Matendo
10 Sasa katika Kaisaria kulikuwa na mwanamume fulani aliyeitwa jina Kornelio, ofisa-jeshi wa kikosi cha Italia, kama kilivyoitwa, 2 mtu mstahifu na mwenye kumhofu Mungu pamoja na watu wa nyumbani mwake wote, naye aliwafanyia watu zawadi nyingi za rehema na kuomba dua kwa Mungu kwa kuendelea. 3 Karibu tu na saa ya tisa ya mchana aliona wazi katika ono malaika wa Mungu akiingia kwake na kumwambia: “Kornelio!” 4 Huyo mtu akamkodolea macho na, akiwa mwenye kuogopa, akasema: “Ni nini, Bwana?” Akamwambia: “Sala na zawadi zako za rehema zimepaa kama ukumbuko mbele ya Mungu. 5 Kwa hiyo sasa tuma wanaume Yopa ukamwite Simoni fulani aitwaye jina la ziada Petro. 6 Mtu huyu anapokewa na Simoni fulani, mtengenezaji-ngozi, aliye na nyumba kando ya bahari.” 7 Mara tu malaika aliyesema naye alipokuwa ameondoka, aliita wawili kati ya watumishi wake wa nyumbani na askari-jeshi mstahifu kutoka miongoni mwa wale waliokuwa wakimhudumia daima, 8 naye akawasimulia kila kitu na kuwatuma kwenda Yopa.
9 Siku iliyofuata walipokuwa wakiendelea na safari yao na wakikaribia hilo jiji, Petro akapanda juu ya paa ya nyumba karibu saa ya sita ili kusali. 10 Lakini akawa mwenye njaa sana na kutaka kula. Walipokuwa wakitayarisha, akaingia katika njozi 11 na akaona mbingu imefunguliwa na chombo cha namna fulani kikishuka kama shuka kubwa ya kitani kikiteremshwa juu ya dunia kwa ncha zacho nne; 12 na ndani yacho mlikuwa namna zote za viumbe wenye miguu minne na vitu vitambaazi vya dunia na ndege wa mbinguni. 13 Na sauti ikamjia: “Inuka, Petro, chinja ule!” 14 Lakini Petro akasema: “Sivyo hata kidogo, Bwana, kwa sababu sijala kamwe kitu chochote kilichotiwa unajisi na kisicho safi.” 15 Na sauti ikasema tena naye, mara ya pili: “Wewe koma kuviita kuwa najisi vitu ambavyo Mungu ametakasa.” 16 Hilo likatokea mara ya tatu, na mara hiyo kile chombo kikachukuliwa juu mbinguni.
17 Basi Petro alipokuwa katika fadhaa kubwa kindani juu ya maana ni nini ya hilo ono alilokuwa ameliona, tazama! wale wanaume waliotumwa na Kornelio walikuwa wameulizia habari juu ya nyumba ya Simoni na walisimama hapo penye lango. 18 Nao wakapaaza sauti na kuulizia habari kama Simoni aliyeitwa jina la ziada Petro alikuwa akipokewa hapo. 19 Petro alipokuwa akiwazawaza katika akili yake juu ya lile ono, roho ikasema: “Tazama! Wanaume watatu wanakutafuta sana. 20 Hata hivyo, inuka, teremka orofani na kushika njia yako uende pamoja nao, bila kuwa na shaka hata kidogo, kwa sababu mimi nimewatuma.” 21 Kwa hiyo Petro akashuka orofani hadi kwa hao wanaume na kusema: “Tazameni! Mimi ndiye mnayetafuta sana. Ni nini sababu ya nyinyi kuwapo hapa?” 22 Wakasema: “Kornelio, ofisa-jeshi, mwanamume mwadilifu na mwenye kumhofu Mungu na mwenye kuripotiwa vema na taifa lote la Wayahudi, alipewa maagizo ya kimungu na malaika mtakatifu kutuma watu ili uitwe uje nyumbani kwake na kuyasikia mambo upaswayo kusema.” 23 Kwa hiyo akawaalika ndani na kuwapokea.
