Luka
6 Basi siku moja ya sabato moja ikatukia kwamba akawa anapita katikati ya mashamba ya nafaka, na wanafunzi wake walikuwa wakikwanyua na kula masuke ya nafaka, wakiyapukusa kwa mikono yao. 2 Ndipo baadhi ya Mafarisayo wakasema: “Kwa nini mnafanya lisiloruhusika kisheria siku ya sabato?” 3 Lakini Yesu akasema kwa kuwajibu: “Je, hamjasoma kamwe jambo lilelile alilofanya Daudi wakati yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye walipoona njaa? 4 Jinsi alivyoingia ndani ya nyumba ya Mungu akapokea mikate ya toleo naye akala na kuwapa watu waliokuwa naye baadhi yayo, ambayo hairuhusiki kisheria kwa mtu yeyote kula ila kwa makuhani tu?” 5 Naye akaendelea kuwaambia: “Mwana wa binadamu ndiye aliye Bwana wa sabato.”
6 Baadaye siku ya sabato nyingine akaingia katika sinagogi akaanza kufundisha. Na kulikuwa na mtu mmoja ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umenyauka. 7 Waandishi na Mafarisayo sasa walikuwa wakimchunguza sana kuona kama angeponya siku ya sabato, ili wapate njia fulani ya kumshtaki. 8 Hata hivyo, yeye alijua mawazowazo yao, lakini akamwambia huyo mtu mwenye mkono ulionyauka: “Inuka usimame katikati.” Naye akainuka akasimama. 9 Ndipo Yesu akawaambia: “Nawauliza nyinyi watu, Je, yaruhusika kisheria siku ya sabato kutenda lililo jema au kutenda lililo baya, kuokoa au kuangamiza nafsi?” 10 Na baada ya kutazama huku na huku kuwaelekea wote, akamwambia huyo mtu: “Nyoosha mkono wako.” Akafanya hivyo, na mkono wake ukaponywa. 11 Lakini wakawa wenye kujawa na kichaa, nao wakaanza kuzungumza wao kwa wao lile ambalo wangeweza kumfanya Yesu.
12 Siku hizo zilipokuwa zikiendelea alitoka kwenda kuingia katika mlima ili asali, naye akaendelea usiku wote katika sala kwa Mungu. 13 Lakini ilipokuwa mchana akawaita wanafunzi wake kwake akachagua kutoka miongoni mwao kumi na wawili, ambao pia aliwaita jina mitume: 14 Simoni, ambaye pia alimwita jina Petro, na Andrea ndugu yake, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartholomayo, 15 na Mathayo na Tomasi, na Yakobo mwana wa Alfayo, na Simoni aitwaye “mwenye bidii,” 16 na Yudasi mwana wa Yakobo, na Yudasi Iskariote, aliyegeuka kuwa haini.
17 Naye akateremka pamoja nao na kuchukua kikao chake mahali penye usawa, na kulikuwa na umati mkubwa wa wanafunzi wake, na umati mkubwa wa watu kutoka Yudea yote na Yerusalemu na mkoa wa mwambao wa Tiro na Sidoni, waliokuja kumsikia na kuponywa magonjwa yao. 18 Hata wale waliotaabishwa na roho wasio safi waliponywa. 19 Na umati wote ulikuwa ukitafuta kumgusa, kwa sababu nguvu ilikuwa ikimtoka na kuwaponya wote.
20 Naye akainua macho yake juu ya wanafunzi wake na kuanza kusema:
“Wenye furaha ni nyinyi maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.
21 “Wenye furaha ni nyinyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashibishwa.
“Wenye furaha ni nyinyi mtoao machozi sasa, kwa sababu mtacheka.
22 “Wenye furaha ni nyinyi wakati wowote ule watu wawachukiapo nyinyi, na wakati wowote ule watu wawatengapo nyinyi na kuwashutumu na kulitupa nje jina lenu kuwa ovu kwa ajili ya Mwana wa binadamu. 23 Shangilieni siku hiyo na kuruka, kwa maana, tazama! thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa maana hayo ni mambo yaleyale ambayo mababa zao wa zamani walikuwa na kawaida ya kuwafanyia manabii.
24 “Lakini ole wenu watu matajiri, kwa sababu mnapata kamili faraja yenu.
25 “Ole wenu ambao mmeshibishwa sasa, kwa sababu mtashikwa na njaa.
“Ole, nyinyi mnaocheka sasa, kwa sababu mtaomboleza na kutoa machozi.
26 “Ole, wakati wowote ule watu wote wasemapo vema juu yenu, kwa maana mambo kama hayo ndiyo ambayo mababa zao wa zamani waliwafanyia manabii wasio wa kweli.
