Mathayo
13 Siku hiyo Yesu, akiisha kuondoka katika ile nyumba, alikuwa ameketi kando ya bahari; 2 na umati mkubwa ukamkusanyikia, hivi kwamba akapanda ndani ya mashua na kuketi, na umati wote ulikuwa umesimama ufuoni. 3 Ndipo akauambia mambo mengi kwa vielezi, akisema: “Tazama! Mpanzi alitoka kwenda kupanda; 4 naye alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu zikaanguka kando ya barabara, na ndege wakaja na kuzila kabisa. 5 Nyingine zikaanguka juu ya mahali penye miamba-miamba ambapo hazikuwa na udongo mwingi, na mara moja zikachipuka kwa sababu ya kutokuwa na kina cha udongo. 6 Lakini jua lilipochomoza zikaunguzwa, na kwa sababu ya kutokuwa na mzizi zikanyauka. 7 Nyingine, pia, zikaanguka katikati ya miiba, na ile miiba ikamea na kuzisonga. 8 Bado nyingine zikaanguka juu ya udongo ulio bora nazo zikaanza kutoa matunda, hii mara mia, ile sitini, ile nyingine thelathini. 9 Acheni yeye aliye na masikio asikilize.”
10 Kwa hiyo wanafunzi wakaja na kumwambia: “Ni kwa nini wewe huwaambia kwa utumizi wa vielezi?” 11 Kwa kujibu akasema: “Nyinyi mmeruhusiwa kuzielewa siri takatifu za ufalme wa mbingu, lakini watu hao hawakuruhusiwa. 12 Kwa maana yeyote aliye nacho, vingi zaidi atapewa naye atafanywa azidi; lakini yeyote asiye nacho, hata kile alicho nacho kitachukuliwa kutoka kwake. 13 Hii ndiyo sababu nawaambia kwa utumizi wa vielezi, kwa sababu, wakitazama, watazama bure, na wakisikia, wasikia bure, wala hawapati maana yake; 14 na kuwaelekea wao unabii wa Isaya unapata utimizo, ambao husema, ‘Kusikia, mtasikia lakini kwa vyovyote hamtapata maana yake; na, kutazama, mtatazama lakini kwa vyovyote hamtaona. 15 Kwa maana moyo wa watu hawa umekuwa usioitikia, na kwa masikio yao wamesikia bila itikio, nao wamefunga macho yao; ili wasipate kuona kamwe kwa macho yao na kusikia kwa masikio yao na kupata maana kwa mioyo yao na kurudi, nami niwaponye.’
16 “Hata hivyo, yenye furaha ni macho yenu kwa sababu hayo hutazama, na masikio yenu kwa sababu hayo husikia. 17 Kwa maana kweli nawaambia nyinyi, Manabii wengi na watu waadilifu walitamani kuyaona mambo mnayoyaona na hawakuyaona, na kuyasikia mambo mnayoyasikia na hawakuyasikia.
18 “Basi, nyinyi sikilizeni kielezi cha mtu aliyepanda. 19 Yeyote asikiapo neno la ufalme lakini haipati maana, yule mwovu huja na kunyakua kile ambacho kimepandwa moyoni mwake; huyo ndiye aliyepandwa kando ya barabara. 20 Kwa habari ya yule aliyepandwa juu ya mahali penye miamba-miamba, huyo ndiye anayelisikia neno na mara moja kulipokea kwa shangwe. 21 Lakini hana mzizi ndani yake mwenyewe bali huendelea kwa wakati fulani, na dhiki au mnyanyaso vikiisha kutokea kwa sababu ya lile neno yeye hukwazika mara moja. 22 Kwa habari ya yule aliyepandwa katikati ya miiba, huyo ndiye anayelisikia neno, lakini hangaiko la mfumo huu wa mambo na nguvu za udanganyifu wa mali hulisonga neno, naye huwa asiyezaa matunda. 23 Kwa habari ya yule aliyepandwa juu ya udongo ulio bora, huyo ndiye anayelisikia neno na kupata maana yalo, ambaye kwa kweli huzaa matunda na kutokeza, huyu mara mia, yule sitini, yule mwingine thelathini.”
24 Kielezi kingine alikiweka mbele yao, akisema: “Ufalme wa mbingu umekuwa kama mtu aliyepanda mbegu bora katika shamba lake. 25 Watu wakiwa wamelala usingizi, adui yake alikuja na kupandilia magugu katikati ya ngano, naye akaondoka. 26 Wakati jani lilipoota na kutokeza matunda, ndipo magugu yalipoonekana pia. 27 Kwa hiyo watumwa wa mwenye nyumba wakaja na kumwambia, ‘Bwana-mkubwa, je, hukupanda mbegu bora katika shamba lako? Jinsi gani, basi, lapata kuwa na magugu?’ 28 Yeye akawaambia, ‘Adui, mtu fulani, alifanya hilo.’ Wakamwambia, ‘Basi, je, wataka sisi tutoke kwenda na kuyakusanya?’ 29 Yeye akasema, ‘La; ili isitukie kuwa, mnapoyakusanya magugu, mwing’oe ngano pamoja nayo. 30 Acheni vyote viwili vikue pamoja mpaka mavuno; na katika majira ya mavuno hakika nitawaambia wavunaji, Kwanza kusanyeni magugu na kuyafunga matita-matita ili kuyachoma kabisa, ndipo nendeni mkusanye ngano ghalani mwangu.’”