Siku iliyofuata akainuka na kwenda zake pamoja nao, na baadhi ya akina ndugu waliokuwa wametoka Yopa wakaenda pamoja naye. 24 Siku ya pili yake akaingia Kaisaria. Bila shaka, Kornelio alikuwa akiwatarajia naye alikuwa amewaita pamoja jamaa zake na marafiki wa karibu sana. 25 Petro alipokuwa akiingia, Kornelio akakutana naye, akaanguka chini kwenye miguu yake na kumsujudia. 26 Lakini Petro akamwinua, akisema: “Inuka; mimi mwenyewe pia ni binadamu.” 27 Naye alipokuwa akiongea naye akaingia na kukuta watu wengi wamekusanyika, 28 naye akawaambia: “Nyinyi mwajua jinsi ilivyo kinyume cha sheria kwa Myahudi kujiunga mwenyewe na mtu wa jamii nyingine au kumkaribia; na bado Mungu amenionyesha sipaswi kuita mtu yeyote kuwa najisi au si safi. 29 Kwa sababu hiyo nikaja, kwa kweli bila kupinga, nilipoitwa nije. Kwa hiyo naulizia habari kwenu ni sababu gani mliyoniitia nije.”
30 Basi Kornelio akasema: “Siku nne zilizopita kuhesabu kutoka saa hii nilikuwa nikisali katika nyumba yangu kwenye saa ya tisa, wakati, tazama! mwanamume aliyevaa vazi jangavu aliposimama mbele yangu 31 na kusema, ‘Kornelio, sala yako imesikiwa kwa kupendelewa na zawadi zako za rehema zimekumbukwa mbele ya Mungu. 32 Kwa hiyo, tuma watu waende Yopa na kumwita Simoni, aitwaye jina la ziada Petro. Mtu huyu anapokewa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji-ngozi, kando ya bahari.’ 33 Kwa hiyo mara moja nikatuma watu kwako, nawe ukafanya vema kuja hapa. Na kwa hiyo wakati huu sisi tupo sote mbele ya Mungu kuyasikia mambo yote ambayo umeamriwa na Yehova kusema.”
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake na kusema: “Kwa hakika nahisi kwamba Mungu si mwenye ubaguzi, 35 bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake. 36 Alituma neno kwa wana wa Israeli kuwatangazia habari njema ya amani kupitia Yesu Kristo: Huyu ni Bwana wa wengine wote. 37 Nyinyi mwaijua habari iliyoongewa kotekote katika Yudea yote, kuanzia Galilaya baada ya ubatizo aliohubiri Yohana, 38 yaani, Yesu aliyekuwa ametoka Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa roho takatifu na nguvu, naye akaenda akipita katika nchi akitenda mema na kuwaponya wote wale walioonewa na Ibilisi; kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. 39 Nasi ni mashahidi wa mambo yote aliyofanya katika nchi ya Wayahudi na pia katika Yerusalemu; lakini wao walimmaliza pia kwa kumwangika juu ya mti. 40 Mungu alimfufua Huyu katika siku ya tatu na kumruhusu awe dhahiri, 41 si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliowekwa rasmi kimbele na Mungu, kwetu sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kwake kutoka kwa wafu. 42 Pia, alituagiza sisi tuwahubiri watu na kutoa ushahidi kamili kwamba Huyu ndiye aliyeagizwa na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 Kwake yeye manabii wote hutoa ushahidi, kwamba kila mtu anayeweka imani katika yeye hupata msamaha wa dhambi kupitia jina lake.”
44 Petro alipokuwa bado akisema juu ya mambo haya roho takatifu ikaangukia wote wale wenye kusikia lile neno. 45 Na waaminifu waliokuwa wamekuja pamoja na Petro ambao walikuwa kati ya wale waliotahiriwa wakashangaa, kwa sababu zawadi ya bure ya roho takatifu ilikuwa ikimwagwa pia juu ya watu wa mataifa. 46 Kwa maana waliwasikia wakisema katika lugha na wakimtukuza Mungu. Ndipo Petro akajibu: 47 “Je, yeyote aweza kukataza maji kwamba hawa wasipate kubatizwa ambao wameipokea roho takatifu kama vile sisi tulivyoipokea?” 48 Ndipo akawaamuru wabatizwe katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae pamoja nao siku kadhaa.