Luka
11 Sasa pindi alipokuwa mahali fulani akisali, alipokoma, mtu fulani kati ya wanafunzi wake alimwambia: “Bwana, tufundishe jinsi ya kusali, sawa na vile Yohana pia alivyofundisha wanafunzi wake.”
2 Ndipo akawaambia: “Wakati wowote msalipo, semeni, ‘Baba, jina lako na litakaswe. Acha ufalme wako uje. 3 Tupe sisi mkate wetu kwa siku kulingana na takwa la siku. 4 Na utusamehe dhambi zetu, kwa maana sisi wenyewe pia husamehe kila mtu aliye na deni letu; na usituingize katika kishawishi.’”
5 Zaidi, yeye akawaambia: “Ni nani kati yenu atakuwa na rafiki naye atamwendea katikati ya usiku na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu, 6 kwa sababu rafiki yangu amenijia sasa hivi kutoka safarini nami sina kitu cha kuweka mbele yake’? 7 Na huyo wa kutoka ndani asema kwa kujibu, ‘Koma kunisumbua. Mlango tayari umefungwa kwa kufuli, na watoto wangu wachanga wapo pamoja nami kitandani; siwezi kuamka nikupe wewe kitu chochote.’ 8 Mimi nawaambia nyinyi, Ijapokuwa hataamka ampe kitu chochote kwa sababu ya kuwa rafiki yake, hakika kwa sababu ya udumifu wake wa ujasiri ataamka na kumpa vitu vile ahitajivyo. 9 Basi nawaambia nyinyi, Fulizeni kuomba, nanyi mtapewa; fulizeni kutafuta sana, nanyi mtapata; fulizeni kubisha hodi, nanyi mtafunguliwa. 10 Kwa maana kila mtu anayeomba hupokea, na kila mtu anayetafuta sana hupata, na kwa kila mtu anayebisha hodi hufunguliwa. 11 Kwa kweli, ni baba yupi miongoni mwenu ambaye, ikiwa mwana wake aomba samaki, labda atampa nyoka badala ya samaki? 12 Au ikiwa pia aomba yai, atampa nge? 13 Kwa hiyo, ikiwa nyinyi, mjapokuwa waovu, mwajua jinsi ya kuwapa watoto wenu zawadi zilizo njema, je, si zaidi sana yule Baba aliye mbinguni atawapa roho takatifu wale wanaomwomba!”
14 Baadaye alikuwa akifukuza roho mwovu aliye bubu. Baada ya roho huyo mwovu kutoka, yule bubu alisema. Nao umati ukastaajabu. 15 Lakini watu fulani kati yao wakasema: “Yeye huwafukuza roho waovu kupitia Beelzebubi mtawala wa roho waovu.” 16 Hata hivyo, wengine, ili kumshawishi, wakaanza kutafuta sana kutoka kwake ishara ya kutoka mbinguni. 17 Akijua mawazo yao akawaambia: “Kila ufalme uliogawanyika dhidi yao wenyewe huja kwenye ukiwa, na nyumba iliyogawanyika dhidi yayo yenyewe huanguka. 18 Kwa hiyo ikiwa Shetani pia amegawanyika dhidi yake mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Kwa sababu nyinyi mwasema mimi hufukuza roho waovu kupitia Beelzebubi. 19 Ikiwa ni kupitia Beelzebubi mimi hufukuza roho waovu, ni kwa nani wana wenu huwafukuza? Kwa sababu ya hilo wao watakuwa mahakimu wenu. 20 Lakini ikiwa ni kupitia kidole cha Mungu mimi huwafukuza roho waovu, ufalme wa Mungu kwa kweli umewapata nyinyi ghafula. 21 Wakati mtu mwenye nguvu, mwenye silaha za kutosha, alindapo ikulu yake, mali zake huendelea kuwako kwa amani. 22 Lakini wakati mtu fulani mwenye nguvu zaidi yake ajapo dhidi yake na kumshinda, yeye huchukua zana zake zote za vita alizokuwa akiitibari, naye hugawanya vitu ambavyo yeye alimpora. 23 Yeye asiye upande wangu yuko dhidi yangu, naye asiyekusanya pamoja nami hutawanya.
24 “Wakati roho asiye safi amtokapo mtu, hupita katika mahali palipokauka akitafuta mahali pa pumziko, na, baada ya kukosa kupata pamoja, husema, ‘Hakika nitarudi kwenye nyumba yangu niliyoihama.’ 25 Naye awasilipo huikuta imefagiwa ikawa safi na kurembwa. 26 Ndipo huyo hushika njia yake kwenda na kuchukua roho saba tofauti walio waovu zaidi yake mwenyewe waambatane naye, na, baada ya kuingia ndani, wao hukaa humo; na hali za mwisho za mtu huyo huwa mbaya zaidi kuliko zile za kwanza.”
27 Sasa alipokuwa akisema mambo haya mwanamke fulani katika umati akainua sauti yake akamwambia: “Lenye furaha ni tumbo la uzazi lililokuchukua wewe na matiti uliyonyonya!” 28 Lakini yeye akasema: “La, badala ya hivyo, Wenye furaha ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika!”
