-
Kumbukumbu la Torati 14:4-20Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya
-
-
4 Hawa ndio wanyama mnaoweza kula:+ ng’ombe, kondoo, mbuzi, 5 paa, swala, kulungu, mbuzi mwitu, mbawala, kondoo mwitu, na kondoo wa mlimani. 6 Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizopasuka na zilizogawanyika mara mbili na ambaye anacheua. 7 Lakini hampaswi kuwala wanyama wafuatao wanaocheua au wenye kwato zilizogawanyika: ngamia, sungura, na wibari, kwa sababu wanacheua lakini kwato zao hazijapasuka. Wao si safi kwenu.+ 8 Pia, msimle nguruwe kwa sababu ana kwato zilizopasuka lakini hacheui. Yeye si safi kwenu. Msile kamwe nyama yao wala kugusa mizoga yao.
9 “Kati ya viumbe wote wanaoishi ndani ya maji, mnaweza kula wafuatao: Mnaweza kumla kiumbe yeyote mwenye mapezi na magamba.+ 10 Lakini hampaswi kumla kiumbe yeyote ambaye hana mapezi na magamba. Yeye si safi kwenu.
11 “Mnaweza kumla ndege yeyote aliye safi. 12 Lakini hampaswi kuwala ndege wafuatao: tai, furukombe, tumbusi mweusi,*+ 13 mwewe mwekundu, mwewe mweusi, kila aina ya ndege mbua, 14 kila aina ya kunguru, 15 mbuni, bundi, shakwe, kila aina ya kipanga, 16 bundi mdogo, bundi mwenye masikio marefu, batamaji, 17 mwari, tumbusi, mnandi, 18 korongo, kila aina ya kulastara, hudihudi, na popo. 19 Pia, kila kiumbe* mwenye mabawa anayeishi katika makundi makubwa si safi kwenu. Hawapaswi kuliwa. 20 Mnaweza kumla kiumbe yeyote safi anayeruka.
-