Luka
10 Baada ya mambo hayo Bwana akachagua sabini wengine na kuwatuma wawili-wawili kumtangulia kuingia katika kila jiji na mahali ambako yeye mwenyewe alikuwa akitaka kwenda. 2 Ndipo akaanza kuwaambia: “Kwa kweli, mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana-mkubwa wa mavuno atume wafanyakazi katika mavuno yake. 3 Nendeni. Tazameni! Mimi nawatuma nyinyi kama wana-kondoo miongoni mwa mbwa-mwitu. 4 Msichukue kibeti, wala mfuko wa chakula, wala makubazi, na msikumbatie yeyote katika kusalimu barabarani. 5 Popote pale mwingiapo katika nyumba semeni kwanza, ‘Nyumba hii na iwe na amani.’ 6 Na ikiwa rafiki wa amani yumo, amani yenu itatulia juu yake. Lakini ikiwa hayumo, itawarudia nyinyi. 7 Kwa hiyo kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa vitu ambavyo wao waandaa, kwa maana mfanyakazi astahili mshahara wake. Msiwe mkihama kutoka nyumba hadi nyumba.
8 “Pia, popote mwingiapo katika jiji nao wawapokea, vileni vitu vilivyowekwa mbele yenu, 9 na waponyeni wagonjwa walio katika hiyo, na endeleeni kuwaambia, ‘Ufalme wa Mungu umekuja karibu nanyi.’ 10 Lakini popote mwingiapo katika jiji nao hawawapokei nyinyi, tokeni mwende mwingie katika njia zalo pana na kusema, 11 ‘Hata vumbi lililoshikamana na miguu yetu kutoka katika jiji lenu twalifuta dhidi yenu. Hata hivyo, wekeni hili akilini, kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12 Nawaambia nyinyi kwamba litakuwa jambo lenye kuvumilika zaidi kwa Sodoma siku hiyo kuliko kwa jiji hilo.
13 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! kwa sababu kama zile kazi zenye nguvu ambazo zimetendeka katika nyinyi zingalikuwa zimetendeka katika Tiro na Sidoni, wangalikuwa wametubu zamani za kale wakiwa wameketi katika nguo ya gunia na majivu. 14 Kwa sababu hiyo litakuwa jambo lenye kuvumilika zaidi kwa Tiro na Sidoni katika hukumu kuliko kwenu. 15 Na wewe, Kapernaumu, je, labda wewe utakwezwa hadi mbinguni? Utateremka kuja chini hadi Hadesi!
16 “Yeye awasikilizaye nyinyi hunisikiliza mimi pia. Naye awapuuzaye nyinyi hunipuuza mimi pia. Zaidi ya hayo, yeye anipuuzaye mimi humpuuza pia yeye aliyenituma.”
17 Ndipo wale sabini wakarudi wakiwa na shangwe, wakisema: “Bwana, hata roho waovu watiishwa kwetu kwa utumizi wa jina lako.” 18 Ndipo akawaambia: “Nilianza kumwona Shetani akiwa tayari ameanguka kama umeme kutoka mbinguni. 19 Tazameni! Nimewapa nyinyi mamlaka ya kukanyaga-kanyaga chini ya miguu nyoka na nge, na juu ya nguvu yote ya adui, na hakuna kitu kitakachowaumiza nyinyi kwa vyovyote. 20 Hata hivyo, msishangilie juu ya hili, kwamba roho watiishwa kwenu, bali shangilieni kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” 21 Katika saa hiyohiyo yeye akawa mwenye shangwe mno katika roho takatifu akasema: “Nakusifu hadharani wewe, Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa sababu umeficha mambo hayo kwa uangalifu kutoka kwa wenye hekima na walio na akili, nawe umeyafunua kwa vitoto. Ndiyo, Ee Baba, kwa sababu kufanya hivyo kulikuja kuwa ndiyo njia ikubaliwayo na wewe. 22 Vitu vyote vimekabidhiwa kwangu na Baba yangu, na ya kwamba Mwana ni nani hakuna ajuaye ila Baba; na ya kwamba Baba ni nani, hakuna ajuaye ila Mwana, na yeye ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”
23 Ndipo akawageukia wanafunzi wakiwa peke yao na kusema: “Yenye furaha ni macho yaonayo mambo ambayo nyinyi mnayaona. 24 Kwa maana nawaambia nyinyi, Manabii na wafalme wengi walitamani kuyaona mambo ambayo nyinyi mnayaona lakini hawakuyaona, na kuyasikia mambo ambayo nyinyi mnayasikia lakini hawakuyasikia.”
