Mathayo
25 “Ndipo ufalme wa mbingu utakuwa kama mabikira kumi waliochukua taa zao na kutoka kwenda kukutana na bwana-arusi. 2 Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano walikuwa wenye busara. 3 Kwa maana wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta pamoja nao, 4 lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. 5 Wakati bwana-arusi alipokuwa akikawia, wote walikupia na kuanza kulala usingizi. 6 Katikati kabisa ya usiku kukatokea kilio, ‘Huyu hapa bwana-arusi! Shikeni njia yenu kukutana naye.’ 7 Ndipo mabikira wote hao wakainuka na kuziweka tayari taa zao. 8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupeni sisi baadhi ya mafuta yenu, kwa sababu taa zetu zakaribia kuzimika.’ 9 Wale wenye busara wakajibu kwa maneno haya, ‘Labda huenda kusiwe na ya kutosha kabisa kwa ajili yetu na nyinyi. Badala ya hivyo, shikeni njia yenu kwenda kwa wale wayauzao mjinunulie wenyewe.’ 10 Walipokuwa wakienda zao kununua, bwana-arusi akawasili, na wale mabikira waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye kwenye karamu ya arusi; nao mlango ukafungwa. 11 Baadaye wale mabikira wengine pia wakaja, wakisema, ‘Bwana, bwana, tufungulie!’ 12 Kwa kujibu akasema, ‘Nawaambia nyinyi kweli, Siwajui nyinyi.’
13 “Kwa hiyo, fulizeni kulinda kwa sababu hamjui wala siku wala saa.
14 “Kwa maana ni kama vile wakati ambapo mtu, akiwa karibu kusafiri nchi ya nje, aliwaita watumwa wake na kuwakabidhi mali zake. 15 Akampa mmoja talanta tano, mwingine mbili, na bado mwingine moja, kila mmoja kulingana na uwezo wake mwenyewe, naye akaenda nchi ya nje. 16 Mara yule aliyezipokea talanta tano akashika njia yake kwenda na kufanya biashara nazo na kupata faida ya tano zaidi. 17 Katika njia ileile yule aliyezipokea mbili akapata faida ya mbili zaidi. 18 Lakini yule aliyepokea moja tu akaenda zake, na kuchimba katika ardhi na kuficha ile sarafu ya fedha ya bwana-mkubwa wake.
19 “Baada ya wakati mrefu bwana-mkubwa wa watumwa hao alikuja na kufanya hesabu pamoja na wao. 20 Kwa hiyo yule aliyekuwa amepokea talanta tano akaja mbele na kuleta talanta tano zaidi, akisema, ‘Bwana-mkubwa, ulinikabidhi talanta tano; ona, nilipata faida ya talanta tano zaidi.’ 21 Bwana-mkubwa wake akamwambia, ‘Vema, mtumwa mwema na mwaminifu! Ulikuwa mwaminifu juu ya mambo machache. Hakika nitakuweka wewe rasmi juu ya mambo mengi. Ingia katika shangwe ya bwana-mkubwa wako.’ 22 Halafu yule aliyekuwa amepokea zile talanta mbili akaja mbele na kusema, ‘Bwana-mkubwa, ulinikabidhi talanta mbili; ona, nilipata faida ya talanta mbili zaidi.’ 23 Bwana-mkubwa wake akamwambia, ‘Vema, mtumwa mwema na mwaminifu! Ulikuwa mwaminifu juu ya mambo machache. Hakika nitakuweka wewe rasmi juu ya mambo mengi. Ingia katika shangwe ya bwana-mkubwa wako.’
24 “Mwishowe yule aliyekuwa amepokea talanta moja akaja mbele na kusema, ‘Bwana-mkubwa nilikujua wewe kuwa mtu mwenye kudai, ukivuna ambapo hukupanda na kukusanya ambapo hukupepeta. 25 Kwa hiyo nikawa mwenye kuogopa na kwenda zangu na kuficha talanta yako katika ardhi. Hiki hapa kilicho chako.’ 26 Kwa kujibu bwana-mkubwa wake akamwambia, ‘Mtumwa mwovu na goigoi, ulijua, sivyo, kwamba mimi nilivuna ambapo sikupanda na kukusanya ambapo sikupepeta? 27 Hivyo, basi, ungalipaswa kuwa umeweka akiba ya sarafu zangu za fedha kwa watunza akiba ya benki, na wakati wa kuwasili kwangu ningekuwa nikipokea kilicho changu pamoja na faida.
