1 Wakorintho
3 Na kwa hiyo, akina ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wa kiroho, bali kama na watu wa kimwili, kama na vitoto katika Kristo. 2 Niliwalisha nyinyi maziwa, si kitu cha kula, kwa maana mlikuwa bado hamna nguvu za kutosha. Kwa kweli, wala sasa hamna nguvu za kutosha, 3 kwa maana bado nyinyi ni wa kimwili. Kwa maana kukiwa kuna wivu na zogo miongoni mwenu, je, nyinyi si wa kimwili na je, hamtembei kama wanadamu? 4 Kwa maana mmoja asemapo: “Mimi ni wa Paulo,” lakini mwingine asema: “Mimi ni wa Apolo,” je, nyinyi si wanadamu tu?
5 Basi, Apolo ni nini? Ndiyo, Paulo ni nini? Wahudumu ambao kupitia wao mlipata kuwa waamini, kama vile Bwana alivyoruhusu kila mmoja. 6 Mimi nilipanda, Apolo akatia maji, lakini Mungu akafuliza kuikuza; 7 hivi kwamba yeye apandaye si kitu chochote wala yeye atiaye maji, bali Mungu aikuzaye. 8 Basi yeye apandaye na yeye atiaye maji ni mmoja, lakini kila mtu atapokea thawabu yake mwenyewe kulingana na kazi yake mwenyewe yenye jasho. 9 Kwa maana sisi ni wafanyakazi wenzi wa Mungu. Nyinyi watu ni shamba la Mungu lenye kulimwa, jengo la Mungu.
10 Kulingana na fadhili isiyostahiliwa ya Mungu niliyopewa, kama mwelekezi wa kazi za ufundi mwenye hekima niliweka msingi, lakini mtu mwingine anajenga juu ya huo. Lakini acheni kila mmoja afulize kuangalia ni jinsi gani anavyojenga juu ya huo. 11 Kwa maana hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine wowote zaidi kuliko uliowekwa, ambao ni Yesu Kristo. 12 Basi yeyote akijenga juu ya huo msingi, dhahabu, fedha, mawe yenye bei, vifaa vya mbao, nyasi kavu, mabua, 13 kazi ya kila mmoja itakuwa dhahiri, kwa maana ile siku itaifichua, kwa sababu itafunuliwa kwa njia ya moto; na moto wenyewe utathibitisha ni ya namna gani kazi ya kila mmoja. 14 Kazi ya yeyote ambayo ameijenga juu ya huo ikibaki, atapokea thawabu; 15 kazi ya yeyote ikichomwa kabisa, atapata hasara, lakini yeye mwenyewe ataokolewa; lakini, ikiwa ndivyo, itakuwa ni kama kupitia moto.
16 Je, hamjui kwamba nyinyi watu ni hekalu la Mungu, na kwamba roho ya Mungu hukaa katika nyinyi? 17 Yeyote akiliangamiza hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, hekalu ambalo ni nyinyi watu.
18 Acheni yeyote asiwe akijishawishi mwenyewe: Ikiwa yeyote miongoni mwenu afikiri yeye ni mwenye hekima katika mfumo huu wa mambo, acheni yeye awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu; kwa maana imeandikwa: “Yeye hunasa wenye hekima katika ujanja wao wenyewe.” 20 Na tena: “Yehova ajua kwamba mawazowazo ya watu wenye hekima ni ya ubatili.” 21 Kwa sababu hiyo acheni yeyote asiwe akijisifu katika watu; kwa maana vitu vyote ni vyenu, 22 kama ni Paulo au Apolo au Kefa au ulimwengu au uhai au kifo au mambo yaliyo hapa sasa au mambo yatakayopaswa kuja, vitu vyote ni vyenu; 23 nanyi ni wa Kristo; naye Kristo ni wa Mungu.