27 “Lakini mimi nawaambia nyinyi mnaosikiliza, Endeleeni kupenda maadui wenu, kuwafanyia mema wale wanaowachukia, 28 kuwabariki wale wanaowalaani nyinyi, kusali kwa ajili ya wale wanaowatusi. 29 Akupigaye kwenye shavu moja, mtolee na lile jingine pia; na achukuaye vazi lako la nje, usimzuie hata vazi lile la ndani. 30 Mpe kila mtu anayekuomba, na kutoka kwa yule anayechukua vitu vyako, usiombe urudishiwe vitu hivyo.
31 “Pia, kama vile mtakavyo watu wawafanyie nyinyi, wafanyieni wao kwa njia hiyohiyo.
32 “Na mkipenda wale wanaowapenda nyinyi, hilo lina sifa gani kwenu? Kwa maana hata watenda-dhambi hupenda wale wanaowapenda. 33 Na mkiwatendea mema wale wanaowatendea nyinyi mema, kwa kweli hilo lina sifa gani kwenu? Hata watenda-dhambi hufanya hivyohivyo. 34 Pia, mkikopesha bila faida wale ambao mwatumaini kupokea kutoka kwao, hilo lina sifa gani kwenu? Hata watenda-dhambi hukopesha watenda-dhambi bila faida ili wapate kurudishiwa kwa kadiri ileile. 35 Kinyume chake, endeleeni kupenda maadui wenu na kutenda mema na kukopesha bila faida, bila kutumainia kurudishiwa chochote; na thawabu yenu itakuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Zaidi Sana, kwa sababu yeye ni mwenye fadhili kuelekea wasio na shukrani na waovu. 36 Endeleeni kuwa wenye rehema, sawa na vile Baba yenu ni mwenye rehema.
37 “Zaidi ya hayo, komeni kuhukumu, nanyi hamtahukumiwa kwa vyovyote; na komeni kulaumu, nanyi hamtalaumiwa kwa vyovyote. Fulizeni kuachilia, nanyi mtaachiliwa. 38 Zoeeni upaji, na watu watawapa nyinyi. Watamwaga katika mapaja yenu kipimo bora, kilichoshindiliwa, kilichotikiswa pamoja na kufurika. Kwa maana kwa kipimo mnachopimia, watawapimia nyinyi katika kurudishia.”
39 Ndipo akawaambia pia kielezi: “Kipofu hawezi kuongoza kipofu, je, aweza? Wote wawili watatumbukia ndani ya shimo, sivyo? 40 Mfunzwa hayuko juu ya mwalimu wake, lakini kila mtu aliyefunzwa kikamili atakuwa kama mwalimu wake. 41 Basi, kwa nini wautazama unyasi ulio katika jicho la ndugu yako lakini huangalii boriti lililo katika jicho lako mwenyewe? 42 Wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, niruhusu niutoe unyasi ulio katika jicho lako,’ hali wewe mwenyewe hutazami boriti katika hilo jicho lako? Mnafiki! Kwanza toa boriti katika jicho lako mwenyewe, na ndipo utaona waziwazi jinsi ya kutoa unyasi ulio katika jicho la ndugu yako.
43 “Kwa maana hakuna mti bora unaotokeza matunda yaliyooza; tena hakuna mti uliooza unaotokeza matunda bora. 44 Kwa maana kila mti hujulikana kwa matunda yao wenyewe. Kwa kielelezo, watu hawakusanyi tini kutoka katika miiba, wala hawakati zabibu kutoka katika kijiti cha miiba. 45 Mtu mwema hutokeza mema katika hazina njema ya moyo wake, lakini mtu mwovu hutokeza ambayo ni maovu katika hazina yake mbovu; kwa maana katika wingi wa moyo kinywa chake husema.
46 “Kwa nini, basi, mwaniita ‘Bwana! Bwana!’ lakini hamfanyi mambo nisemayo? 47 Kila mtu ajaye kwangu na kusikia maneno yangu na kuyafanya, hakika nitawaonyesha nyinyi yeye yuko kama nani: 48 Yeye ni kama mtu anayejenga nyumba, ambaye alichimba akaenda chini kina kirefu na kuweka msingi juu ya tungamo-mwamba. Baadaye, furiko lilipotokea, mto ulipiga dhidi ya nyumba hiyo kwa nguvu, lakini haukuwa na nguvu za kutosha kuitikisa, kwa sababu ya kuwa imejengwa vema. 49 Kwa upande ule mwingine, yeye asikiaye na hafanyi, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila msingi. Mto uliipiga kwa nguvu, na mara ikaporomoka, na uharibifu wa nyumba hiyo ukawa mkubwa.”