Matendo
11 Sasa mitume na akina ndugu waliokuwa katika Yudea wakasikia kwamba watu wa mataifa walikuwa pia wamepokea neno la Mungu. 2 Kwa hiyo Petro alipopanda hadi Yerusalemu, waunga-mkono tohara wakaanza kushindana naye, 3 wakisema alikuwa ameingia ndani ya nyumba ya watu waliokuwa hawajatahiriwa na alikuwa amekula pamoja nao. 4 Ndipo Petro akaanza na kuendelea kuwaeleza jambo moja-moja, akisema:
5 “Mimi nilikuwa katika jiji la Yopa nikisali, na katika njozi nikaona ono, chombo cha namna fulani kikishuka kama shuka kubwa ya kitani kikiteremshwa kwa ncha zacho nne kutoka mbinguni, nacho kikaja moja kwa moja nilipokuwa mimi. 6 Nikikodoa macho ndani yacho, niliangalia-angalia na kuona viumbe wenye miguu minne wa dunia na mahayawani-mwitu na vitu vitambaazi na ndege wa mbinguni. 7 Pia nilisikia sauti ikiniambia, ‘Inuka, Petro, chinja ule!’ 8 Lakini nikasema, ‘Sivyo hata kidogo, Bwana, kwa sababu kitu najisi au kisicho safi hakijapata kamwe kuingia ndani ya kinywa changu.’ 9 Mara ya pili sauti kutoka mbinguni ikajibu, ‘Wewe koma kuviita najisi vitu ambavyo Mungu ametakasa.’ 10 Hilo likatokea mara ya tatu, na kila kitu kikavutwa juu tena kuingia mbinguni. 11 Pia, tazama! dakika hiyohiyo kulikuwa na wanaume watatu wamesimama kwenye nyumba tuliyokuwamo, wao wakiwa wametumwa kutoka Kaisaria kuja kwangu. 12 Kwa hiyo roho ikaniambia niende pamoja nao, bila kuwa na shaka hata kidogo. Lakini ndugu sita hawa pia walikwenda pamoja nami, nasi tukaingia ndani ya nyumba ya huyo mwanamume.
13 “Aliripoti kwetu jinsi alivyomwona malaika amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yopa wakamwite Simoni aitwaye jina la ziada Petro, 14 naye atasema nawe mambo yale ambayo kwayo wewe na watu wote wa nyumbani mwako mwaweza kupata kuokolewa.’ 15 Lakini mimi nilipoanza kusema, roho takatifu ikawaangukia kama vile ilivyofanya pia juu yetu mwanzoni. 16 Ndipo nikakumbuka juu ya usemi wa Bwana, jinsi alivyokuwa na kawaida ya kusema, ‘Yohana, kwa upande wake, alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa katika roho takatifu.’ 17 Kwa hiyo, ikiwa Mungu aliwapa wao zawadi ileile ya bure kama vile pia alivyotupa sisi ambao tumemwamini Bwana Yesu Kristo, mimi nilikuwa nani hata niweze kumzuia Mungu?”
18 Basi waliposikia mambo hayo, wakakubali kwa kimya, nao wakamtukuza Mungu, wakisema: “Kwa hiyo, basi, Mungu ameruhusu toba kwa kusudi la uhai kwa watu wa mataifa pia.”
19 Kwa sababu hiyo wale waliokuwa wametawanywa na dhiki iliyotokea kwa sababu ya Stefano wakaenda wakipita hadi Foinike na Saiprasi na Antiokia, lakini wakiwa hawasemi lile neno kwa yeyote ila kwa Wayahudi tu. 20 Hata hivyo, kutoka kati yao kulikuwa na wanaume fulani wa Saiprasi na Kirene waliokuja Antiokia na kuanza kuongea na watu wenye kusema Kigiriki, wakitangaza habari njema ya Bwana Yesu. 21 Zaidi ya hilo, mkono wa Yehova ulikuwa pamoja nao, na idadi kubwa waliopata kuwa waamini wakageuka kuelekea Bwana.
22 Simulizi juu yao likafika masikioni mwa kutaniko lililokuwa katika Yerusalemu, nao wakatuma Barnaba hadi Antiokia. 23 Alipowasili na kuiona fadhili isiyostahiliwa ya Mungu, akashangilia na kuanza kuwatia wote moyo waendelee katika Bwana wakiwa na kusudi la moyo; 24 kwa maana alikuwa mwanamume mwema na mwenye kujaa roho takatifu na imani. Na umati mkubwa ukaongezwa kwa Bwana. 25 Kwa hiyo akaenda zake hadi Tarso ili kumtafuta Sauli kwa ukamili 26 na, baada ya yeye kumpata, akamleta Antiokia. Hivyo ikatukia kwamba kwa mwaka mzima walikusanyika pamoja nao katika kutaniko na kufundisha umati mkubwa, na ilikuwa kwanza katika Antiokia kwamba wanafunzi kwa uongozi wa kimungu waliitwa Wakristo.
27 Basi katika siku hizi manabii waliteremka kutoka Yerusalemu hadi Antiokia. 28 Mmoja kati yao aitwaye jina Agabo akainuka na kuendelea kuonyesha kupitia roho kwamba njaa kali iliyo kubwa ilikuwa karibu kuja juu ya dunia nzima inayokaliwa; ambayo, kama ilivyo, ilitukia wakati wa Klaudio. 29 Kwa hiyo wale kati ya wanafunzi wakaamua, kila mmoja kwa kadiri ambayo yeyote angeweza kutoa, kupeleka uhudumiaji wa kutuliza kwa akina ndugu wenye kukaa katika Yudea; 30 na hilo wakafanya, wakiipeleka kwa wanaume wazee kwa mkono wa Barnaba na Sauli.