Matendo
27 Basi kwa kuwa iliamuliwa sisi tusafiri kwa mashua kwenda Italia, walikuwa wakikabidhi Paulo na pia wafungwa fulani wengine kwa ofisa-jeshi aitwaye jina Yuliasi wa kikosi cha Augusto. 2 Tukipanda ndani ya mashua kutoka Adramitiamu iliyokuwa karibu kusafiri hadi mahali pa kandokando ya pwani ya wilaya ya Asia, tukasafiri kwa mashua, kukiwa pamoja nasi Aristarko Mmakedonia kutoka Thesalonike. 3 Na siku iliyofuata tukateremka hadi katika Sidoni, na Yuliasi akamtendea Paulo kwa fadhili ya kibinadamu na kumruhusu aende kwa marafiki wake na kuonea shangwe utunzaji wao.
4 Na tukitweka kutoka huko tukasafiri kwa mashua chini ya kinga ya Saiprasi, kwa sababu pepo zilikuwa zenye kukabili; 5 nasi tukaendesha kupitia bahari iliyo wazi kandokando ya Kilikia na Pamfilia na kuegesha bandarini Mira katika Likia. 6 Lakini huko ofisa-jeshi akapata mashua kutoka Aleksandria iliyokuwa ikisafiri kwenda Italia, naye akatufanya tuipande. 7 Ndipo, baada ya kusafiri kwa mashua polepole kwa siku kadhaa na kuja Kinido kwa shida, kwa sababu upepo haukuturuhusu tuendelee mbele, tukasafiri chini ya kinga ya Krete katika Salmone, 8 na tukipita kandokando ya pwani yayo kwa shida tukaja mahali fulani paitwapo Bandari Nzuri, ambapo karibu napo palikuwa jiji Lasea.
9 Kwa kuwa muda mrefu ulikuwa umepita na kufikia sasa ilikuwa hatari kuendesha kwa sababu hata mfungo [wa siku ya kufunika] ulikuwa tayari umepita, Paulo alitoa pendekezo, 10 akiwaambia: “Wanaume, nahisi kwamba uendeshaji utakuwa na dhara na hasara kubwa si ya shehena na mashua tu bali pia ya nafsi zetu.” 11 Hata hivyo, ofisa-jeshi akawa anasikiza rubani na mwenye meli badala ya mambo yaliyosemwa na Paulo. 12 Sasa kwa kuwa hiyo bandari haikufaa kukaa wakati wa majira ya baridi, walio wengi wakashauri kusafiri kwa mashua kutoka hapo, ili kuona kama wangeweza kwa njia fulani kufaulu kufika Foinikse ili kukaa huko wakati wa majira ya baridi, ambayo ni bandari ya Krete ifungukayo kuelekea kaskazini-mashariki na kuelekea kusini-mashariki.
13 Zaidi ya hayo, upepo wa kusini ulipovuma kwa uanana, walifikiri walikuwa ni kama kwamba wamefikia kusudi lao, nao wakang’oa nanga na kuanza kufuata pwani karibu na ufuo wa Krete. 14 Hata hivyo, baada ya muda usiokuwa mrefu, upepo wenye tufani uitwao Euroakilo ukavuma kasi kushuka juu yayo. 15 Kwa kuwa mashua ilikamatwa kwa nguvu nyingi na haikuweza kuweka kichwa chayo dhidi ya upepo, tukajiachilia na kuchukuliwa pamoja nao. 16 Basi tukaenda upesi chini ya kinga ya kisiwa fulani kidogo kiitwacho Kauda, na bado tuliweza kwa shida kupata kuidhibiti kikamili mashua ndogo kwenye tezi. 17 Lakini baada ya kuinyanyua ndani wakaanza kutumia misaada ili kuikaza mashua chini; nao wakihofu kupanda mwamba katika Sirtisi, wakateremsha vifaa vya kuendeshea na hivyo wakaendeshwa. 18 Lakini kwa sababu tulikuwa tukirushwarushwa kwa nguvu nyingi pamoja na hiyo tufani, siku iliyofuata tukaanza kufanya meli iwe nyepesi; 19 na siku ya tatu, kwa mikono yao wenyewe, wakatupilia mbali ayari za hiyo mashua.
