Mathayo
22 Kwa kujibu zaidi Yesu akawaambia tena kwa vielezi, akisema: 2 “Ufalme wa mbingu umekuwa kama mtu, mfalme, aliyefanya karamu ya ndoa kwa ajili ya mwana wake. 3 Naye akatuma watumwa wake kuita wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa, lakini hawakutaka kuja. 4 Tena akatuma watumwa wengine, akisema, ‘Waambie wale walioalikwa: “Tazama! Nimetayarisha mlo-mkuu wangu, mafahali wangu na wanyama waliononeshwa wamechinjwa, na vitu vyote viko tayari. Njoni kwenye karamu ya ndoa.”’ 5 Lakini bila kujali wakaenda zao, mmoja kwenye shamba lake mwenyewe, mwingine kwenye shughuli yake ya kibiashara; 6 lakini wale wengine, wakiwashika watumwa wake, wakawatenda ufidhuli na kuwaua.
7 “Lakini mfalme akawa na hasira ya kisasi, akatuma majeshi yake na kuangamiza wauaji-kimakusudi hao na kuchoma jiji lao. 8 Ndipo akawaambia watumwa wake, ‘Karamu ya ndoa kwa kweli iko tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. 9 Kwa hiyo nendeni kwenye barabara zenye kuelekea nje ya jiji, na yeyote mmkutaye mwalikeni kwenye karamu ya ndoa.’ 10 Basi watumwa hao wakatoka kwenda kwenye barabara na kukusanya pamoja wote waliowakuta, waovu na wema pia; na chumba cha sherehe za arusi kikajazwa wale wenye kuegama kwenye meza.
11 “Mfalme alipoingia kuwakagua wageni-waalikwa aliona mara hiyo hapo mtu asiyevishwa vazi la ndoa. 12 Kwa hiyo akamwambia, ‘Jamaa, uliingiaje humu ukiwa hujavaa vazi la ndoa?’ Akafanywa kuwa bila la kusema. 13 Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu na kumtupa ndani ya giza kule nje. Huko ndiko kutoa kwake machozi na kusaga meno yake kutakuwa.’
14 “Kwa maana kuna wengi walioalikwa, lakini wachache waliochaguliwa.”
15 Ndipo Mafarisayo wakashika njia yao kwenda na kufanya shauri pamoja kusudi wamtege katika usemi wake. 16 Basi wakatuma wanafunzi wao kwake, pamoja na wafuasi wa chama cha Herode, wakisema: “Mwalimu, twajua wewe ni mwenye ukweli nawe hufundisha njia ya Mungu katika kweli, nawe hujali yeyote, kwa maana wewe hutazami kuonekana kwa mtu kwa nje. 17 Kwa hiyo, tuambie, Wewe wafikiri nini? Je, yaruhusika kisheria kumlipa Kaisari kodi ya kichwa au la?” 18 Lakini Yesu, akijua uovu wao, akasema: “Kwa nini mwanitia kwenye jaribu, wanafiki? 19 Nionyesheni sarafu ya kodi ya kichwa.” Wakamletea dinari. 20 Naye akawaambia: “Sanamu na mwandiko huu ni wa nani?” 21 Wakasema: “Wa Kaisari.” Ndipo akawaambia: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini mlipeni Mungu vitu vya Mungu.” 22 Basi, waliposikia hilo, walistaajabu, nao wakimwacha wakaenda zao.
23 Siku hiyo Masadukayo, wasemao hakuna ufufuo, wakamjia na kumuuliza: 24 “Mwalimu, Musa alisema, ‘Ikiwa mtu yeyote afa bila kuwa na watoto, ndugu yake lazima amwoe mke wake na kumwinulia ndugu yake uzao.’ 25 Basi kulikuwa na ndugu saba pamoja nasi; naye wa kwanza akaoa na kufa, na, bila kuwa na uzao, akaachia ndugu yake mke wake. 26 Ilienda kwa njia ileile pia na yule wa pili na yule wa tatu, mpaka wote saba. 27 Mwisho wa wote yule mwanamke akafa. 28 Kwa sababu hiyo, katika ufufuo, yeye atakuwa mke wa yupi kati ya hao saba? Kwa maana wote walimpata.”
29 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Mwakosea, kwa sababu hamjui wala Maandiko wala nguvu ya Mungu; 30 kwa maana katika ufufuo wala wanaume hawaoi wala wanawake hawaozwi, bali wao ni kama malaika mbinguni. 31 Kwa habari ya ufufuo wa wafu, je, hamkusoma mliloambiwa na Mungu, akisema, 32 ‘Mimi ndiye Mungu wa Abrahamu na ndiye Mungu wa Isaka na ndiye Mungu wa Yakobo’? Yeye ndiye Mungu, si wa wafu, bali wa walio hai.” 33 Uliposikia hilo, umati ulistaajabishwa na fundisho lake.
34 Baada ya Mafarisayo kusikia kwamba alikuwa amewanyamazisha kimya Masadukayo, walikuja pamoja katika kikundi kimoja. 35 Na mmoja wao, mwenye ujuzi mwingi katika Sheria, akauliza, akimjaribu: 36 “Mwalimu, ni ipi iliyo amri kubwa zaidi sana katika ile Sheria?” 37 Akamwambia: “‘Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote.’ 38 Hii ndiyo amri kubwa zaidi sana na ya kwanza. 39 Ya pili, kama hiyo, ni hii, ‘Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.’ 40 Juu ya amri mbili hizi Sheria yote yaning’inia, na Manabii.”
41 Sasa Mafarisayo walipokuwa wamekusanyika pamoja Yesu akawauliza: 42 “Nyinyi mwafikiri nini juu ya Kristo? Yeye ni mwana wa nani?” Wakamwambia: “Wa Daudi.” 43 Akawaambia: “Basi, ni jinsi gani, kwamba Daudi kwa upulizio amwita yeye ‘Bwana,’ akisema, 44 ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume mpaka niwekapo maadui wako chini ya miguu yako”’? 45 Kwa hiyo, ikiwa Daudi humwita yeye ‘Bwana,’ ni jinsi gani yeye ni mwana wake?” 46 Na hakuna mtu aliyeweza kumwambia hata neno moja kwa kumjibu, wala tangu siku hiyo na kuendelea hakuthubutu yeyote kumuuliza swali zaidi tena.