Mathayo
21 Basi, walipokaribia Yerusalemu na kuwasili Bethfage katika Mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu akatuma wanafunzi wawili, 2 akiwaambia: “Shikeni njia mwende mwingie katika kijiji kilicho karibu yenu, nanyi mara moja mtakuta punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni na kuwaleta kwangu. 3 Na ikiwa mtu fulani awaambia jambo lolote, lazima mseme, ‘Bwana awahitaji.’ Ndipo atawatuma mara.”
4 Kwa kweli hilo lilitukia ili kupate kutimizwa lililosemwa kupitia nabii, akisema: 5 “Mwambieni binti wa Zayoni, ‘Tazama! Mfalme wako anakuja kwako, mwenye tabia-pole, na amepanda juu ya punda, ndiyo, juu ya mwana-punda, uzao wa hayawani mchukua-mizigo yenye kulemea.’”
6 Kwa hiyo wanafunzi wakashika njia yao kwenda wakafanya kama vile Yesu alivyowaagiza. 7 Nao wakamleta huyo punda na mwana-punda wake, nao wakaweka juu ya hao mavazi yao ya nje, naye akajiketisha mwenyewe juu yayo. 8 Walio wengi zaidi katika umati wakatandaza mavazi yao ya nje barabarani, huku wengine wakianza kukata matawi kutoka kwenye miti na kuyatandaza barabarani. 9 Kwa habari ya ule umati, wale waliokuwa wakienda mbele yake na wale waliokuwa wakifuata wakafuliza kupaaza kilio: “Okoa Mwana wa Daudi, twasihi! Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova! Mwokoe, twasihi, katika mahali palipo juu!”
10 Basi alipoingia Yerusalemu, jiji lote likawekwa katika msukosuko, wakisema: “Ni nani huyu?” 11 Umati ukafuliza kusema: “Huyu ndiye nabii Yesu, kutoka Nazareti ya Galilaya!”
12 Na Yesu akaingia katika hekalu na kuwafukuza nje wale wote waliokuwa wakiuza na kununua katika hekalu, na kuzipindua meza za wabadili-fedha na mabenchi ya hao waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Naye akawaambia: “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini nyinyi mnaifanya pango la wapokonyaji.” 14 Pia, vipofu na vilema wakaja kwake katika hekalu, naye akawaponya.
15 Makuhani wakuu na waandishi walipoyaona mambo ya kustaajabisha aliyofanya na wale wavulana waliokuwa wakipaaza kilio katika hekalu na kusema: “Okoa Mwana wa Daudi, twasihi!” wakawa wenye kughadhibika 16 na kumwambia: “Je, wasikia yale wanayosema hawa?” Yesu akawaambia: “Ndiyo. Je, nyinyi hamkusoma kamwe hili, ‘Kutoka kinywani mwa vitoto na watoto wanyonyao umetoa sifa’?” 17 Naye akiwaacha nyuma akaenda nje ya jiji hadi Bethania na kupisha usiku huko.
18 Alipokuwa akirudi kwenye jiji mapema asubuhi, aliona njaa. 19 Naye akaona mara hiyo mtini kando ya barabara na kuuendea, lakini hakukuta kitu juu ya huo ila majani tu, naye akauambia: “Acha matunda yasitoke kwako tena kamwe milele.” Na huo mtini ukanyauka mara hiyo. 20 Lakini wanafunzi walipoona hilo, walistaajabu, wakisema: “Ni jinsi gani mtini ukanyauka mara hiyo?” 21 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Mkiwa tu na imani na msitie shaka, si kwamba tu mtafanya nililofanya kwa huo mtini, bali pia mkiambia mlima huu, ‘Inuliwa na utupwe ndani ya bahari,’ litatukia. 22 Na mambo yote mwombayo katika sala, mkiwa na imani, mtapokea.”
