Matendo
12 Karibu na wakati maalumu huo Herode mfalme alitumia mikono yake kutenda vibaya baadhi ya wale wa kutaniko. 2 Alimmaliza Yakobo ndugu ya Yohana kwa upanga. 3 Alipoona hilo lilikuwa lenye kuwapendeza Wayahudi, aliendelea kumkamata Petro pia. (Ikawa kwamba, hizo zilikuwa siku za keki zisizotiwa chachu.) 4 Na akimshika, akamweka gerezani, akimkabidhi kwenye zamu nne za askari-jeshi wanne kila moja ili kumlinda, kwa kuwa alikusudia kumtokeza kwa watu baada ya sikukuu ya kupitwa. 5 Kwa sababu hiyo Petro alikuwa akiwekwa gerezani; lakini sala kwa Mungu kwa ajili yake ilikuwa ikiendeshwa kwa juhudi nyingi na kutaniko.
6 Sasa Herode alipokuwa karibu kumtokeza, usiku huo Petro alikuwa amelala akiwa amefungwa kwa minyororo miwili katikati ya askari-jeshi wawili, na walindaji mbele ya mlango walikuwa wakilitunza gereza. 7 Lakini, tazama! malaika wa Yehova akasimama kando, na nuru ikang’aa katika chumba cha gereza. Akimpiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema: “Inuka upesi!” Na minyororo yake ikaanguka kutoka kwenye mikono yake. 8 Malaika akamwambia: “Jifunge kiuno na funga makubazi yako.” Akafanya hivyo. Mwishowe akamwambia: “Vaa vazi lako la nje na ufulize kunifuata.” 9 Naye akatoka kwenda na kufuliza kumfuata, lakini hakujua kwamba lile lililokuwa likitukia kupitia malaika lilikuwa halisi. Kwa kweli, alidhani alikuwa akiona ono. 10 Wakipita askari-mlinzi wa kwanza na wa pili wakafika kwenye lango la chuma lenye kuongoza ndani ya jiji, nalo likawafungukia kwa hiari yalo lenyewe. Na baada ya wao kutoka wakashukia barabara moja, na mara malaika akamwacha. 11 Na Petro, akirudiwa na fahamu, akasema: “Sasa najua hakika kwamba Yehova alituma malaika wake na kunikomboa kutoka kwenye mkono wa Herode na kutoka katika yote ambayo watu kati ya Wayahudi walikuwa wakitarajia.”
12 Na baada ya yeye kufikiria hilo, akaenda kwenye nyumba ya Maria mama ya Yohana aliyeitwa jina la ziada Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekusanyika na wakisali. 13 Alipobisha mlango wa njia ya lango, msichana-mtumishi aliyeitwa jina Roda akaja kuuitikia wito, 14 na, alipoitambua sauti ya Petro, hakulifungua lango kwa sababu ya shangwe, bali akakimbia ndani na kuripoti kwamba Petro alikuwa amesimama mbele ya njia ya lango. 15 Wakamwambia: “Una kichaa.” Lakini yeye akafuliza kusisitiza kwa nguvu ndivyo ilivyokuwa. Wakaanza kusema: “Ni malaika wake.” 16 Lakini Petro akakaa hapo akibisha mlango. Walipofungua, wakamwona nao wakashangaa. 17 Lakini yeye akawapungia mkono wake wawe kimya na kuwaambia kirefu jinsi Yehova alivyomleta nje ya gereza, naye akasema: “Ripotini mambo haya kwa Yakobo na akina ndugu.” Ndipo akatoka kwenda na kufunga safari kwenda mahali pengine.
18 Basi, ilipokuwa mchana, kulikuwa na msukosuko usio mdogo miongoni mwa askari-jeshi juu ya ni nini kwa kweli lililokuwa limempata Petro. 19 Herode akamtafuta kwa bidii yenye kuendelea na, alipokosa kumpata, akawachunguza walindaji na kuwaamuru wapelekwe kwenye adhabu; naye akateremka kwenda Yudea hadi Kaisaria na kutumia wakati fulani huko.
20 Sasa alikuwa katika hali ya kutaka kupigana dhidi ya watu wa Tiro na wa Sidoni. Kwa hiyo wakamjia kwa umoja na, baada ya kumshawishi Blasto, aliyekuwa mwenye kusimamia chumba cha kulala cha mfalme, wakaanza kutoa ombi la kutaka amani, kwa sababu nchi yao iligawiwa chakula kutokana na kile cha mfalme. 21 Lakini siku fulani iliyowekwa Herode akajivika mwenyewe vazi la kifalme na kuketi juu ya kiti cha hukumu na kuanza kuwatolea hotuba ya watu wote. 22 Nao watu waliokusanyika wakaanza kupaaza sauti: “Sauti ya mungu, na si ya binadamu!” 23 Hapohapo malaika wa Yehova akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; naye akaliwa kabisa na mabuu akaisha.
24 Lakini neno la Yehova likaendelea kukua na kusambaa.
25 Kwa habari ya Barnaba na Sauli, baada ya kuwa wametekeleza kikamili uhudumiaji wa kutuliza katika Yerusalemu, wakarudi na kumchukua pamoja nao Yohana, aliyeitwa jina la ziada Marko.