Mathayo
23 Ndipo Yesu akasema na umati na wanafunzi wake, akisema: 2 “Waandishi na Mafarisayo wamejiketisha wenyewe katika kiti cha Musa. 3 Kwa hiyo mambo yote wawaambiayo nyinyi, yafanyeni na kuyashika, lakini msifanye kulingana na vitendo vyao, kwa maana wao husema lakini hawafanyi. 4 Wao hufunga mizigo mizito na kuiweka juu ya mabega ya watu, lakini wao wenyewe hawataki kuisogeza kwa kidole chao. 5 Kazi zote wazifanyazo wao huzifanya ili watazamwe na watu; kwa maana wao hupanua vibweta [vyenye maandiko] ambavyo wao huvaa kama ulinzi, na kuongeza ukubwa wa pindo zenye matamvua za mavazi yao. 6 Wao hupendezwa na mahali penye kutokeza zaidi sana kwenye milo ya jioni na viti vya mbele katika masinagogi, 7 na salamu katika mahali pa masoko na kuitwa Rabi na watu. 8 Lakini nyinyi, msiitwe Rabi, kwa maana mmoja ni mwalimu wenu, lakini nyinyi nyote ni akina ndugu. 9 Zaidi ya hayo, msiite yeyote baba yenu duniani, kwa maana mmoja ni Baba yenu, Aliye wa kimbingu. 10 Wala msiitwe ‘viongozi,’ kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, Kristo. 11 Lakini aliye mkubwa zaidi sana miongoni mwenu lazima awe mhudumu wenu. 12 Yeyote yule ajikwezaye mwenyewe atanyenyekezwa, na yeyote yule ajinyenyekezaye mwenyewe atakwezwa.
13 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mwafunga ufalme wa mbingu mbele ya watu; kwa maana nyinyi wenyewe hamwingii, wala hamruhusu wale wenye kushika njia ya kuingia waingie. 14 ——
15 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mwavuka bahari na nchi kavu kufanya mgeuzwa-imani mmoja, na awapo mmoja nyinyi humfanya mwana-Gehena mara mbili zaidi kuliko nyinyi wenyewe.
16 “Ole wenu nyinyi, viongozi vipofu, msemao, ‘Ikiwa yeyote aapa kwa hekalu, si kitu; lakini ikiwa yeyote aapa kwa dhahabu ya hekalu, yeye yuko chini ya wajibu.’ 17 Wapumbavu na vipofu! Kwa kweli, ni kipi kilicho kikubwa zaidi, dhahabu au hekalu ambalo limeitakasa dhahabu? 18 Pia, ‘Ikiwa yeyote aapa kwa madhabahu, si kitu; lakini ikiwa yeyote aapa kwa zawadi iliyo juu yayo, yeye yuko chini ya wajibu.’ 19 Vipofu! Kwa kweli, ni kipi kilicho kikubwa zaidi, zawadi au madhabahu ambayo huitakasa zawadi? 20 Kwa hiyo yeye aapaye kwa madhabahu anaapa kwa hiyo na kwa vitu vyote vilivyo juu yayo; 21 naye aapaye kwa hekalu anaapa kwa hilo na kwa yeye anayekaa ndani yalo; 22 naye aapaye kwa mbingu anaapa kwa kiti cha ufalme cha Mungu na kwa yeye anayeketi juu yacho.
23 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu nyinyi huitoa sehemu ya kumi ya mnanaa na dili na jira, lakini mmepuuza mambo yenye uzito zaidi ya Sheria, yaani, haki na rehema na uaminifu. Ilikuwa lazima mambo haya kuyafanya, na bado kutopuuza yale mambo mengine. 24 Viongozi vipofu, ambao humchuja inzi mwenye kuuma lakini humgugumia ngamia!
25 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu nyinyi husafisha upande wa nje wa kikombe na wa sahani, lakini upande wa ndani vimejaa vitu vilivyoporwa na upitaji-kiasi. 26 Farisayo kipofu, kwanza safisha upande wa ndani wa kikombe na wa sahani, ili upande wayo wa nje upate kuwa safi pia.
27 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mwafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo kwa nje yaonekana kwa kweli kuwa mazuri lakini ndani yamejaa mifupa ya binadamu wafu na kila namna ya ukosefu wa usafi. 28 Katika njia hiyo nyinyi pia, kwa kweli, mwaonekana kwa nje kuwa waadilifu kwa watu, lakini ndani mmejaa unafiki na uasi-sheria.
29 “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu nyinyi mwajenga makaburi ya manabii na kuyarembesha makaburi ya ukumbusho ya waadilifu, 30 nanyi mwasema, ‘Kama tungekuwa katika siku za baba zetu wa zamani, hatungekuwa washiriki pamoja nao katika damu ya manabii.’ 31 Kwa hiyo mnatoa ushahidi dhidi yenu wenyewe kwamba nyinyi ni wana wa wale waliowaua manabii kimakusudi. 32 Hivyo, basi, jalizeni kipimo cha baba zenu wa zamani.
33 “Nyoka, uzao wa nyoka-vipiri, nyinyi mtaikimbiaje hukumu ya Gehena? 34 Kwa sababu hiyo, hapa ninatuma kwenu manabii na watu wenye hekima na wafunzi wa watu wote. Baadhi yao mtawaua na kuwatundika mtini, na baadhi yao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwanyanyasa kutoka jiji hadi jiji; 35 ili kupate kuja juu yenu damu yote ya uadilifu iliyomwagwa juu ya dunia, tangu damu ya Abeli mwadilifu mpaka damu ya Zekaria mwana wa Barakia, ambaye mlimuua kimakusudi kati ya patakatifu na madhabahu. 36 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Mambo yote haya yatakuja juu ya kizazi hiki.
37 “Yerusalemu, Yerusalemu, muuaji wa manabii na mpigaji kwa mawe wale waliotumwa kwake, —ni mara nyingi kadiri gani nilitaka kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku hukusanya vifaranga vyake pamoja chini ya mabawa yake! Lakini nyinyi watu hamkutaka hilo. 38 Tazameni! Nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. 39 Kwa maana nawaambia nyinyi, Hamtaniona mimi kwa vyovyote tangu sasa mpaka msemapo, ‘Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova!’”