Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani
Sehemu ya 7: Utafutaji wa Kisiasa wa Serikali Kamilifu Isiyopatikana
Usoshalisti: mfumo wa ujamaa ambao hutetea umiliki na udhibiti wa Taifa wa njia za uzalishaji ambao wakomunisti huuona kuwa hatua ya kati baina ya ubepari na ukomunisti; Ukomunisti: mfumo wa kijamii ambao hutetea kutokuwapo kwa tabaka za watu, umiliki wa pamoja wa uzalishaji chakula, na kugawanywa kwa bidhaa kwa usawa.
HEKAYA ya Kigiriki husema juu ya mungu wa Wagiriki aitwaye Cronus, ambaye wakati wa utawala wake Ugiriki ulifurahia sana muhula wenye amani na ufanisi. “Wote walishirikiana vitu vyote kwa usawa, umiliki wa vitu vya kibinafsi haukuwapo, na amani na upatano zilitawala bila kukatizwa,” yaeleza Dictionary of the History of Ideas. Kamusi hiyo inaongezea: “Dalili za kwanza za usoshalisti zinaonekana katika kuombolezea ‘enzi ya amani na ufanisi.’”
Hata hivyo, usoshalisti ulikuja kuonekana kwa mara ya kwanza ukiwa harakati ya ki-siku-hizi ya kisiasa katika miongo ya mapema na ya katikati ya karne ya 19. Ilikubaliwa mara moja, hasa katika Ufaransa, ambako Mapinduzi ya Ufaransa yalikuwa yametikisa sana maoni yaliyokuwapo tangu zamani. Mvuvumko wa viwanda ulisababisha matatizo mabaya ya kijamii huko kama ilivyokuwa na nchi nyinginezo za Ulaya. Watu walikuwa tayari kwa wazo la kwamba kumiliki mali kwa umma badala ya kwa watu binafsi kungewezesha umma washirikiane kwa usawa zaidi mavuno ya kazi ya ushirikiano.
Usoshalisti si jambo geni. Wanafalsafa Wagiriki Aristotle na Plato waliandika juu ya huo. Baadaye katika karne ya 16 wakati wa Marekebisho ya Kiprotestanti, Thomas Müntzer, kasisi Mjerumani wa Katoliki mwenye kupendelea mageuzo makubwa, alidai kuwe na jamii isiyo na tabaka za vyeo mbalimbali. Lakini maoni yake yalikuwa yenye kuzusha upinzani, hasa mwito wake wa kuwa na mapinduzi, ikihitajika, ili kutimiza mradi huo. Katika karne ya 19, Robert Owen kutoka Wales, Wafaransa Étienne Cabet na Pierre-Joseph Proudhon, na wengine wengi wa kupendelea marekebisho ya kijamii, wakiwamo ndani yao makasisi mashuhuri, walifundisha kwamba usoshalisti ulikuwa tu Ukristo kwa jina jingine.
Serikali Kamilifu za Marx na More Ambazo Hazikupatikana
Lakini “hakuna wowote wa watetezi hao wa usoshalisti aliyekuwa mwenye matokeo makubwa yenye kulinganika na yale yaliyotokezwa na Karl Marx, ambaye maandishi yake yalipata kuwa ndio mwanzo wa fikira na vitendo vya kisoshalisti,” chasema kitabu cha marejezo kilichotajwa juu.”a Marx alifundisha kwamba kupitia mashindano ya tabaka, historia husonga mbele hatua kwa hatua; mara tu mfumo wa kisiasa unaofaa kabisa ukiisha kupatikana, historia kwa maana hiyo itakoma. Mfumo huo unaofaa utatatua matatizo ya jamii zilizopita. Kila mmoja ataishi kwa amani, uhuru, na ufanisi, bila uhitaji wa kwamba serikali ziweko au majeshi.