23 Basi baada ya yeye kwenda ndani ya hekalu, makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu wakamjia alipokuwa akifundisha nao wakasema: “Ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya? Na ni nani aliyekupa wewe mamlaka hii?” 24 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Hakika, mimi pia, nitawauliza nyinyi jambo moja. Mkiniambia hilo, hakika mimi pia nitawaambia nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya: 25 Ubatizo wa Yohana, ulikuwa wa kutoka chanzo gani? Kutoka mbinguni au kutoka kwa wanadamu?” Lakini wakaanza kujadiliana kwa kutoa sababu miongoni mwao wenyewe, wakisema: “Tukisema, ‘Kutoka mbinguni,’ atatuambia, ‘Basi, kwa nini hamkumwamini?’ 26 Ingawa hivyo, tukisema, ‘Kutoka kwa wanadamu,’ tunao umati kuuhofu, kwa maana wao wote wamchukua Yohana kuwa nabii.” 27 Kwa hiyo kwa kumjibu Yesu wakasema: “Hatujui.” Yeye, naye, akawaambia: “Wala mimi siwaambii nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.
28 “Nyinyi mwafikiri nini? Mtu alikuwa na watoto wawili. Akimwendea wa kwanza, akasema, ‘Mtoto, nenda kafanye kazi leo katika shamba la mizabibu.’ 29 Kwa kujibu, huyu akasema, ‘Hakika nitakwenda, bwana,’ lakini hakutoka aende. 30 Akimkaribia wa pili, akasema lilelile. Kwa kujibu, huyu akasema, ‘Hakika sitakwenda.’ Baadaye alihisi majuto na kutoka akaenda. 31 Ni yupi wa hao wawili aliyefanya mapenzi ya baba yake?” Wakasema: “Huyo wa mwisho.” Yesu akawaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba wakusanya-kodi na makahaba wanaenda mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. 32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu katika njia ya uadilifu, lakini hamkumwamini. Hata hivyo, wakusanya-kodi na makahaba walimwamini, nanyi, ijapokuwa mliona hilo, hamkuhisi majuto baadaye ili kumwamini.
33 “Sikieni kielezi kingine: Kulikuwa na mtu, mwenye nyumba, aliyepanda shamba la mizabibu na kuweka ua kulizunguka naye akachimba sindikio la divai katika hilo akasimamisha mnara, na kulikodisha kwa walimaji, na kusafiri nchi ya nje. 34 Majira ya matunda yalipowadia, alituma watumwa wake kwa walimaji wakapate matunda yake. 35 Hata hivyo, walimaji wakachukua watumwa wake, na mmoja wakampiga sana, mwingine wakamuua, mwingine wakampiga kwa mawe. 36 Tena akatuma watumwa wengine, zaidi ya wale wa kwanza, lakini wakawafanya lilelile. 37 Mwishowe akatuma mwana wake kwao, akisema, ‘Watamstahi mwana wangu.’ 38 Walipomwona mwana walimaji wakasema miongoni mwao wenyewe, ‘Huyu ndiye mrithi; njoni, acheni tumuue na kupata urithi wake!’ 39 Kwa hiyo wakamchukua na kumtupa nje ya shamba la mizabibu na kumuua. 40 Basi, mwenye kumiliki shamba la mizabibu ajapo, atawafanya nini walimaji hao?” 41 Wakamwambia: “Kwa sababu wao ni waovu, ataleta uharibifu mwovu juu yao na kukodisha shamba la mizabibu kwa walimaji wengine, ambao watamtolea yeye matunda yakiwa yamewadia wakati wayo.”
42 Yesu akawaambia: “Je, hamkusoma kamwe katika Maandiko, ‘Jiwe walilolikataa wajenzi ndilo limekuwa jiwe la pembeni lililo kuu. Kutoka kwa Yehova hilo limekuja kuwa, nalo ni la kustaajabisha machoni petu’? 43 Hiyo ndiyo sababu nawaambia nyinyi, Ufalme wa Mungu utachukuliwa kutoka kwenu na kupewa kwa taifa lenye kutokeza matunda yao. 44 Pia, mtu mwenye kuanguka juu ya jiwe hilo atavunjwa-vunjwa. Kwa habari ya yeyote ambaye laanguka juu yake, litamponda tikitiki.”
45 Basi makuhani wakuu na Mafarisayo walipokuwa wamesikia vielezi vyake, wakajua kwamba alikuwa akisema juu yao. 46 Lakini, ijapokuwa walikuwa wakitafuta kumkamata, walihofu ule umati, kwa sababu ulimchukua yeye kuwa nabii.