Matendo
14 Basi katika Ikoniamu wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi na kusema kwa namna ambayo umati mkubwa wa Wayahudi na pia Wagiriki ukapata kuwa waamini. 2 Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakazichochea na kuzivuta vibaya nafsi za watu wa mataifa dhidi ya akina ndugu. 3 Kwa hiyo wakatumia muda mrefu wakisema kwa ujasiri kwa mamlaka ya Yehova, aliyetoa ushahidi kuhusu neno la fadhili yake isiyostahiliwa kwa kuruhusu ishara na mambo ya ajabu kutukia kupitia mikono yao. 4 Hata hivyo, umati wa jiji ukagawanyika, na baadhi yao walikuwa upande wa Wayahudi lakini wengine upande wa mitume. 5 Basi wakati jaribio lenye jeuri lilipotendeka kwa upande wa watu wa mataifa na pia wa Wayahudi pamoja na watawala wao, ili kuwatenda ufidhuli na kuwavurumishia mawe, 6 wao, walipoarifiwa juu ya hilo, wakakimbia hadi kwenye majiji ya Likaonia, Listra na Derbe na nchi yenye kuzunguka; 7 na huko wakaendelea kutangaza habari njema.
8 Sasa katika Listra kulikuwa kumeketi mwanamume fulani asiyejiweza katika miguu yake, kilema kutoka kwenye tumbo la uzazi la mama yake, naye alikuwa hajatembea kamwe hata kidogo. 9 Mtu huyu alikuwa akisikiliza Paulo akisema, ambaye, alipomkazia macho na kuona alikuwa na imani ya kufanywa apone, 10 alisema kwa sauti kubwa: “Simama wima kwa miguu yako.” Naye akasimama mara na kuanza kutembea. 11 Na umati, ulipoona lile ambalo Paulo alikuwa amefanya, ukainua sauti zao, ukisema katika lugha ya Kilikaonia: “Miungu imekuwa kama binadamu na imeteremka kwetu!” 12 Nao ukaanza kuita Barnaba Zeusi, lakini Paulo Hermesi, kwa kuwa alikuwa ndiye mwenye kuongoza katika kusema. 13 Na kuhani wa Zeusi, ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya jiji, akaleta mafahali na makoja kwenye malango na alikuwa akitaka kutoa dhabihu pamoja na umati.
14 Hata hivyo, mitume Barnaba na Paulo waliposikia juu ya hilo, wakararua mavazi yao ya nje na kuruka ndani ya umati, wakipaaza kilio 15 na kusema: “Wanaume, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi pia ni wanadamu wenye udhaifu uleule kama nyinyi mlivyo nao, nasi tunawatangazia nyinyi habari njema, ili mgeuke kutoka kwa mambo haya ya bure mmjie Mungu aliye hai, aliyefanya mbingu na dunia na bahari na vitu vyote vilivyo ndani yazo. 16 Katika vizazi vilivyopita yeye aliruhusu mataifa yote yaendelee katika njia zayo, 17 ijapokuwa, kwa kweli, hakujiacha mwenyewe bila ushahidi kwa kuwa alitenda mema, akiwapa nyinyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.” 18 Na bado kwa kusema mambo haya walizuia kwa shida umati wasiwadhabihie wao.
19 Lakini Wayahudi wakawasili kutoka Antiokia na Ikoniamu wakashawishi umati, nao wakampiga Paulo kwa mawe na kumkokota nje ya jiji, wakiwazia alikuwa amekufa. 20 Hata hivyo, wanafunzi walipomzingira, akainuka na kuingia ndani ya jiji. Na katika siku iliyofuata akaondoka pamoja na Barnaba kwenda Derbe. 21 Na baada ya kutangaza habari njema kwa jiji hilo na kufanya wanafunzi wengi, wakarudi Listra na Ikoniamu na Antiokia, 22 wakizitia nguvu nafsi za wanafunzi, wakiwatia moyo kubaki katika imani na kusema: “Lazima tuingie katika ufalme wa Mungu kupitia dhiki nyingi.” 23 Zaidi ya hayo, wakawaweka rasmi wanaume wazee kwa ajili yao katika kila kutaniko na, wakitoa sala pamoja na mifungo, wakawakabidhi kwa Yehova ambaye katika yeye walikuwa wamepata kuwa waamini.
24 Nao wakapita katika Pisidia na kuja ndani ya Pamfilia, 25 na, baada ya kulisema neno katika Perga, wakateremka kwenda Atalia. 26 Na kutoka huko wakasafiri kwa mashua kuondoka kwenda Antiokia, walikokuwa wamekabidhiwa kwenye fadhili isiyostahiliwa ya Mungu kwa ajili ya kazi waliyokuwa wameifanya kikamili.
27 Walipokuwa wamewasili na wakiwa wamelikusanya kutaniko pamoja, waliendelea kuyasimulia mambo mengi ambayo Mungu alikuwa amefanya kwa njia yao, na kwamba alikuwa ameyafungulia mataifa mlango wa kuingia katika imani. 28 Kwa hiyo wakatumia muda usio mdogo wakiwa pamoja na wanafunzi.