Hilo laonekana kuwa karibu sana kufanana na yale aliyoeleza Sir Thomas More katika kitabu chake Utopia mwaka wa 1516. Neno hilo, ambalo ni jina la Kigiriki lililobuniwa na More, linamaanisha “si mahali” (ou-topos), na huenda neno hilo likawa lilitumiwa kwa mchezo wa maneno na neno jingine kama hilo eu-topos, linalomaanisha “mahali pazuri.” Utopia (serikali kamilifu isiyopatikana) ambayo More aliandika juu yayo ilikuwa ni nchi ya kuwaziwa tu (si mahali) ambayo, hata hivyo, ilikuwa nchi nzuri kabisa (mahali pazuri). Hivyo, “Utopia” limekuja kumaanisha “mahali pa ukamilifu kabisa hasa katika mambo ya sheria, serikali, na hali za kijamii.” Kitabu cha More kilikuwa shtaka la wazi juu ya hali za kiuchumi na kijamii zilizozorota ambazo zilienea wakati wake katika Ulaya na hasa Uingereza, na baadaye zikachangia ukuzi wa usoshalisti.
Nadharia za Marx zilifanana pia na maoni ya mwanafalsafa Mjerumani Georg Wilhelm Friedrich Hegel. Kulingana na Dictionary of the History of Ideas, “ile hali ya uanadini nusunusu ya usoshalisti wa Marx wa uangamizaji ilifanyizwa na Hegel kwa kutumia falsafa kurudisha theolojia ya Kikristo yenye kutaka mapinduzi makubwa.” Kwa kufuatia hali hiyo ya “theolojia ya Kikristo yenye kutaka mapinduzi makubwa,” Marx alisitawisha “uvutio wenye nguvu sana kiadili, wenye kutegemezwa na usadikisho wa uanadini nusunusu,” aeleza mtungaji Georg Sabine. Uvutuo huo ulikuwa wa kujiunga kabisa na mwendo wa kuelekea ustaarabu na haki.” Usoshalisti ukawa ndio mtindo wa wakati ujao; wengine walifikiri kwamba labda huo ulikuwa kwa kweli ni Ukristo ukisonga mbele kwenye ushindi ukiwa na jina jipya!
Kutoka Ubepari Hadi Serikali Kamilifu
Marx aliweza kuishi hadi kuchapisha buku la kwanza tu la kazi yake Das Kapital. Mabuku mawili ya mwisho yalihaririwa na kuchapishwa katika 1885 na jingine katika 1894 na mwenzi wake wa karibu zaidi, Friedrich Engels, ambaye alikuwa ni mwanafalsafa wa kisoshalisti Mjerumani. Das Kapital lilichukua jukumu la kueleza historia ya nyuma ya ubepari, ambayo ni aina ya mfumo wa kiuchumi wa demokrasi ya Magharibi. Ukitegemeza biashara isiyorekebiwa na sheria na iliyo na ushindani usiodhibitiwa na Taifa, ubepari kama ulivyoelezwa na Marx huweka umiliki wa njia za uzalishaji na ugawanyaji katika mikono ya watu binafsi na mashirika. Kulingana na Marx, ubepari hutokeza tabaka ya jamii ya kati na tabaka ya jamii ya wafanya kazi, hiyo ikitokeza uadui kati ya tabaka hizo mbili na kuiletea uonevu tabaka ya wafanya kazi. Akitumia maandishi ya wanauchumi yaliyo sahihi ili kutegemeza maoni yake, Marx alibisha kwamba ubepari kwa hakika si demokrasi, na kwamba usoshalisti ndio demokrasi halisi, ukisaidia watu kwa kuinua usawa na uhuru wa kibinadamu.
Serikali kamilifu ingefikiwa mara tu tabaka ya akina yahe ikiinuka katika mapinduzi na kutupilia mbali uonevu wa tabaka ya wenye mali, na kuweka kile ambacho Marx alikiita “udikteta wa wafanya kazi.” (Ona sanduku, ukurasa 21.) Hata hivyo, maoni yake yalilainika muda ulipopita. Akaanza kukubali mawazo mawili tofauti ya mapinduzi, moja la kutumia nguvu na jingine lenye kudumu, la pole kwa pole. Hilo likazusha swali lenye kupendeza.
