Mathayo
27 Ilipokuwa imekuwa asubuhi, makuhani wakuu wote na wanaume wazee wa watu wakafanya ushauriano dhidi ya Yesu ili kufanya auawe. 2 Na, baada ya kumfunga, wakamwongoza na kumkabidhi kwa Pilato gavana.
3 Ndipo Yudasi, aliyemsaliti, alipoona kuwa amekwisha kuhukumiwa adhabu, akahisi majuto akavirudisha vile vipande thelathini vya fedha kwa makuhani wakuu na wanaume wazee, 4 akisema: “Nilifanya dhambi niliposaliti damu yenye uadilifu.” Wakasema: “Hilo ni nini kwetu? Ni lazima uone hilo!” 5 Kwa hiyo akatupa vile vipande vya fedha ndani ya hekalu akaondoka, akaenda zake akajinyonga mwenyewe. 6 Lakini makuhani wakuu wakachukua hivyo vipande vya fedha na kusema: “Hairuhusiki kisheria kuvitumbukiza ndani ya hazina takatifu, kwa sababu hivyo ni bei ya damu.” 7 Baada ya kushauriana pamoja, wakanunua kwavyo shamba la mfinyanzi ili kuzikia wageni. 8 Kwa hiyo shamba hilo limeitwa “Shamba la Damu” hadi siku hiihii. 9 Ndipo lililosemwa kupitia Yeremia nabii likatimizwa, akisema: “Nao walichukua vile vipande thelathini vya fedha, ambayo ni bei juu ya mtu aliyepigwa bei, ambaye juu yake baadhi ya wana wa Israeli walipiga bei, 10 nao wakavitoa kwa ajili ya shamba la mfinyanzi, kulingana na lile ambalo Yehova alikuwa ameniamuru mimi.”
11 Yesu sasa akasimama mbele ya gavana; naye gavana akamtokezea swali hili: “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu: “Wewe mwenyewe wasema hilo.” 12 Lakini, yeye alipokuwa akishtakiwa na makuhani wakuu na wanaume wazee, hakutoa jibu. 13 Ndipo Pilato akamwambia: “Je, husikii ni mambo mangapi wanashuhudia dhidi yako?” 14 Lakini hakumjibu, la, hata neno moja, hivi kwamba gavana akastaajabu sana.
15 Sasa kutoka msherehekeo hadi msherehekeo ilikuwa desturi ya gavana kufungulia umati mfungwa mmoja, ambaye walimtaka. 16 Wakati huohuo walikuwa wakishika mfungwa mwenye sifa mbaya aitwaye Baraba. 17 Kwa sababu hiyo walipokuwa wamekusanywa pamoja Pilato akawaambia: “Ni yupi mwataka niwafungulie, Baraba au Yesu aitwaye kwa kawaida Kristo?” 18 Kwa maana alijua kwamba ni kutokana na husuda walikuwa wamemkabidhi. 19 Zaidi ya hayo, alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mke wake akampelekea habari, akisema: “Usijihusishe kwa vyovyote na mtu huyo mwadilifu, kwa maana niliteseka sana leo katika ndoto kwa sababu yake.” 20 Lakini makuhani wakuu na wanaume wazee wakashawishi umati kuomba wapewe Baraba, lakini kufanya Yesu aangamizwe. 21 Sasa kwa kujibu gavana akawaambia: “Ni yupi wa hao wawili mwataka niwafungulie?” Wakasema: “Baraba.” 22 Pilato akawaambia: “Basi, nitafanya nini na Yesu aitwaye kwa kawaida Kristo?” Wote wakasema: “Acha atundikwe mtini!” 23 Akasema: “Kwa nini, amefanya ubaya gani?” Bado wao wakafuliza kupaaza kilio hata zaidi: “Acha atundikwe mtini!”
24 Alipoona kwamba haikufaidi kitu bali, badala ya hivyo, ghasia ilikuwa ikitokea, Pilato alichukua maji na kuosha mikono yake mbele ya ule umati, akisema: “Mimi sina hatia ya damu ya mtu huyu. Nyinyi wenyewe lazima mwone hilo.” 25 Ndipo watu wote wakasema kwa kujibu: “Damu yake ije juu yetu na juu ya watoto wetu.” 26 Ndipo akawafungulia Baraba, lakini akaagiza Yesu apigwe mijeledi na kumkabidhi ili atundikwe mtini.
27 Ndipo askari-jeshi wa gavana wakampeleka Yesu ndani ya ikulu ya gavana na kukusanya kikosi chote cha askari pamoja kwake. 28 Nao wakimvua kanzu yake, wakampamba kwa joho jekundu-jangavu, 29 nao wakasuka taji kutokana na miiba na kuliweka juu ya kichwa chake na tete katika mkono wake wa kuume. Na, wakipiga magoti mbele yake, wakamfanyia ucheshi, wakisema: “Siku njema, wewe Mfalme wa Wayahudi!” 30 Nao wakatema mate juu yake na kuchukua lile tete na kuanza kumpiga juu ya kichwa chake. 31 Mwishowe, walipokuwa wamemfanyia ucheshi, walivua lile joho na kumvisha mavazi yake ya nje na kumwongoza ili kutundikwa mtini.
