Mathayo
26 Basi Yesu alipokuwa amemaliza semi zote hizo, aliwaambia wanafunzi wake: 2 “Mwajua kwamba siku mbili tangu sasa kutakuwa sikukuu ya kupitwa, naye Mwana wa binadamu apaswa kukabidhiwa ili atundikwe mtini.”
3 Ndipo makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu wakakusanyika pamoja katika ua wa kuhani wa cheo cha juu aliyeitwa Kayafa, 4 na kufanya shauri pamoja ili wamkamate Yesu kwa mbinu ya kiufundi wamuue. 5 Hata hivyo, wao walifuliza kusema: “Si kwenye msherehekeo, ili ghasia isipate kutokea miongoni mwa watu.”
6 Ilipotukia Yesu akawa katika Bethania katika nyumba ya Simoni mwenye ukoma, 7 mwanamke mwenye chupa ya alabasta iliyo na mafuta ghali yenye marashi akamkaribia, naye akaanza kuyamwaga juu ya kichwa cha Yesu alipokuwa akiegama kwenye meza. 8 Walipoona hilo wanafunzi wakawa wenye kughadhibika na kusema: “Kwa nini upotevu huu wa bure? 9 Kwa maana haya yangaliweza kuuzwa kwa kiasi kikubwa na kupewa kwa maskini.” 10 Akijua hilo, Yesu akawaambia: “Kwa nini mwajaribu kumsumbua huyo mwanamke? Kwa maana alifanya kitendo bora kunielekea mimi. 11 Kwa maana sikuzote mna maskini pamoja nanyi, lakini hamtakuwa nami sikuzote. 12 Kwa maana mwanamke huyu alipoweka mafuta haya yenye marashi juu ya mwili wangu, alifanya hivyo kunitayarisha mimi kwa maziko. 13 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kokote ambako habari njema hii ihubiriwako katika ulimwengu wote, alilofanya mwanamke huyu hakika litasimuliwa pia kuwa ukumbuko juu yake.”
14 Ndipo mmoja wa wale kumi na wawili, yule aitwaye Yudasi Iskariote, akaenda kwa makuhani wakuu 15 na kusema: “Mtanipa nini ili nimsaliti kwenu?” Wakamwagizia vipande thelathini vya fedha. 16 Kwa hiyo tangu wakati huo na kuendelea akafuliza kutafuta fursa nzuri ya kumsaliti.
17 Katika siku ya kwanza ya keki zisizotiwa chachu wanafunzi walimjia Yesu, wakisema: “Ni wapi utakapo tukutayarishie kula sikukuu ya kupitwa?” 18 Akasema: “Nendeni ndani ya jiji kwa Fulani-wa-fulani na mmwambie, Mwalimu asema, ‘Wakati wangu uliowekwa uko karibu; hakika nitasherehekea sikukuu ya kupitwa pamoja na wanafunzi wangu nyumbani mwako.’” 19 Nao wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, nao wakatayarisha vitu kwa ajili ya sikukuu ya kupitwa.
20 Wakati, sasa, ilipokuwa imekuwa jioni, alikuwa akiegama kwenye meza pamoja na wale wanafunzi kumi na wawili. 21 Walipokuwa wakila, alisema: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Mmoja wenu atanisaliti mimi.” 22 Wakiwa wametiwa kihoro sana na hilo, walianza kila mmoja kumwambia: “Bwana, si mimi, je, ndimi?” 23 Kwa kujibu akasema: “Yeye achovyaye mkono wake pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti. 24 Kweli, Mwana wa binadamu anaenda zake, kama vile imeandikwa kumhusu, lakini ole wake mtu huyo ambaye kupitia yeye Mwana wa binadamu asalitiwa! Ingalikuwa bora zaidi kwake kama mtu huyo hangalizaliwa.” 25 Kwa kujibu Yudasi, aliyekuwa karibu kumsaliti, akasema: “Si mimi, je, ndimi, Rabi?” Akamwambia: “Wewe mwenyewe umesema hilo.”
