‘Shambulizi la Elektroniki Kwenye Ubongo’
TELEVISHENI yaweza kuwa yenye kutumbuiza na kuelimisha. Hata hivyo, Profesa Moshe Aronson wa Chuo Kikuu cha Tel-Aviv aonya kwamba utazamaji wa televisheni kupita kiasi waweza kuwa hatari kwa afya yako. Jinsi gani?
Aronson adai kwamba, mtazamaji wa kupitisha wakati hupatwa na mrundamano wa mkakamano ambao hauwezi kutulizika anapokuwa amekaa mbele ya kiwambo cha televisheni. Jambo hili hutokeza homoni za mkazo ambazo katika viwango vya juu zaweza kuharibu chembe za neva kwenye hippocampus—eneo la ubongo ambalo ni muhimu kwa kumbukumbu. Ingawa alionelea kwamba machunguzi zaidi yahitajiwa, Aronson ashuku kwamba kudhoofika huku kwaweza kuchangia kupatwa na kichaa, labda hata kukikufanyiza uwe na uelekeo wa kupatwa na maradhi ya kunywea kwa mfumo wa kati wa hisi baadaye maishani. Katika tukio lolote, gazeti la New Scientist huita utazamaji wa televisheni kupita kiasi “shambulizi la elektroniki kwenye ubongo.”
Kinyume na utazamaji wa televisheni, kusoma huamsha mawazo na kuchochea uwezo wa kusababu—si utendaji wa kupitisha wakati kamwe! Huku kila mwono na sauti zikifasiriwa kwa mtazamaji wa televisheni, msomaji hubuni mandhari zake mwenyewe na mitokeo ya toni. Utumizi huu wa ubuni wa nyenzo za kiakili hukomesha kudumaa kwa kiakili, hivyo ukinufaisha afya ya mmoja. Kutokana na hili, je, halingekuwa jambo la hekima kuweka mipaka kwa kiasi cha wakati unachotumia mbele ya kiwambo cha televisheni?
Televisheni ama kusoma—ni ipi iliyo bora kwa ajili yako?