Kulinda Salama Watoto Wenu na Matumizi Mabaya ya Damu
1 “Tazama! Wana ni urithi kutoka kwa Yehova.” (Zab. 127:3, NW) Ikiwa mna urithi wenye thamani jinsi hiyo kutoka kwa Yehova, nyinyi mkiwa wazazi mna daraka zito, lakini lenye kufurahisha, la kuwazoeza, kuwatunza, na kuwalinda watoto wenu. Kwa mfano, je! mmechukua kila hatua ifaayo kulinda watoto wenu wachanga wasitiwe damu mishipani? Watoto wenu wangeitikiaje iwapo wangekabiliwa na mataraja ya kutiwa damu? Je! mkiwa familia, mmezungumzia yale ambayo mnaweza kufanya ili kushughulikia kikamili hali ya dharura inayotokea yenye tisho la kutiwa damu mishipani?
2 Si lazima mpatwe na wasiwasi au mkazo usiohitajiwa kwa sababu ya kutayarisha familia yenu kwa ajili ya hali kama hizo. Hamwezi kutarajia na kujitayarishia kila tukio maishani, lakini kuna mambo mengi ambayo nyinyi, mkiwa wazazi, mnaweza kufanya kimbele ili kulinda watoto wenu wasitiwe damu. Kupuuza madaraka hayo kwaweza kufanya mtoto wenu atiwe damu anapopata matibabu. Ni nini chaweza kufanywa?
3 Usadikisho Imara ni wa Muhimu: Fikirini kwa uzito jinsi usadikisho wenu wenyewe ulivyo imara kuhusu sheria ya Mungu juu ya damu. Je! mnawafunza watoto wenu kumtii Yehova katika jambo hilo, kama vile mnavyowafunza sheria yake juu ya unyoofu, adili, kutokuwamo, na mambo mengine ya maisha? Je! kwelikweli tunahisi kama vile sheria ya Mungu ilivyoamuru kwenye Kumbukumbu la Torati 12:23: “Ujihadhari [Azimia kabisa, NW] usile damu”? Mstari wa 25 unaongeza: “Usiile ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako, utakapofanya yaliyoelekea machoni pa BWANA [Yehova, NW].” Huenda daktari akadai kwamba damu ‘itafanya mambo yafanikiwe’ kwa mtoto wenu mgonjwa, lakini kabla ya hali yoyote ya dharura kuwapo, ni lazima mwazimie kabisa kukataa kutiwa damu nyinyi wenyewe na watoto wenu, mkithamini uhusiano wenu na Yehova kuwa wa juu kuliko dai lolote la kurefusha uhai ambalo linaweza kuhusisha kuvunja sheria yake ya kimungu. Upendeleo wa Mungu sasa na uhai wa milele wakati ujao unahusika!
4 Naam, Mashahidi wa Yehova wanathamini uhai. Hawatamani kufa. Wanataka kuishi ili waweze kumsifu Yehova na kufanya mapenzi yake. Hiyo ndiyo sababu moja wao huenda hospitali na kuwapeleka watoto wao kupata matibabu. Wao huwauliza matabibu wawatibu, na wanapoambiwa kwamba damu ndio utibabu wa msingi au njia ya kitiba iliyoidhinishwa, wao huomba utibabu mwingine usiohusisha damu. Kuna utibabu mwingine mwingi usiohusisha damu. Matabibu wenye ujuzi wanautumia. Utibabu mwingine wa aina hiyo si tiba bandia bali ni utibabu na utaratibu wa kitiba unaofaa ambao umethibitishwa na majarida maarufu ya kitiba. Maelfu ya matabibu ulimwenguni kote wanashirikiana nasi katika kuandaa matibabu mazuri bila kutumia damu, ingawa wakati mwingine lingali tatizo kuwapata matabibu watakaotibu watoto Mashahidi bila kutumia damu.