29 Wakati umati ulipokuwa ukisongamana pamoja, yeye alianza kusema: “Kizazi hiki ni kizazi kiovu; hutafuta ishara. Lakini hakuna ishara kitakayopewa ila ishara ya Yona. 30 Kwa maana sawa na vile Yona alivyopata kuwa ishara kwa Waninewi, ndivyo Mwana wa binadamu atakavyokuwa pia kwa kizazi hiki. 31 Malkia wa kusini atainuliwa katika hukumu pamoja na wanaume wa kizazi hiki naye atawalaumu; kwa sababu yeye alikuja kutoka miisho ya dunia aisikie hekima ya Solomoni, lakini, tazameni! kitu fulani zaidi ya Solomoni kipo hapa. 32 Wanaume wa Ninewi watainuka katika hukumu pamoja na kizazi hiki nao watakilaumu; kwa sababu wao walitubia alilohubiri Yona; lakini, tazameni! kitu fulani zaidi ya Yona kipo hapa. 33 Baada ya kuwasha taa, mtu huiweka, si katika stoo iliyo chini ya ardhi wala chini ya kikapu cha kupimia, bali juu ya kinara cha taa, ili wale wanaoingia ndani wapate kuiona nuru. 34 Taa ya mwili ni jicho lako. Wakati jicho lako ni sahili, mwili wako wote ni mwangavu pia; lakini wakati ni ovu, mwili wako ni wenye giza pia. 35 Kwa hiyo, uwe chonjo. Labda nuru iliyo ndani yako ni giza. 36 Kwa hiyo, ikiwa mwili wako wote ni mwangavu bila sehemu yenye giza hata kidogo, wote utakuwa mwangavu kama wakati taa ikupapo wewe nuru kwa miale yayo.”
37 Alipokuwa amesema hili, Farisayo mmoja alimwomba ale mlo-mkuu pamoja naye. Kwa hiyo yeye akaingia na kuegama kwenye meza. 38 Hata hivyo, huyo Farisayo alishangaa kuona kwamba yeye hakujiosha kwanza kabla ya huo mlo-mkuu. 39 Lakini Bwana akamwambia: “Sasa nyinyi Mafarisayo, husafisha upande wa nje wa kikombe na sahani, lakini upande wenu wa ndani umejaa uporaji na uovu. 40 Nyinyi watu wenye kukosa akili! Yeye aliyeufanya upande wa nje aliufanya upande wa ndani pia, sivyo? 41 Hata hivyo, vitoeni viwe kama zawadi za rehema vitu vilivyo ndani, na, tazameni! vitu vingine vyote ni safi kuwahusu nyinyi. 42 Lakini ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu nyinyi hutoa sehemu ya kumi ya mnanaa na mchicha na ya kila mboga nyingine, lakini nyinyi hupita kando ya haki na upendo kwa Mungu! Mambo hayo mlikuwa chini ya wajibu kuyafanya, lakini mambo yale mengine kutoyaacha nje. 43 Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu nyinyi hupenda viti vya mbele katika masinagogi na zile salamu katika mahali pa masoko! 44 Ole wenu, kwa sababu nyinyi mko kama yale makaburi ya ukumbusho yasiyoonekana, hivi kwamba watu hutembea juu yayo na hawajui hilo!”
45 Kwa kujibu mtu fulani kati ya wale wenye ujuzi mwingi katika Sheria akamwambia: “Mwalimu, katika kusema mambo hayo wewe watutusi pia.” 46 Ndipo akasema: “Ole wenu pia nyinyi mlio na ujuzi mwingi katika Sheria, kwa sababu nyinyi hutwika watu mizigo iliyo migumu kuhimiliwa, lakini nyinyi wenyewe hamgusi hiyo mizigo kwa kimoja cha vidole vyenu!
47 “Ole wenu nyinyi, kwa sababu nyinyi huyajenga makaburi ya ukumbusho ya manabii, lakini mababa zenu wa zamani waliwaua! 48 Hakika nyinyi ni mashahidi wa vitendo vya baba zenu wa zamani na bado nyinyi mwawapa kibali, kwa sababu hao waliwaua manabii lakini nyinyi mnajenga makaburi yao. 49 Kwa ajili ya hili hekima ya Mungu ilisema pia, ‘Hakika mimi nitatuma kwao manabii na mitume, nao wataua na kunyanyasa baadhi yao, 50 ili damu ya manabii wote iliyomwagwa tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu ipate kutakwa kutoka kwa kizazi hiki, 51 tangu damu ya Abeli mpaka kwenye damu ya Zekaria, aliyechinjwa katikati ya madhabahu na ile nyumba.’ Ndiyo, nawaambia nyinyi, itatakwa kutoka kwa kizazi hiki.
52 “Ole wenu nyinyi wenye ujuzi mwingi katika Sheria, kwa sababu mliondoa ufunguo wa ujuzi; nyinyi wenyewe hamkuingia, na wale wanaoingia nyinyi mliwazuia!”
53 Basi alipoenda kutoka huko waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga sana na kumuuliza-uliza maswali juu ya mambo zaidi, 54 wakimwotea, ili wanase kitu fulani kutoka kinywani mwake.