Matendo
7 Lakini kuhani wa cheo cha juu akasema: “Je, mambo haya ndivyo yalivyo?” 2 Yeye akasema: “Wanaume, akina ndugu na akina baba, sikieni. Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu wa zamani Abrahamu alipokuwa katika Mesopotamia, kabla ya yeye kuanza kukaa katika Harani, 3 naye akamwambia, ‘Nenda utoke katika nchi yako na kutoka katika jamaa zako na uje hadi kuingia katika nchi ambayo nitakuonyesha wewe.’ 4 Ndipo akaenda kutoka nchi ya Wakaldayo na kuanza kukaa katika Harani. Na kutoka huko, baada ya baba yake kufa, Mungu akamsababisha abadili makao yake hadi kwenye nchi hii ambamo nyinyi sasa mwakaa. 5 Na bado yeye hakumpa miliki yoyote yenye kurithiwa ndani yalo, la, hata upana wa wayo; bali aliahidi kumpa yeye hiyo kuwa miliki, na baada yake mbegu yake, wakati alipokuwa bado hana mtoto. 6 Zaidi ya hayo, Mungu alisema kama hivi, kwamba mbegu yake wangekuwa wakazi wa kutoka nchi nyingine katika nchi ya ugenini na wale watu wangewafanya watumwa na kuwataabisha kwa miaka mia nne. 7 ‘Na taifa lile ambalo hakika watalitumikia kama watumwa nitalihukumu,’ Mungu akasema, ‘na baada ya mambo haya watatoka hakika na kunitolea utumishi mtakatifu mahali hapa.’
8 “Alimpa pia agano la tohara; na hivyo akawa baba ya Isaka na kumtahiri siku ya nane, na Isaka baba ya Yakobo, na Yakobo baba ya vile vichwa vya familia kumi na viwili. 9 Na vile vichwa vya familia vikawa na wivu juu ya Yosefu na kumuuza katika Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10 naye akamkomboa kutoka katika dhiki zake zote na kumpa wema na hekima mbele ya macho ya Farao mfalme wa Misri. Naye akamweka rasmi aongoze Misri na nyumba yake yote. 11 Lakini njaa kali ikaja juu ya Misri yote na Kanaani, hata dhiki kubwa; na baba zetu wa zamani hawakuwa wakipata maakuli yoyote. 12 Lakini Yakobo akasikia kulikuwa na vyakula katika Misri naye akatuma nje baba zetu wa zamani mara ya kwanza. 13 Na katika mara ya pili Yosefu akajulishwa kwa ndugu zake; na ukoo wa familia ya Yosefu ukawa dhahiri kwa Farao. 14 Kwa hiyo Yosefu akatuma watu waite Yakobo baba yake na jamaa zake wote kutoka mahali hapo, wenye kufikia idadi ya nafsi sabini na tano. 15 Yakobo akateremka kwenda kuingia katika Misri. Naye akafa; na ndivyo baba zetu wa zamani, 16 nao wakahamishwa hadi Shekemu na kulazwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kwa bei fulani na sarafu ya fedha kutoka kwa wana wa Hamori katika Shekemu.
17 “Wakati ule tu ulipokuwa ukikaribia kwa ajili ya utimizo wa ahadi ambayo Mungu alikuwa amemtangazia Abrahamu waziwazi, watu walikua na kuzidi katika Misri, 18 mpaka kukainuka mfalme tofauti juu ya Misri, ambaye hakujua habari za Yosefu. 19 Huyu alitumia mbinu ya kiserikali dhidi ya jamii yetu na kulazimisha kimakosa akina baba watie hatarini vitoto vyao vichanga, ili visipate kuhifadhiwa hai. 20 Katika wakati maalumu huo Musa alizaliwa, naye alikuwa mzuri kwa njia ya kimungu. Naye alinyonyeshwa miezi mitatu nyumbani mwa baba yake. 21 Lakini alipotolewa nje, binti ya Farao alimwokota na kumlea kama mwana wake mwenyewe. 22 Kwa sababu hiyo Musa akafunzwa katika hekima yote ya Wamisri. Kwa kweli, yeye alikuwa mwenye nguvu katika maneno na vitendo.
