Matendo
13 Basi katika Antiokia kulikuwa na manabii na walimu katika kutaniko la mahali hapo, Barnaba vilevile Simioni aliyeitwa Nigeri, na Lukio wa Kirene, na Manaeni aliyeelimishwa pamoja na Herode mtawala wa wilaya, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimhudumia Yehova hadharani na kufunga, roho takatifu ikasema: “Kati ya watu wote wekeni kando Barnaba na Sauli kwa ajili yangu kwa kazi ambayo nimewaitia.” 3 Ndipo wakafunga na kusali na kuweka juu yao mikono yao na kuwaacha waende.
4 Basi watu hawa, waliotumwa na roho takatifu, wakateremka kwenda Seleukia, na kutoka huko wakasafiri kwa mashua kwenda zao Saiprasi. 5 Na walipopata kuwa katika Salamisi wakaanza kulitangaza neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana akiwa hadimu.
6 Walipokuwa wamepita katika kisiwa chote hadi Pafosi, wakakutana na mwanamume fulani, mlozi, nabii asiye wa kweli, Myahudi ambaye jina lake lilikuwa Bar-Yesu, 7 naye alikuwa pamoja na prokonso Sergio Paulo, mwanamume mwenye akili. Akiita kwake Barnaba na Sauli, mtu huyu alitafuta kwa bidii kulisikia neno la Mungu. 8 Lakini Elimasi mlozi (hiyo, kwa kweli, ndivyo jina lake litafsiriwavyo) akaanza kuwapinga, akitafuta sana kumgeuza mbali prokonso kutoka kwenye ile imani. 9 Sauli, ambaye pia ni Paulo, akiwa mwenye kujazwa roho takatifu, akamkazia macho 10 na kusema: “Ewe mtu mwenye kujaa kila namna ya kupunja na kila namna ya ulaghai, wewe mwana wa Ibilisi, wewe adui wa kila jambo la uadilifu, je, hutakoma kuzipotoa njia zilizo sawa za Yehova? 11 Hivyo, basi, tazama! mkono wa Yehova uko juu yako wewe, nawe utakuwa kipofu, bila kuona nuru ya jua kwa kipindi fulani.” Hapohapo ukungu mzito na giza vikaanguka juu yake, naye akaenda akizunguka kutafuta sana watu wa kumwongoza wakiwa wamemshika mkono. 12 Ndipo prokonso, alipoona lililokuwa limetukia, akawa mwamini, kwa kuwa alistaajabishwa na fundisho la Yehova.
13 Hao watu, pamoja na Paulo, sasa wakasafiri baharini kutoka Pafosi na kuwasili Perga katika Pamfilia. Lakini Yohana akajiondoa kwao na kurudi Yerusalemu. 14 Hata hivyo, wao wakaendelea kutoka Perga na kuja Antiokia katika Pisidia na, wakienda ndani ya sinagogi siku ya sabato, wakaketi. 15 Baada ya usomaji wa Sheria na wa Manabii mbele ya watu wote maofisa-wasimamizi wa sinagogi wakatuma watu kwao, wakisema: “Wanaume, akina ndugu, ikiwa kuna neno lolote la kitia-moyo mlilo nalo kwa ajili ya watu, lisemeni.” 16 Kwa hiyo Paulo akainuka, naye akipunga mkono wake, akasema:
“Wanaume, Waisraeli na nyinyi wengine ambao mwamhofu Mungu, sikieni. 17 Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu wa zamani, naye akawakweza watu wakati wa ukaaji wao wa nchi ya kigeni katika nchi ya Misri na kuwatoa katika hiyo kwa mkono ulioinuliwa. 18 Na kwa kipindi cha karibu miaka arobaini akachukuliana na namna yao ya kutenda nyikani. 19 Baada ya kuangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani, aligawanya nchi yao kwa kura: 20 yote haya wakati wa karibu miaka mia nne na hamsini.
“Na baada ya mambo hayo aliwapa mahakimu mpaka Samweli nabii. 21 Lakini tangu hapo na kuendelea wakadai mfalme, na Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mwanamume wa kabila la Benyamini, kwa miaka arobaini. 22 Na baada ya kumwondoa yeye, aliwainulia Daudi kuwa mfalme, ambaye kwa habari yake yeye alitoa ushahidi na kusema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mwanamume mwenye kukubalika kwa moyo wangu, atakayefanya mambo yote ambayo natamani.’ 23 Kutoka katika uzao wa mwanamume huyu kulingana na ahadi yake Mungu ameleta kwa Israeli mwokozi, Yesu, 24 baada ya Yohana, kwa kutangulia mwingio wa Huyo, akiwa amekwisha kuhubiri hadharani kwa watu wote wa Israeli ubatizo katika ufananisho wa toba. 25 Lakini Yohana alipokuwa akitimiza mwendo wake, akawa akisema ‘Mwadhani mimi ni nini? Mimi si yeye. Lakini, tazameni! mmoja anakuja baada yangu ambaye makubazi ya miguu yake mimi sistahili kuyafungua.’
