Mathayo
20 “Kwa maana ufalme wa mbingu ni kama mtu, mwenye nyumba, aliyetoka kwenda mapema asubuhi ili kuajiri wafanyakazi kwa ajili ya shamba lake la mizabibu. 2 Alipokuwa amepatana na hao wafanyakazi juu ya dinari moja kwa siku, aliwatuma katika shamba lake la mizabibu. 3 Akitoka kwenda pia karibu saa ya tatu, aliona wengine wasioajiriwa kazi wamesimama mahali pa soko; 4 akawaambia hao, ‘Nyinyi pia, nendeni katika shamba la mizabibu, na lolote lile lililo haki hakika nitawapa nyinyi.’ 5 Kwa hiyo wakaenda zao. Tena akatoka kwenda karibu na saa ya sita na saa ya tisa na kufanya hivyohivyo. 6 Mwishowe, karibu na saa ya kumi na moja akatoka kwenda na kukuta wengine wamesimama, naye akawaambia, ‘Kwa nini mmekuwa mkisimama hapa mchana wote bila kuajiriwa kazi?’ 7 Wakamwambia, ‘Kwa sababu hakuna mtu ambaye ametuajiri sisi.’ Akawaambia, ‘Nyinyi pia nendeni katika shamba la mizabibu.’
8 “Ilipokuwa jioni, bwana-mkubwa wa shamba la mizabibu akamwambia mtu wake mwenye kusimamia, ‘Waite wafanyakazi na kuwalipa mshahara wao, ukianza na yule wa mwisho mpaka yule wa kwanza.’ 9 Wakati wale watu wa saa ya kumi na moja walipokuja, wakapokea kila mmoja dinari moja. 10 Kwa hiyo, wale wa kwanza walipokuja, walikata kauli wangepokea zaidi; lakini wao pia wakapokea malipo kwa kiasi cha dinari moja. 11 Walipoipokea wakaanza kunung’unika dhidi ya mwenye nyumba 12 na kusema, ‘Hawa wa mwisho walitumia saa moja katika kazi; na bado uliwafanya sawa na sisi tuliochukua ule mzigo wenye kulemea wa mchana na lile joto lenye kuchoma!’ 13 Lakini yeye kwa kumjibu mmoja wao akasema, ‘Jamaa, sikutendi kosa. Ulipatana nami juu ya dinari moja, sivyo? 14 Chukua kilicho chako uende. Nataka kumpa wa mwisho huyu kilekile kama wewe. 15 Je, hairuhusiki kisheria mimi kufanya kile nitakacho na vitu vyangu mwenyewe? Au je, jicho lako ni ovu kwa sababu mimi ni mwema?’ 16 Katika njia hiyo walio wa mwisho watakuwa wa kwanza, na walio wa kwanza wa mwisho.”
17 Akiwa sasa karibu kupanda kwenda Yerusalemu, Yesu alichukua wale wanafunzi kumi na wawili kwa faragha na kuwaambia wakiwa barabarani: 18 “Tazameni! Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa binadamu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waandishi, nao watamhukumia adhabu ya kifo, 19 na watamkabidhi kwa watu wa mataifa wamfanyie ucheshi na kumpiga mijeledi na kumtundika mtini, na siku ya tatu atafufuliwa.”
20 Ndipo mama ya wana wa Zebedayo akamkaribia akiwa pamoja na wana wake, akimsujudia na kuomba kitu fulani kutoka kwake. 21 Yeye akamwambia: “Wataka nini?” Akamwambia: “Toa agizo ili wana wangu wawili hawa wapate kuketi, mmoja kwenye mkono wako wa kuume na mmoja kwenye mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.” 22 Yesu akasema kwa kujibu: “Nyinyi watu hamjui ni nini mnachoomba. Je, mwaweza kukinywa kikombe ambacho mimi niko karibu kunywa?” Wakamwambia: “Twaweza.” 23 Akawaambia: “Kwa kweli mtakunywa kikombe changu, lakini huku kuketi kwenye mkono wangu wa kuume na kwenye mkono wangu wa kushoto si kwangu mimi kutoa, bali ni kwa wale ambao kwa ajili yao kumetayarishwa na Baba yangu.”
24 Wale wengine kumi waliposikia juu ya hilo, wakawa wenye kughadhibikia hao ndugu wawili. 25 Lakini Yesu, akiwaita kwake, akasema: “Mwajua kwamba watawala wa mataifa hupiga ubwana juu yao na watu wakubwa hutumia mamlaka juu yao. 26 Hivyo sivyo ilivyo miongoni mwenu; bali yeyote yule atakaye kuwa mkubwa miongoni mwenu lazima awe mhudumu wenu, 27 na yeyote yule atakaye kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima awe mtumwa wenu. 28 Kama vile Mwana wa binadamu alivyokuja, si kuhudumiwa, bali kuhudumu na kutoa nafsi yake kuwa fidia katika kubadilishana kwa ajili ya wengi.”
29 Sasa walipokuwa wakienda kutoka Yeriko umati mkubwa ulimfuata. 30 Na, tazama! wanaume wawili vipofu wakiwa wameketi kando ya barabara, waliposikia kwamba Yesu anapitia hapo, wakapaaza sauti, wakisema: “Bwana, uwe na rehema juu yetu, Mwana wa Daudi!” 31 Lakini umati ukawaambia kwa kusisitiza wafulize kukaa kimya; na bado wao wakalia kwa sauti kubwa hata zaidi, wakisema: “Bwana, uwe na rehema juu yetu, Mwana wa Daudi!” 32 Kwa hiyo Yesu akasimama, akawaita na kusema: “Mwataka niwafanyie nini?” 33 Wakamwambia: “Bwana, acha macho yetu yafunguliwe.” 34 Akasukumwa na sikitiko, Yesu akagusa macho yao, na mara wakapata kuona, nao wakamfuata.