Matendo
9 Lakini Sauli, bado akipumua tisho na uuaji-kimakusudi dhidi ya wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani wa cheo cha juu 2 na kumwomba barua za kwenda kwenye masinagogi katika Damasko, ili apate kuwaleta hadi Yerusalemu wakiwa wamefungwa wowote ambao angewapata walio wa Ile Njia, wanaume na pia wanawake.
3 Basi alipokuwa akisafiri alikaribia Damasko, wakati ghafula nuru kutoka mbinguni ilipomweka kumzunguka, 4 naye akaanguka kwenye ardhi na kusikia sauti ikimwambia: “Sauli, Sauli, kwa nini unaninyanyasa?” 5 Akasema: “Wewe ni nani, Bwana?” Akasema: “Mimi ni Yesu, ambaye wewe unanyanyasa. 6 Hata hivyo, inuka uingie katika jiji, na lile ambalo ni lazima ufanye utaambiwa.” 7 Basi wanaume waliokuwa wakisafiri pamoja naye walikuwa wamesimama bila kusema, wakisikia, kwa kweli, mvumo wa sauti, lakini bila kuona mtu yeyote. 8 Lakini Sauli akainuka kutoka kwenye ardhi, na ingawa macho yake yalifunguliwa alikuwa haoni kitu. Kwa hiyo wakamwongoza kwa kumshika mkono na kumpeleka kuingia katika Damasko. 9 Na kwa siku tatu hakuona kitu chochote, naye hakula wala kunywa.
10 Katika Damasko kulikuwa na mwanafunzi fulani aliyeitwa jina Anania, naye Bwana alimwambia katika ono: “Anania!” Yeye akasema: “Mimi hapa, Bwana.” 11 Bwana akamwambia: “Inuka, nenda kwenye barabara iitwayo Nyoofu, na kwenye nyumba ya Yudasi tafuta mtu aitwaye jina Sauli, kutoka Tarso. Kwa maana, tazama! yeye anasali, 12 na katika ono ameona mwanamume aitwaye jina Anania akiingia na kuweka mikono yake juu yake ili apate kuona tena.” 13 Lakini Anania akajibu: “Bwana, nimesikia kutoka kwa wengi juu ya mtu huyu, mambo mengi mabaya aliyowafanya watakatifu wako katika Yerusalemu. 14 Naye hapa ana mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwaweka vifungoni wote wale wanaoita jina lako.” 15 Lakini Bwana akamwambia: “Shika njia yako uende, kwa sababu mtu huyu ni chombo-kichaguliwa kwangu ili kupeleka jina langu kwa mataifa vilevile kwa wafalme na wana wa Israeli. 16 Kwa maana mimi nitamwonyesha wazi ni mambo mengi kama nini ambayo lazima ateseke kwa ajili ya jina langu.”
17 Kwa hiyo Anania akaenda zake na kuingia katika ile nyumba, naye akaweka mikono yake juu yake na kusema: “Sauli, ndugu, Bwana, yule Yesu aliyekutokea katika barabara uliyokuwa ukijia, amenituma, ili upate kuona tena na kujazwa roho takatifu.” 18 Na mara kukaanguka kutoka kwenye macho yake kile kilichoonekana kama magamba, naye akapata kuona tena; naye akainuka na kubatizwa, 19 naye akala chakula na kupata nguvu.
Kwa siku kadhaa akapata kuwa pamoja na wanafunzi katika Damasko, 20 na mara katika masinagogi akaanza kuhubiri juu ya Yesu, kwamba Huyu ndiye Mwana wa Mungu. 21 Lakini wote wale wenye kumsikia wakaingiwa na mshangao nao wakawa wakisema: “Je, huyu si yule mtu aliyewaharibu kabisa wale walio katika Yerusalemu waitiao jina hili, na aliyekuwa amekuja hapa kwa kusudi hilihili, ili apate kuwaongoza wakiwa wamefungwa hadi kwa makuhani wakuu?” 22 Lakini Sauli akafuliza kujipatia nguvu hata zaidi naye alikuwa akiwatatanisha Wayahudi waliokaa katika Damasko alipokuwa akithibitisha kwa mawazo yenye kufuatana vizuri kwamba huyu ndiye Kristo.