5 Kumpata Daktari Mwenye Kushirikiana: Matabibu wana mahangaikio mengi katika kuwatibu wagonjwa, na mnapowaomba watibu mtoto wenu bila damu, hilo huongezea ugumu. Matabibu wengine watakubali kuwatibu watu wazima huku wakiheshimu matakwa yao juu ya damu maadamu fomu inayokubalika ya kuondolea daktari lawama inajazwa. Vivyo hivyo, huenda wengine wakakubali kuwatibu watoto ambao wameonyesha kwamba ni wakomavu, kwa kuwa baadhi ya mahakama zimetambua kwamba watoto wakomavu wana haki ya kufanya maamuzi yao wenyewe ya kitiba. (Ona Mnara wa Mlinzi, Juni 15, 1991, kurasa 16-17, kwa mazungumzo juu ya yale yanayoonyesha kuwa mtoto ni mkomavu.) Hata hivyo, huenda matabibu wakakataa kuwatibu watoto wadogo, hasa vitoto, isipokuwa wawe wameruhusiwa kutumia damu. Kwa kweli, ni matabibu wachache sana watakaohakikisha kabisa kwamba hawatatumia damu chini ya hali zozote wanapotibu mtoto. Madaktari wengi huhisi kwamba hawawezi kutoa uhakikisho huo kwa sababu za kitiba na kisheria. Hata hivyo, idadi inayozidi kuongezeka wanataka kuwatibu watoto wa Mashahidi wa Yehova wakiheshimu matakwa yetu juu ya damu kwa kadiri wawezavyo.
6 Kwa kufikiria hilo, namna gani ikiwa mnapomtafuta daktari anayefaa kwa ajili ya mtoto wenu, mnampata mmoja anayejulikana kwa kushirikiana vizuri na Mashahidi wa Yehova na ambaye amepata kufuata utaratibu huohuo wa kitiba kwa ajili ya Mashahidi wengine bila kutumia damu katika wakati uliopita na bado anahisi kwamba sheria haimruhusu awahakikishie kikamili kwamba damu haitatumiwa? Hata hivyo, yeye anawahakikishia kwamba anahisi hakutakuwa na tatizo lolote wakati huu pia. Huenda mkaamua kwamba hiyo ndiyo njia bora ya kufuata. Chini ya hali hizo huenda mkaamua kwamba anaweza kuendelea. Hata hivyo, elewesheni wazi kabisa; kwamba katika kuruhusu matibabu kwa ajili ya mtoto wenu, nyinyi hamtoi ruhusa atiwe damu mishipani. Kufuata njia hiyo kungekuwa daraka ambalo mngelazimika kuchukua bila uamuzi wenu kuonwa kuwa ni kuridhiana.
7 Bila shaka, ikiwa mngeweza kupata utibabu mwingine unaofaa unaoweza kupunguza zaidi au labda kuondoa tatizo la damu kutumiwa, basi inaelekea mngechagua njia hiyo isiyo hatari sana. Ingetazamiwa kwamba mngejitahidi sana kumpata tabibu au mpasuaji ambaye angekubali kutotumia damu kwa kadiri awezavyo kuliko matabibu wengine. Ulinzi bora zaidi ni kutazamia matatizo. Jitahidi sana kumpata kimbele daktari mwenye kushirikiana. Jaribu kuepuka madaktari na hospitali zisizo na ushirikiano inapowezekana.
8 Katika nchi fulani jambo jingine linaloweza kutokeza tofauti ya kama damu itatiwa mishipani au la ni jinsi matibabu ya hospitali yatakavyolipiwa. Mahali ambapo wazazi wana bima ya afya au ulinzi mwingineo unaowaruhusu watafute daktari wanayependelea, ni rahisi zaidi kutowapeleka watoto kwa matabibu na wafanyakazi wa hospitali wasioshirikiana. Fedha za kutosha mara nyingi huamua aina ya utumishi na ushirikiano ambao familia inapokea kutoka madaktari na hospitali. Pia, kama hospitali au tabibu atakubali kuhamishwa kwa mtoto mara nyingi kunategemea uwezo wa wazazi wa kulipia matibabu. Na wale wanaotazamia kupata watoto, ni jambo la muhimu kutunza afya yenu wakati wa kuwa mjamzito! Hilo litasaidia sana kuzuia kuzaa kabla ya wakati barabara na matatizo yanayotokana nako, kwa kuwa matibabu ya kawaida kwa vitoto vilivyozaliwa kabla ya wakati barabara na matatizo yavyo mara nyingi huhusisha damu.
9 Nyakati nyingine matabibu hulalamika kwamba Mashahidi wa Yehova hawazungumzi juu ya kukataa kwao damu hadi dakika ya mwisho. Haipaswi iwe hivyo kamwe. Mojayapo mambo ya kwanza ambayo wazazi Mashahidi wapaswa kufanya wanapoenda hospitali au wanapopata utumishi wa tabibu ni kuzungumzia msimamo wao juu ya damu. Ikiwa upasuaji unahusika, ombeni mkutane kimbele na daktari wa dawa nusukaputi. Huenda mpasuaji akaweza kuwasaidia kufanya hivyo. Fomu za kulazwa zapaswa zichunguzwe kwa uangalifu. Mna haki ya kufuta chochote msichokubaliana nacho. Ili kuondoa shaka lolote, andikeni waziwazi katika fomu ya kulazwa kwamba damu, haitakiwi wala isitumiwe chini ya hali zozote kwa sababu za kidini na kitiba.