32 Walipokuwa wakitoka kwenda walikuta mzaliwa wa Kirene aitwaye jina Simoni. Mtu huyu wakamshurutisha kufanya utumishi kuinua mti wake wa mateso. 33 Nao walipokuja mahali paitwapo Golgotha, ndiyo kusema, Mahali pa Fuvu la Kichwa, 34 wakampa divai iliyochanganywa na nyongo anywe; lakini, baada ya kuionja, alikataa kunywa. 35 Walipokuwa wamemtundika mtini wakagawa mavazi yake ya nje kwa kupiga kura, 36 na, wakiwa wameketi, wakamlinda hapo. 37 Pia, wakaangika juu ya kichwa chake shtaka dhidi yake, kwa kuandika: “Huyu ni Yesu Mfalme wa Wayahudi.”
38 Ndipo wapokonyaji wawili wakatundikwa mtini pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mmoja upande wake wa kushoto. 39 Kwa hiyo wapita-njia wakaanza kusema kwa maneno yenye kuudhi juu yake, wakitikisa vichwa vyao 40 na kusema: “Ewe mtaka-kuangusha chini hekalu na mjenzi walo katika siku tatu, jiokoe mwenyewe! Ikiwa wewe ni mwana wa Mungu, teremka kutoka kwenye mti wa mateso!” 41 Kwa namna kama hiyo pia makuhani wakuu pamoja na waandishi na wanaume wazee wakaanza kumfanyia ucheshi na kusema: 42 “Wengine aliokoa; mwenyewe hawezi kujiokoa! Yeye ni Mfalme wa Israeli; acheni sasa ateremke kutoka kwenye mti wa mateso na hakika sisi tutaamini juu yake. 43 Ameweka itibari yake katika Mungu; acheni Yeye sasa amwokoe ikiwa Yeye amtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Katika njia hiyohiyo hata wapokonyaji waliotundikwa mtini pamoja naye wakaanza kumshutumu.
45 Tangu saa ya sita na kuendelea giza likawa juu ya nchi yote, hadi saa ya tisa. 46 Karibu saa ya tisa Yesu akapaaza kilio kwa sauti kubwa, akisema: “Eli, Eli, lama sabakthani?” yaani, “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniachilia mbali?” 47 Waliposikia hilo, baadhi ya wale wenye kusimama hapo wakaanza kusema: “Mtu huyu anamwita Eliya.” 48 Na mara, mmoja wao akakimbia na kuchukua sponji na kuilowesha kwa divai iliyochacha na kuiweka juu ya tete na kuanza kumnywesha. 49 Lakini wale wengine wao wakasema: “Acha iwe hivyo kwake! Acheni tuone kama Eliya aja kumwokoa.” [[Mtu mwingine akachukua mkuki na kudunga upande wake, na damu na maji vikatoka.]] 50 Tena Yesu akapaaza kilio kwa sauti kubwa, akatoa roho yake.
51 Na, tazama! pazia la patakatifu likapasuliwa vipande viwili, kutoka juu hadi chini, na dunia ikatetema, na matungamo-miamba yakapasuliwa. 52 Na makaburi ya ukumbusho yakafunguliwa na miili mingi ya watakatifu waliokuwa wamelala usingizi ikainuliwa, 53 (na watu, wakitoka kati ya makaburi ya ukumbusho baada ya kufufuliwa kwake, wakaingia katika jiji takatifu,) nayo ikawa yenye kuonekana kwa watu wengi. 54 Lakini yule ofisa-jeshi na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoona tetemeko la dunia na mambo yenye kutukia, wakawa wenye kuogopa sana, wakisema: “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
55 Zaidi ya hayo, wanawake wengi walikuwa hapo wakitazama kwa umbali, waliokuwa wameandamana na Yesu kutoka Galilaya kumhudumia; 56 ambao miongoni mwao alikuwamo Maria Magdalene, pia Maria mama ya Yakobo na Yosesi, na mama ya wana wa Zebedayo.
57 Sasa kwa kuwa ilikuwa jioni-jioni, kulikuja mtu mmoja tajiri wa Arimathea, aitwaye jina Yosefu, ambaye yeye mwenyewe pia alikuwa amepata kuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 Mtu huyu alimwendea Pilato na kuomba apewe mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe huo. 59 Na Yosefu akachukua huo mwili, akaufunga katika kitani safi bora, 60 na kuulaza katika kaburi lake jipya la ukumbusho, alilokuwa amechimba katika tungamo-mwamba. Na, baada ya kubingirisha jiwe kubwa kwenye mlango wa hilo kaburi la ukumbusho, akaondoka. 61 Lakini Maria Magdalene na Maria mwingine wakaendelea kuwa hapo, wakiwa wameketi mbele ya hilo kaburi.
62 Siku iliyofuata, iliyokuwa baada ya yale Matayarisho, makuhani wakuu na Mafarisayo walikusanyika pamoja mbele ya Pilato, 63 wakisema: “Bwana, tumekumbuka kwamba mlaghai huyo alisema alipokuwa bado yuko hai, ‘Baada ya siku tatu mimi napaswa kufufuliwa.’ 64 Kwa hiyo amuru kaburi lifanywe salama hadi siku ya tatu, ili wanafunzi wake wasipate kamwe kuja na kumwiba na kuwaambia watu, ‘Alifufuliwa kutoka kwa wafu!’ na ulaghai huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa kwanza.” 65 Pilato akawaambia: “Nyinyi mna walinzi. Nendeni mkalifanye salama kwa jinsi nyinyi mjuavyo.” 66 Kwa hiyo wakaenda na kulifanya salama kaburi kwa kulitia jiwe muhuri na kuwa na wale walinzi.