Matendo
16 Kwa hiyo akawasili Derbe na pia Listra. Na, tazama! mwanafunzi fulani alikuwa huko mwenye jina Timotheo, mwana wa mwanamke wa Kiyahudi mwenye kuamini lakini wa baba Mgiriki, 2 naye aliripotiwa vema na akina ndugu katika Listra na Ikoniamu. 3 Paulo alionyesha tamaa mtu huyu atoke kwenda pamoja naye, naye akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa katika sehemu hizo, kwa maana wote walijua kwamba baba yake alikuwa Mgiriki. 4 Basi walipoendelea kusafiri kuyapitia majiji walikuwa wakiwakabidhi wale wa huko maagizo yaliyokuwa yameamuliwa na mitume na wanaume wazee waliokuwa katika Yerusalemu ili yashikwe. 5 Kwa hiyo, kwa kweli, makutaniko yakaendelea kufanywa imara katika imani na kuongezeka idadi siku baada ya siku.
6 Zaidi ya hayo, wakapitia Frigia na nchi ya Galatia, kwa sababu walikatazwa na roho takatifu wasiseme neno katika wilaya ya Asia. 7 Zaidi, walipofika Misia wakafanya jitihada za kuingia Bithinia, lakini roho ya Yesu haikuwaruhusu. 8 Kwa hiyo wakapita Misia na kuteremka hadi Troasi. 9 Na wakati wa usiku ono lilimtokea Paulo: mwanamume fulani Mmakedonia alikuwa amesimama akimsihi sana na kusema: “Vuka uingie Makedonia utusaidie.” 10 Basi mara tu alipokuwa amekwisha kuona ono hilo, tukajaribu sana kuingia Makedonia, tukikata kauli kwamba Mungu alikuwa ametuita tuwatangazie habari njema.
11 Kwa hiyo tukasafiri baharini kutoka Troasi na kuja kwa safari ya moja kwa moja hadi Samothrake, lakini siku iliyofuata tukaja hadi Neapolisi, 12 na kutoka huko hadi Filipi, koloni, ambalo ni jiji kubwa la wilaya ya Makedonia. Tulibaki katika jiji hili, tukitumia siku kadhaa. 13 Na siku ya sabato tulitoka nje ya lango kando ya mto, ambako tulikuwa tukifikiri kulikuwako mahali pa sala; nasi tukaketi na kuanza kusema na wanawake waliokuwa wamekusanyika. 14 Na mwanamke fulani aitwaye jina Lidia, muuzaji wa rangi ya zambarau, wa jiji la Thiatira na mwabudu wa Mungu, alikuwa akisikiliza, na Yehova akafungua wazi moyo wake ukazie uangalifu mambo yaliyokuwa yakisemwa na Paulo. 15 Basi wakati yeye na watu wa nyumbani mwake walipobatizwa, alisema hivi kwa kusihi sana: “Ikiwa nyinyi watu mmenihukumu mimi kuwa mwaminifu kwa Yehova, ingieni ndani ya nyumba yangu mkae.” Naye akatushurutisha kwelikweli tuingie.
16 Na ikatukia kwamba tulipokuwa tukienda pale mahali pa sala, msichana-mtumishi fulani mwenye roho, roho mwovu wa uaguzi, alikutana nasi. Yeye alikuwa na kawaida ya kuwapatia mabwana-wakubwa wake faida nyingi kwa kufanya ufundi wa kutabiri. 17 Msichana huyo alifuliza kufuata Paulo na sisi akipaaza kilio kwa maneno haya: “Watu hawa ni watumwa wa Mungu Aliye Juu Zaidi Sana, wanaowatangazia nyinyi njia ya wokovu.” 18 Akafuliza kufanya hilo kwa siku nyingi. Mwishowe Paulo akachoshwa na hilo akageuka na kuambia huyo roho: “Nakuagiza wewe katika jina la Yesu Kristo umtoke yeye.” Naye akatoka saa ileile.
