1 Wakorintho
2 Na kwa hiyo mimi, nilipowajia nyinyi, akina ndugu, nikiwatangazia siri ya Mungu, sikuja nikiwa na usemi wenye kupita kiasi wala wa hekima nikiwatangazia siri takatifu ya Mungu. 2 Kwa maana niliamua kutojua kitu chochote miongoni mwenu ila Yesu Kristo, naye akiwa aliyetundikwa mtini. 3 Nami niliwajia katika udhaifu na katika hofu na kwa kutetemeka sana; 4 na usemi wangu na lile nililohubiri halikuwa kwa maneno yenye ushawishi ya hekima bali kwa wonyesho wa roho na nguvu, 5 ili imani yenu ipate kuwa, si katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu ya Mungu.
6 Sasa twasema hekima miongoni mwa wale walio wakomavu, lakini si hekima ya mfumo huu wa mambo wala ile ya watawala wa mfumo huu wa mambo, ambao watapaswa kuwa si kitu. 7 Bali twasema hekima ya Mungu katika siri takatifu, hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliagiza kimbele kabla ya mifumo ya mambo kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hekima hii hakuna hata mmoja wa watawala wa mfumo huu wa mambo aliyekuja kuijua, kwa maana kama wao wangaliijua hawangalimtundika mtini Bwana mwenye utukufu. 9 Lakini kama vile imeandikwa: “Jicho halijaona na sikio halijasikia, wala hayajawaziwa katika moyo wa mwanadamu mambo ambayo Mungu amewatayarishia wampendao.” 10 Kwa maana ni kwetu sisi Mungu ameyafunua kupitia roho yake, kwa maana roho huchunguza ndani ya mambo yote, hata mambo yenye kina kirefu ya Mungu.
11 Kwa maana ni nani miongoni mwa wanadamu ayajuaye mambo ya mwanadamu isipokuwa roho ya mwanadamu iliyo katika yeye? Hivyo, pia, hakuna mwanadamu ambaye amekuja kuyajua mambo ya Mungu, isipokuwa roho ya Mungu. 12 Basi sisi tulipokea, si roho ya ulimwengu, bali roho itokayo kwa Mungu, ili tupate kuyajua mambo ambayo tumepewa kwa fadhili na Mungu. 13 Mambo hayo twayasema pia, si kwa maneno yafundishwayo na hekima ya kibinadamu, bali kwa yale yafundishwayo na roho, tuunganishapo mambo ya kiroho pamoja na maneno ya kiroho.
14 Lakini mtu wa kimwili hayapokei mambo ya roho ya Mungu, kwa maana hayo ni upumbavu kwake; naye hawezi kupata kuyajua, kwa sababu hayo huchunguzwa kiroho. 15 Hata hivyo, kwa kweli mtu wa kiroho huchunguza mambo yote, lakini yeye mwenyewe hachunguzwi na mwanadamu yeyote. 16 Kwa maana “ni nani amekuja kuijua akili ya Yehova, kwamba apate kumfundisha?” Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.