10 Msaada wa Tengenezo la Yehova: Ni maandalizi gani ambayo tengenezo la Yehova limefanya ili kuwasaidia kulinda watoto wenu wasitiwe damu? Kuna mengi. Sosaiti imechapisha mengi ili kutuelimisha juu ya damu na utibabu mwingine usiohusisha damu. Mmejifunza broshua Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako? na vichapo vingine juu ya habari hiyo. Na mna ndugu na dada zenu kundini wanaoweza kuwapa msaada na utegemezo mwingi. Kunapokuwa na tatizo kubwa, huenda wazee wakaona kuwa yafaa kupanga kuwa na ulinzi wa saa 24 hospitalini, hasa na mzee pamoja na mzazi wa mgonjwa au mshiriki mwingine wa karibu wa familia. Mara nyingi damu hutiwa mishipani wakati watu wote wa familia ya karibu na marafiki wameenda nyumbani kulala.
11 Katika United States, kuna Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali zaidi ya mia moja katika miji mikubwa. Makundi yote yamegawiwa halmashauri ya ndugu waliozoezwa wanaopatikana ili kusaidia. Kupitia kwa wazee wenu, mwaite wanapohitajiwa. Hawapaswi kuitwa kuhusiana na matatizo madogo-madogo, lakini msingoje mno kuwaita inapoonwa kwamba tatizo kubwa laweza kuwa linatokea. Mara nyingi wanaweza kutoa majina ya matabibu wanaoshirikiana na madokezo juu ya matibabu mengine. Inapokuwa lazima na inapowezekana, ndugu hao hupanga kuwapo na kusaidia kushughulikia tatizo hilo.
12 Kutazamia na Kushughulikia Kuhusika kwa Mahakama: Namna gani ikiwa daktari au hospitali inanuia kupata agizo la mahakama ili kumtia damu mtoto wenu? Je! huo ndio wakati wa kuacha, ukiwaza kwamba hakuna jambo jingine zaidi linaloweza kufanywa? La hasha! Huenda bado ikawezekana kuepuka kutiwa damu mishipani. Matayarisho kwa uwezekano kama huo yapaswa kufanywa kimbele. Ni nini laweza kufanywa?
13 Kuelewa baadhi ya kanuni za kisheria ambazo huongoza au huwa na uvutano juu ya hospitali na mahakimu katika mambo hayo kutakusaidia sana katika kufanya utetezi. Mojayapo kanuni hizo iliyo ya muhimu sana ni jamblo la kwamba sheria haiwapi wazazi uwezo usio na mipaka kukubali au kukataa matibabu kwa ajili ya watoto wao. Ingawa kwa ujumla watu wazima wana haki ya kukubali au kukataa matibabu kama wapendavyo, wazazi hawako huru kukataa matibabu yanayoonwa kuwa ya lazima kwa hali njema ya mtoto wao hata iwapo kukataa kwao kuna msingi wa imani za kidini zilizoshikiliwa kwa unyoofu.
14 Kanuni hiyo ya msingi ilionyeshwa katika uamuzi wa 1944 wa Mahakama Kuu ya U.S. uliosema: “Wazazi wenyewe wanaweza kuwa wafia-imani. Lakini haimaanishi kwamba, chini ya hali hizohizo wao wako huru kufanya watoto wao wawe wafia-imani kabla ya hao [watoto] kufikia umri wa kukomaa kikamili kunakotambuliwa kisheria wakati ambapo wanaweza kufanya uchaguzi huo wao wenyewe.” Hangaiko hilohilo la msingi kwa ajili ya afya ya kimwili na hali njema ya mtoto imetiwa katika sheria za hali njema ya watoto leo. Sheria hizo, ambazo kusudi lazo ni kuzuia kutendwa vibaya kwa watoto, zakusudiwa pia kulinda watoto wasinyimwe matibabu.