26 “Wanaume, akina ndugu, nyinyi wana wa ukoo wa Abrahamu na wale wengine miongoni mwenu ambao mwamhofu Mungu, neno la wokovu huu limepelekwa kwetu sisi. 27 Kwa maana wakaaji wa Yerusalemu na watawala wao hawakumjua Huyu, bali, walipokuwa wakitenda wakiwa mahakimu, walitimiza mambo yaliyosemwa na Manabii, mambo ambayo husomwa kwa sauti kubwa kila Sabato, 28 na, ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kifo walidai kwa Pilato kwamba yeye afishwe. 29 Basi, walipokuwa wametimiza mambo yote yaliyoandikwa juu yake, walimshusha chini kutoka kwenye mti na kumlaza katika kaburi la ukumbusho. 30 Lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu; 31 na kwa siku nyingi akawa mwenye kuonekana kwa wale ambao walikuwa wamepanda kwenda pamoja naye kutoka Galilaya hadi Yerusalemu, ambao sasa ni mashahidi wake kwa watu.
32 “Na kwa hiyo sisi tunawatangazia nyinyi habari njema juu ya ahadi iliyotolewa kwa akina baba wa zamani, 33 kwamba Mungu ameitimiza kabisa kwetu sisi watoto wao kwa kuwa alimfufua Yesu; hata kama vile imeandikwa katika zaburi ya pili, ‘Wewe ni mwana wangu, mimi nimekuwa Baba yako siku hii.’ 34 Na jambo hilo la kwamba yeye alimfufua kutoka kwa wafu akikusudiwa asirudi tena kwenye uharibifu, yeye amelitaarifu katika njia hii, ‘Hakika mimi nitawapa nyinyi watu fadhili zenye upendo kwa Daudi zilizo za uaminifu.’ 35 Kwa sababu hiyo asema pia katika zaburi nyingine, ‘Hutaruhusu mwaminifu-mshikamanifu wako aone uharibifu.’ 36 Kwa maana Daudi, kwa upande mmoja, alitumikia mapenzi kamili ya Mungu katika kizazi chake mwenyewe na kulala katika kifo na alilazwa pamoja na baba zake wa zamani na kuona uharibifu. 37 Kwa upande mwingine, yeye ambaye Mungu alimfufua hakuona uharibifu.
38 “Kwa hiyo acheni ijulikane kwenu, akina ndugu, kwamba kupitia Huyu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu; 39 na kwamba kutokana na mambo yote ambayo nyinyi hamngeweza kutangazwa kuwa bila hatia kwa njia ya sheria ya Musa, kila mtu aaminiye atangazwa kuwa bila hatia kwa njia ya Huyu. 40 Kwa hiyo hakikisheni kwamba lile lisemwalo katika Manabii haliji juu yenu, 41 ‘Ioneni, nyinyi wenye kudharau, mwistaajabie, na mtoweke, kwa sababu mimi ninafanya kazi katika siku zenu, kazi ambayo nyinyi hamtaiamini kwa vyovyote hata ikiwa yeyote awasimulia kirefu.’”
42 Basi walipokuwa wakitoka, watu wakaanza kusihi sana mambo haya yasemwe kwao siku ya sabato inayofuata. 43 Kwa hiyo baada ya kusanyiko la sinagogi kufumuliwa, wengi kati ya Wayahudi na kati ya wageuzwa-imani walioabudu Mungu walifuata Paulo na Barnaba, ambao wakisema nao walianza kuwahimiza waendelee katika fadhili isiyostahiliwa ya Mungu.
44 Siku ya Sabato iliyofuata karibu jiji lote lilikusanyika pamoja kulisikia neno la Yehova. 45 Wayahudi walipoona umati, walijawa na wivu na kuanza kuyapinga kwa kukufuru mambo yaliyokuwa yakisemwa na Paulo. 46 Na kwa hiyo, wakiongea kwa ujasiri, Paulo na Barnaba wakasema: “Ilikuwa lazima neno la Mungu lisemwe kwanza kwenu. Kwa kuwa mnalisukuma mbali kutoka kwenu na hamjihukumu wenyewe kuwa mwastahili uhai udumuo milele, tazameni! twawageukia mataifa. 47 Kwa kweli, Yehova ameweka amri juu yetu kwa maneno haya, ‘Nimewaweka nyinyi rasmi kuwa nuru ya mataifa, ili nyinyi muwe wokovu hadi ncha ya dunia.’”
48 Wale wa mataifa waliposikia hilo, wakaanza kushangilia na kulitukuza neno la Yehova, na wote wale waliokuwa na mwelekeo ufaao kwa ajili ya uhai udumuo milele wakawa waamini. 49 Zaidi ya hilo, neno la Yehova likaendelea kupelekwa kotekote katika nchi yote. 50 Lakini Wayahudi wakachochea wanawake wenye kusifika walioabudu Mungu na watu walio wakubwa wa jiji, nao wakainusha mnyanyaso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwatupa nje ya mipaka yao. 51 Hawa walikung’uta mavumbi kutoka kwenye miguu yao dhidi yao na kwenda Ikoniamu. 52 Na wanafunzi wakaendelea kujawa na shangwe na roho takatifu.