23 “Sasa wakati wa mwaka wake wa arobaini ulipokuwa ukitimizwa, ikaja ndani ya moyo wake kufanya ukaguzi wa ndugu zake, wana wa Israeli. 24 Naye alipoona mara hiyo mtu fulani akitendwa isivyo haki, alimtetea na kutekeleza kisasi kwa ajili ya yule mwenye kutendwa vibaya kwa kumpiga hata chini Mmisri. 25 Alikuwa akidhani ndugu zake wangefahamu ya kwamba Mungu alikuwa akiwapa wao wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu hilo. 26 Na siku iliyofuata akawatokea walipokuwa wakipigana, naye akajaribu kuwapatanisha tena wawe na amani, akisema, ‘Wanaume, nyinyi ni ndugu. Kwa nini mwatendeana isivyo haki?’ 27 Lakini yeye aliyekuwa akimtendea jirani yake isivyo haki akamsukumia mbali, akisema, ‘Nani aliyekuweka wewe rasmi kuwa mtawala na hakimu juu yetu? 28 Je, wewe wataka kunimaliza kwa namna ileile uliyommaliza Mmisri jana, sivyo?’ 29 Kwa usemi huo Musa akaanza kukimbia na kuwa mkazi wa nchi ya Midiani kutoka nchi nyingine, ambako alipata kuwa baba ya wana wawili.
30 “Na miaka arobaini ilipotimizwa, kulitokea kwake katika nyika ya Mlima Sinai malaika katika mwali wa moto wa kijiti cha miiba. 31 Sasa Musa alipouona alistaajabia hilo ono. Lakini alipokuwa akikaribia ili kuchunguza, sauti ya Yehova ikaja, 32 ‘Mimi ndiye Mungu wa baba zako wa zamani, Mungu wa Abrahamu na wa Isaka na wa Yakobo.’ Akiwa ameshikwa na mtetemeko, Musa hakuthubutu kuchunguza zaidi. 33 Yehova akamwambia, ‘Vua makubazi miguuni mwako, kwa maana mahali ambapo wewe umesimama ni ardhi takatifu. 34 Kwa hakika nimeona kutendwa kimakosa kwa watu wangu walio katika Misri, nami nimesikia kupiga kite kwao na nimeteremka ili kuwakomboa. Na sasa njoo, hakika mimi nitakutuma uende zako Misri.’ 35 Musa huyu, ambaye wao walimkana, wakisema, ‘Nani aliyekuweka wewe rasmi kuwa mtawala na hakimu?’ mtu huyu Mungu alimtuma aende zake akiwa mtawala na pia mkombozi kwa mkono wa malaika aliyemtokea katika kile kijiti cha miiba. 36 Mtu huyu aliwaongoza watoke baada ya kufanya mambo ya ajabu na ishara katika Misri na katika Bahari Nyekundu na katika nyika kwa miaka arobaini.
37 “Huyu ndiye Musa aliyewaambia wana wa Israeli, ‘Mungu atawainulia kutoka miongoni mwa ndugu zenu nabii kama mimi.’ 38 Huyu ni yeye aliyekuja kuwa miongoni mwa kutaniko katika nyika pamoja na malaika aliyesema juu ya Mlima Sinai na pamoja na baba zetu wa zamani, naye akapokea matamko matakatifu yaliyo hai ili awape nyinyi. 39 Baba zetu wa zamani walikataa kuwa watiifu kwake, bali wakamsukumia kando na katika mioyo yao wakageuka kurudi Misri, 40 wakimwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu iende mbele yetu. Kwa maana Musa huyu, aliyetuongoza tutoke nchi ya Misri, sisi hatujui lile ambalo limetukia kwake.’ 41 Kwa hiyo wakafanya ndama siku hizo wakailetea dhabihu hiyo sanamu na kuanza kujifurahisha wenyewe katika kazi za mikono yao. 42 Kwa hiyo Mungu akageuka na kuwakabidhi watoe utumishi mtakatifu kwa jeshi la mbinguni, kama vile imeandikwa katika kitabu cha manabii, ‘Haikuwa kwangu mimi kwamba nyinyi mlitoa kafara na dhabihu kwa miaka arobaini nyikani, sivyo, Ewe nyumba ya Israeli? 43 Bali ni hema la Moloki na nyota ya mungu Refani ambavyo nyinyi mlichukua, maumbo ambayo nyinyi mliyafanya ili kuyaabudu. Kwa sababu hiyo hakika mimi nitawahamisha nyinyi ng’ambo ya Babiloni.’