15 Kulinda watoto ili wasitendwe vibaya na wazazi na wasikose kutunzwa kwa kweli kunakubaliwa na wazazi Wakristo. Lakini sheria dhidi ya kutotunza watoto na taarifa ya Mahakama Kuu iliyonukuliwa juu mara nyingi hutumiwa isivyofaa katika visa vinavyohusu watoto wa Mashahidi wa Yehova. Kwa nini? Kwanza, wazazi Mashahidi hawanuii kuwafanya watoto wao “wafia-imani.” Ikiwa wangenuia hivyo, basi kwa nini wawapeleke watoto wao hospitali? Kinyume cha hivyo, wazazi Mashahidi huwatafutia watoto wao matibabu kwa hiari. Wanapenda watoto wao na wanataka wawe na afya njema. Lakini wanaamini kwamba wana jukumu walilopewa na Mungu la kuchagua ifaavyo aina ya matibabu iliyo bora zaidi kwa watoto wao. Wanataka matatizo ya afya ya watoto wao yashughulikiwe bila damu. Si kwamba matibabu mengine ya aina hiyo yasiyohusisha damu ni bora na salama tu zaidi ya damu, bali la maana zaidi, watoto wao hubaki wakiwa na upendeleo wa yule Mpaji-Uhai mkuu, Yehova Mungu.
16 Ijapokuwa manufaa za matibabu yasiyohusisha damu, madaktari wengi na maofisa wanaoshughulikia hali njema ya watoto huona utibabu wa kutia damu mishipani kuwa utibabu uliokubaliwa ambao huenda ukawa wa lazima au hata wenye kuokoa uhai katika hali fulani. Hivyo, wazazi Mashahidi wanapokataa damu iliyopendekezwa itiwe mishipani, matatizo yanaweza kuzuka. Kwa ujumla, madaktari hawawezi kutibu watoto kihalali bila idhini ya wazazi wao. Ili kushinda kukataa kwa wazazi kutoa idhini ya kutumia damu, katika nchi fulani huenda madaktari au wafanyakazi wengine wa hospitali wakajaribu kupata idhini kutoka kwa hakimu kwa njia ya agizo la mahakama. Idhini kama hiyo inayoamriwa na mahakama yaweza kupatikana kupitia maofisa wanaoshughulikia hali njema ya watoto au madaktari au maofisa wa hospitali wanaotenda kulinda mtoto dhidi ya kile wanachoona kuwa kumnyima mtoto matibabu.a
17 Mara nyingi maagizo ya mahakama yanayotoa idhini ya utumizi wa damu hupatikana upesi sana huku wazazi wakijulishwa kijuujuu tu ikiwa wanajulishwa kwa vyovyote. Madaktari, wasimamizi wa hospitali, au maofisa wanaoshughulikia hali njema ya watoto hujaribu kutetea maagizo kama hayo yaliyotekelezwa kwa kudai kwamba kuna hali ya dharura ya kitiba ambayo hairuhusu kuwe na wakati wa wazazi kujulishwa kikamili juu ya yale yanayoendelea. Hata hivyo, mara nyingi wanapohojiwa, madaktari hukiri kwamba hali ya dharura halisi haimo na kwamba wanataka agizo la mahakama “endapo tu” kutiwa damu mishipani kuhitajiwe wakati ujao kwa maoni yao. Mkiwa watunzi asilia wa mtoto wenu, mna haki ya kimsingi kujua nyakati zote wafanyayo madaktari, wasimamizi wa hospitali, au maofisa wanaoshughulikia hali njema ya watoto kuhusiana na mtoto wenu. Katika nchi fulani sheria hutaka kwamba, ikiwa inawezekana, mnapaswa kujulishwa juu ya jitihada za kupata agizo la mahakama na mnapaswa kuruhusiwa kutetea upande wenu wa ubishi huo mbele ya mahakama.
18 Mambo hayo halisi ya kisheria yanakazia thamani ya kupata daktari mwenye kushirikiana. Fanyeni kazi naye, na kwa msaada wa washiriki wa Halmashauri ya Kupatanisha na Hospitali yenu, au wazee wenyeji, msaidieni afuatilie matibabu yasiyohusisha damu katika tatizo la kitiba la mtoto wenu au mmhamishe mtoto wenu kwa daktari au hospitali ambayo itaandaa matibabu hayo. Lakini ikiwa kuna ishara kwamba daktari, msimamizi wa hospitali, au mfanyakazi anayeshughulikia hali njema ya watoto anafikiria kupata agizo la mahakama, iweni macho kuuliza ikiwa hilo ndilo linalopangiwa. Nyakati nyingine hilo hufanywa kisiri kwa simu. Ikiwa kuna mpango wa kwenda mahakamani, kazieni kwamba mnataka kujua juu ya hilo ili kwamba mweze pia kutetea upande wenu kwa hakimu. (Mit. 18:17) Ikiwa kuna wakati, mara nyingi inapendekezwa kutafuta msaada wa wakili. Katika pindi fulani mawakili wamewekwa na mahakama. Ikiwa mna wakili wenu wenyewe au yule aliyewekwa na mahakama, Idara ya Sheria ya Sosaiti yaweza kushiriki naye habari zitakazomsaidia atoe utetezi ulio bora kwa kadiri iwezekanavyo chini ya hali hizo.