Serikali Kamilifu kwa Njia ya Mapinduzi au Mageuzi?
“Ukomunisti unatokana na neno la Kilatini communis, linalomaanisha “-a kawaida, -a watu wote.” Kama ilivyo na usoshalisti, ukomunisti hudai kwamba uchumi huru huongoza kwenye ukosefu wa kazi, umaskini, kufanyika kwa biashara kati ya watu wale wale, na mahitilafiano juu ya kusimamia kazi. Suluhisho kwa matatizo hayo ni kugawa mali ya taifa kwa usawa na kwa haki zaidi.
Lakini kufikia mwisho wa karne iliyopita, wafuasi wa Marx tayari walikuwa wakibishana juu ya namna ya kutekeleza makusudi hayo yaliyokuwa yamekwisha kukubaliwa. Katika miaka ya mapema ya 1900, ile sehemu ya harakati ya kisoshalisti iliyopinga mapinduzi ya kutumia nguvu na kupendelea kufanya kazi kulingana na mfumo wa kidemokrasi wa bunge ilizidi kupata nguvu, ikisitawi kuwa kile ambacho sasa huitwa usoshalisti wa kidemokrasi. Huo ndio usoshalisti unaopatikana leo katika demokrasi nyingi kama vile Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. Kwa vyovyote vile, vyama hivyo vimekataa fikira halisi za Marx na vinapendezwa tu na kufanyiza hali njema ya raia wavyo.
Hata hivyo, mfuasi mmoja wa Marx aliyejitoa na aliyeshikilia sana kwamba Serikali Kamilifu ingeweza kupatikana tu kupitia mapinduzi ya kutumia nguvu alikuwa ni Lenin. Mafundisho yake, pamoja na ya Marx, hutumika kuwa msingi wa ukomunisti halisi leo. Lenin, ambalo ni jina la kubuniwa la Vladimir Ilich Ulyanov, alizaliwa katika 1870 katika ile ambayo sasa ni Urusi. Aligeuka akawa mfuasi wa Marx katika 1889. Baada ya 1900, kufuatia maisha ya uhamishoni kule Siberia, aliishi sana sana katika Ulaya Magharibi. Utawala wa czar ulipopinduliwa, alirudi Urusi, akaanzisha Chama cha Kikomunisti cha Urusi, na kuongoza Mapinduzi ya Bolshevik ya 1917. Baada ya hapo alitumika akiwa mkuu wa Urusi hadi kifo chake katika 1924. Alikiona Chama cha Kikomunisti kuwa chenye nidhamu ya hali ya juu, chenye uongozi mmoja wa kikundi cha wanamapinduzi wanaotumika wakiwa watetezi wa akina yahe. Wamensheviki hawakukubaliana.—Ona kisanduku, ukurasa wa 30.
Mpaka ulio kati ya mapinduzi na mageuzi hautambuliwi tena waziwazi sana. Kitabu Comparing Political Systems: Power and Policy in Three Worlds kilionelea hivi katika 1978: “Ukomunisti umekuwa kigeugeu juu ya jinsi ya kutekeleza miradi ya Kisoshalisti. . . . Tofauti kati ya Ukomunisti na Usoshalisti wa Kidemokrasi umepunguzwa sana.” Sasa, katika 1990, maneno hayo yapata umaana zaidi wakati ukomunisti unapopitia mabadiliko makubwa katika Ulaya ya Mashariki.
