Mathayo
12 Kwenye majira hayo Yesu alienda akipita katikati ya mashamba ya nafaka siku ya sabato. Wanafunzi wake wakaona njaa na kuanza kukwanyua masuke ya nafaka na kula. 2 Kwa kuona hilo Mafarisayo wakamwambia: “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya lisiloruhusika kisheria kufanya siku ya sabato.” 3 Yeye akawaambia: “Je, hamjasoma alilofanya Daudi wakati yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye walipoona njaa? 4 Jinsi alivyoingia ndani ya nyumba ya Mungu nao wakala mikate ya toleo, jambo ambalo halikuruhusika kisheria kwake kula, wala kwa wale pamoja naye, ila kwa makuhani tu? 5 Au, je, hamjasoma katika Sheria kwamba siku za sabato makuhani katika hekalu huitendea sabato kama si takatifu na huendelea kuwa bila hatia? 6 Lakini nawaambia nyinyi kwamba kitu kikubwa zaidi kuliko hekalu kipo hapa. 7 Hata hivyo, kama mngalielewa ambalo hili lamaanisha, ‘Mimi nataka rehema, na si dhabihu,’ msingaliwalaumu wasio na hatia. 8 Kwa maana Mwana wa binadamu ndiye aliye Bwana wa sabato.”
9 Baada ya kuondoka mahali hapo akaenda ndani ya sinagogi lao; 10 na, tazama! mtu mwenye mkono ulionyauka! Kwa hiyo wakamuuliza, “Je, yaruhusika kisheria kuponya siku ya sabato?” ili waweze kupata shtaka dhidi yake. 11 Yeye akawaambia: “Atakuwa ni nani huyo mtu miongoni mwenu aliye na kondoo mmoja na, ikiwa huyo aanguka ndani ya shimo siku ya sabato, hatamshika na kumwinua nje? 12 Kwa kufikiria yote hayo, binadamu ni mwenye thamani zaidi sana kama nini kuliko kondoo! Kwa hiyo yaruhusika kisheria kufanya jambo bora siku ya sabato.” 13 Ndipo akamwambia huyo mtu: “Nyoosha mkono wako.” Naye akaunyoosha, nao ukarudishwa kuwa timamu kama ule mkono mwingine. 14 Lakini Mafarisayo wakatoka kwenda na kufanya shauri dhidi yake ili wapate kumwangamiza. 15 Akiisha kujua hilo, Yesu akaondoka hapo. Wengi pia wakamfuata, naye akawaponya wote, 16 lakini akawaagiza kwa kusisitiza wasimfanye kuwa dhahiri; 17 ili kupate kutimizwa lililosemwa kupitia Isaya nabii, aliyesema:
18 “Tazama! Mtumishi wangu ambaye nilimchagua, mpendwa wangu, ambaye nafsi yangu ilimkubali! Hakika nitaweka roho yangu juu yake, na lililo haki atafanya kuwa wazi kwa mataifa. 19 Hatazoza, wala hatalia kwa sauti kubwa, wala yeyote hatasikia sauti yake katika zile njia pana. 20 Hakuna tete lililochubuliwa ambalo ataliponda, na hakuna utambi wa kitani-ghafi unaofuka moshi atakaouzima, mpaka atakapoipeleka haki kwenye fanikio. 21 Kwa kweli, katika jina lake mataifa yatatumaini.”
22 Ndipo wakamletea mtu aliyepagawa na roho mwovu, aliye kipofu na bubu; naye akamponya, hivi kwamba yule bubu akasema na kuona. 23 Basi, umati wote ukavutwa na hisia na kuanza kusema: “Je, si yaelekea kuwa labda huyu ndiye Mwana wa Daudi?” 24 Waliposikia hilo, Mafarisayo wakasema: “Jamaa huyu hatoi roho waovu ila kupitia Beelzebubi, mtawala wa roho waovu.” 25 Akijua fikira zao, akawaambia: “Kila ufalme uliogawanyika dhidi yao wenyewe huja kwenye ukiwa, na kila jiji au nyumba iliyogawanyika dhidi yayo yenyewe haitasimama. 26 Katika njia hiyohiyo, ikiwa Shetani afukuza Shetani, amekuwa mwenye kugawanyika dhidi yake mwenyewe; basi, ufalme wake utasimamaje? 27 Zaidi ya hayo, ikiwa mimi nafukuza roho waovu kwa njia ya Beelzebubi, ni kwa njia ya nani wana wenu huwafukuza? Hiyo ndiyo sababu wao watakuwa mahakimu wenu. 28 Lakini ikiwa ni kwa njia ya roho ya Mungu kwamba mimi nawatoa roho waovu, ufalme wa Mungu umewapata ghafula nyinyi kwa kweli. 29 Au yeyote awezaje kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kukamata bidhaa zake zenye kuchukulika, isipokuwa kwanza amfunge huyo mtu mwenye nguvu? Na ndipo atakapoipora nyumba yake. 30 Yeye asiyekuwa upande wangu yuko dhidi yangu, naye asiyekusanya pamoja nami hutawanya.