19 Mkishtakiwa mahakamani kwa sababu ya kukataa damu, maoni ya daktari kwamba damu ni ya lazima ili kuhifadhi uhai au afya ya mtoto wenu yaweza kuwa yenye kusadikisha sana. Mara nyingi, kwa kuwa hakimu hajui sana tiba, ataelekea kupendelea ustadi wa tiba wa daktari. Hilo hasa ni kweli wakati wazazi wanapopewa nafasi ndogo ikiwa wanapewa kwa vyovyote ili kutetea upande wao wa kesi hiyo na daktari, akiwa hana ushindani, anaruhusiwa kueleza madai yake kuhusu uhitaji wa “dharura” wa damu. Kusikilizwa kwa kesi upande mmoja hakuwezi kutokeza kweli. Jambo ni kwamba, wakati na sababu zinazofanya madaktari kuhisi kwamba damu inahitajiwa ni jambo la kubishaniwa sana na lisilo na hakika. Mara nyingi, wakati daktari mmoja anaposema kwamba damu ni ya lazima kabisa ili kuokoa uhai wa mtoto, daktari mwingine, aliye na ustadi wa kutibu ugonjwa huohuo bila damu, atasema damu si ya lazima ili kumtibu mgonjwa.
20 Utafanya nini ikiwa wakili au hakimu anakuuliza sababu ya wewe kukataa mtio wa damu “unaookoa uhai” wa mtoto wako? Ingawa huenda mwelekeo wako wa kwanza ukawa kueleza imani yako katika ufufuo na kuonyesha imani yako yenye nguvu kwamba Mungu atamleta mtoto wako tena ikiwa atakufa, jibu kama hilo peke yalo litamsadikisha tu hakimu, ambaye hangaiko lake kuu ni hali njema ya yule mtoto, kwamba wewe ni mshupavu wa kidini asiyetumia akili na kwamba ni lazima aingilie ili alinde mtoto wako.
21 Yale ambayo mahakama yahitaji kujua ni kwamba, ingawa mnakataa damu kwa sababu za kidini zilizoshikiliwa sana, nyinyi hamkatai matibabu. Hakimu anahitaji kujua kwamba nyinyi si wazazi wasiojali au wanaotendea watoto vibaya, bali, kinyume cha hilo, nyinyi ni wazazi wenye upendo wanaotaka mtoto wao atibiwe. Yale tu msiyokubaliana nayo ni madai kwamba damu ina manufaa zinazopita matatizo na mashaka yanayoweza kuua, hasa wakati matibabu mengine yasiyo na hatari hizo yanapatikana.
22 Ikitegemea hali, huenda mkamjulisha hakimu kwamba ni maoni ya daktari mmoja kwamba damu inahitajiwa, lakini madaktari hutofautiana katika njia za kitiba, na kwamba mngependa kuwa na fursa ya kumpata daktari atakayetibu mtoto wenu kwa njia mbalimbali zinazopatikana za tiba bila kutumia damu. Kwa msaada wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali au wazee wenyeji, huenda ikawa tayari mmepata daktari atakayetibu mtoto wenu bila damu na ambaye anaweza kutoa ushuhuda wenye msaada mahakamani, labda kwa simu. Inaelekea halmashauri ya uhusiano itaweza kushiriki na hakimu—hata na daktari anayejaribu kupata agizo la mahakama—makala za kitiba ambazo zaonyesha jinsi ugonjwa wa mtoto wenu waweza kutibiwa vizuri bila kutumia damu.
