Luka
13 Kwenye majira hayohayo palikuwapo watu fulani walioripoti kwake juu ya Wagalilaya ambao Pilato alikuwa amechanganya damu yao pamoja na dhabihu zao. 2 Kwa hiyo kwa kujibu akawaambia: “Je, nyinyi mwawazia kwamba Wagalilaya hawa walithibitishwa kuwa watenda-dhambi wabaya zaidi kuliko Wagalilaya wengine wote kwa sababu wao wamepatwa na mambo haya? 3 La, hasha, mimi nawaambia nyinyi; lakini, isipokuwa mtubu, nyote mtaangamizwa hivyohivyo. 4 Au wale kumi na wanane ambao mnara katika Siloamu uliangukia, kwa njia hiyo ukiwaua, je, mwawazia kwamba walithibitishwa kuwa wadeni wakubwa zaidi kuliko watu wengine wote wenye kukaa Yerusalemu? 5 La, hasha, nawaambia nyinyi; lakini, isipokuwa mtubu, nyinyi nyote mtaangamizwa kwa njia hiyohiyo.”
6 Ndipo akaendelea kusema kielezi hiki: “Mtu fulani alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu, naye akaja akitafuta matunda juu yao, lakini hakupata yoyote. 7 Ndipo yeye akamwambia mtunza-mizabibu, ‘Sasa ni miaka mitatu ambayo nimekuja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, lakini sijapata yoyote. Ukate! Kwa kweli kwa nini huo uiweke nchi bila mafaa?’ 8 Kwa kujibu yeye akamwambia, ‘Bwana-mkubwa, uuache mwaka huu pia, mpaka nilime kuuzunguka na kuweka mbolea; 9 na ndipo ukitokeza matunda wakati ujao, basi ni vema; lakini ikiwa sivyo, hakika utaukata.’”
10 Basi yeye alikuwa akifundisha katika mojawapo ya masinagogi siku ya sabato. 11 Na, tazama! mwanamke mwenye roho ya udhaifu kwa miaka kumi na minane, naye alikuwa amepindika sana na alikuwa hawezi kujiinua mwenyewe kamwe. 12 Alipomwona mwanamke huyo, Yesu alimsemesha na kumwambia: “Mwanamke, umefunguliwa kutoka udhaifu wako.” 13 Naye akaweka mikono yake juu ya mwanamke huyo; na mara hiyo akanyooka, akaanza kumtukuza Mungu. 14 Lakini kwa kujibu ofisa-msimamizi wa sinagogi, akiwa ameghadhibika kwa sababu Yesu alifanya hilo ponyo siku ya sabato, akaanza kuuambia umati: “Kuna siku sita ambazo katika hizo kazi yapasa kufanywa; kwa hiyo, mje mponywe katika hizo, wala si siku ya sabato.” 15 Hata hivyo, Bwana akamjibu na kusema: “Wanafiki, je, kila mmoja wenu siku ya sabato hafungui fahali wake au punda wake kutoka kwenye kibanda na kumwongoza akamnyweshe? 16 Basi, je, haikuwa haki mwanamke huyu aliye binti ya Abrahamu, na ambaye Shetani alimshika akiwa amefungwa, tazama! miaka kumi na minane, afunguliwe kutoka kwenye kifungo hiki siku ya sabato?” 17 Basi, aliposema mambo hayo, wapingaji wake wote wakaanza kuona aibu; lakini umati wote ukaanza kuyashangilia mambo matukufu yote yaliyofanywa naye.
18 Kwa hiyo yeye akaendelea kusema: “Ufalme wa Mungu ni kama nini, nami nitaulinganisha na nini? 19 Ni kama punje ya haradali ambayo mtu alichukua akaiweka katika bustani yake, nayo ikakua ikawa mti, nao ndege wa mbinguni wakapata makao katika matawi yao.”
20 Naye tena akasema: “Nitaulinganisha ufalme wa Mungu na nini? 21 Ni kama chachu, ambayo mwanamke alichukua na kuificha katika vipimo vikubwa vitatu vya unga mpaka tungamo lote lilipochachushwa.”
22 Naye akasafiri kupita kutoka jiji hadi jiji na kutoka kijiji hadi kijiji, akifundisha na kuendelea katika safari yake hadi Yerusalemu. 23 Sasa mtu fulani akamwambia: “Bwana, je, wale wanaookolewa ni wachache?” Yeye akawaambia: 24 “Jikakamueni wenyewe kisulubu ili mwingie ndani kupitia mlango mwembamba, kwa sababu wengi, mimi nawaambia nyinyi, watatafuta sana kuingia ndani lakini hawataweza, 25 mara mwenye nyumba akiisha kuinuka na kuufunga mlango kwa kufuli, nanyi mwaanza kusimama nje na kubisha hodi kwenye mlango, mkisema, ‘Bwana, tufungulie.’ Lakini kwa kujibu atawaambia nyinyi, ‘Mimi sijui nyinyi mwatoka wapi.’ 26 Ndipo mtakapoanza kusema, ‘Tulikula na kunywa mbele yako, na wewe ulifundisha katika njia zetu pana.’ 27 Lakini yeye atasema na kuwaambia nyinyi, ‘Sijui nyinyi mwatoka wapi. Ondokeni kwangu, nyinyi nyote wafanyakazi wa ukosefu wa uadilifu!’ 28 Hapo ndipo kutoa machozi kwenu na kusaga meno yenu kutakuwa, wakati mwonapo Abrahamu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, lakini nyinyi wenyewe mkiwa mmetupwa nje. 29 Zaidi ya hilo, watu watakuja kutoka sehemu za mashariki na za magharibi, na kutoka kaskazini na kusini, nao wataegama kwenye meza katika ufalme wa Mungu. 30 Na, tazama! kuna wale wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na kuna wale wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
31 Saa hiyohiyo Mafarisayo fulani wakaja, wakimwambia: “Toka ushike njia yako uende kutoka hapa, kwa sababu Herode ataka kukuua.” 32 Naye akawaambia: “Nendeni mkamwambie mbweha huyo, ‘Tazama! Mimi ninatoa roho waovu na kutimiza kuponya leo na kesho, na siku ya tatu nitakuwa nimemaliza.’ 33 Hata hivyo, lazima nishike njia yangu kwenda leo na kesho na siku ifuatayo, kwa sababu haikubaliki nabii kuangamizwa nje ya Yerusalemu. 34 Yerusalemu, Yerusalemu, muuaji wa manabii na mpigaji kwa mawe wa hao waliotumwa kwake—ni mara nyingi kadiri gani nilitaka kukusanya watoto wako pamoja kwa namna ambayo kuku hukusanya makinda yake ya vifaranga chini ya mabawa yake, lakini nyinyi watu hamkutaka hilo! 35 Tazameni! Nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. Nawaambia, Nyinyi hamtaniona kwa vyovyote mpaka msemapo, ‘Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova!’”