Matendo
26 Agripa akamwambia Paulo: “Waruhusiwa kusema kwa ajili yako mwenyewe.” Ndipo Paulo akanyoosha mkono wake na kuanza kusema katika kujitetea:
2 “Kuhusu mambo yote ambayo juu yayo nashtakiwa na Wayahudi, Mfalme Agripa, najihesabu mwenyewe kuwa mwenye furaha kwamba ni mbele yako napaswa kujitetea siku hii, 3 hasa kwa kuwa wewe ni mtaalamu katika desturi zote na vilevile mabishano miongoni mwa Wayahudi. Kwa hiyo nakuomba unisikie kwa subira.
4 “Kwa kweli, juu ya namna ya maisha ya tangu ujana na kuendelea ambayo mimi niliendesha tangu mwanzo miongoni mwa taifa langu na katika Yerusalemu, Wayahudi wote 5 ambao hapo awali wamejuana nami tangu mwanzo wajua, kama tu wangetaka kutoa ushahidi, kwamba kulingana na usahihi kabisa wa farakano la namna yetu ya ibada mimi niliishi nikiwa Farisayo. 6 Lakini sasa kwa sababu ya tumaini la ahadi iliyofanywa na Mungu kwa baba zetu wa zamani nasimama nikiwa nimeitwa kwenye hukumu; 7 lakini makabila yetu kumi na mawili yanatumaini kufikia utimizo wa ahadi hii kwa kumtolea yeye utumishi mtakatifu kwa juhudi nyingi usiku na mchana. Kuhusu tumaini hili nashtakiwa na Wayahudi, Ewe mfalme.
8 “Kwa nini yahukumiwa kuwa haiaminiki miongoni mwenu nyinyi watu kwamba Mungu hufufua wafu? 9 Mimi, kwa upande wangu, kwa kweli nilifikiri ndani yangu mwenyewe kwamba napaswa kufanya matendo mengi ya upinzani dhidi ya jina la Yesu Mnazareti; 10 ambayo, kwa kweli, niliyafanya katika Yerusalemu, na wengi kati ya watakatifu niliwafunga gerezani, kwa kuwa nilikuwa nimepokea mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu; na walipokuwa wapaswa kufishwa, mimi nilitupa kura yangu dhidi yao. 11 Na kwa kuwaadhibu nyakati nyingi katika masinagogi yote nilijaribu kuwalazimisha wakane imani yao; na kwa kuwa nilikuwa mwenye kujawa na kichaa kupita kiasi dhidi yao, nilifikia hatua ya kuwanyanyasa hata katika majiji ya nje.
12 “Katikati ya hizi jitihada nilipokuwa nikisafiri kwenda Damasko nikiwa na mamlaka na agizo kutoka kwa makuhani wakuu, 13 Katikati ya mchana niliona kwenye barabara, Ewe mfalme, nuru ipitayo wangavu wa jua ikimweka kutoka mbinguni kunizunguka huku na huku na kuwazunguka huku na huku wale wenye kusafiri pamoja nami. 14 Na sisi sote tulipokuwa tumeanguka hadi chini nikasikia sauti ikiniambia katika lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unaninyanyasa mimi? Kufuliza kupiga teke dhidi ya michokoo hufanya iwe vigumu kwako.’ 15 Lakini nikasema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Naye Bwana akasema, ‘Mimi ni Yesu, ambaye wewe unanyanyasa. 16 Hata hivyo, inuka usimame kwa miguu yako. Kwa maana kwa madhumuni haya nimejifanya mwenyewe nionekane kwako, ili nikuchague wewe uwe hadimu na shahidi wa mambo ambayo umeona na pia mambo nitakayokufanya uyaone kwa habari yangu; 17 huku mimi nikikukomboa kutoka watu hawa na kutoka katika mataifa, ambao kwao ninakutuma wewe, 18 kufungua macho yao, kuwageuza kutoka kwenye giza hadi kwenye nuru na kutoka kwenye mamlaka ya Shetani hadi kwa Mungu, kusudi wao wapokee msamaha wa dhambi na urithi miongoni mwa wale waliotakaswa kwa imani yao katika mimi.’
19 “Kwa sababu hii, Mfalme Agripa, mimi sikupata kuwa asiyetii hilo ono la kimbingu, 20 lakini kwa wale katika Damasko kwanza na pia kwa wale katika Yerusalemu, na juu ya nchi yote ya Yudea, na kwa mataifa nilienda nikiuleta ujumbe kwamba wao wapaswa kutubu na kugeuka kuelekea Mungu kwa kufanya kazi zinazofaa toba. 21 Kwa sababu ya mambo haya Wayahudi walinikamata katika hekalu na kujaribu kuniua kikatili. 22 Hata hivyo, kwa sababu nimeupata msaada ambao ni kutoka kwa Mungu naendelea hadi siku hii kutoa ushahidi kwa wadogo na wakubwa pia, lakini bila kusema lolote ila mambo ambayo Manabii na vilevile Musa walitaarifu yalipaswa yatukie, 23 kwamba Kristo angepaswa kuteseka na, akiwa wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, angetangaza nuru kwa watu hawa na pia kwa mataifa.”
24 Sasa alipokuwa akisema mambo haya katika kujitetea kwake, Festo akasema kwa sauti kubwa: “Unashikwa na kichaa, Paulo! Kusoma kwingi kunakusukuma kuingia katika kichaa!” 25 Lakini Paulo akasema: “Mimi sishikwi na kichaa, Ewe Mtukuzwa Festo, bali ninatamka semi za kweli na za utimamu wa akili. 26 Kwa kweli, mfalme ambaye ninasema naye kwa uhuru wa usemi ajua vema juu ya mambo haya; kwa maana nimeshawishika kwamba hakuna hata moja kati ya mambo haya liponyokalo kujulikana naye, kwa maana jambo hili halijafanywa pembeni. 27 Je, wewe, Mfalme Agripa, wawaamini Manabii? Najua waamini.” 28 Lakini Agripa akamwambia Paulo: “Kwa muda mfupi ungenishawishi niwe Mkristo.” 29 Ndipo Paulo akasema: “Kama ingekuwa kwa muda mfupi au kwa muda mrefu mimi ningeweza kutaka kwa Mungu kwamba iwe si wewe tu bali pia wote wanisikiao leo wangepata kuwa watu wa namna niliyo mimi, isipokuwa vifungo hivi.”
30 Naye mfalme akainuka na pia gavana na Bernike na watu walioketi pamoja nao. 31 Lakini walipokuwa wakiondoka wakaanza kuongea wao kwa wao, wakisema: “Mtu huyu hazoei kufanya lolote linalostahili kifo au vifungo.” 32 Zaidi ya hayo, Agripa akamwambia Festo: “Mtu huyu angaliweza kufunguliwa kama hakuwa amekata rufani kwa Kaisari.”