31 Kielezi kingine alikiweka mbele yao, akisema: “Ufalme wa mbingu ni kama punje ya haradali, ambayo mtu alichukua na kupanda katika shamba lake; 32 ambayo, kwa kweli, ndiyo mbegu ndogo zaidi sana kati ya zote, lakini wakati imepata kukua ndiyo iwayo kubwa zaidi sana kati ya mboga zote nayo huwa mti, hivi kwamba ndege wa mbinguni huja na kupata makao katikati ya matawi yake.”
33 Kielezi kingine aliwaambia: “Ufalme wa mbingu ni kama chachu, ambayo mwanamke alichukua na kuficha katika vipimo vikubwa vitatu vya unga, mpaka tungamo lote likachachushwa.”
34 Mambo yote hayo Yesu aliyasema kwa umati kwa vielezi. Kwa kweli, bila kielezi hakuwa akisema nao; 35 ili kupate kutimizwa lililosemwa kupitia nabii aliyesema: “Hakika mimi nitafungua kinywa changu kwa vielezi, hakika nitatangaza mambo yaliyofichwa tangu kuwekwa msingi.”
36 Ndipo baada ya kuuruhusu umati uende akaingia ndani ya nyumba. Na wanafunzi wake wakamjia na kusema: “Tueleze kile kielezi cha magugu katika shamba.” 37 Kwa kujibu yeye akasema: “Mpanzi wa mbegu iliyo bora ndiye Mwana wa binadamu; 38 shamba ndio ulimwengu; kwa habari ya mbegu iliyo bora, hao ndio wana wa ufalme; lakini magugu ndio wana wa yule mwovu, 39 na yule adui aliyeyapanda ndiye Ibilisi. Yale mavuno ni umalizio wa mfumo wa mambo, na wavunaji ni malaika. 40 Kwa hiyo, kama vile magugu hukusanywa na kuchomwa kwa moto, ndivyo itakavyokuwa katika umalizio wa mfumo wa mambo. 41 Mwana wa binadamu atatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake vitu vyote ambavyo husababisha kukwazika na watu wanaofanya uasi-sheria, 42 nao watawatupa ndani ya tanuri la moto. Humo ndimo kutoa machozi kwao na kusaga meno yao kutakuwa. 43 Wakati huo waadilifu watang’aa kwa uangavu kama jua katika ufalme wa Baba yao. Acheni yeye aliye na masikio asikilize.
44 “Ufalme wa mbingu ni kama hazina iliyofichwa katika shamba, ambayo mtu aliipata na kuificha; na kwa sababu ya shangwe aliyo nayo yeye aenda na kuuza vitu alivyo navyo na kununua shamba hilo.
45 “Tena ufalme wa mbingu ni kama mfanya-biashara msafiri anayetafuta sana lulu zilizo bora. 46 Akiisha kupata lulu moja ya thamani ya juu, alienda zake na mara hiyo akauza vitu vyote alivyokuwa navyo na kuinunua.
47 “Tena ufalme wa mbingu ni kama wavu wa kukokota ulioshushwa ndani ya bahari na kukusanya samaki wa kila aina. 48 Ulipopata kujaa waliuvuta ufuoni na, wakiketi, wakakusanya walio bora ndani ya vyombo, lakini wasiofaa wakawatupilia mbali. 49 Hivyo ndivyo itakavyokuwa katika umalizio wa mfumo wa mambo: malaika watatoka kwenda na kuwatenga waovu kutoka miongoni mwa waadilifu 50 nao watawatupa ndani ya tanuri la moto. Humo ndimo kutoa machozi kwao na kusaga meno yao kutakuwa.
51 “Je, mlipata maana ya mambo yote haya?” Wakamwambia: “Ndiyo.” 52 Ndipo yeye akawaambia: “Ikiwa ni hivyo, kila mfunzi wa watu wote, afundishwapo kuhusiana na ufalme wa mbingu, ni kama mtu, mwenye nyumba, ambaye hutoa nje ya akiba ya hazina yake vitu vipya na vya zamani.”
53 Sasa Yesu alipokuwa amemaliza vielezi hivi alienda akipita kati ya nchi kutoka hapo. 54 Na baada ya kuja kuingia eneo lake la nyumbani akaanza kuwafundisha katika sinagogi lao, hivi kwamba wakastaajabu na kusema: “Mtu huyu alipata wapi hekima hii na kazi hizi zenye nguvu? 55 Je, huyu si mwana wa yule seremala? Je, mama yake haitwi Maria, na ndugu zake Yakobo na Yosefu na Simoni na Yudasi? 56 Na dada zake, je, hawapo wote pamoja nasi? Basi, ni wapi mtu huyu alikopata mambo yote haya?” 57 Kwa hiyo wakaanza kukwazika juu yake. Lakini Yesu akawaambia: “Nabii hakosi kuheshimiwa ila katika eneo lake la nyumbani na katika nyumba yake mwenyewe.” 58 Naye hakufanya kazi nyingi zenye nguvu huko kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.