26 Walipokuwa wakiendelea kula, Yesu alichukua mkate na, baada ya kusema baraka, akaumega na, akiwapa wanafunzi, akasema: “Chukueni, kuleni. Huu wamaanisha mwili wangu.” 27 Pia, alichukua kikombe na, akiisha kushukuru, akawapa hicho, akisema: “Nyweni kutoka hicho, nyinyi nyote; 28 kwa maana hii yamaanisha ‘damu yangu ya agano,’ inayopaswa kumwagwa kwa niaba ya wengi kwa msamaha wa dhambi. 29 Lakini nawaambia nyinyi, tangu sasa hakika mimi sitakunywa kwa vyovyote chochote cha zao hili la mzabibu hadi siku ile nitakapokinywa kikiwa kipya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” 30 Mwishowe, baada ya kuziimba sifa, wakatoka kwenda kwenye Mlima wa Mizeituni.
31 Ndipo Yesu akawaambia: “Nyinyi nyote mtakwazika kuhusiana nami usiku huu, kwa maana imeandikwa, ‘Hakika nitampiga mchungaji, nao kondoo wa kundi watatawanywa huku na huku.’ 32 Lakini baada ya mimi kuwa nimefufuliwa hakika nitawatangulia kuingia katika Galilaya.” 33 Lakini Petro, kwa kujibu, akamwambia: “Ijapokuwa wengine wote wakwazika kuhusiana nawe, hakika mimi sitakwazika kamwe!” 34 Yesu akamwambia: “Kwa kweli nakuambia wewe, Usiku huu, kabla ya jogoo kuwika, utanikana mimi mara tatu.” 35 Petro akamwambia: “Hata kama nitapaswa kufa pamoja nawe, hakika mimi sitakukana kwa vyovyote.” Wanafunzi wale wengine wote wakasema jambo lilelile pia.
36 Ndipo Yesu akaja pamoja nao hadi mahali paitwapo Gethsemane, naye akawaambia wanafunzi: “Ketini hapa wakati niendapo pale na kusali.” 37 Naye akichukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo pamoja naye, akaanza kuwa na kihoro na kutaabika sana. 38 Ndipo akawaambia: “Nafsi yangu ina kihoro sana, hata kufikia kifo. Kaeni hapa na kufuliza kulinda pamoja nami.” 39 Naye akienda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akisali na kusema: “Baba yangu, ikiwa yawezekana, acha kikombe hiki kipitilie mbali nami. Lakini, si kama mimi nipendavyo, bali kama wewe upendavyo.”
40 Naye akawajia wanafunzi na kuwakuta wamelala usingizi, naye akamwambia Petro: “Je, nyinyi watu hamngeweza kulinda hata saa moja pamoja nami? 41 Fulizeni kulinda na kusali kwa kuendelea, ili msipate kuingia ndani ya jaribu. Bila shaka, roho ni yenye hamu, lakini mwili ni dhaifu.” 42 Tena, kwa mara ya pili, akaenda zake na kusali, akisema: “Baba yangu, ikiwa haiwezekani hiki kipitilie mbali ila nikinywe, acha mapenzi yako yatendeke.” 43 Naye akaja tena na kuwakuta wamelala usingizi, kwa maana macho yao yalikuwa mazito. 44 Kwa hiyo akiwaacha, akaenda zake tena na kusali kwa mara ya tatu, akisema mara moja tena neno lilelile. 45 Kisha akawajia wanafunzi na kuwaambia: “Kwa wakati kama huu nyinyi mmelala usingizi na kupumzika! Tazameni! Saa imekaribia Mwana wa binadamu asalitiwe kuingia katika mikono ya watenda-dhambi. 46 Inukeni, twendeni. Tazameni! Msaliti wangu amekaribia.” 47 Na alipokuwa bado akisema, tazama! Yudasi, mmoja wa wale kumi na wawili, akaja na pamoja naye umati mkubwa ukiwa na mapanga na marungu umetoka kwa makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu.