31 “Kwa sababu hiyo mimi nawaambia nyinyi, Kila namna ya dhambi na kufuru watasamehewa watu, lakini kufuru dhidi ya roho hawatasamehewa. 32 Kwa kielelezo, yeyote yule asemaye neno dhidi ya Mwana wa binadamu, atasamehewa; lakini yeyote yule asemaye dhidi ya roho takatifu, hilo hatasamehewa, la, si katika mfumo huu wa mambo wala katika ule utakaokuja.
33 “Ama nyinyi watu ufanyeni mti uwe bora na matunda yao yawe bora ama ufanyeni mti uwe uliooza na matunda yao yawe yaliyooza; kwa maana kwa matunda yao mti hujulikana. 34 Uzao wa nyoka-vipiri, mwawezaje kusema mambo mema, wakati nyinyi ni waovu? Kwa maana kutoka katika wingi wa moyo kinywa husema. 35 Mtu mwema kutoka katika hazina yake njema hupeleka nje mambo mema, lakini mtu mwovu kutoka katika hazina yake mbovu hupeleka nje mambo maovu. 36 Nawaambia nyinyi kwamba kila usemi usio na faida ambao watu husema, watatoa hesabu kuhusu huo Siku ya Hukumu; 37 kwa maana kwa maneno yako wewe utatangazwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
38 Ndipo kwa kumjibu baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakasema: “Mwalimu, twataka kuona ishara kutoka kwako.” 39 Kwa kujibu yeye akawaambia: “Kizazi kiovu na chenye uzinzi chafuliza kutafuta ishara, lakini hakuna ishara kitakayopewa ila ishara ya Yona nabii. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa katika tumbo la samaki mkubwa mno siku tatu mchana na usiku, ndivyo Mwana wa binadamu atakavyokuwa katika moyo wa dunia siku tatu mchana na usiku. 41 Wanaume wa Ninewi watainuka katika hukumu pamoja na kizazi hiki nao watakilaumu; kwa sababu wao walitubu juu ya lile alilohubiri Yona, lakini, tazama! kitu fulani zaidi ya Yona kipo hapa. 42 Malkia wa kusini atainuliwa katika hukumu pamoja na kizazi hiki naye atakilaumu; kwa sababu alikuja kutoka miisho ya dunia kuisikia hekima ya Solomoni, lakini, tazama! kitu fulani zaidi ya Solomoni kipo hapa.
43 “Wakati roho asiye safi amtokapo mtu, hupita katika mahali palipokauka akitafuta mahali pa pumziko, na hapati popote. 44 Ndipo asemapo, ‘Hakika nitarudi kwenye nyumba yangu niliyoihama’; naye awasilipo huikuta haijakaliwa lakini imefagiwa kuwa safi na kurembwa. 45 Ndipo ashikapo njia yake na kwenda kuchukua roho tofauti saba walio waovu zaidi yake mwenyewe, na, baada ya kuingia ndani, wao hukaa humo; na hali za mwisho za mtu huyo huwa mbaya zaidi kuliko zile za kwanza. Hivyo ndivyo itakavyokuwa pia kwa kizazi kiovu hiki.”
46 Alipokuwa bado akisema na umati, tazama! mama yake na ndugu zake wakachukua msimamo nje wakitafuta sana kusema naye. 47 Kwa hiyo mtu fulani akamwambia: “Tazama! Mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wakitafuta sana kusema nawe.” 48 Akimjibu huyo mwenye kumwambia akasema: “Ni nani mama yangu, na ni nani ndugu zangu?” 49 Naye akinyoosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema: “Tazama! Mama yangu na ndugu zangu! 50 Kwa maana yeyote yule afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, yeye huyo ni ndugu yangu, na dada, na mama.”