23 Sasa wakati siku nyingi zilipokuwa zikija kwenye ukomo, Wayahudi walifanya shauri pamoja kummaliza. 24 Hata hivyo, njama yao dhidi yake ikapata kujulikana kwa Sauli. Lakini walikuwa pia wakiyaangalia sana malango mchana na pia usiku ili kummaliza. 25 Kwa hiyo wanafunzi wake wakamchukua na kumshusha usiku kupitia kipenyo katika ukuta, wakimteremsha katika kapu.
26 Alipowasili Yerusalemu alifanya jitihada za kujiunga mwenyewe na wanafunzi; lakini wote walimwogopa, kwa sababu hawakuamini alikuwa mwanafunzi. 27 Kwa hiyo Barnaba akaja kumsaidia na kumwongoza kwa mitume, naye akawaambia kirefu jinsi katika barabara alivyokuwa amemwona Bwana na kwamba alikuwa amesema naye, na jinsi katika Damasko alivyokuwa amesema kwa ujasiri katika jina la Yesu. 28 Naye akaendelea kuwa pamoja nao, akitembea ndani na nje katika Yerusalemu, akisema kwa ujasiri katika jina la Bwana; 29 naye alikuwa akiongea na kubishana na Wayahudi wenye kusema Kigiriki. Lakini hawa wakafanya majaribio ya kummaliza. 30 Akina ndugu walipogundua hili, wakamteremsha hadi Kaisaria na kumtuma aende zake hadi Tarso.
31 Ndipo, kwa kweli, kutaniko kotekote katika Yudea na Galilaya na Samaria likaingia katika kipindi cha amani, likijengwa; nalo lilipokuwa likitembea katika hofu ya Yehova na katika faraja ya roho takatifu likafuliza kuzidi.
32 Sasa Petro alipokuwa akienda kupitia sehemu zote akateremka pia kwa watakatifu waliokaa Lida. 33 Huko akapata mwanamume fulani aliyeitwa jina Ainea, aliyekuwa amelala juu ya kitanda chake kwa miaka minane, kwa kuwa alikuwa amepooza. 34 Naye Petro akamwambia: “Ainea, Yesu Kristo akuponya wewe. Inuka na utandike kitanda chako.” Naye akainuka mara. 35 Na wote wale waliokaa Lida na uwanda wa Sharoni wakamwona, na hawa wakageuka kuelekea Bwana.
36 Lakini katika Yopa kulikuwako mwanafunzi fulani aliyeitwa jina Tabitha, ambalo, litafsiriwapo, lamaanisha Dorkasi. Yeye alizidi katika vitendo vyema na zawadi za rehema alizokuwa akitoa. 37 Lakini ilitukia kwamba siku hizo yeye akashikwa na ugonjwa akafa. Kwa hiyo wakamwogesha na kumlaza katika chumba cha juu. 38 Sasa kwa kuwa Lida lilikuwa karibu na Yopa, wanafunzi waliposikia kwamba Petro alikuwa katika jiji hilo wakatuma wanaume wawili kwake kumsihi sana: “Tafadhali usikawie kuja hadi kwetu sisi.” 39 Ndipo Petro akainuka na kwenda pamoja nao. Naye alipowasili, wakamwongoza kuingia katika chumba cha juu; na wajane wote wakajitokeza kwake wakitoa machozi na kuonyesha mavazi mengi ya ndani na mavazi ya nje ambayo Dorkasi alikuwa na kawaida ya kuyafanya alipokuwa pamoja nao. 40 Lakini Petro akaondoa kila mtu aende nje na, akikunja magoti yake, akasali, na, akigeukia ule mwili, akasema: “Tabitha, inuka!” Akafungua macho yake na, alipomwona mara hiyo Petro, akaketi wima. 41 Petro akimpa mkono wake, akamwinua, naye akawaita watakatifu na wajane na kumkabidhi akiwa hai. 42 Hili likapata kujulikana kotekote katika Yopa, na wengi wakawa waamini juu ya Bwana. 43 Kwa siku nyingi akabaki katika Yopa pamoja na Simoni fulani, mtengenezaji-ngozi.