Luka
12 Wakati huohuo, umati ulipokuwa umekusanyika pamoja kwa maelfu mengi sana hivi kwamba walikuwa wakikanyagana, yeye alianza kwa kuwaambia kwanza wanafunzi wake: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. 2 Lakini hakuna kitu kilichositiriwa kwa uangalifu ambacho hakitafunuliwa, na cha siri ambacho hakitakuwa chenye kujulikana. 3 Kwa sababu hiyo mambo msemayo gizani yatasikiwa nuruni, na mnong’onalo katika vyumba vya faragha litahubiriwa kutoka paa za nyumba. 4 Zaidi ya hayo, mimi nawaambia nyinyi, marafiki wangu, Msiwahofu wale wauuao mwili na baada ya hilo hawawezi kufanya jambo lolote zaidi. 5 Lakini hakika mimi nitawaonyesha nyinyi nani wa kumhofu: Mhofuni yeye ambaye baada ya kuua ana mamlaka ya kutupa ndani ya Gehena. Ndiyo, mimi nawaambia nyinyi, mhofuni Huyu. 6 Shore watano huuzwa kwa sarafu mbili za thamani ndogo, sivyo? Na bado hakuna hata mmoja wao hupata kusahaulika mbele ya Mungu. 7 Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiwe na hofu; nyinyi ni bora zaidi kuliko shore wengi.
8 “Basi, mimi nawaambia nyinyi, Kila mtu aungamaye muungano pamoja nami mbele ya wanadamu, Mwana wa binadamu ataungama pia muungano pamoja naye mbele ya malaika za Mungu. 9 Lakini yeye anikanaye mbele ya wanadamu atakanwa mbele ya malaika za Mungu. 10 Na kila mtu asemaye neno dhidi ya Mwana wa binadamu, hilo atasamehewa; lakini yeye akufuruye dhidi ya roho takatifu hatasamehewa hilo. 11 Lakini wawaletapo nyinyi ndani mbele ya makusanyiko ya watu wote na maofisa wa serikali na mamlaka, msiwe wenye kuhangaikia jinsi gani au ni jambo gani mtasema kwa kujitetea au ni jambo gani mtasema; 12 kwa maana roho takatifu itawafundisha nyinyi saa hiyohiyo mambo mpaswayo kusema.”
13 Ndipo mtu fulani kati ya umati akamwambia: “Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi.” 14 Yeye akamwambia: “Wewe mtu, nani aliyeniweka mimi rasmi hakimu au mgawaji-fungu juu ya nyinyi watu?” 15 Ndipo yeye akawaambia: “Fulizeni kufungua macho yenu na mlinde dhidi ya kila namna ya tamaa, kwa sababu hata wakati mtu ana wingi uhai wake hautokani na vitu alivyo navyo.” 16 Ndipo akawaambia kielezi, akisema: “Shamba la mtu fulani tajiri lilizaa vema. 17 Kwa sababu hiyo yeye akaanza kuwazawaza ndani yake mwenyewe, akisema, ‘Nitafanya nini, sasa kwa kuwa sina mahali popote pa kukusanya mazao yangu?’ 18 Kwa hiyo akasema, ‘Hakika nitafanya hili: Hakika nitabomoa ghala zangu na kujenga zilizo kubwa zaidi, na humo hakika nitakusanya nafaka yangu yote na vitu vyangu vyema vyote; 19 nami hakika nitaiambia nafsi yangu: “Nafsi, wewe una vitu vyema vingi vilivyolimbikwa kwa miaka mingi; starehe, kula, kunywa, jifurahishe mwenyewe.”’ 20 Lakini Mungu akamwambia, ‘Wewe mwenye kukosa akili, usiku huu wanadai nafsi yako kutoka kwako. Ni nani, basi, atakayepaswa kuwa na vitu ulivyoviweka akiba?’ 21 Hivyo ndivyo huwa kwa mtu ajilimbikiaye hazina mwenyewe lakini si tajiri kuelekea Mungu.”
22 Ndipo akawaambia wanafunzi wake: “Kwa sababu ya hilo mimi nawaambia nyinyi, Komeni kuwa wenye kuhangaikia nafsi zenu kuhusu ni nini mtakachokula au juu ya miili yenu kuhusu ni nini mtakachovaa. 23 Kwa maana nafsi ni yenye thamani zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi. 24 Angalieni vema kwamba kunguru hawapandi mbegu wala hawavuni, nao hawana bohari wala ghala, na bado Mungu huwalisha. Nyinyi ni wenye ubora zaidi kama nini kuliko ndege? 25 Ni nani kati yenu kwa kuhangaika aweza kuongeza dhiraa kwenye muda wake wa maisha? 26 Kwa hiyo, ikiwa nyinyi hamwezi kufanya jambo lililo dogo zaidi, kwa nini mhangaikie mambo yaliyobaki? 27 Angalieni vema jinsi mayungiyungi hukua; hayo hayamenyeki wala hayasokoti; lakini nawaambia nyinyi, Hata Solomoni katika utukufu wake wote hakupambwa kama moja kati yayo. 28 Ikiwa, basi, Mungu huvisha hivyo mimea shambani ambayo ipo leo na kesho hutupwa ndani ya joko, si zaidi sana atawavisha nyinyi, nyinyi wenye imani kidogo! 29 Kwa hiyo komeni kutafuta sana ni nini huenda mkala na ni nini huenda mkanywa, na komeni kuwa katika wasiwasi wenye hangaiko; 30 kwa maana yote hayo ndiyo mambo ambayo mataifa ya ulimwengu yanafuatia kwa hamu, lakini Baba yenu ajua mwahitaji mambo haya. 31 Hata hivyo, tafuteni ufalme wake kwa kuendelea, na mambo haya mtaongezewa.