20 Basi, wakati ambapo jua wala nyota hazikuonekana kwa siku nyingi, nayo tufani iliyotulalia ikiwa si ndogo, tumaini lote la sisi kuokolewa mwishowe likaanza kukatiliwa mbali. 21 Na kulipokuwa kumekuwa na kujiepusha na chakula kwa muda mrefu, ndipo Paulo akasimama katikati yao na kusema: “Wanaume, hakika nyinyi mngalipaswa kufuata shauri langu na kutosafiri katika bahari kutoka Krete na hivyo kutopatwa na dhara na hasara hii. 22 Hata hivyo, sasa napendekeza kwenu mwe wenye uchangamfu mwingi, kwa maana hakuna nafsi kati yenu itakayopotea, ni mashua tu itakayopotea. 23 Kwa maana usiku huu kulisimama karibu nami malaika wa Mungu ambaye mimi ni mali yake na ambaye mimi namtolea utumishi mtakatifu, 24 akisema, ‘Usiwe na hofu, Paulo. Lazima usimame mbele ya Kaisari, na, tazama! Mungu amekupa kwa hiari wote wale wanaosafiri kwa mashua wakiwa pamoja nawe.’ 25 Kwa hiyo iweni wenye uchangamfu mwingi, wanaume; kwa maana namwamini Mungu kwamba itakuwa kama vile mimi nimeambiwa. 26 Hata hivyo, lazima tutupwe ufuoni juu ya kisiwa fulani.”
27 Sasa usiku wa kumi na nne ulipofika nasi tukawa tukirushwa huku na huku katika bahari ya Adria, katikati ya usiku mabaharia wakaanza kushuku walikuwa wakikaribia bara fulani. 28 Nao wakapima kina kwa bildi na kupata kuwa ni pima ishirini; kwa hiyo wakaendelea mbele umbali mfupi na wakatia bildi tena na kupata kuwa ni pima kumi na tano. 29 Na kwa sababu ya kuhofu kwamba tungeweza kutupwa mahali fulani juu ya miamba, wakatupa nje nanga nne kutoka kwenye tezi na kuanza kutaka kuwe mchana. 30 Lakini mabaharia walipoanza kutafuta sana kutoroka katika mashua na kuteremsha mashua ndogo ndani ya bahari kwa kusingizia kuwa walikusudia kuzishusha nanga kutoka kwenye omo, 31 Paulo akamwambia ofisa-jeshi na askari-jeshi: “Isipokuwa watu hawa wabaki katika mashua, nyinyi hamwezi kuokolewa.” 32 Ndipo askari-jeshi wakakata kamba za mashua ndogo na kuiacha ianguke.
33 Sasa karibu na mfikio wa mchana Paulo akaanza kutia moyo wote kutwaa chakula, akisema: “Leo ni siku ya kumi na nne ambayo mmekuwa katika lindo na mnaendelea bila chakula, mkiwa hamjajitwalia wenyewe kitu chochote. 34 Kwa hiyo nawatia moyo nyinyi mtwae chakula, kwa maana hii ni kwa faida ya usalama wenu; kwa maana hata unywele mmoja wa kichwa cha mmoja kati yenu hautaangamia.” 35 Baada ya kusema hili, pia akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega na kuanza kula. 36 Kwa hiyo wote wakawa wenye uchangamfu wakaanza wao wenyewe kutwaa chakula. 37 Basi, wote pamoja, sisi nafsi tuliomo ndani ya mashua tulikuwa mia mbili na sabini na sita. 38 Walipokuwa wameshiba chakula, wakaanza kupunguza uzito wa mashua kwa kutupa ngano ndani ya bahari kutoka katika mashua.
39 Mwishowe kulipokuwa mchana, hawangeweza kutambua hiyo nchi lakini walikuwa wakiangalia ghuba fulani yenye ufuo, na kwenye hii ndiko walikuwa wameazimia, ikiwa wangeweza, kuipeleka mashua pwani. 40 Kwa hiyo, wakizikata nanga, wakaziacha zianguke ndani ya bahari, wakati huohuo wakifungua amari za makasia ya mtambo-usukani na, baada ya kutweka tanga la mbele kwenye upepo, wakashika njia kwenda pwani. 41 Walipotua juu ya fungu la mchanga lililorundikwa na bahari pande zote mbili, wakaiendesha meli juu ya mwamba na omo ikakwama na kukaa bila kuondoleka, lakini tezi likaanza kuvunjwa vipande-vipande kwa nguvu nyingi. 42 Ndipo likawa azimio la askari-jeshi kuwaua wafungwa, ili yeyote asipate kuogelea kwenda mbali na kutoroka. 43 Lakini ofisa-jeshi akataka kumpitisha Paulo akiwa salama naye akawazuilia wasitekeleze kusudi lao. Naye akawaamuru wale wenye kuweza kuogelea wajitupe wenyewe ndani ya bahari na kufaulu kufika kwenye nchi kavu kwanza, 44 na wale wengine wafanye hivyo, wengine wakiwa juu ya mbao na wengine juu ya vitu fulani kutoka katika mashua. Na hivyo ikatukia kwamba wote wakaletwa salama kwenye nchi kavu.