Ukomunisti Waanzisha Tena Dini
“Tunahitaji viwango vya kiroho . . . Viwango vya maadili vilivyoendelezwa na dini na kutumiwa kwa karne kadhaa vyaweza kusaidia katika kazi ya kutengeneza upya nchi yetu, pia.” Watu wengi walidhani kuwa hawangesikia maneno hayo kinywani mwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Urusi. Lakini katika Novemba 30, 1989, Mikhail Gorbachev alitangaza mgeuko huo wa kuelekea dini ulioshangaza alipozuru Italia.
Je! hilo labda linaunga mkono ile nadharia ya kwamba Wakristo wa mapema wenyewe walikuwa wakomunisti, wakijizoeza aina ya usoshalisti wa Kikristo? Watu wengine hudai hivyo, wakielekeza kwenye Matendo 4:32, inayosimulia juu ya Wakristo waliomo Yerusalemu hivi: “Walikuwa na vitu vyote shirika.” Hata hivyo, uchunguzi wafunua kwamba huo ulikuwa mpango wa muda tu uliotokezwa na hali zisizotazamiwa, wala si mfumo wa kudumu wa usoshalisti wa “Kikristo.” Kwa sababu walishiriki vitu vya kimwili kwa njia ya upendo, “hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji.” Ndiyo, “kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.”—Matendo 4:34, 35.
“Glasnost” na “Perestroika”
Kutokea miezi ya mwisho ya 1989, Urusi na serikali wenzi wake wa Kikomunisti katika Ulaya Mashariki wamekuwa wakipatwa na mabadiliko ya kisiasa yanayotatanisha akili. Mabadiliko hayo yameonwa na wote kwa sababu ya ule mwongozo wa glasnost, au kutoa maoni waziwazi. Wazungu wa Ulaya Mashariki wamedai mabadiliko yenye kuhusisha mambo mengi ambayo, kwa kadiri fulani, yamekubaliwa. Viongozi wa Kikomunisti wamekiri uhitaji wa mfuno unaojali binadamu na wenye huruma na wameitisha “kuanzishwa upya kwa usoshalisti katika namna iliyo tofauti, yenye kuelimika na inayofaa zaidi,” kama mwanauchumi mmoja wa Polandi alivyoweka wazo hilo.
Mwenye kutokeza zaidi katika viongozi hao amekuwa ni Gorbachev, ambaye, muda mfupi baada ya kuja mamlakani katika 1985, alianzisha wazo la perestroika (kutengeneza upya). Wakati wa ziara yake kule Italia, alitetea perestroika kuwa ya lazima ili kukabiliana na magumu ya miaka ya 1990. Alisema hivi: “Nchi za kisoshalisti zikiwa tayari zimeanza kuifuata njia ya marekebisho makubwa, zinavuka mpaka ambao sasa haziwezi kurudia mambo ya zamani.” Hata hivyo, ni makosa kushikilia kama wengi wafanyavyo katika Magharibi, kwamba hilo ndilo anguko la usoshalisti. Kwa kinyume, yamaanisha kwamba mwendo wa usoshalisti katika ulimwengu utafuatia ukuzi zaidi wa namna nyingi.”
Kwa hiyo, viongozi wa kikomunisti hawako tayari kuafikiana na kadirio lililofanywa na mwandishi wa safu za magazeti Charles Krauthamer, aliyeandika hivi: “Swali ambalo limeendelea daima kushughulisha kila mwanafalsafa wa kisiasa tangu Plato—ni upi ulio mfumo bora zaidi wa uongozi?—limejibiwa. Baada ya mileani chache za kujaribu kila namna ya mfumo wa kisiasa, twafunga milieani hii tukijua hakika kwamba katika demokrasi ya mabepari wengi inayoruhusu uhuru mwingi, tumekipata tulichokuwa tukitafuta.”
Hata hivyo, gazeti la Ujerumani Die Zeit linakiri kwa unyofu mambo ya kusikitisha yanayoletwa na aina ya demokrasi ya Magharibi, likivuta fikira kwenye “ukosefu wa kazi, utumiaji mbaya wa vileo na dawa za kulevya, umalaya, kupunguzwa kwa programu za kijamii, upungufu wa kodi na hasara kwa gharama ya serikali,” kisha lauliza: “Je! hiyo kweli ndiyo jamii kamilifu ambayo kwa wakati wote imeshinda usoshalisti?”
