwa maana nira yangu ni ya fadhili na mzigo wangu ni mwepesi.”