Mathayo
28 Baada ya siku ya sabato, nuru ilipozidi kuongezeka katika siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na Maria mwingine wakaja kulitazama kaburi.
2 Na, tazama! tetemeko la dunia lililo kubwa lilikuwa limetukia; kwa maana malaika wa Yehova alikuwa ameshuka kutoka mbinguni akakaribia na kulibingirisha jiwe, na alikuwa ameketi juu yalo. 3 Kuonekana kwake kwa nje kulikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. 4 Ndiyo, kwa kumhofu wale walinzi walitetemeka na kuwa kama wafu.
5 Lakini malaika kwa kujibu akawaambia hao wanawake: “Msiwe na hofu nyinyi, kwa maana najua mnamtafuta Yesu aliyetundikwa mtini. 6 Hayupo hapa, kwa maana alifufuliwa, kama alivyosema. Njoni, oneni mahali alipokuwa amelala. 7 Nanyi nendeni upesi na waambieni wanafunzi wake kwamba alifufuliwa kutoka kwa wafu, na, tazameni! anawatangulia kuingia Galilaya; huko mtamwona yeye. Tazameni! Nimewaambia nyinyi.”
8 Kwa hiyo, wakiondoka upesi kwenye kaburi la ukumbusho, wakiwa na hofu na shangwe kubwa, wakakimbia kuripoti kwa wanafunzi wake. 9 Na, tazama! Yesu akakutana nao na kusema: “Siku njema!” Wao wakakaribia wakamshika kwenye miguu yake wakamsujudia. 10 Ndipo Yesu akawaambia: “Msiwe na hofu! Nendeni, ripotini kwa ndugu zangu, ili wapate kwenda zao kuingia Galilaya; na huko wataniona mimi.”
11 Walipokuwa wameshika njia yao kwenda, tazama! baadhi ya walinzi wakaenda ndani ya jiji na kuripoti kwa makuhani wakuu mambo yote yaliyokuwa yametukia. 12 Na walipokuwa wamekusanyika pamoja wakiwa na wanaume wazee na kufanya shauri, wakawapa hao askari-jeshi kiasi cha kutosha cha vipande vya fedha 13 na kusema: “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba tulipokuwa tumelala usingizi.’ 14 Na hilo likifika masikioni mwa gavana, hakika sisi tutamshawishi na hakika tutawaondolea nyinyi wasiwasi.” 15 Kwa hiyo wakachukua vile vipande vya fedha wakafanya kama walivyoagizwa; na usemi huo umesambazwa kotekote miongoni mwa Wayahudi hata siku hiihii.
16 Hata hivyo, wale wanafunzi kumi na mmoja wakaingia Galilaya hadi mlima ambako Yesu alikuwa amewafanyia mpango, 17 nao walipomwona wakasujudu, lakini baadhi yao walitia shaka. 18 Naye Yesu akakaribia na kuwaambia, akisema: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na juu ya dunia. 19 Kwa hiyo nendeni mkafanye wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, kuwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la roho takatifu, 20 kuwafundisha kushika mambo yote ambayo mimi nimewaamuru nyinyi. Na, tazameni! mimi nipo pamoja nanyi siku zote hadi umalizio wa mfumo wa mambo.”