Luka
4 Basi Yesu, akiwa amejaa roho takatifu, akarudi kutoka Yordani, naye akaongozwa na ile roho huku na huku nyikani 2 kwa siku arobaini, alipokuwa akishawishwa na Ibilisi. Zaidi ya hilo, hakula kitu chochote katika siku hizo, na kwa hiyo, zilipomalizika, akaona njaa. 3 Ndipo Ibilisi akamwambia: “Ikiwa wewe ni mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.” 4 Lakini Yesu akamjibu: “Imeandikwa, ‘Binadamu lazima aishi, si kwa mkate pekee.’”
5 Kwa hiyo akamleta juu na kumwonyesha kwa mara moja falme zote za dunia inayokaliwa; 6 na Ibilisi akamwambia: “Hakika nitakupa mamlaka yote hii na utukufu wazo, kwa sababu nimekabidhiwa hiyo, na yeyote nimtakaye mimi humpa hiyo. 7 Kwa hiyo, wewe ukifanya tendo la ibada mbele yangu, yote itakuwa yako.” 8 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Imeandikwa, ‘Ni Yehova Mungu wako ambaye lazima uabudu, na ni kwake peke yake lazima utoe utumishi mtakatifu.’”
9 Sasa akamwongoza kuingia Yerusalemu akamsimamisha juu ya buruji ya hekalu na kumwambia: “Ikiwa wewe ni mwana wa Mungu, jivurumize chini kutoka hapa; 10 kwa maana imeandikwa, ‘Yeye atawapa malaika zake agizo kukuhusu wewe, ili wakuhifadhi,’ 11 na, ‘Watakuchukua mikononi mwao, ili usipate kupiga mguu wako dhidi ya jiwe wakati wowote.’” 12 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Imesemwa, ‘Lazima usimtie Yehova Mungu wako kwenye jaribu.’” 13 Kwa hiyo Ibilisi, akiisha kumaliza kishawishi chote, akaondoka kwake hadi wakati mwingine unaofaa.
14 Basi Yesu akarudi katika nguvu ya roho kuingia Galilaya. Na maongezi mazuri kumhusu yakasambaa katika nchi yote yenye kuzunguka. 15 Pia, akaanza kufundisha katika masinagogi yao, akionwa kwa heshima na wote.
16 Naye akaja hadi Nazareti, ambako alikuwa amelelewa; na, kulingana na desturi yake siku ya sabato, akaingia katika sinagogi, naye akasimama ili asome. 17 Kwa hiyo akapewa hati-kunjo ya nabii Isaya, naye akafungua hiyo hati-kunjo na kupata mahali palipokuwa pameandikwa: 18 “Roho ya Yehova iko juu yangu, kwa sababu alinitia mafuta kutangaza habari njema kwa walio maskini, alinituma kuhubiri kuachiliwa kwa mateka na kupata kuona tena kwa vipofu, kuacha waliopondeka waende zao wakiwa wameachiliwa, 19 kuhubiri mwaka wa Yehova wenye kukubalika.” 20 Ndipo akabiringa hiyo hati-kunjo, akairudisha kwa hadimu akaketi; na macho ya wote katika sinagogi yalikazwa sana juu yake. 21 Ndipo akaanza kuwaambia: “Leo andiko hili ambalo mmetoka tu kusikia limetimizwa.”
22 Nao wote wakaanza kutoa ushahidi mwema juu yake wakistaajabia maneno yenye uvutio mwingi yenye kutoka kinywani mwake, na walikuwa wakisema: “Huyu ni mwana wa Yosefu, sivyo?” 23 Ndipo akawaambia: “Hapana shaka mtatumia kielezi hiki kwangu, ‘Tabibu, jiponye mwenyewe; mambo tuliyosikia kuwa yamekwisha kutukia katika Kapernaumu yafanye pia hapa katika eneo la nyumbani kwako.’” 24 Lakini akawaambia: “Kweli nawaambia nyinyi kwamba hakuna nabii akubaliwaye katika eneo la nyumbani kwake. 25 Kwa mfano, nawaambia nyinyi kikweli, Kulikuwa na wajane wengi katika Israeli siku za Eliya, wakati mbingu ilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita, hivi kwamba njaa kali iliyo kubwa ikawa juu ya nchi yote, 26 lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa hata mmoja wa wanawake hao, ila tu kwenda Zarefathi katika nchi ya Sidoni kwa mjane mmoja. 27 Pia, kulikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli wakati wa Elisha nabii, lakini hakuna hata mmoja wao aliyesafishwa, ila Naamani yule mtu wa Siria.” 28 Basi wote hao waliokuwa wakisikia mambo hayo katika sinagogi wakawa wenye kujawa na hasira; 29 nao wakainuka wakamharakisha nje ya jiji, nao wakamwongoza hadi ukingo wa mlima ambao juu yake jiji lao lilikuwa limejengwa, kusudi wamwangushe chini kichwa-mbele. 30 Lakini yeye akapita katikati yao na kuendelea kushika njia yake akaenda.
31 Naye akateremka kwenda Kapernaumu, jiji moja la Galilaya. Naye alikuwa akiwafundisha siku ya sabato; 32 nao wakastaajabia njia yake ya kufundisha, kwa sababu usemi wake ulikuwa wenye mamlaka. 33 Basi katika sinagogi kulikuwa na mtu mwenye roho, roho mwovu asiye safi, naye akapaaza sauti kwa sauti kubwa: 34 “Ah! Tuna jambo gani nawe, Yesu wewe Mnazareti? Je, ulikuja kutuangamiza sisi? Najua sawasawa wewe ni nani, Mtakatifu wa Mungu.” 35 Lakini Yesu akamkemea, akisema: “Kimya, na umtoke.” Kwa hiyo, baada ya kumwangusha chini huyo mtu katikati yao, yule roho mwovu akamtoka bila kumuumiza. 36 Ndipo, mshangao ukawa juu ya wote, nao wakaanza kuongea wao kwa wao, wakisema: “Ni wa namna gani usemi huu, kwa sababu kwa mamlaka na nguvu yeye huagiza roho wasio safi, nao hutoka?” 37 Kwa hiyo habari kumhusu yeye zikafuliza kutoka na kuingia kila pembe ya nchi yenye kuzunguka.
38 Baada ya kuinuka kutoka katika sinagogi akaingia katika nyumba ya Simoni. Basi mama-mkwe wa Simoni alikuwa akitaabishwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu kwa ajili yake. 39 Kwa hiyo akasimama kando yake akaikemea homa, nayo ikamwacha. Akainuka mara hiyo akaanza kuwahudumia.
40 Lakini jua lilipokuwa likitua, wale wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi ya namna mbalimbali wakawaleta kwake. Kwa kuweka mikono yake juu ya kila mmoja wao akawa awaponya. 41 Roho waovu pia wakawa wakiwatoka wengi, wakipaaza kilio na kusema: “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” Lakini, kwa kuwakemea, hakuwa akiwaruhusu kusema, kwa sababu walimjua yeye kuwa ndiye Kristo.
42 Hata hivyo, kulipokuwa mchana, akatoka kwenda na kuendelea mbele hadi mahali pa upweke. Lakini umati ukaanza kumtafuta huku na huku na kuja hadi alikokuwa, nao ukajaribu kumzuia asiende zake kutoka kwao. 43 Lakini yeye akawaambia: “Pia kwenye majiji mengine ni lazima nitangaze habari njema ya ufalme wa Mungu, kwa sababu kwa ajili ya hili nilitumwa.” 44 Basi akaendelea kuhubiri katika masinagogi ya Yudea.