Mithali ijulikanayo na wengi yasema kwamba watu wanaoishi katika nyumba za kioo ni sharti kwao kutotupa mawe. Ni aina gani ya serikali isiyokamilika iwezayo kuthubutu kuchambua mapungufu ya serikali nyingine? Mambo ya hakika yaonyesha kwamba serikali ya kibinadamu iliyo kamilifu—aina ya Utopia—haiko. Wanasiasa bado wanatafuta pale “mahali pazuri.” Lakini bado hapo “si mahali” penye kupatikana.
[Maelezo ya Chini]
a Marx, aliyezaliwa na wazazi Wayahudi katika 1818 katika ile iliyokuwa Prussia wakati huo, alielimishwa katika Ujerumani na kufanya kazi huko akiwa mwandishi wa habari; baada ya 1849 alitumia kadiri kubwa ya maisha yake katika London, alikokufa katika 1883.
[Sanduku katika ukurasa wa 30]
MANENO NA MAJINA YA KISOSHALISTI NA KIKOMUNISTI
WABOLSHEVIKI/WAMENSHEVIKI: Chama cha Wafanya Kazi cha Jamii ya Kidemokrasi cha Urusi kilichoanzishwa katika 1898 kiligawanyika kuwa vikundi viwili katika 1903; Wabolsheviki, ikimaanisha kwa halisi “washiriki wa walio wengi,” wakiongozwa na Lenin walipendelea kudumisha chama kikiwa kidogo kukiwa na wanamapinduzi wachache wenye nidhamu; Wamensheviki, ikimaanisha “washiriki wa walio wachache,” walipendelea chama kiwe na washiriki wengi zaidi wakitumia njia za kidemokrasi.
TABAKA YA KATI/TABAKA YA WAFANYA KAZI: Marx alifundisha kwamba tabaka ya wafanya kazi ingepindua tabaki ya kati; kutia na wenye viwanda, na kusimamisha “udikteta wa tabaka ya wafanya kazi,” hiyo ikitokeza jamii isiyo na tabaka zozote.
“COMINTERN”: Ufupi wa “Communist International” (Ukomunisti wa Umataifa wa Kikomunisti, au “Third International,” Umataifa wa Tatu) ni tengenezo lililofanyizwa na Lenini katika 1919 ili kuendeleza ukomunisti; likavunjwa katika 1943, na lilikuwa limetanguliwa na Umataifa wa Kwanza (1864-76), uliozaa vikundi vingi vya kisoshalisti vya Ulaya, na Umataifa wa Pili (1889-1919), hilo likiwa ni bunge la kimataifa la vyama vya kisoshalisti.
AZIMIO LA KIKOMUNISTI: Taarifa ya 1848 ya Marx na Engels ya mafundisho makuu ya usoshalisti wa kisayansi ambao ulitumika kwa muda mrefu kuwa msingi wa vyama vya Kisoshalisti na Kikomunisti vya Ulaya.
UKOMUNISTI WA ULAYA: Ukomunisti wa vyama vya Kikomunisti vya Ulaya Magharibi; vikiwa huru na uongozi wa Urusi na vyenye nia ya kutumika katika serikali za mapatano, hutoa hoja kwamba “udikteta wa tabaka ya wafanya kazi” hauhitajiki tena.
USOSHALISTI WA KISAYANSI NA WA SERIKALI KAMILIFU: Maneno yatumiwayo na Marx kutofautisha kati ya mafundisho yake, yadhaniwayo kuwa na msingi wa uchunguzi wa kisayansi wa historia na kazi za ubepari na mafundisho ya Serikali Kamilifu ya kisoshalisti yaliyofundishwa na waliomtangulia.