23 Mahakimu wanapoombwa watoe maagizo ya mahakama upesi, mara nyingi huwa hawajafikiria au kukumbushwa juu ya hatari nyingi za damu, kutia na UKIMWI, mchochota wa ini, na matatizo mengine mengi. Mnaweza kumtajia hakimu juu ya hayo, na mnaweza pia kumjulisha kwamba nyinyi mkiwa wazazi Wakristo, mngeona kule kutumia damu ya mtu mwingine katika jitihada za kuendeleza uhai kuwa ni uvunjaji mzito wa sheria ya Mungu na kwamba kulazimisha mtoto wenu atiwe damu kungeonwa kuwa kama kulalwa kinguvu. Nyinyi na mtoto wenu (ikiwa yeye ni mkubwa vya kutosha kuwa na masadikisho yake mwenyewe) mwaweza kueleza kukirihi kwenu mvamio huo wa mwili na mnaweza kumwomba hakimu asitoe agizo bali awaruhusu kufuatilia utibabu mwingine kwa ajili ya mtoto wenu.
24 Wakati utetezi mzuri unapofanywa, mahakimu huweza kuelewa vema zaidi ule upande mwingine—upande wenu—mkiwa wazazi. Halafu hawawi na haraka sana kuagiza mtio wa damu. Katika visa fulani mahakimu wamepunguza sana uhuru wa daktari wa kutumia damu, hata wakitaka kwamba njia nyingine za tiba zifikiriwe kwanza, au wamewapa wazazi fursa ya kupata madaktari watakaotibu bila damu.
25 Katika kushughulika na wale wanaojaribu kulazimisha mtio wa damu, ni jambo la maana kwamba msitoe kamwe uthibitisho wowote wa kuyumbayumba katika masadikisho yenu. Nyakati nyingine mahakimu (na madaktari) huwauliza wazazi ikiwa wangeona ugumu wa “kuwakabidhi” daraka la uamuzi wa kutia damu, wakihisi kwamba hilo litafanya iwe rahisi zaidi kwa wazazi kuishi bila kusumbuliwa na dhamiri. Lakini inapaswa ieleweshwe wazi kwa wote wanaohusika kwamba, nyinyi mkiwa wazazi, mnahisi mkiwa na jukumu la kuendelea kufanya yote mwezayo ili kuepuka mtio wa damu. Hilo ni daraka mlilopewa na Mungu. Haliwezi kukabidhiwa wengine.
26 Kwa hiyo, katika kuzungumza na madaktari na mahakimu, mnahitaji kujitayarisha kueleza msimamo wenu waziwazi na kwa kusadikisha. Ikiwa agizo la mahakama linatolewa kujapokuwa jitihada zenu bora, endeleeni kumwomba tabibu asitie damu na mhimize atumie matibabu mengine. Endeleeni kumfanya afikirie makala za kitiba na ushauri wa madaktari wengineo ambao wanaweza kuombwa mashauri katika tatizo hilo la kitiba ili kuepuka damu. Katika pindi zaidi ya moja, daktari aliyeonekana kuwa hapindiki ametoka kwenye chumba cha upasuaji na kutangaza kwa furaha kwamba hakutumia damu. Kwa hiyo, hata baada ya agizo la mahakama kutolewa, msikate tamaa kamwe, hata iweje!—Ona toleo la Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 1991, “Maswali Kutoka kwa Wasomaji.”
27 Kumbuka, Yesu alisema hivi: “Jihadharini na wanadamu; kwa maaana watawapeleka mabarazani . . . Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.” Ili kupata faraja chini ya hali hizo, Yesu aliongeza kwamba roho takatifu ingetusaidia tukumbuke yale ambayo yangefaa na yangenufaisha kusema katika pindi hizo.—Mt. 10:16-20.
28 “Atakayelitafakari neno atapata mema, na kila amwaminiye BWANA [Yehova, NW] ana heri [furaha, NW].” (Mit. 16:20) Wazazi, fanyeni matayarisho yanayohitajika kimbele ili kulinda mtoto wenu na mtio wa damu mishipani unaochafua kiroho. (Mit. 22:3) Watoto, itikieni mazoezi ya wazazi wenu katika kufanya matayarisho hayo na kuyatumia mioyoni mwenu. Mkiwa familia, ‘azimieni kabisa msile damu . . . ili mpate kufanikiwa’ kwa sababu ya kuwa na baraka na tabasamu ya kibali cha Yehova.—Kum. 12:23-25.
[Maelezo ya Chini]
a Ni katika hali ya dharura pekee iliyoko wakati huo na ambayo kwa maoni ya daktari, inataka matibabu ya mara hiyo ndipo matibabu yanayoonwa kuwa ya lazima kwa maisha au afya ya mtoto (kutia na mitio ya damu mishipani) yanapoweza kutolewa kihalali bila idhini ya wazazi au mahakama. Bila shaka, ni lazima tabibu atoe hesabu anapotegemea uwezo huo wa dharura ulio katika sheria.