25 Sasa, tazama! mtu fulani mwenye ujuzi mwingi katika Sheria akainuka, ili kumjaribu, akasema: “Mwalimu, ni kwa kufanya nini mimi nitarithi uhai udumuo milele?” 26 Yeye akamwambia: “Ni nini limeandikwa katika Sheria? Wewe wasomaje?” 27 Kwa kujibu akasema: “‘Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote,’ na, ‘jirani yako kama wewe mwenyewe.’” 28 Akamwambia: “Ulijibu kwa usahihi; ‘endelea kufanya hilo nawe utapata uhai.’”
29 Lakini, akitaka kujithibitisha mwenyewe kuwa mwadilifu, huyo mtu akamwambia Yesu: “Ni nani kwa kweli aliye jirani yangu?” 30 Kwa kujibu Yesu akasema: “Mtu fulani alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko akaanguka miongoni mwa wapokonyaji, ambao walimvua nguo na pia kumpiga, wakaenda zao, wakimwacha yeye nusura kufa. 31 Sasa, kwa sadfa, kuhani fulani alikuwa akiteremka katika barabara hiyo, lakini, alipomwona, akaenda kupita kando upande wa pili. 32 Hivyohivyo, Mlawi pia, alipofika chini kwenye mahali hapo na kumwona, akaenda kupita kando upande wa pili. 33 Lakini Msamaria fulani mwenye kusafiri katika ile barabara alikuja akamkuta na, alipomwona, akasukumwa na sikitiko. 34 Kwa hiyo akamkaribia akafunga majeraha yake, akimwaga mafuta na divai juu yayo. Kisha akampandisha juu ya hayawani wake mwenyewe akamleta kwenye hoteli ndogo na kumtunza. 35 Na siku iliyofuata akatoa dinari mbili, akampa hizo mtunza-hoteli, na kusema, ‘Mtunze, na chochote kile utumiacho mbali na hiki, mimi nitakulipa nirudipo hapa.’ 36 Ni nani kati ya watatu hawa aonekana kwako kuwa alijifanya mwenyewe jirani kwa mtu aliyeanguka miongoni mwa wapokonyaji?” 37 Akasema: “Yeye aliyetenda kwa rehema kumwelekea.” Ndipo Yesu akamwambia: “Shika njia yako uende na uwe ukifanya hilohilo wewe mwenyewe.”
38 Basi walipokuwa wameshika njia yao kwenda aliingia katika kijiji fulani. Hapa mwanamke fulani aitwaye jina Martha alimpokea awe mgeni ndani ya nyumba. 39 Mwanamke huyu alikuwa pia na dada aitwaye Maria, ambaye, hata hivyo, aliketi kwenye miguu ya Bwana na kufuliza kulisikiliza neno lake. 40 Martha, kwa upande mwingine, alivutwa fikira kwa kushughulikia kazi nyingi. Kwa hiyo, akaja karibu na kusema: “Bwana, si kitu kwako kwamba dada yangu ameniacha mimi peke yangu kushughulikia mambo? Kwa hiyo, mwambie ajiunge katika kunisaidia.” 41 Kwa kujibu Bwana akamwambia: “Martha, Martha, wewe wahangaika na kusumbuka juu ya mambo mengi. 42 Ingawa hivyo, mambo machache yahitajiwa, au moja tu. Kwa sehemu yake, Maria alichagua fungu jema, nalo halitaondolewa mbali naye.”