28 “‘Kwa hiyo chukueni talanta kutoka kwake na kumpa yeye aliye na talanta kumi. 29 Kwa maana kwa kila mtu aliye na kitu, atapewa zaidi naye atakuwa na wingi; lakini kwa habari yake asiye na kitu, hata alicho nacho kitaondolewa mbali kutoka kwake. 30 Nanyi mtupeni nje katika giza lililo nje mtumwa asiyefaa kitu. Huko ndiko kutoa kwake machozi na kusaga meno yake kutakuwa.’
31 “Wakati Mwana wa binadamu awasilipo katika utukufu wake, na malaika wote pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti chake cha ufalme chenye utukufu. 32 Na mataifa yote yatakusanywa mbele yake, naye atatenganisha watu mmoja na mwenzake, kama vile mchungaji atenganishavyo kondoo na mbuzi. 33 Naye atawaweka kondoo kwenye mkono wake wa kuume, lakini mbuzi kwenye mkono wake wa kushoto.
34 “Ndipo mfalme atakapowaambia wale walio kwenye mkono wake wa kuume, ‘Njoni, nyinyi ambao mmebarikiwa na Baba yangu, rithini ufalme uliotayarishwa kwa ajili yenu tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu. 35 Kwa maana nilipata kuwa mwenye njaa nanyi mkanipa kitu cha kula; nilipatwa na kiu nanyi mkanipa kitu cha kunywa. Nilikuwa mgeni nanyi mkanipokea kwa ukaribishaji-wageni; 36 uchi, nanyi mkanivisha. Nilishikwa na ugonjwa nanyi mkanitunza. Nilikuwa gerezani nanyi mkanijia.’ 37 Ndipo waadilifu watamjibu yeye kwa haya maneno, ‘Bwana, ni wakati gani tulipokuona wewe ukiwa mwenye njaa na kukulisha, au ukiwa mwenye kiu, na kukupa kitu cha kunywa? 38 Ni wakati gani tulipokuona wewe ukiwa mgeni na kukupokea kwa ukaribishaji-wageni, au ukiwa uchi, na kukuvisha wewe? 39 Ni wakati gani tulipokuona wewe ukiwa mgonjwa au gerezani na kukuendea wewe?’ 40 Na kwa kujibu mfalme atawaambia wao, ‘Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kwa kadiri ambayo mlimfanyia hilo mmoja wa wadogo zaidi sana wa ndugu zangu hawa, mlinifanyia mimi hilo.’
41 “Ndipo naye atawaambia, wale walio kwenye mkono wake wa kushoto, ‘Shikeni njia yenu mtoke kwangu, nyinyi ambao mmelaaniwa, mkaingie katika moto udumuo milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilipata kuwa mwenye njaa, lakini hamkunipa kitu chochote cha kula, nami nilipatwa na kiu, lakini hamkunipa kitu chochote cha kunywa. 43 Nilikuwa mgeni, lakini hamkunipokea kwa ukaribishaji-wageni; uchi, lakini hamkunivisha; mgonjwa na gerezani, lakini hamkunitunza.’ 44 Ndipo wao pia watamjibu kwa maneno haya, ‘Bwana, ni wakati gani tulipokuona ukiwa mwenye njaa au ukiwa mwenye kiu au ukiwa mgeni au ukiwa uchi au mgonjwa au gerezani na tukakosa kukuhudumia?’ 45 Ndipo atawajibu wao kwa maneno haya, ‘Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kwa kadiri ambayo hamkumfanyia hilo mmoja wa hawa wadogo zaidi sana, hamkunifanyia mimi.’ 46 Na hawa wataondoka kuingia katika kukatiliwa-mbali kudumuko milele, lakini waadilifu kuingia katika uhai udumuo milele.”