19 Basi, mabwana-wakubwa wake walipoona kwamba tumaini lao la kupata faida lilikuwa limeondoka, walishika Paulo na Sila wakawakokota kuwaingiza mahali pa soko kwa watawala, 20 na, wakiwaongoza hadi kwa wasimamizi wa raia, wakasema: “Watu hawa wanasumbua sana jiji letu, wao wakiwa ni Wayahudi, 21 nao wanatangaza desturi ambazo haziruhusiki kisheria ili sisi tuzikubali au kuzizoea, kwa kuwa sisi ni Waroma.” 22 Nao umati ukainuka pamoja dhidi yao; na wale mahakimu wa raia, baada ya kuyararua mavazi yao ya nje yawatoke, wakaitoa amri wapigwe kwa fito. 23 Baada ya kuwafanya wapigwe mapigo mengi, wakawatupa ndani ya gereza, wakimwagiza mlinzi wa jela awatunze sana. 24 Kwa sababu alipata agizo la namna hiyo, akawatupa ndani ya gereza la ndani zaidi na kufunga sana miguu yao katika mikatale.
25 Lakini karibu na katikati ya usiku Paulo na Sila walikuwa wakisali na kumsifu Mungu kwa wimbo; ndiyo, wafungwa walikuwa wakiwasikia. 26 Kwa ghafula tetemeko kubwa la dunia likatukia, hivi kwamba misingi ya jela ikatikiswa. Zaidi ya hayo, milango yote ikafunguliwa hapohapo, na vifungo vya wote vikafunguliwa. 27 Mlinzi wa jela, akiamshwa usingizini na kuona milango ya gereza ilikuwa imefunguka, akafuta upanga wake na alikuwa karibu kujimaliza mwenyewe, akiwazia kwamba wafungwa walikuwa wametoroka. 28 Lakini Paulo akapaaza kwa sauti kubwa, akisema: “Usijiumize mwenyewe, kwa maana sisi sote tupo hapa!” 29 Kwa hiyo akaomba taa akaruka ndani na, akiwa ameshikwa na mtetemeko, akaanguka chini mbele ya Paulo na Sila. 30 Naye akawaleta nje na kusema: “Mabwana, ni nini ambalo lazima nifanye ili nipate kuokolewa?” 31 Wakasema: “Amini juu ya Bwana Yesu nawe utapata kuokolewa, wewe na watu wa nyumbani mwako.” 32 Nao wakamwambia neno la Yehova pamoja na wote wale walio katika nyumba yake. 33 Naye akawachukua pamoja naye katika saa hiyo ya usiku akaosha mapigo yao; na, wote, yeye na walio wake wakabatizwa bila kukawia. 34 Naye akawaleta ndani ya nyumba yake na kutandika meza mbele yao, naye akashangilia sana pamoja na watu wote wa nyumbani mwake kwa kuwa sasa alikuwa amemwamini Mungu.
35 Ilipokuwa mchana mahakimu wa raia wakawatuma makonstebo wakaseme: “Wafungue watu wale.” 36 Kwa hiyo mlinzi wa jela akaripoti maneno yao kwa Paulo: “Mahakimu wa raia wamewatuma watu kwamba nyinyi wawili mpate kufunguliwa. Kwa hiyo, sasa, tokeni mshike njia yenu mwende kwa amani.” 37 Lakini Paulo akawaambia: “Walitupiga viboko hadharani bila kuhukumiwa kuwa wenye hatia, watu walio Waroma, na kututupa ndani ya gereza; na je, sasa wanatufukuza kwa siri? La, hasha! lakini acha wao wenyewe waje watutoe nje.” 38 Kwa hiyo wale makonstebo wakaripoti semi hizo kwa mahakimu wa raia. Hawa wakawa na hofu waliposikia kwamba watu hao walikuwa ni Waroma. 39 Kwa sababu hiyo wakaja na kuwasihi sana na, baada ya kuwatoa nje, wakawaomba waondoke katika jiji hilo. 40 Lakini wao wakatoka katika gereza hilo na kwenda nyumbani mwa Lidia, nao walipowaona akina ndugu wakawatia moyo wakaondoka.