44 “Baba zetu wa zamani walikuwa na hema la ushahidi nyikani, kama vile yeye alivyotoa maagizo alipokuwa akisema na Musa ili kulifanya kulingana na kiolezo alichokuwa ameona. 45 Na baba zetu wa zamani waliolirithi waliliingiza pamoja na Yoshua ndani ya nchi iliyomilikiwa na mataifa, ambayo Mungu aliyafukuza kutoka mbele ya baba zetu wa zamani. Hapo lilibaki hadi siku za Daudi. 46 Yeye alipata upendeleo mbele ya macho ya Mungu na kuomba pendeleo la kuandaa kao kwa ajili ya Mungu wa Yakobo. 47 Hata hivyo, Solomoni alimjengea yeye nyumba. 48 Ingawa hivyo, Aliye Juu Zaidi Sana hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono; kama vile nabii asemavyo, 49 ‘Mbingu ni kiti changu cha ufalme, nayo dunia ni kibago cha miguu yangu. Ni nyumba ya namna gani ambayo mtanijengea mimi? Yehova asema. Au ni mahali pangu gani pa kupumzika? 50 Mikono yangu ilifanya vitu vyote hivi, sivyo?’
51 “Nyinyi watu wenye shingo ngumu na wasiotahiriwa katika mioyo na masikio, sikuzote mnaikinza roho takatifu; kama baba zenu wa zamani walivyofanya, ndivyo nyinyi mfanyavyo. 52 Ni yupi kati ya manabii ambaye baba zenu wa zamani hawakumnyanyasa? Ndiyo, waliwaua wale waliofanya tangazo kimbele kuhusu kuja kwa Aliye mwadilifu, ambaye nyinyi sasa mmekuwa wasaliti na wauaji-kimakusudi wake, 53 nyinyi mliopokea Sheria kama ilivyopitishwa na malaika lakini hamkuishika.”
54 Basi, waliposikia mambo haya wakahisi wamekatwa hadi kwenye mioyo yao na kuanza kumsagia meno yao. 55 Lakini yeye, akiwa amejaa roho takatifu, alikodoa macho ndani ya mbingu akaona mara hiyo utukufu wa Mungu na wa Yesu akiwa amesimama kwenye mkono wa kuume wa Mungu, 56 naye akasema: “Tazameni! Naziona mbingu zimefunguliwa na Mwana wa binadamu akiwa amesimama kwenye mkono wa kuume wa Mungu.” 57 Ndipo wakapaaza kilio kwa sauti ya juu na kuweka mikono yao juu ya masikio yao wakamrukia kwa umoja. 58 Na baada ya kumtupa nje ya jiji, wakaanza kumtupia mawe. Na wale mashahidi wakaweka chini mavazi yao ya nje kwenye miguu ya mwanamume kijana aliyeitwa Sauli. 59 Nao wakaendelea kumtupia Stefano mawe alipokuwa akitoa ombi na kusema: “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Ndipo, akikunja magoti yake, akapaaza kilio kwa sauti yenye nguvu: “Yehova, usihesabu dhambi hii dhidi yao.” Na baada ya kusema hilo akalala usingizi katika kifo.