Luka
5 Pindi moja umati ulipokuwa ukisonga karibu naye na kusikiliza neno la Mungu, alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti. 2 Naye akaona mashua mbili zimeegeshwa kando ya ziwa, lakini wavuvi walikuwa wametoka ndani yazo na walikuwa wakiosha nyavu zao. 3 Akipanda ndani ya mojawapo ya hizo mashua, iliyokuwa ya Simoni, akamwomba aivute mbali kidogo kutoka nchi kavu. Ndipo akaketi, na kutoka kwenye hiyo mashua akaanza kufundisha umati. 4 Alipoacha kusema, akamwambia Simoni: “Vuta hadi mahali ambapo ni kilindi, nanyi watu shusheni nyavu zenu ili kupata mvuo.” 5 Lakini Simoni kwa kujibu akasema: “Mfunzi, usiku wote tulimenyeka na hatukupata kitu chochote, lakini kwa amri yako hakika nitaziteremsha nyavu.” 6 Basi, walipofanya hili, walizingira wingi mkubwa wa samaki. Kwa kweli, nyavu zao zikaanza kukatika. 7 Kwa hiyo wakawapungia wenzao mkono katika ile mashua nyingine waje kuwasaidia; nao wakaja, wakajaza mashua zote mbili, hivi kwamba zikaanza kuzama. 8 Alipoona hili, Simoni Petro akaanguka chini kwenye magoti ya Yesu, akisema: “Ondoka kwangu mimi, kwa sababu mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” 9 Kwa maana kwa mvuo wa samaki ambao waliteka alishikwa kabisa na mshangao, na wote waliokuwa pamoja naye, 10 na hivyohivyo Yakobo na Yohana pia, wana wa Zebedayo, ambao walikuwa washiriki pamoja na Simoni. Lakini Yesu akamwambia Simoni: “Koma kuogopa. Tangu sasa na kuendelea utakuwa ukivua watu wakiwa hai.” 11 Kwa hiyo wakarudisha hizo mashua kwenye nchi kavu, na kuacha kila kitu wakamfuata.
12 Pindi moja zaidi alipokuwa katika mojawapo ya hayo majiji, tazama! mwanamume mwenye kujaa ukoma! Alipomwona Yesu mara hiyo akajiangusha kifudifudi akamwomba, akisema: “Bwana, ikiwa tu wewe wataka, waweza kunifanya safi.” 13 Na kwa hiyo, akinyoosha mkono wake, akamgusa, akisema: “Mimi nataka. Fanywa safi.” Na mara ule ukoma ukamtoka. 14 Naye akampa mtu huyo maagizo asimwambie mtu yeyote: “Lakini nenda zako na ujionyeshe mwenyewe kwa kuhani, na kutoa toleo kuhusiana na kutakaswa kwako, sawa na vile Musa alielekeza, kuwa ushahidi kwao.” 15 Lakini neno juu yake lilikuwa likisambaa hata zaidi, na umati mkubwa ukawa ukija pamoja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Hata hivyo, akaendelea kukaa kwa faragha katika majangwa na kusali.
17 Baadaye katika mojawapo ya hizo siku alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wamekuja kutoka kila kijiji cha Galilaya na Yudea na Yerusalemu walikuwa wameketi hapo; na nguvu ya Yehova ilikuwa hapo ili afanye uponyaji. 18 Na, tazama! wanaume waliokuwa wamechukua kitandani mtu aliyekuwa amepooza, nao walikuwa wakitafuta sana njia ya kumwingiza na kumweka mbele yake. 19 Kwa hiyo, wakikosa kupata njia ya kumwingiza kwa sababu ya umati, wakapanda juu kwenye paa, na kupitia vigae wakamshusha chini pamoja na kile kitanda kidogo miongoni mwa wale waliokuwa mbele ya Yesu. 20 Na alipoona imani yao akasema: “Ewe mtu, dhambi zako umesamehewa.” 21 Basi waandishi na Mafarisayo wakaanza kujadiliana kwa kutoa sababu, wakisema: “Ni nani huyu anayesema makufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake?” 22 Lakini Yesu, akifahamu mawazo yao, akasema katika kuwajibu: “Ni nini mnachowazawaza ndani ya mioyo yenu? 23 Ni jipi lililo rahisi zaidi, kusema, ‘Dhambi zako umesamehewa,’ au kusema, ‘Inuka utembee’? 24 Lakini kusudi nyinyi mjue kwamba Mwana wa binadamu ana mamlaka juu ya dunia kusamehe dhambi—” akamwambia mtu aliyepooza: “Mimi nakuambia, Inuka uchukue kitanda chako kidogo na shika njia yako uende nyumbani.” 25 Na mara hiyo akainuka mbele yao, akachukua kile ambacho ilikuwa kawaida yake kulalia akaenda zake nyumbani kwake, akimtukuza Mungu. 26 Ndipo upeo wa shangwe ukashika wote, nao wakaanza kumtukuza Mungu, nao wakawa wenye kujawa na hofu, wakisema: “Tumeona mambo mageni leo!”
27 Basi baada ya mambo haya alitoka akaenda akamwona mkusanya-kodi aitwaye jina Lawi akiwa ameketi kwenye ofisi ya kodi, naye akamwambia: “Uwe mfuasi wangu.” 28 Na akiacha nyuma kila kitu akainuka akaanza kumfuata. 29 Pia, Lawi akamwandalia karamu kubwa ya makaribisho katika nyumba yake; na kulikuwa na umati mkubwa wa wakusanya-kodi na wengine waliokuwa pamoja nao wakiegama kwenye mlo. 30 Ndipo Mafarisayo na waandishi wao wakaanza kunung’unikia wanafunzi wake, wakisema: “Ni kwa nini mnakula na kunywa pamoja na wakusanya-kodi na watenda-dhambi?” 31 Kwa kujibu Yesu akawaambia: “Wale walio na afya hawahitaji tabibu, bali wale wenye kuugua. 32 Nimekuja kuita, si watu waadilifu, bali watenda-dhambi waje kwenye toba.”
33 Wakamwambia: “Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi na kutoa dua, na ndivyo wafanyavyo wale wa Mafarisayo, lakini wako hula na kunywa.” 34 Yesu akawaambia: “Hamwezi kufanya marafiki wa bwana-arusi wafunge wakati bwana-arusi yupo pamoja nao, sivyo? 35 Lakini siku zitakuja wakati bwana-arusi atakapoondolewa mbali kutoka kwao kwa kweli; ndipo watakapofunga siku hizo.”
36 Zaidi, akaendelea kuwapa kielezi: “Hakuna akataye kiraka kutoka vazi jipya la nje na kukishonelea vazi kuukuu la nje; lakini akifanya hivyo, ndipo kiraka kipya huraruka kikajiondoa na pia kiraka kutoka katika vazi jipya hakilingani na lile kuukuu. 37 Zaidi ya hayo, hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vikuukuu vya divai; lakini akifanya hivyo, ndipo divai mpya itapasua viriba vya divai, na itamwagika na viriba vya divai vitaharibika. 38 Lakini divai mpya lazima iwekwe ndani ya viriba vipya vya divai. 39 Hakuna ambaye amekunywa divai kuukuu atakaye mpya; kwa maana husema, ‘Ile kuukuu ni nzuri.’”