48 Sasa msaliti wake alikuwa amewapa ishara, akisema: “Yeyote yule nibusuye, huyo ndiye; mkamateni.” 49 Naye akienda moja kwa moja kwa Yesu akasema: “Siku njema, Rabi!” na kumbusu kwa wororo sana. 50 Lakini Yesu akamwambia: “Jamaa, wewe upo kwa kusudi gani?” Ndipo wakaja mbele wakaweka mikono juu ya Yesu na kumkamata. 51 Lakini, tazama! mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyoosha mkono wake na kufuta upanga wake na kumpiga mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu na kuondoa sikio lake. 52 Ndipo Yesu akamwambia: “Rudisha upanga wako mahali pao, kwa maana wale wote wauchukuao upanga wataangamia kwa upanga. 53 Au wafikiri kwamba siwezi kuomba Baba yangu anipe mimi katika dakika hii malejioni zaidi ya kumi na mawili ya malaika? 54 Katika kisa hicho, Maandiko yangetimizwaje kwamba lazima itendeke kwa njia hii?” 55 Katika saa hiyo Yesu akauambia umati: “Je, mmetoka mkiwa na mapanga na marungu kama dhidi ya mpokonyaji ili kunikamata? Siku baada ya siku nilikuwa na kawaida ya kuketi katika hekalu nikifundisha, na bado hamkunikamata. 56 Lakini yote haya yametukia ili maandiko ya manabii yatimizwe.” Ndipo wanafunzi wote wakamwacha na kukimbia.
57 Wale waliomkamata Yesu wakamwongoza kwa Kayafa kuhani wa cheo cha juu, ambako waandishi na wanaume wazee walikuwa wamekusanywa pamoja. 58 Lakini Petro akafuliza kumfuata akiwa umbali wa kutosha, hadi ua wa kuhani wa cheo cha juu, na, baada ya kuingia ndani, alikuwa ameketi pamoja na mahadimu wa nyumba ili kuona matokeo.
59 Wakati huohuo makuhani wakuu na Sanhedrini nzima walikuwa wakitafuta ushahidi usio wa kweli dhidi ya Yesu kusudi wafanye auawe, 60 lakini hawakupata wowote, ijapokuwa mashahidi wengi wasio wa kweli walikuja mbele. Baadaye wawili wakaja mbele 61 na kusema: “Mtu huyu alisema, ‘Naweza kuliangusha chini hekalu la Mungu na kulijenga katika siku tatu.’” 62 Ndipo kuhani wa cheo cha juu akasimama na kumwambia: “Je, huna jibu? Ni nini hili ambalo hawa wanashuhudia dhidi yako?” 63 Lakini Yesu akafuliza kukaa kimya. Kwa hiyo kuhani wa cheo cha juu akamwambia: “Kwa Mungu aliye hai nakuweka chini ya kiapo utuambie kama wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu!” 64 Yesu akamwambia: “Wewe mwenyewe umesema hilo. Lakini nawaambia nyinyi watu, Tangu sasa mtaona Mwana wa binadamu ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” 65 Ndipo kuhani wa cheo cha juu akararua mavazi yake ya nje, akisema: “Amekufuru! Ni uhitaji gani zaidi tulio nao wa mashahidi? Ona! Sasa mmelisikia kufuru. 66 Ni nini kauli yenu?” Wakarudisha jibu: “Yeye ni mwenye kustahili kifo.” 67 Ndipo wakatema mate usoni mwake na kumpiga kwa ngumi zao. Wengine wakampiga makofi usoni, 68 wakisema: “Tutolee unabii, wewe Kristo. Ni nani aliyekupiga?”
69 Sasa Petro alikuwa ameketi nje katika ua; na msichana mtumishi akamjia, akisema: “Wewe, pia, ulikuwa pamoja na Yesu Mgalilaya!” 70 Lakini akakana hilo mbele yao wote, akisema: “Sijui unaloongea juu yalo.” 71 Alipokuwa amekwisha kutoka kwenda kwenye nyumba ya langoni, msichana mwingine alimwona na kuwaambia wale waliokuwa hapo: “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” 72 Naye akakana hilo tena, kwa kiapo: “Simjui huyo mtu!” 73 Baada ya muda kidogo wale waliosimama kuzunguka wakaja na kumwambia Petro: “Hakika wewe pia ni mmoja wao, kwa maana, kwa kweli, lahaja yako yakutambulisha wazi.” 74 Ndipo akaanza kulaani na kuapa: “Simjui huyo mtu!” Na mara jogoo akawika. 75 Naye Petro akakumbuka usemi ambao Yesu alisema, yaani: “Kabla ya jogoo kuwika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje na kutoa machozi kwa uchungu.