Matendo
8 Sauli, kwa upande wake, alikuwa akikubali kuuawa kimakusudi kwake.
Katika siku hiyo mnyanyaso mkubwa ulitokea dhidi ya kutaniko lililokuwa katika Yerusalemu; wote isipokuwa mitume walitawanywa kotekote katika mikoa ya Yudea na Samaria. 2 Lakini wanaume wenye kumhofu Mungu wakamchukua Stefano hadi kwenye maziko, nao wakafanya maombolezo makubwa juu yake. 3 Ingawa hivyo, Sauli akaanza kushughulikia kutaniko kwa njia mbaya kabisa. Akivamia nyumba moja baada ya nyingine na, kukokota nje wanaume na pia wanawake, akawa akiwakabidhi gerezani.
4 Hata hivyo, wale waliokuwa wametawanywa walipita katika nchi wakitangaza habari njema ya lile neno. 5 Filipo, kwa upande wake, aliteremka kwenda jiji la Samaria na kuanza kuwahubiria Kristo. 6 Kwa umoja umati ulikuwa ukikazia uangalifu mambo yaliyosemwa na Filipo ulipokuwa ukisikiliza na kuzitazama ishara alizokuwa akifanya. 7 Kwa maana kulikuwa na wengi waliokuwa na roho wasio safi, na hawa walikuwa wakipaaza kilio kwa sauti kubwa na kutoka. Zaidi ya hayo, wengi waliokuwa wamepooza na walio vilema waliponywa. 8 Kwa hiyo kukaja kuwa na kadiri kubwa ya shangwe katika jiji hilo.
9 Sasa katika jiji hilo kulikuwa na mtu fulani aliyeitwa jina Simoni, ambaye, kabla ya hili, alikuwa amekuwa akifanya ufundi wa kimzungu na kushangaza taifa la Samaria, akisema yeye mwenyewe alikuwa mtu mkubwa. 10 Na wote, kutoka aliye mdogo zaidi sana mpaka aliye mkubwa zaidi sana, walikuwa wakimkazia uangalifu na kusema: “Mtu huyu ndiye Nguvu ya Mungu, iwezayo kuitwa Kubwa.” 11 Kwa hiyo walikuwa wakimkazia uangalifu kwa sababu ya kuwa aliwashangaza kwa muda mwingi kwa ufundi wake wa kimzungu. 12 Lakini walipomwamini Filipo, aliyekuwa akitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu na juu ya jina la Yesu Kristo, waliendelea kubatizwa, wanaume na pia wanawake. 13 Simoni mwenyewe pia akawa mwamini, na, baada ya kubatizwa, akawa akimhudumia Filipo daima; naye alishangaa kwa kuona ishara na kazi kubwa zenye nguvu zikitendeka.
14 Wakati mitume katika Yerusalemu waliposikia kwamba Samaria ilikuwa imelikubali neno la Mungu, wakatuma Petro na Yohana kwao; 15 na hawa wakateremka kwenda na kusali kwa ajili yao wapate roho takatifu. 16 Kwa maana ilikuwa haijaanguka bado juu ya yeyote kati yao, bali walikuwa wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. 17 Ndipo wakaanza kuweka mikono yao juu yao, nao wakaanza kupokea roho takatifu.
18 Sasa wakati Simoni alipoona kwamba roho ilipewa kupitia kuwekewa mikono ya mitume, aliwatolea fedha, 19 akisema: “Nipeni mimi pia mamlaka hii, ili yeyote ambaye mimi naweka mikono yangu juu yake apate kupokea roho takatifu.” 20 Lakini Petro akamwambia: “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu kupitia fedha ulifikiri kupata umiliki wa zawadi ya bure ya Mungu. 21 Wewe huna sehemu wala fungu katika jambo hili, kwa maana moyo wako si mnyoofu mbele ya macho ya Mungu. 22 Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu, na omba dua kwa Yehova ili, ikiwezekana, upate kusamehewa mbinu ya moyo wako; 23 kwa maana naona wewe ni nyongo yenye sumu na kifungo cha ukosefu wa uadilifu.” 24 Kwa kujibu Simoni akasema: “Nyinyi watu, fanyeni ombi la dua kwa Yehova kwa ajili yangu ili hata moja kati ya mambo mliyosema lisipate kuja juu yangu.”
25 Kwa hiyo, walipokuwa wametoa ushahidi kikamili na wakiwa wamelisema neno la Yehova, wakageuka kurudi Yerusalemu, nao wakaenda wakitangaza habari njema kwenye vijiji vingi vya Wasamaria.
26 Hata hivyo, malaika wa Yehova akasema na Filipo, akisema: “Inuka na uende kusini kwenye barabara iteremkayo chini kutoka Yerusalemu hadi Gaza.” (Hii ni barabara ya jangwani.) 27 Ndipo yeye akainuka akaenda, na, tazama! towashi Mwethiopia, mwanamume aliye na mamlaka chini ya Kandake malkia wa Waethiopia, na ambaye alikuwa juu ya hazina yote ya malkia. Yeye alikuwa ameenda Yerusalemu kuabudu, 28 lakini alikuwa akirudi na alikuwa ameketi katika gari lake na akimsoma kwa sauti kubwa nabii Isaya. 29 Kwa hiyo roho ikamwambia Filipo: “Karibia ujiunge mwenyewe na gari hili.” 30 Filipo akakimbia kandokando na kumsikia akimsoma kwa sauti kubwa Isaya nabii, naye akasema: “Je, wewe kwa hakika wajua unayoyasoma?” 31 Akasema: “Kwa kweli, ningewezaje kufanya hivyo, isipokuwa mtu fulani angeniongoza?” Naye akamsihi Filipo kwa bidii apande na kuketi pamoja naye. 32 Sasa kifungu cha Andiko alichokuwa akisoma kwa sauti kubwa kilikuwa hiki: “Kama kondoo aliletwa kwenye machinjo, na kama mwana-kondoo asiye na sauti mbele ya mnyoaji wake, ndivyo yeye asivyofungua kinywa chake. 33 Wakati wa kutwezwa kwake hukumu iliondolewa mbali kutoka kwake. Ni nani atakayeeleza kirefu habari za kizazi chake? Kwa sababu uhai wake waondolewa kutoka dunia.”
34 Kwa kujibu yule towashi akamwambia Filipo: “Nakuomba, Ni juu ya nani nabii asema hili? Juu yake mwenyewe au juu ya mtu fulani mwingine?” 35 Filipo akafungua kinywa chake na, akianza na Andiko hilo, akamtangazia habari njema juu ya Yesu. 36 Sasa walipokuwa wakienda juu ya ile barabara, walikuja kwenye maji fulani, na towashi akasema: “Tazama! Maji; ni nini chenye kunizuia nisibatizwe?” 37 —— 38 Ndipo yeye akaamuru gari lisimame, nao wote wawili wakateremka kwenda kuingia katika maji, Filipo na pia towashi; naye akambatiza. 39 Walipokuwa wamepanda kutoka kwenye maji, roho ya Yehova ikamwondoa Filipo upesi, na towashi hakumwona tena kamwe, kwa maana alifuliza kwenda njia yake akishangilia. 40 Lakini Filipo akaonekana katika Ashdodi, naye akaenda akipita katika hilo eneo na kufuliza kuitangaza habari njema kwa majiji yote mpaka alipofika Kaisaria.