Matendo
15 Na watu fulani wakateremka kutoka Yudea na kuanza kuwafundisha ndugu: “Msipotahiriwa kulingana na desturi ya Musa, hamwezi kuokolewa.” 2 Lakini kulipokuwa kumetokea mtengano na bishano lisilo dogo kati ya Paulo na Barnaba pamoja nao, wakapanga Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine kati yao wapande kwenda kwa mitume na wanaume wazee katika Yerusalemu kuhusu bishano hilo.
3 Basi, baada ya kusindikizwa na kutaniko, watu hawa waliendelea katika njia yao kupitia Foinike na pia Samaria, wakisimulia kirefu kugeuka kwa watu wa mataifa, nao walikuwa wakisababisha shangwe kubwa kwa akina ndugu wote. 4 Walipowasili Yerusalemu walipokewa kwa fadhili na kutaniko na mitume na wanaume wazee, nao wakasimulia mambo mengi ambayo Mungu alikuwa ameyafanya kupitia wao. 5 Lakini, baadhi ya wale wa farakano la Mafarisayo waliokuwa wameamini wakainuka kutoka kwenye viti vyao na kusema: “Ni lazima kuwatahiri na kuwaamuru wao washike sheria ya Musa.”
6 Na mitume na wanaume wazee wakakusanyika pamoja waone juu ya jambo hili. 7 Basi bishano kubwa lilipokuwa limetukia, Petro aliinuka na kuwaambia: “Wanaume, akina ndugu, nyinyi mwajua vema kwamba tangu siku za mapema Mungu alifanya uchaguzi miongoni mwenu kwamba kupitia kinywa changu watu wa mataifa wasikie neno la habari njema na kuamini; 8 na Mungu, aujuaye moyo, alitoa ushahidi kwa kuwapa wao roho takatifu, kama vile alivyotufanyia sisi pia. 9 Naye hakufanya tofauti hata kidogo kati yetu na wao, bali aliisafisha mioyo yao kwa imani. 10 Kwa hiyo, sasa kwa nini mnamtia Mungu kwenye jaribu kwa kutwika juu ya shingo ya wanafunzi nira ambayo baba zetu wa zamani wala sisi hatukuweza kuhimili? 11 Kinyume chake, sisi twaitibari kupata kuokolewa kupitia fadhili isiyostahiliwa ya Bwana Yesu katika njia ileile kama watu hao pia.”
12 Ndipo umati mzima ukawa kimya, nao wakaanza kusikiliza Barnaba na Paulo wakisimulia ishara nyingi na mambo mengi ya ajabu ambayo Mungu alifanya kupitia kwao miongoni mwa mataifa. 13 Baada ya wao kukoma kusema, Yakobo akajibu, akisema: “Wanaume, akina ndugu, nisikieni. 14 Simioni amesimulia kikamili jinsi Mungu kwa mara ya kwanza alivyoelekeza uangalifu wake kwa mataifa ili achukue kutoka kwayo watu kwa ajili ya jina lake. 15 Na pamoja na hili maneno ya Manabii yapatana, kama vile imeandikwa, 16 ‘Baada ya mambo haya mimi nitarudi na kujenga upya banda la Daudi lililoanguka chini; nami nitajenga upya magofu yalo na kulisimamisha tena, 17 ili wale wabakio kati ya watu wapate kumtafuta Yehova kwa bidii, pamoja na watu wa mataifa yote, watu waitwao kwa jina langu, asema Yehova, anayefanya mambo haya, 18 yajulikanayo tangu zamani za kale.’ 19 Kwa sababu hiyo uamuzi wangu ni kutowataabisha wale wa kutoka katika mataifa wanaomgeukia Mungu, 20 bali kuwaandikia wajiepushe na vitu vilivyochafuliwa na sanamu na uasherati na kile kilichonyongwa na damu. 21 Kwa maana tangu nyakati za kale katika jiji baada ya jiji Musa amekuwa na wale wamhubirio, kwa sababu yeye husomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila siku ya sabato.”
22 Ndipo mitume na wanaume wazee pamoja na kutaniko lote wakapendelea kutuma wanaume waliochaguliwa kutoka miongoni mwao hadi Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba, yaani, Yudasi aliyeitwa Barsaba na Sila, wanaume wenye kuongoza miongoni mwa akina ndugu; 23 na kwa mkono wao wakaandika:
“Mitume na wanaume wazee, akina ndugu, kwa wale ndugu katika Antiokia na Siria na Kilikia ambao ni wa kutoka kwa mataifa: Salamu! 24 Kwa kuwa tumesikia kwamba baadhi ya waliotoka miongoni mwetu wamewasababishia nyinyi taabu kwa maneno mengi, wakijaribu kupindua nafsi zenu, ijapokuwa sisi hatukuwapa maagizo yoyote, 25 sisi tumefikia kauli moja nasi tumependelea kuchagua wanaume tuwatume kwenu pamoja na wapendwa wetu, Barnaba na Paulo, 26 watu ambao wametoa nafsi zao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Kwa hiyo tunawatuma Yudasi na Sila, ili wao pia wapate kuripoti mambo hayohayo kwa neno. 28 Kwa maana roho takatifu na sisi wenyewe tumependelea kutowaongezea nyinyi mzigo zaidi wenye kulemea, ila mambo haya ya lazima, 29 kuendelea kujiepusha na vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu na damu na kutokana na vitu vilivyonyongwa na uasherati. Mkijitunza wenyewe kwa uangalifu kutokana na mambo haya, mtafanikiwa. Afya njema kwenu!”
30 Basi, watu hawa walipoachwa waende, wakateremka kwenda Antiokia, nao wakaukusanya umati pamoja na kuwapa hiyo barua. 31 Baada ya kuisoma, walishangilia juu ya kitia-moyo hicho. 32 Nao Yudasi na Sila, kwa kuwa wao wenyewe walikuwa manabii pia, wakawatia moyo akina ndugu kwa hotuba nyingi na kuwatia nguvu. 33 Kwa hiyo, walipokuwa wamepisha wakati fulani, waliachwa na hao ndugu ili wawaendee kwa amani wale waliokuwa wamewatuma nje. 34 —— 35 Hata hivyo, Paulo na Barnaba wakaendelea kukaa Antiokia wakifundisha na kutangaza habari njema ya neno la Yehova, wakiwa pamoja na wengine wengi pia.
36 Sasa baada ya siku kadhaa Paulo akamwambia Barnaba: “Zaidi ya mambo yote, na turudi tuwazuru akina ndugu katika kila moja la majiji ambamo katika hayo tulitangaza neno la Yehova tuone jinsi walivyo.” 37 Kwa upande wake, Barnaba alikuwa ameazimia kumchukua Yohana pia, aliyeitwa Marko. 38 Lakini Paulo hakufikiri kuwa yafaa kumchukua huyu pamoja nao, kwa kuwa yeye alikuwa amewaacha Pamfilia na hakuwa ameenda nao kwenye kazi. 39 Ndipo kukatokea mfoko mkali wa hasira, hivi kwamba wakatengana; na Barnaba akamchukua Marko pamoja naye na kusafiri kwa mashua kwenda Saiprasi. 40 Paulo alimteua Sila akaondoka kwenda zake baada ya yeye kuwa amekabidhiwa na akina ndugu kwenye fadhili isiyostahiliwa ya Yehova. 41 Lakini yeye akapitia Siria na Kilikia, akiyatia nguvu makutaniko.