32 “Msiwe na hofu, kundi dogo, kwa sababu Baba yenu amekubali kuwapa nyinyi ufalme. 33 Uzeni mali yenu na toeni zawadi za rehema. Jifanyieni wenyewe vibeti visivyochakaa, hazina isiyopungua kamwe katika mbingu, ambapo mwizi hakaribii wala nondo hali kabisa. 34 Kwa maana ilipo hazina yenu, hapo mioyo yenu itakuwapo pia.
35 “Viuno vyenu na vifungwe mishipi na taa zenu ziwe zikiwaka, 36 nanyi wenyewe mtakuwa kama watu wanaongoja bwana-mkubwa wao wakati arudipo kutoka kwenye ndoa, ili wakati wa kuwasili kwake na kubisha hodi wapate kumfungulia mara moja. 37 Wenye furaha ni watumwa wale ambao bwana-mkubwa awasilipo awakuta wakilinda! Kwa kweli nawaambia nyinyi, Yeye atajifunga mwenyewe na kuwafanya waegame kwenye meza naye atakuja kando na kuwahudumia. 38 Na ikiwa yeye awasili katika lindo la pili, hata ikiwa ni katika la tatu, na awakuta hivyo, wenye furaha ni wao! 39 Lakini jueni hili, kwamba ikiwa mwenye nyumba angalijua ni saa gani mwizi angalikuja, angalifuliza kulinda na asingaliacha nyumba yake ivunjwe iingiwe. 40 Nyinyi pia, fulizeni kuwa tayari, kwa sababu kwenye saa msiyofikiri yaelekea kuwa, Mwana wa binadamu anakuja.”
41 Ndipo Petro akasema: “Bwana, unatuambia kielezi hiki sisi au wote pia?” 42 Naye Bwana akasema: “Ni nani kwa kweli aliye msimamizi-nyumba mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana-mkubwa wake atamweka rasmi juu ya baraza la mahadimu wake kufuliza kuwapa kipimo chao cha magawio ya chakula kwenye wakati ufaao? 43 Mwenye furaha ni mtumwa huyo, ikiwa bwana-mkubwa wake awasilipo amkuta akifanya hivyo! 44 Nawaambia nyinyi kwa kweli, Yeye atamweka rasmi juu ya mali zake zote. 45 Lakini ikiwa wakati wowote mtumwa huyo atasema moyoni mwake, ‘Bwana-mkubwa wangu akawia kuja,’ naye aanze kuwapiga watumishi-wanaume na watumishi-wasichana, na kula na kunywa na kupata kulewa, 46 bwana-mkubwa wa mtumwa huyo hakika atakuja siku ambayo hatarajii na saa asiyojua, naye atamwadhibu kwa ukali ulio mkubwa zaidi na kumgawia sehemu pamoja na wale wasio waaminifu. 47 Ndipo mtumwa huyo aliyeelewa mapenzi ya bwana-mkubwa wake lakini hakujitayarisha au kufanya kupatana na mapenzi yake atapigwa kwa mapigo mengi. 48 Lakini yeye ambaye hakuelewa na kwa hiyo akafanya mambo yanayostahili mapigo hakika atapigwa kwa machache. Kwa kweli, kila mtu ambaye alipewa mengi, mengi yatadaiwa kutoka kwake; na yeye ambaye watu wamweka katika usimamizi wa mengi, watadai zaidi kutoka kwake kuliko ilivyo kawaida.
49 “Nilikuja kuanza moto juu ya dunia, na kuna nini zaidi cha mimi kutaka ikiwa tayari umewashwa? 50 Kwa kweli, nina ubatizo wa kubatizwa kwao, na jinsi ninavyotaabishwa mpaka umalizike! 51 Je, mwawazia nilikuja kuleta amani juu ya dunia? La, hasha, nawaambia nyinyi, bali badala ya hivyo mgawanyiko. 52 Kwa maana tangu sasa na kuendelea kutakuwa na watano katika nyumba moja waliogawanyika, watatu dhidi ya wawili na wawili dhidi ya watatu. 53 Watagawanyika, baba dhidi ya mwana na mwana dhidi ya baba, mama dhidi ya binti na binti dhidi ya mama yake, mama-mkwe dhidi ya binti-mkwe wake na binti-mkwe dhidi ya mama-mkwe wake.”
54 Ndipo akaendelea kuuambia pia umati: “Wakati mwonapo wingu likizuka katika sehemu za magharibi, mara moja nyinyi husema, ‘Dhoruba inakuja,’ na huwa hivyo. 55 Nanyi mwonapo kwamba upepo wa kusini unavuma, nyinyi husema, ‘Kutakuwa na wimbi la joto,’ na hutukia. 56 Wanafiki, mwajua jinsi ya kuchunguza kuonekana kwa nje kwa dunia na anga, lakini yawaje hamjui jinsi ya kuuchunguza wakati maalumu huu? 57 Kwa nini hamjihukumii wenyewe pia lililo adilifu? 58 Kwa kielelezo, wakati unapoenda kwa mtawala pamoja na mpinzani wako sheriani, anza kazi, mkiwa njiani, kujiondolea mwenyewe ubishi pamoja naye, ili asipate kamwe kukuburuta mbele ya hakimu, naye hakimu akukabidhi kwa ofisa wa mahakama, na ofisa wa mahakama akutupe gerezani. 59 Mimi nakuambia, Hakika wewe hutatoka humo mpaka umalize kulipa sarafu ya mwisho iliyo ndogo yenye thamani ndogo sana.”